Vipi Atubie Kiapo Cha Uongo?

 

Vipi Atubie Kiapo Cha Uongo?

 

Alhidaaya.com

 

Swali:

 

Assalamu aleikum

 

Kwa jina la Allaah mwingi wa rehma, naomba mnijulishe nini hukmu ya kiapo cha uongo na kama mtu aliapa uongo na anataka atubie basi atatubia vipi. Jazzakumullah Kheir

 

 

Jibu:

 

AlhamduliLLaah - Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

 

Yamini katika shari'ah ni kula kiapo kwa Majina ya Allaah Aliyetukuka au sifa Zake. Kwa mfano kusema, “Wa-Allaahi nitafanya kitu kadhaa” au “Naapa kwa yule ambaye nafsi yangu iko mikononi Mwake au Mgeuza nyoyo”. Inajuzu kuapa kwa njia hiyo. Lakini haijuzu kuapa bila ya majina ya Allaah na sifa Zake, ni sawa kinachoapiwa kinatukuzwa na shariy'ah au la. Kama vile kuapa kwa Ka‘bah, au kuapa kwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).  Hii ni kwa kauli ya Nabiy(Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):

 

"Anayeapa aape kwa Allaah au anyamaze" [Al-Bukhaariy, Muslim na Ahmad].

 

Na kauli ya Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): "Msiape ila kwa Allaah na msiape ila muwe wakweli" [Abuu Daawuwd na An-Nasaaiy].

 

Kuapa kwa asiyekuwa Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) ni haramu, nayo ni shirki. Hii ni kwa mujibu wa kauli ya Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): "Atayemuapia asiyekuwa Allaah basi amemshirikisha Allaah au amekufuru" [Abu Daawuwd, At-Tirmidhiy na Ahmad].

 

Yamini inagawanyika sehemu, nazo ni:

 

 

1. Al-Ghamuws:

Maana yake ni mtu kula kiapo huku anakusudia kuongopa, kama vile kusema: "Wa-Allaahi nimenunua kitu kadhaa kwa shilingi mia moja", naye hakukinunua hivyo. Au kusema: "Wa-Allaahi nimefanya kadhaa", na hali hakufanya. Hii imepatiwa jina hilo kwa sababu yamzamisha mwenye yamini hiyo ndani ya dhambi na yamini hii ndiyo iliyokusudiwa katika kauli ya Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):

 

"Atakayekula yamini hali yeye katika yamini hiyo anaongopa (anasema uongo) ili apate kwa yamini hiyo kumega mali ya mtu mwingine Muislamu basi mtu huyo atakutana na Allaah hali Amemkasirikia" [Al-Bukhaariy na Muslim].

 

 

Mhusika anapaswa afanye tawbah na kuomba maghfirah (msamaha) kwani kosa hili ni kubwa sana na kwa kauli sahihi kati ya kauli mbili, ni kuwa, Yamini ya uongo haina kafara bali kujutia na kutubu tawbah ya kweli. Ama ikiwa yamini hiyo itamfikisha kwenye kumega haki ya mtu mwengine Muislamu kwa njia isiyo ya halali, wako Wanachuoni waliona atalipa kafara na kufanya tawbah, lakini rai ya Imaam Ash-Shaafi‘iy ni kinyume na hivyo, kwani yeye anawajibisha kafara tu. Mtu katika kutaka msamaha na kutubia anatakiwa afanye hivyo kikweli kweli, kwani Allaah Aliyetukuka Anatufahamisha:

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا تُوبُوا إِلَى اللَّـهِ تَوْبَةً نَّصُوحًا عَسَىٰ رَبُّكُمْ أَن يُكَفِّرَ عَنكُمْ سَيِّئَاتِكُمْ وَيُدْخِلَكُمْ جَنَّاتٍ تَجْرِي مِن تَحْتِهَا الْأَنْهَارُ يَوْمَ لَا يُخْزِي اللَّـهُ النَّبِيَّ وَالَّذِينَ آمَنُوا مَعَهُ ۖ 

Enyi walioamini! Tubieni kwa Allaah tawbah ya nasuha (kwelikweli); asaa Rabb   wenu Akakufutieni maovu yenu, na Akakuingizeni Jannaat zipitazo chini yake mito. Siku ambayo Allaah Hatomfedhehesha Nabiy (Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم) na wale walioamini pamoja naye.  [At-Tahriym: 8].

 

 

Katika hayo aweke azma na niyyah thabiti ya kutorudia kosa hilo, ajute kwa kufanya kosa hilo, afanye mambo ya kheri, ajiepushe na maasiya hayo. Ikiwa amemdhulumu mja mwenziwe basi amrudishie haki yake pamoja na kumuomba msamaha.

 

 

2. Laghwul Yamiyn:

Hii ni ile ipitayo ulimini mwa Muislamu bila kuikusudia, kama yule ambaye katika mazungumzo yake hujitokeza kwa wingi mno wa neno: “Wa-Allaahi hapana”. Hii ni kufuatia kauli ya mama wa waumini ‘Aaishah (Radhwiya Allaahu ‘anhaa):

 

"Upuuzi katika yamini ni maneno anayozungumza mtu nyumbani mwake, “Wa-Allaahi hapana." [Al-Bukhaariy]. Jumla ya yamini ya upuuzi Muislamu akala kiapo juu ya jambo fulani akilidhania liko hivyo ikaja ikabainika tofauti na alivyodhania. Hukumu ya yamini aina hii ni kuwa haina dhambi wala kafara kwa mhusika, kwa kauli yake Allaah Aliyetukuka:

لَا يُؤَاخِذُكُمُ اللَّـهُ بِاللَّغْوِ فِي أَيْمَانِكُمْ

Allaah Hatokuchukulieni kwa viapo vyenu vya upuuzi, [Al-Maaidah: 89].

 

 

3. Yamini Iliyofungika:

Hii ni yamini inayochukuliwa kwa kukusudia jambo la baadaye. Kama vile Muislamu kusema: “Wa-Allaahi nitalifanya jambo kadhaa... au Wa-Allaahi sitalifanya…” Hii ndio yamini atakayoadhibiwa atakayefanya kinyume chake kwa kauli ya Aliyetukuka:

وَلَـٰكِن يُؤَاخِذُكُم بِمَا عَقَّدتُّمُ الْأَيْمَانَ ۖ

Lakini Atakuchukulieni kwa (kuvunja) viapo mlivyoapa kwa niyyah mlioifunga thabiti. [Al-Maaidah: 89].

 

 

Hukumu ya yamini aina hii ni kuwa atakaye kwenda kinyume na alivyoapa atapata dhambi na atawajibika afanye kafara, kama atafanya kafara dhambi itaanguka na kumuondokea.

 

Kafara na dhambi itaondoka kwa mwenye kula yamini kwa mambo mawili:

1. Kutoweza kutekeleza yamini kwa kusahau au kwa bahati mbaya au kwa kulazimishwa. Hii ni kwa kauli ya Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):

 

"Limeondolewa dhambi kwa Ummah wangu walilofanya kwa kutokusudia, kusahau au kulazimishwa" [Ibn Maajah].

 

2. Avue wakati wa kuapa kwa kusema In shaa Allaah (Allaah Akitaka) au pindi atakapotaka Allaah, kama kuvua huko kutafanyika katika kikao cha yamini, kwa kauli ya Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): 

 

"Atakayekula yamini akasema In shaa Allaah hakwenda kinyume na yamini yake" [Ahmad, At-Tirmidhiy na An-Nasaaiy].

 

Yasuniwa kwa Muislamu kama atakula yamini ya kuacha jambo fulani miongoni mwa mambo ya kheri basi asifanye, na afanye kafara la yamini yake, kwa kauli ya Allaah Aliyetukuka: “ [Al-Baqarah: 224].

 وَلَا تَجْعَلُوا اللَّـهَ عُرْضَةً لِّأَيْمَانِكُمْ أَن تَبَرُّوا وَتَتَّقُوا وَتُصْلِحُوا بَيْنَ النَّاسِ ۗ

Na wala msifanye (Jina la) Allaah kuwa ni nyudhuru ya viapo vyenu kukuzuieni katika kutenda wema na kuwa na taqwa na kusuluhisha baina ya watu. 

 

 

Na kwa kauli ya Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):

 

"Kama utakula yamini ukaona lingine ni bora kuliko hilo basi lifanye hilo bora na fanya kafara ya yamini yako" [Muslim].

 

 

Muislamu anapomlia yamini Muislamu mwenzake kuwa atafanya kitu, basi inamuwajibikia atekeleze kama alivyokula yamini, na asiende kinyume na yamini yake, na kufanya kafara muda upo uwezekano wa kutekeleza yamini yake. kinachozingatiwa katika kwenda kinyume na yamini na kutovunja ni nia na kusudio la mla yamini, kwa sababu matendo huthibitishwa na nia, na kila mtu atakipata alichokusudia.

 

 

Kafara ya yamini ni vitu vinne, kama ilivyo katika kauli ya Aliyetukuka:

فَكَفَّارَتُهُ إِطْعَامُ عَشَرَةِ مَسَاكِينَ مِنْ أَوْسَطِ مَا تُطْعِمُونَ أَهْلِيكُمْ أَوْ كِسْوَتُهُمْ أَوْ تَحْرِيرُ رَقَبَةٍ ۖ فَمَن لَّمْ يَجِدْ فَصِيَامُ ثَلَاثَةِ أَيَّامٍ ۚ ذَٰلِكَ كَفَّارَةُ أَيْمَانِكُمْ إِذَا حَلَفْتُمْ ۚ وَاحْفَظُوا أَيْمَانَكُمْ ۚ 

Basi kafara yake ni kulisha maskini kumi chakula cha wastani mnachowalisha ahli zenu, au kuwavisha nguo, au kuacha huru mtumwa. Lakini asiyeweza kupata (katika hayo), basi afunge Swiyaam siku tatu. Hiyo ndio kafara ya viapo vyenu mnapoapa. Na hifadhini yamini zenu. [Al-Maaidah: 89].

 

 

1. Kulisha masikini kumi kwa kuwapa kila mmoja kibaba cha ngano, au kuwakusanya wote katika chakula cha mchana au usiku wale mpaka washibe.

2. Kuwavisha nguo inayotosheleza katika Swaalah, na kama atampa mtu mwanamke ampe kanzu (nguo ndefu) na mtandio kwa sababu huo ndio uchache wa vazi linalomtosheleza katika Swaalah.

3. Kumuacha huru mtumwa Muislamu.

4. Kufunga siku tatu mfululizo kama ataweza na asipoweza basi atazifunga mbali mbali.

Hafungi ila baada ya kushindwa kulisha au kuvisha au kuacha mtumwa huru kwa mujibu wa Aayah iliyopo hapo juu.

 

 

Tumeonelea tutaje vipengele kadhaa kuhusu yamini ili iwe ni faida kwa wengi wengine ambao mambo haya huwatokea. Na jibu la muulizaji lipo katika kigawanyo cha awali kabisa.

 

 

Tunamuomba Allaah Atufaidishe sote na Atupatie hima ya Dini Yake.

 

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share