Skip navigation.
Home kabah

Mume Anaweza Kuoa Kwa Siri Mke Wa Pili

SWALI:

 

Assalam aleykum warahmatullahi wabarakatu…..........

Swali langu ni hili kwamba baba yangu aliowa mke wa pili ila kisiri hakutuambia sisi wanae wala mama yetu ila aliwaambia ndugu zake tumekuja kujuwa baada ya kama mwaka hivi sasa swali langu linauliza ya kwamba je mume anafaa kidini kuoa kisiri bila ya kumwambia mke wake na kama haifai nini hukumu ya mwanaume anaeoa kisiri?


 

JIBU

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu ndoa ya siri.

Hakika ni kuwa hili suala limekithiri kuulizwa katika tovuti hii ya alhidaya na pia katika darsa na mawaidha tofauti.

 

Ifahamike kuwa kidini mume halazimiki kumwambia mkewe wa kwanza, watoto wake na wengineo anapotaka kuoa mke wa pili au watatu. Ndoa kama ‘Ibaadah nyingine ina masharti yake lau yatatimia basi ndoa inakuwa ni sawa na mke wa pili halali ya mume huyo. Hata hivyo, ni katika utu na ubinaadamu kwa mume kumueleza mkewe wa awali kuhusu hilo.

 

Pia tufahamu kuwa katika Uislamu hakuna ndoa ya siri kwa maana ya mume na mke kuchukuana na kukaa pamoja. Ama ikiwa siri hii ni ya kumficha mke wa awali na hali masharti ya ndoa yamekamilika basi haitosababisha ndoa ile kuwa haraam. Lakini tujue pia kutangaza ndoa ni Sunnah na Mtume wetu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kasisitizia kwenye Hadiyth. Lau katika ndoa kutapatikana masharti yafuatayo basi ndoa hiyo ni sawa kabisa kidini:

 

  1. Kuridhia mume kumuoa mwanamke huyo.
  2. Kukubali kwa mwanamke kuolewa na mume huyo.
  3. Kuwepo na walii wa mwanamke kama baba yake, babu yake kuumeni, kakake na mfano wao.
  4. Kuwepo na mashahidi wawili waadilifu.
  5. Na mume kulipa mahari waliyoafikiana.

 

Kukipatikana hayo ndoa hiyo inakuwa ni halali katika Uislam.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Assalaamu alaykum

Assalaamu alaykum warahmatullahi wabarakatuh

Mie naona huyo mume kwa kufanya hivyo kwa namna moja ama nyingine anaweza akajikuta anaingia katika madhambi mengine kutokana na namna yake hii ya kuongeza mke wa pili ukiachilia mbali utu na ubinadamu.Jambo la mke wa pili linahitaji makubaliano katika maisha.Je huyu mume alikuwa anazigawa vipi siku kwa wake zake wawili katika huu muda wa mwaka mmoja? alikuwa anaaga vipi nyumbani anapoenda kulala kwa mkewe wa pili? au alikuwa haagi? au alikuwa akiongopa? Mie sidhani kama ni uisilamu tabia hizi, kwani hatujifunzi popote katika uisilamu kunapotufundisha kuliendea jambo hili katika namna hii.
Jambo la msingi sio kuswihi kwa ndoa peke yake. Bali pia ni athari yake katika jamii.Na nini maana yake.
Laweza maanisha kuwa mume anamuogopa mkewe katika kuliendea jambo hili na sidhani kama Allah anaridhia hili.
Ushauri: Wanaume wawe na ujasiri wa kuwaambia wake zao wanapoongeza mke ili kuepukana na madhambi mengine yanayoweza kuwafikisha mahala pabaya kesho akhera hasa la uongo kwani twajifunza ya kuwa muumini hawezi kuwa muongo kutokana na hadithi ya Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).Kama tunamfuata Mtume katika jambo hili basi na tufuate pia namna alivyoongeza wakeze na namna alivyoishi na wake zake.Twatakiwa kuingia katika uisilamu wote wote na si katika kuongeza tu mradi masharti ya ndoa yametimia na tukashindwa kumfuata Mtume namna alivyoishi na wakeze.
Allah anajua zaidi

Maasalaam!

Wa 'alaykumus-salaam wa

Wa 'alaykumus-salaam wa RahmatuLLaahi wa Barakaatuh.

Inavyoeleeka kwamba hukufahamu vizuri jibu la swali, kwani hakuna mahala palipojibiwa kwamba mume aseme uongo. Pia inaonyesha kama kwamba hukubaliani na amri hii ya ukewenza. Hivyo basi tafadhali soma makala ifuatayo upate kufahamu vizuri na Inshaa-Allaah ukinaike na amri hii.

Hikma Ya Ruhusa Ya Ukewenza

Ndugu Zako

AL HIDAAYA

 

Assalaamu alaykum

Assalaamu alaykum warahmatullahi taala wabarakatuh
Shukrani kwa kuendelea kuelimisha umma (Jazzakallahu khaira)
Haifai kwa muisilamu kupinga amri au ruhusa iliyotolewa na Allah aliyetukuka kwa mfano hili la kuoa mke zaidi ya mmoja.Maoni yangu si kupinga hili (Allah aliyetukuka aniepushe na hili na mengineyo mabaya).Yalikuwa ni vipi mume aweza kuishi na wake wawili au zaidi na akafanikiwa kufanya uadilifu ikiwa wa kwanza hana habari na vipi alifanikiwa kugawa siku kati ya wakeze ikiwa wa kwanza hana taarifa katika muda huu wa mwaka mmoja?
Suala linabakia palepale: alikuwa anaondoka vipi nyumbani kwa mkewe wa kwanza wakati anaenda kwa mkewe wa pili? alikuwa halali kwa mkewe wa pili usiku anaenda mchana? usiku alikuwa anamuambia vipi mkewe wa kwanza? hata ikiwa ni mchana alikuwa anasema vipi nyumbani, anatoka kidogo? au alikuwa haagi? (ndiyo maana tukasema hali hii yaweza sababisha uongo japo yawezekana mume huyu hajawahi kusema uongo katika hili kwa muda wa mwaka mmoja)
Ushauri: Wanaume waongeze wake lakini wawe na ujasiri wa kuwapa taarifa wake zao waliotangulia ili waweze kuwa waadilifu katika ndoa zao kwani kuongeza mke ni haki yao.Kumbe wanaogopa nini hadi wakafanya siri? wanawaogopa wake zao katika kutekeleza amri/ruhusa ya Allah aliyetukuka? Kwa maoni yangu, Katika usiri huu haki baina ya wake, na uadilifu wa mume utakuwa ni mtihani kwa kweli!
Allah aliyetukuka anajua zaidi

Wa 'alaykumus-salam wa

Wa 'alaykumus-salam wa RahmatuLLaahi wa Barakaatuh.

Swali limejibiwa kutokana na nukta za muulizaji nazo ni; Kuoa siri na kuoa bila kumjulisha mke wa kwanza. Na ndivyo lilivyojibiwa kuwa; kuoa siri haifai lazima masharti yake yapatikane. Ama kutokumjulisha mke wa kwanza sio lazima mume kufanya hivyo. Kwa hiyo hayo maelezo mengine tunaona kuwa hapa sio mahala pake kwani muulizaji hakulalamika hayo. Huenda nukta hii imeshaulizwa kwengine na imejibiwa kihaki kama ulivyogusia kuhusu kutekeleza haki za kila mke.

Tutambue kwamba maswali yanajibiwa kutokana na jambo liloulizwa, hivyo haiwezekani kuweka maelezo yasiyohusu mahali pake.

Tunatumai kuwa utaelewa.

Ndugu Zako
AL HIDAAYA

Assalaamu alaykum

Assalaamu alaykum warahmatullahi wabarakatuh
Ndugu zangu alhidaaya, hayo ni maoni yangu tu binafsi yaweza kuwa sio sahihi na ni maswali ninayojiuliza.Hata hivyo poleni kwa usumbufu.
Ndugu yenu katika uisilamu
Tausi