Hilaal: Kumfuata Mume Kwa Msimamo Wa Mwezi Wa Kitaifa
Hilaal (Mwandamo Wa Mwezi)
Je Inafaa Kumfuata Mume Kwa Msimamo Wa Mwezi Wa Kitaifa
Japokuwa Alikuwa Akifuata Unapoonekana Popote Duniani?
SWALI:
Suali langu ni juu ya mwanamke aliolewa na mwanamme ambaye akifuata msimamo mmoja wa mwezi unapoonekana popote duniani hufunga. Baada ya mume wake kufariki, baadae aliolewa na mwanamme ambaye msimamo wake ulikua ni tofauti. Hufuata mwezi unaonekana katika nchi yake au unapotangaziwa na mufti au kadhi wa nchi bila kuzingatia nchi nyengine ulionekanwa siku iliyopita. Mume huyu wa pili amesoma sana dini. Sasa mwanamke ameambiwa na mume wake huyu wa pili abadilishe msimamo wake. Na amempatia ushahidi ambao unatumiliwa sana na wenye msimamo huo. Jee mwanamke huyu amtii mume wake katika jambo hili? Ingawa alizoea huko nyuma kufuata mwezi mmoja tu (unapoonekana popote)? Shukran
JIBU:
AlhamduliLLaah Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Rabb wa walimwengu, Swalaah na Salaam zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.
Ifahamike kuwa rai zote mbili za kufuatwa mwezi wa kitaifa na mwandamo wa kimataifa zinapatikana katika vitabu vya Fiqhi na Shariy'ah. Mbali na hayo ni kuwa dalili na hoja za kufuata mwandamo wa kimataifa una nguvu zaidi.
Mbali na tofauti hizo kusiwe na mzozano au migongano katika nyumba ambayo wanandoa wanatakiwa wawe ni wenye kuwa na mapenzi na huruma baina yao. Na pia itakuwa haileti kabisa katika nyumba moja kuwe na kuanzwa kufungwa siku mbali mbali na kuidi (kusherekea 'Iyd) siku tofauti. Hili ni jambo ambalo halitakiwi katika Uislamu wetu. Kwa hivyo, suluhisho la hilo ni nini? Nasaha zetu kuhusu hilo ni kama ifuatavyo:
1. Mke ajaribu kwa njia nzuri kumuelewesha na kumuelimisha mumewe kuhusu muono wa kimataifa. Na ikiwa ni msomi kweli na si mtu wa kufuata kimbumbumbu basi huenda akabadilika. Anaweza kumpatia makala na vitabu vilivyoandikwa kumfahamisha kuhusu rai hii kwani wengi wanaielewa kimakosa na wanafuata kwa kuwa tu babu zetu walikuwa na msimamo huo.
2. Ikiwa haikuleta natija yoyote ajaribu kumtumia watu ambao ni wasomi wenye msimamo wa mwandamo wa kimataifa ili waweze kumueleimisha kuhusu hilo.
3. Ikiwa bado ameshikilia msimamo wake huo itabidi amfuate mume kwani utiifu ni katika maarufu na mume ana haki ya kutiiwa na mkewe maadamu hajamuamrisha katika maasiya. Na katika kufuata huko hakuna madhambi yoyote. Na hili si suala la watu kuhasimiana na hata kuharibu ndoa zao.
4. Mke amfuate mumewe katika hilo lakini asichoke aendelee na juhudi yake katika kumuelimisha katika hilo na mengine ya msingi kwenye Dini.
Huenda hili likawa ni funzo kwa wenye kuoa au kuolewa kulitizama kabla ya ndoa ili migogoro kama hiyo isiwe ni yenye kutokea kwa wanandoa. Mara nyingi watu hutoka katika misimamo yao iliyo sahihi kwa sababu ya kuolewa na wasiokuwa na misimamo au wenye misimamo tofauti kabisa.
Twakuombea kila la kheri dada yetu na Allaah Akusahilishie hayo yanayokukabili.
Na Allaah Anajua zaidi