Mtu Anapokuwa Karibu Na Kufariki Huwa Anaona Dalili Kabla Ya Siku 40?

SWALI:

 

Assalam alaykum warahmatu llah wabarakat amma baada yak kumshukuru allah subhanahu wataala na kumtakia rehma mtume wetu Muhammad swalla llahu alaih wassalam tunawashkuru sana ndugu zetu wa alhidaya kwa kutufunza mengi inshaallah Mola atawapa kila la kheri dunian na akhera kuna mtu nilimsikia kuwa eti mtu akitaka kufa hujijua siku 40 kabla na dalili alonitolea kuwa hungara paji lake la uso jasho lake la mwili hubadilika  huona haya kumuangalia mtu na pia ndoto anazoota humfanyisha ajue kuwa anakaribia kufa je hii kweli maanake sina uhakika nataka nijue


 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

 

 

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu dalili za kufa kabla ya siku arobaini.

 

Hakika suala hili la siku arobaini halijathibiti katika chanzo chochote kile cha Sheria. Na mas-ala haya ya mtu kujua siku yake ya kufa ni miongoni mwa mambo matano ambayo hakuna ayajuaye, na hata Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa alihi wa sallam) hakuwa na elimu nayo. Anayataja Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala):

 

 إِنَّ اللَّهَ عِندَهُ عِلْمُ السَّاعَةِ وَيُنَزِّلُ الْغَيْثَ وَيَعْلَمُ مَا فِي الْأَرْحَامِ وَمَا تَدْرِي نَفْسٌ مَّاذَا تَكْسِبُ غَدًا وَمَا تَدْرِي نَفْسٌ بِأَيِّ أَرْضٍ تَمُوتُ إِنَّ اللَّهَ عَلِيمٌ خَبِيرٌ 

 

((Hakika kuijua Saa (ya Qiyaamah) kuko kwa Allaah. Na Yeye Ndiye Anayeiteremsha mvua. Na Anavijua viliomo ndani ya matumbo ya uzazi. Na haijui nafsi yoyote itachuma nini kesho. Wala nafsi yoyote haijui itafia nchi gani. Hakika Allaah Ndiye Mwenye kujua, Mwenye khabari)) [Luqmaan: 34]

 

Ama pale mtu mwema anapotolewa roho yake, Malaika humbashiria mambo mema lakini hakuna anayejua au kuyasikia isipokuwa yeye mwenyewe.  Dalili tunapata kutokana na kauli mojawapo ya Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala):

 

 إِنَّ الَّذِينَ قَالُوا رَبُّنَا اللَّهُ ثُمَّ اسْتَقَامُوا تَتَنَزَّلُ عَلَيْهِمُ الْمَلَائِكَةُ أَلَّا تَخَافُوا وَلَا تَحْزَنُوا وَأَبْشِرُوا بِالْجَنَّةِ الَّتِي كُنتُمْ تُوعَدُونَ    نَحْنُ أَوْلِيَاؤُكُمْ فِي الْحَيَاةِ الدُّنْيَا وَفِي الْآخِرَةِ وَلَكُمْ فِيهَا مَا تَشْتَهِي أَنفُسُكُمْ وَلَكُمْ فِيهَا مَا تَدَّعُونَ)) (( نُزُلًا مِّنْ غَفُورٍ رَّحِيمٍ

 

((Hakika waliosema: Mola wetu ni Allaah! Kisha wakanyooka sawa, hao huwateremkia Malaika wakawaambia: Msiogope, wala msihuzunike; nanyi furahini kwa Pepo mliyokuwa mkiahidiwa)) ((Sisi ni vipenzi vyenu katika maisha ya dunia na katika Akhera, na humo mtapata kinachotamaniwa na nafsi zenu, na humo mtapata mtakavyovitaka)) ((Ni takrima itokayo kwa Mwenye kusamehe, Mwenye kurehemu)) [Fusw-swilat: 30-32]

Baadhi ya makundi kama Masufi wao huamini kuwa mtu mwema ambaye ana makarama anaweza kujua siku yake anayoaga dunia. Hii ni ‘Aqiydah potofu na isiyopasa kabisa kuaminiwa, na ni sawa na ‘Aqiydah potofu ya Mashia ya kuamini kuwa Maimaam wao wanajua watakufa lini na kifo watakachokufa!

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share