Kufukiza Ubani Na Mwanamke Kukaa Arubaini Anapojifungua Inafaa?

 

SWALI:

 

Nimesoma kuwa kuchoma ubani ni mila ya makafiri walioingia ktk uislam lakini ktk usilamu hakuna arobaini ila kwa mama aliyejifungua tu hebu nipe ufafanuzi.


 

JIBU

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola  wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu arobaini. Hakika ni kuwa sisi Waislamu tumepata neema ya kuwa Dini hii yetu imekamilishwa na Yeye Mwenyewe Muumba wetu, Allaah Aliyetukuka, kama Alivyosema:

 

Leo Nimekukamiliishieni Dini yenu, na Nimekutimizieni neema Yangu, na Nimekupendeleeni UISLAMU uwe ndiyo Dini” (5: 3).

Kwa ajili hakuna nyongeza juu ya yale aliyokuja nayo Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) wala kupunguzwa. Kinachoongezwa au kupunguzwa ni kile kilichokuwa na kasoro ndani yake sio kilichokamilika.

Hakuna mafunzo ya dini kuhusu kufukiza ubani, na kwa maelezo zaidi ingia katika kiungo kifuatacho upate maelezo zaidi:

Kufukiza Ubani Wakati Wa Kuomba Duaa Inafaa?

Ama tukija katika arobaini, ni kuwa arobaini kwa mwanamke aliyezaa ni ada na sio Dini. Hiyo ni kwa sababu wamechukulia kauli ya kuwa damu ya nifasi baada ya mwanamke kuzaa mwisho ni lazima iwe siku arobaini. Lakini hakika ni kuwa damu hiyo inaweza kukatika na kwisha hata kwa masaa machache na baada ya hapo asione tena damu na mara nyingine inaweza ikamchukua yeye akiwa katika damu hiyo ya uzazi siku arobaini au zaidi ya hapo au chini ya hapo.

Akiona hivyo, kuwa damu yake imesimama, ikiwa ima ni baada ya masaa au siku chache mwanamke mzazi ni lazima ajitwahirishe na baada ya hapo afanye Ibaadah zake zote kama kufunga na kuswali.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share