Je, Ninaweza Kuanza Kusoma Surah Katikati Ninaposwalisha?

SWALI:

S.aleykum,

Nina swali,wakati mtu anaswalisha yuaweza kuanza kusoma sura popote anapotaka (yaani si lazima aanze mwanzo wa sura).Swali langu ni hili je kuna masharti yoyote ama mtu aweza kusoma atakavyo? Shukran

 


JIBU:

 

AlhamduliLlaah - Himdi Na Sifa Zote Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Mola wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Anaweza mtu kuanza kusoma popote katika Surah, ikiwa anaswalisha au anaswali mwenyewe, kwani kawaida katika Surah moja ya Qur-aan huwa ina maelezo mbali mbali, kwa hiyo hakuna kipingamizi kufanya hivyo.

Kuhusu sharti za kusoma katika Swalah, ni vizuri kufuata adabu za Swalah kama alivyokuwa akifanya Mtume صلى الله عليه وآله وسلم  

1. Kisomo cha Surah kinaweza kuwa kirefu mara nyingine na mara nyingine kifupi kutokana na hali ya mtu kama yuko katika safari, au anaumwa au kama mtoto analia.

2. Kisomo kinakuwa tofauti kutokana na hali ya Swalah.

3. Kisomo cha Swalah ya Alfajiri ni kirefu kuliko Swalah zote. Kisha kinafuatia kisomo cha Swalah ya Adhuhuri, kisha Alasiri, kisha 'Ishaa na mwisho ni Magharibi.

4.  Kisomo cha Swalah ya usiku (Tahajjud) ni kirefu zaidi kuliko Swalah zote hizo.

5. Ni Sunnah kufanya kisomo cha Raka'ah ya mwanzo kirefu kuliko Raka'ah ya pili.

6. Suratul-Faatiha ni fardhi katika kila Raka'ah.

7. Imaam haruhisiwi kusoma kisomo kirefu sana zaidi ya kilivyoelezwa katika Sunnah, kwa sababu kutowatia mashakani wanaoswali nyuma yake kama watu wazima, wagonjwa, na walio dhaifu.

Kisomo cha sauti na cha kimya:

1. Qur-aan isomwe kwa sauti katika Swalah ya Alfajiri, Swalah ya Ijumaa, Swalah za 'Iyd, ya mvua, ya kupatwa jua na katika Raka'ah mbili za mwanzo kwenye Swalah ya Magharibi na 'Ishaa.

2. Ni Sunnah kusoma Qur-aan kwa tartiyl, yaani kusoma inavyopaswa kusomwa kwa kufuata sheria zake za Tajwiyd, na kwa kuipendezesha sauti.

Na Allaah Anajua zaidi.

 

 

 

Share