Istiqaamah (Kuthibitika Katika Dini)

Istiqaamah (Kuthibitika Katika Dini)

 

Kutoka Katika Kitabu ‘Riyaadhus Swaalihiyn

Imekusanywa na ‘Abdallaah Mu’aawiyah

 

Alhidaaya.com

 

 

Istiqaamah: (Kulingamana Sawa, Kuthibitika Katika Dini)

 

 

"Istiqaamah" ni mtu kuthibiti juu ya Shariy’ah ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)    kama Alivyoamrisha Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)    na kumtakasia niyyah Allaah kama Anavosema:

 

فاستقم كما أمرت

Basi simama sawasawa kama ulivyoamrishwa [Huwd: 112]

 

Anayesemeshwa hapa ni Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Na kauli inayoelekezwa kwa Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)  hukusudiwa yeye na umma wake isipokuwa kama kutakuwepo dalili inayoonyesha kuwa kauli hiyo inamhusu yeye tu. Na kama hakuna dalili, basi kauli hiyo itakuwa ni yake na ya umma wake.

 

Kila mmoja ni lazima asimame sawa kama alivyoamriwa. Asibadili chochote katika Dini ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)   na wala asizidishe kitu wala asipunguze. Na kwa ajili hiyo, Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)    Anasema katika Aayah nyingine:

 

واستقم كما أمرت ولا تتبع أهواءهم

Na simama sawasawa na wala usifuate matamanio yao. [Huwd: 112]

 

Na Anasema pia Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

إِنَّ الَّذِينَ قَالُوا رَبُّنَا اللَّـهُ ثُمَّ اسْتَقَامُوا تَتَنَزَّلُ عَلَيْهِمُ الْمَلَائِكَةُ أَلَّا تَخَافُوا وَلَا تَحْزَنُوا وَأَبْشِرُوا بِالْجَنَّةِ الَّتِي كُنتُمْ تُوعَدُونَ﴿٣٠﴾

Hakika wale waliosema: Rabb wetu ni Allaah. Kisha wakathibitika imara; Malaika huwateremkia: (kuwaambia): Msikhofu, na wala msihuzunike, na pokeeni bishara njema ya Jannah ambayo mlikuwa mkiahidiwa.

 

نَحْنُ أَوْلِيَاؤُكُمْ فِي الْحَيَاةِ الدُّنْيَا وَفِي الْآخِرَةِ ۖ وَلَكُمْ فِيهَا مَا تَشْتَهِي أَنفُسُكُمْ وَلَكُمْ فِيهَا مَا تَدَّعُونَ﴿٣١﴾

Sisi ni rafiki zenu walinzi katika uhai wa dunia na katika Aakhirah. Na mtapata humo yale yanayotamani nafsi zenu, na mtapata humo yale mtakayoomba.

 

نُزُلًا مِّنْ غَفُورٍ رَّحِيمٍ﴿٣٢﴾

Ni mapokezi ya takrima kutoka kwa Mwenye kughufuria, Mwenye kurehemu. [Fusswilat: 30-32]

 

 

Sharh:

 

 ربنا الله

Rabb wetu:

 

Kwa maana:  Muumbaji wetu, Mmiliki wetu na Mwendeshaji mambo yetu. Nasi tunamtakasia.

  ثم استقاموا  

Kisha wakathibitika imara;

 

Juu ya hilo, yaani neno lao: Rabb wetu ni Allaah na wakaitekeleza Shariy’ah Yake.

Hawa waliosifika kwa sifa hizi mbili:

 

 تتنزل عليهم الملائكة

Malaika huwateremkia: (kuwaambia):

 

 

Malaika baada ya Malaika

 

 ألا تخافوا ولا تحزنوا

Msikhofu, na wala msihuzunike,

 

Yaani Malaika wanawateremkia kwa amri ya Allaah ('Azza wa Jalla)  katika kila sehemu inayoogopesha na hususan wakati wa kufa wakiwaambia:

 

 ألا تخافوا ولا تحزنوا

Msikhofu, na wala msihuzunike,

 

Msikhofu katika mambo yenu mnayoyaelekea, wala msihuzunike kwa mambo yenu yaliwowapita.

  وأبشروا بالجنة التي كنتم توعدون  

na pokeeni bishara njema ya Jannah ambayo mlikuwa mkiahidiwa.

 

Bishara ni kuelezea jambo lenye kufurahisha. Na hakuna shaka kuwa mwana Aadam kunamfurahisha yeye kuwa ni katika watu wa Jannah. Na kila mwenye kusema: "Rabb wangu ni Allaah kisha akathibitika  juu ya Dini ya Allaah, basi huyo ni katika watu wa Jannah.

 نحن أولياءكم في الحياة الدنيا والأخرة

 

Sisi ni rafiki zenu walinzi katika uhai wa dunia na katika Aakhirah.

 

Malaika ndio walinzi wa wale waliosema: "Rabb wetu ni Allaah", kisha wakathibitika sawa katika maisha ya duniani; huwaweka sawa, huwaongoza ya haki na huwasaidia. Pia vile vile huko Aakhirah, Malaika watawapokea siku ya kufufuliwa na kuhesabiwa wawaambie:

 

 هذا يومكم الذي كنتم توعدون

Hii ni siku yenu ambayo mliahidiwa [Al-Anbiyaa: 103]

 

ولكم فيها ما تشتهي أنفسكم ولكم فيها ما تدعون

Na mtapata humo yale yanayotamani nafsi zenu, na mtapata humo yale mtakayoomba.

 

  لكم فيها  

 

Humo mtapata

 

Yaani Aakhirah

  ما تشتهي أنفسكم  

 

yale yanayotamani nafsi zenu

 

Na hii ni katika neema za Jannah, kwa vile huko Jannah kuna vile ambavyo nafsi inavitamani na macho kuburudika.

  ولكم فيها ما تدعون  

 na mtapata humo yale mtakayoomba.

 

Yaani mnavyovitaka, bali watapata zaidi ya hivyo

 

 لهم ما يشاءون فيها ولدينا مزيد

Watapata humo wayatakayo, na Kwetu kuna ziada (kumuona Allaah عز وجل). [Qaaf: 35]

 

Yaani watapata zaidi ya wanavyovitaka na kuvitamani.

 

 نزلا من غفور رحيم

Ni mapokezi ya takrima kutoka kwa Mwenye kughufuria, Mwenye kurehemu

 

Yaani huko Jannah ndio mashukio yao na makaribisho toka kwa Mwingi wa kughufiria na Mwingi wa kurehemu.

 

Haya ndiyo malipo ya wale waliosema:

 

  رَبُّنَا اللَّـهُ ثُمَّ اسْتَقَامُوا 

"Rabb wetu ni Allaah kisha wakathibitika imara”

 

Na katika haya, kuna dalili juu ya umuhimu wa kuthibitika juu ya Dini ya Allaah ('Azza wa Jalla)  kwa kushikamana mtu vyema, hazidishi wala hapunguzi wala habadilishi wala hageuzi.

 

Ama yule anayevuka mipaka au akajiweka mbali na Dini ya Allaah, au akabadili, basi huyo si mwenye kuthibitika juu ya Shariy’ah ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa). Na kuthibitika ni lazima kuwe na uwastani katika kila kitu ili mtu awe ni mwenye kuthibitika.

 

Na katika Hadiyth Imepokelewa toka kwa Abu 'Amri na inasemekana kuwa ni Abu 'Amrah Sufyaan bin ‘Abdillaah Allaah (Radhwiya-Allaahu 'anhu) akisema:

 

قلت: يا رسول الله قل لي فى الإسلام قولا لا أسأل عنه أحدا غيرك: قال: (( قل آمنت بالله ثم استقم))

"Nilisema: Ee Rasuli  wa  Allaah! Niambie mimi katika Uislamu kauli ambayo simuulizi mwengine yeyote zaidi yako wewe. Akasema: ((Sema: Nimemwamini Allaah, kisha thibitika)).

Imepokelewa na Muslim.

 

 

Sharh

 

- Neno lake:  Niambie mimi katika Uislamu kauli ambayo simuulizi mwingine yeyote zaidi yako;

 

Niambie mimi kauli ambayo simuulizi mwingine yeyote zaidi yako iwe ni kipambanuzi na ya mwisho isiyohitajia kumwuuliza tena yeyote. Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akamwambia:

"Sema: Nimemwamini Allaah, kisha thibitika".

 

- Neno lake:   Sema nimeamini;

 

Makusudio si tu kusema kwa ulimi, kwani kuna watu wanaosema: "Tumemwamini Allaah na siku ya mwisho nailhali wao si wenye kuamini". Lakini makusudio ya hilo ni kutamka kwa moyo na ulimi vile vile.

Na kwa ajili hii, Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akisema huku anawalingania watu kuingia Uislamu:

"Enyi watu! Semeni:

لا إله الاّ الله

Hapana  mwabudiwa wa haki ila Allaah mtafaulu".

 

- Neno lake: Nimemwamini Allaah

 

Inakusanya kuamini kuwepo kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)   Uola Wake, Majina Yake, Sifa Zake, Hukumu Zake, na yote yanayokuja kutoka Kwake. Ukiamini hivyo, basi thibitika sawa juu ya Dini ya Allaah wala usijiweke kando nayo; si kulia wala kushoto, usipunguze wala usiongeze.

 

Thibitika sawa juu ya shahada ya kuwa hapana Rabb wala ilaah isipokuwa  Allaah na kwamba Muhammad ni Rasuli wa Allaah, na hiyo ni kwa kumtakasia Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)  na kumfuata Rasuli Wake.

 

Thibitika sawa juu ya Swalaah na juu ya Zakaah, Swawm, Hijjah na juu ya Shariy’ah zote.

 

- Neno lake:  Nimemwamini Allaah kisha thibitika  

 

Ni dalili kwamba kuthibitika hakuwi ila baada ya kuamini na kwamba kati ya masharti ya kuswihi na kukubaliwa matendo mema, ni kuwa yawe yemejengewa juu ya iymaan.

 

Tunayojifunza kutokana na Hadiyth hii:

 

Ni kuwa, inatakikana kwa mtu anapofanya tendo lolote, ahisi kwamba amelifanya kwa ajili ya Allaah, na kwamba yeye analifanya kwa msaada wa Allaah, na kwamba yeye analifanya kwa kufuata Shariy’ah ya Allaah. Hii ni kwa vile, mtu huyu hathibitiki juu ya Dini ya Allaah ila baada ya kumwamini Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)   

 

 

 

Share