Zingatio: Nyumba Ya Aakhirah Umeshaijenga?

 

Zingatio: Nyumba Ya Aakhirah Umeshaijenga?

 

Naaswir Haamid

 

Alhidaaya.com

 

 

Miongoni mwa nguzo za iymaan ni kuamini kwamba kuna hesabu Siku ya Qiyaamah. Hesabu ambayo itamtambua kwamba ni mtu wa Jannah ama ni motoni. Rabb Atujaalie kuwa miongoni mwa watu wa Jannah, Aamiyn.

 

Lakini tunaitika du’aa kwani hiyo Jannah tutaingia kwa kula na kulala tu? Balaa – Sivyo hivyo! Mwanadamu anapokuja duniani huzaliwa akiwa hata nguo hanazo mwilini. Anapofika hapa ulimwenguni ndio hutafuta ama kutafutiwa vitu vya kumsaidia maisha hapa duniani. Na ndivyo ilivyo kwa Qiyaamah. Muislamu anatakiwa akumbuke kwamba hakuna atakayemjengea makaazi mema baada ya kufa isipokuwa nafsi yake mwenyewe.

 

Tusiwe ni wenye kupiga mbio usiku na mchana kuifikiria nyumba ya duniani tukikosa hamasa za kuijenga nyumba ya Akhera. Tena kwa bahati nzuri, nyumba ya Akhera ndio ya milele isiyobomoka katu. Sasa ni nani mwenye akili hapa? Yule aliyepata maskani akaridhika nayo akamuabudu Rabb wake, ama yule anayetaka kukusanya majumba kwa majumba yaliyo na ghorofa za aina wa aina? Bila ya shaka mwenye akili ni yule anayeelewa kwamba ipo siku atazikwa na ndani ya kaburi yataanza maisha yake ya kweli kweli.

 

Tupige hisabu ya maiti zetu tuliowazika, ni miaka mingapi washaishi ndani ya kaburi zao? Hawatarudi hapa duniani, na umri walioishi duniani ni mdogo kulinganisha na umri wanaoendelea kuutumikia chini ya ardhi. Bado Qiyaamah hakijasimama, ambapo siku zake Qiyaamah ndio za milele daima wa dawaam.

 

Ndugu Waislamu hiyo ndio siku ya kuiweka akilini katika harakati zetu. Siku ambayo nyoyo za walioghafilika na ulimwengu zitakuwa na majuto makubwa. Nyumba walioijenga huko itakuwa ni yenye kushtadi kwa adhabu za kila aina. Miili yao itakaangwa kwa moto kama vile maandazi ya mafuta. Qur-aan inatupasha habari za watu hao:

 

 وَقَالُوا رَبَّنَا إِنَّا أَطَعْنَا سَادَتَنَا وَكُبَرَاءَنَا فَأَضَلُّونَا السَّبِيلَا ﴿٦٧﴾

Na watasema: Rabb wetu! Hakika sisi tumewatii mabwana zetu, na wakuu wetu, basi wametupoteza njia. [Al-Ahzaab: 67]

 

Imaam an-Nawawiy (Rahimahu Allaahu) amenukuliwa akisema ubeti ufuatao kuhusu maisha ya dunia: 

Mapigo ya moto ya mtu yanamwambia:

"Hakika maisha ni dakika na sekunde."

Basi inyanyue nafsi yako baada ya mauti yako,

Kutajwa kwako ni kama kutajwa kwako mara ya pili.

 

Naam hiyo ndio hali, kama ulijenga majumba ya ghorofa duniani, hata pale utakapozikwa, utasifika kwamba umeipamba dunia kwa majumba ya kifakhari. Lakini yahasrataa (ni hasara iliyoje) kama hukuijenga nyumba ya Qiyaamah!

 

Rabb Atuoneshe haki tuiweze kuifuata na batili tuiweze kuiepuka. Atujaalie kuwa na makaazi mema hapa duniani na Aakhirah, Aamiyn.

 

 

Share