Zingatio: Haipasi Kusherehekea Maulidi

 

 Zingatio: Haipasi Kusherehekea Maulidi

 

Naaswir Haamid

 

 

Alhidaaya.com

 

 

Dini ya Kiislamu ni mwenendo ambao umekamilika usiotaka kuzidishwa mapambo ukawa mbaya wala kupunguzwa ukawa pungufu. Ni kufuata maamrisho ya Qur-aan na Sunnah ya Nabiy Habiybul-Mustwaafa (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).

 

 

Kuna mambo mengi sahihi ambayo Muislamu wa kweli anaweza kukithiri kuyafanya bila ya kuyamaliza hadi kufikia hatima ya maisha yake. Kwa mfano aweza kukithiri kwa funga za Sunnah, kisimamo cha usiku, kusema ukweli na mengineyo mengi tu.

 

 

Kwa wengine mambo hayo ni magumu na mazito kuyatenda. Ndipo hutafuta yale mepesi na kuyafanya ndio ibada zao. Na bila ya shaka binaadamu wote sio wavumbuzi, ni wachache wanaovumbua na wengine hufuata mkumbo tu. Mayahudi na vibaraka vyao wameupamba ulimwengu kwa michezo ya mpira, michezo ya sinema na muziki. Hapo wengi ndio wanaotumbukia. Kaanza Yahudi na watu wengine wakiwemo Waislamu wakafuatia.

 

 

Hatari mbaya zaidi ni pale tunapoyaingiza hayo mambo yao ya uzushi kwenye dini yetu tukitarajia kwamba tunapata thawabu ilihali tunaingia kwenye maangamizo zaidi. Manaswara wakaanza kuitukuza dai la siku ya kuzaliwa Yesu kwa ibada za kuvumbua na hatimaye leo tunawaona wakibadili ibada hizo kwa matendo ya uzinzi, pombe, kamari na israfu.

 

 

Nao Waislamu wametumbukia hapo hapo, kwa kuvumbua ibada ya Maulidi wakidai kuitukuza siku inayodaiwa kazaliwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Hakuna shaka yoyote kwamba Maulidi ni mwigo wa Manaswara na tusipokuwa makini, vizazi vyetu vitakuja kusherehekea siku hiyo kwa uzinifu, pombe, kamari na israfu.

 

 

Akili inakuwa haielewi pale mtu mwenyewe anaposhindwa kusherehekea siku yake ya kuzaliwa, vikaja vizazi vya karne za baadaye wakaanza kuisherehekea siku yake. Ni ajabu kweli kweli. Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akifunga siku ya Jumatatu ambayo alizaliwa yeye. Kama aliielewa siku ya kuzaliwa (ambayo ni Jumatatu) kwanini ashindwe kuifahamu tarehe yake akaanza kuitukuza kwa kuwakusanya Swahaba wakaanza kusoma hayo Maulidi?

 

 

Na vipi wasilione hilo kina Abu Bakr, ‘Umar, ‘Uthmaan na ‘Aliy na Swahaba wengine (Radhwiya Allaahu ‘anhum) ambao hakuna anayewashinda kwa mapenzi yao waliyokuwa nayo kwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)? Je, sisi tuna mapenzi ya Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kuwashinda watukufu hao? Basi kwanini wao wasimsherehekee mazazi yake? Hatujiulizi hilo? Hatuna akili ya kupambanua na kufikiri?

 

 

Haya ni mambo yanayohitaji Muislamu kupambanua bila ya kupata taabu yoyote. Tuangalie namna hayo Maulidi yanavyofanywa katika maeneo yetu ya makaazi. Huanza kusherehekewa baada ya Swalatul-Ishaa hadi Alfajiri siku ya pili. Mtindo huu unafanana kabisa na mkesha wa Krismasi unaofanywa kanisani hadi siku hiyo ya Krismasi. Na kwani Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alizaliwa usiku?!

 

 

Jengine ni kwamba hapo panapofanywa hiyo sherehe kitaifa, ni sehemu ya ukanda wa bahari. Kuna mkusanyiko wa wanawake na wanaume. Kwenye gubi gubi la usiku, ni jambo gani litakalowazuia wasizigeuze fukwe za bahari kuwa ni vitanda vya sita kwa sita?

 

 

Mara kadhaa Maulidi yamekuwa yakifanyika ndani ya kumbi za pombe au tamasha za muziki. Huenda ikawa sio kwa kuadhimisha kuzaliwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), lakini Maulidi ya kusherehekea harusi, matamasha ya muziki au siku za kuzaliwa baadhi ya Waislamu huwa zinaadhimishwa ndani ya kumbi hizi. Ibada ya kweli kweli haitakubali kushirikishwa ndani ya kumbi hizi.

 

 

Hayo ndio Maulidi ambayo wengi wao wanaamini kuwa ni ibada. Na kuna hoja nyingi zenye ushahidi wa Qur-aan na Sunnah zilizokusanywa ndani ya alhidaaya zitakazomtosheleza Muislamu kutosherehekea siku hiyo.

 

 

Tunamuomba Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Atuhidi kwa kutuonesha yaliyo haki ili tuyafuate na Atuoneshe yaliyo baatil tujiepushe nayo. Aamiyn.

 

 

Share