Kutumia Tasbiyh Kwa Khofu Ya Kupotewa Hesabu Inajuzu?

SWALI:

 

Assalam alaykum, nimesoma majibu yanayohusiana na matumizi ya tasbihi, ila mimi nina tatizo moja kwamba nikifanya nyiradi wingi kwa kutumia vidole huwa ninakosa umakini kuliko kwa kutumia tasbihi, sasa sijiu nifanyaje?

 


 

 

 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu kutumia tasbiyh kwa hofu ya kupoteza hesabu.

Hofu aina hiyo katika ‘Ibaadah inatokana na kutiwa wasiwasi na Shaytwaan na mazoea. Tufahamu kuwa kuleta dhikri au adhkaar ni katika ‘Ibaadah, kwani Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

Ulimi wako uwe majimaji kwa kumtaja Allaah”.

 

Na Allaah Aliyetukuka Amesema:

 

 

Na wanaume wanaomtaja Allaah kwa wingi na wanawake wanaomtaja Allaah kwa wingi...” (33: 35).

 

Ikiwa amri hiyo ni hivyo inabidi ufuate hivyo, kwani Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa anatumia vidole vya mkono wa kulia katika kuleta adhkaar. Na hivyo inatakiwa nasi tuige kwani Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ameletwa kwetu sisi tumuige kwa yote. Mambo mengi ni mazoea na wala usiwe na hofu kabisa kuhusu hayo ya kuleta tasbihi kidogo kuliko ulivyotaka au zaidi. Bila shaka yoyote utamshinda Shaytwaan, utaondosha wasiwasi na utazoea njia hii ya ki-Sunnah.

 

Kwa maelezo kwa kirefu soma jibu lingine kuhusu kutumia Tasbiyh:

 

Kutumia Tasbihi Katika Kumdhukuru Allaah Inafaa?

 

Tunakutakia kila la kheri.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share