Kuhusu Zabuwr, Tawraat, Injiyl Na Qur-aan

 

Kuhusu Zabuwr, Tawraat, Injiyl Na Qur-aan

Alhidaaya.com

 

 

 

SWALI:

 

Assalam Aleikum,

 

1- Kitabu cha mwisho kushuka ni Qur´ani cha kwanza kilikuwa Biblia au vipi?

 

2- Nifahamisheni maana ya Taurati, Injili na Zaburi na kazi zake?

 

3- Nini maana ya Agano la kale na Agano Jipya?

 

 

 

 

JIBU:

 

AlhamduliLLaah Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na Salaam zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

 

Tufahamu kuwa Biblia si kitabu kitakatifu kama wanavyofahamu wengi miongoni mwa Waislamu wa kawaida. Biblia imetokana na neno Biblos, ambalo ni neno la Kigirki lemye maana ya mkusanyiko wa Vitabu. Katika Biblia utapata maneno ya Allaah Aliyetukuka yaliyobaki katika usahihi wake, kauli za Rusuli (‘Alayhim-Salaam) na maneno ya watu wasiojulikana. Na yapo maneno mengi yaliyozuliwa ambayo hayawezi kuwa maneno ya Allaah wala Mitume.

 

Kitabu cha kwanza kuteremshwa ni kile alichopewa Nabii Ibraahiym (‘Alayhis Salaam). Allaah Aliyetukuka Anasema:

صُحُفِ إِبْرَاهِيمَ وَمُوسَىٰ ﴿١٩﴾

Maandiko tukufu ya Ibraahiym na Muwsaa. [Al-A'laa: 19]

 

Tawraat ni kitabu alichoteremshiwa Nabiy Muwsaa (‘Alayhis-salaam) kilichokuwa na amri kumi. Ama Injiyl ni habari njema, nacho ni kitabu alichoteremshiwa na Allaah Aliyetukuka Nabiy ‘Iysa (‘Alayhis-salaam) ama maana ya Zabuwr ni nyimbo na maombi. Hicho ni kitabu alichoteremshiwa Nabii Daawuud (‘Alayhis-salaam). Kazi za vitabu vyote ambavyo kwa sasa vimepotea katika mfumo wake wa kiasili ni kuwaongoza Bani Israili katika kumjua na kufuata maamrisho ya Allaah Aliyetukuka pamoja na kuwa na maadili mema hapa duniani ili kupata ufanisi Kesho Aakhirah.

 

Ama maana ya Agano la kale kwa Wakristo ina maana vile vitabu vya kale kabla ya kuja kwa ‘Iysa mwana wa Maryam katika Biblia. Vitabu vyenyewe vinaanza kitabu cha Mwanzo hadi Malaki. Ilhali Agano Jipya ni vitabu vinavyosimulia kuhusu Yesu pamoja na barua ambazo wafuasi Wakristo waliokuwa wakiandikiana. Hivi ni vitabu ambavyo vipo katika Biblia inayofuatwa na Wakristo, hata hivyo Mayahudi hawaiamini Agano hiyo mpya. Vitabu vyenyewe vinaanza kuanzia Injili kama ilivyoandikwa na Mathayo hadi Ufunuo.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

 

Share