Siku Ya Wajinga (April Fool) Na Hukumu Yake Kishari'ah

 

Siku Ya Wajinga (April Fool) Na Hukumu Yake Kishari'ah

 

Abuu 'Abdillaah

 

BismiLlaah Rahmaani Rahiim

 

Alhidaaya.com

 

 

BismiLLaah walhamduliLLaah Rabbil 'Aalamiyn. Wasw-Swalaatu was-Salaamu ‘alaa Nabbiyihi Asw-Swaadiq Al-Amiyn, wa ‘alaa aalihi wa Swahaabatihi Al-Ghurr Al-Mayaamiyn, wa man Tabi'ahum bi Ihsaani ilaa Yawmid Diyn.

Amma ba’d:

 

 

Asili Ya April Fool 

 

Asili ya April Fool haikujulikana kwa uhakika na kuna rai mbali mbali zinazohusiana nayo.

 

Wengine wamesema imeanza kutokana na sherehe za majira ya kuchipua (Spring) katika ikwinoksi (siku ya mlingano) tarehe 21 Machi.

 

Wengine wamesema kuwa huu ni uzushi uliochomoza France mwaka 1564 M, baada ya utangulizi wa kalenda mpya. Wakati mtu alipogoma kukubali kalenda mpya akaishia kuwa ni mwathirika wa baadhi ya watu ambao wamemsababisha aathirike kufedheheka na wakamfanyia istihzai na kumtania, akawa ni kichekesho kwa watu.

 

Wengine wanasema kuwa uzushi huu umeanza asili yake katika nyakati za kale na sherehe za mapagani zilikuwa na uhusiano na siku hasa mwanzo wa majira ya kuchipua. Kwa hiyo hii ni kasumba ya ibada za mapagani. Inasemekana kuwa nchi nyingine, kuwinda hakukufaulu siku za mwanzo za uwindaji.

 

 

Le poisson d'avril (Samaki wa Aprili)

 

Wazungu wameiita April Fool kwa jina la 'le poisson d'avril' (Samaki wa Aprili). Na sababu hii ni kutokana na jua linavyosogea kutoka nyumba ya zodiaki (nyota za unajimu) ya Pisces (Nyota ya samaki) ikielekea nyumba nyingine. Au kwa sababu ya neno la poisson ambalo maana yake ni samaki, hivyo ni ugeuzaji wa neno la 'passion' ambayo ina maana ya 'kuteseka'. Kwa hiyo ni alama ya kuteseka aliyovumulia Nabii 'Iysaa (Alayhis Salaam) kama walivyodai Wakristo. Na madai yao haya yalitokea wiki ya kwanza katika mwezi wa April.

 

Baadhi ya makafiri wameiita siku hii 'Siku nzima ya wajinga' kama inavyojulikana Kingereza. Hii ni kwa sababu uongo wanaousema ili wale wanaousikia waamini kwa hiyo wanakuwa ni waathirika wa wale wanaowafanyia dhihaka.

 

Utajo wa mwanzo kabisa kwa Lugha ya Kingereza ilikuwa ni katika gazeti la Dreck. Siku ya pili ya Aprili 1698 M, gazeti hili lilitaja kwamba idadi kadha ya watu walialikwa kuhudhuria uoshaji wa watu weusi katika mnara wa London asubuhi ya siku ya mwanzo ya Aprili.

 

Tukio maarufu kabisa lililotokea Ulaya tarehe 1 Aprili lilikuwa wakati gazeti la Kingereza 'Evening star' lilipotangaza mwezi wa Machi 1746 M kwamba siku ya pili tarehe 1 Aprili, kutakuwa na gwaride la punda mji wa Islington Uingereza. Watu wakakimbilia kuwatazama wanyama hao na kulikuwa na zahma kubwa. Wakaendelea kusubiri na walipochoka kusubiri, waliuliza kutaka kujua hili gwaride litakuweko baada ya muda gani. Hawakupata jibu, hivyo wakatambua kuwa wamekuja kufanya maonyesho yao wenyewe kama kwamba wao ndio mapunda.

 

Mmoja wao ameandika kuhusu asili ya uzushi huu kwa kusema: Wengi wetu tunasherehekea siku inayojulikana kuwa ni April Fool, au ikiwa itafasiriwa kihalisi 'Siku ya Ujanja'. Lakini je, tunajua siri chungu inayohusikana na siku hii?

 

Habari nyingine ambazo usahihi wake umetiliwa shaka na wanahistoria ni kuwa:

Waislamu walipotawala Hispania (Spain) takriban miaka elfu iliyopita, kulikuwa na nguvu kubwa ya utawala wa Kiislam ambayo haikuwezekana kuivunja. Wakristo wa Kimagharibi walitamani kuufuta Uislamu katika mgongo wa ardhi na walifaulu kwa kiwango fulani.

 

Walijaribu kuzuia Uislamu kusambaa Hispania na walitaka kuuzima na wautoweshe kabisa lakini hawakufaulu, ingawa walijaribu mara nyingi bila ya kufaulu.

 

Baada ya hapo, makafiri walituma majasusi Hispania kufanya utafiti ili kujua siri ya nguvu za Waislamu ambayo haikuwezekana kuishinda. Wakatambua kuwa kushikamana na Taqwa (Uchaji Allaah) ndio sababu.

 

Wakristo walipotambua siri ya nguvu za Waislamu, wakaanza kufikiria mikakati za kuvunja nguvu hiyo. Na kwa ajili hii wakaanza kupeleka ulevi na sigara bure huko Hispania.

 

Mbinu hizi kwa upande wa Magharibi zilifaulu kuleta taathira na imani za Waislamu zikaanza kulegea, hasa miongoni mwa vizazi vipya Hispania. Matokeo yake ni kwamba Wakristo Wakatholiki waliikandamiza Hispania nzima na wakauangamiza utawala wa Kiislamu katika ardhi hiyo, utawala ambao ulidumu zaidi ya miaka mia. Ngome ya mwisho ya Waislamu Grenada ilianguka tarehe 1 Aprili, hivyo wakaichukulia kuwa ni 'Siku ya Ujanja ya Aprili' au 'Siku ya Wajinga ya April'.  Ujanja kwa wale walioufanya, na Ujinga kwa wale waliofanyiwa na kutumbikia ndani yake.

 

Tokea mwaka huo hadi sasa, wanasherehekea siku hii na wanachukulia kuwa Waislamu ndio wajinga. Hawakuuhusisha ujinga huu na jeshi la Granada pekee kuwa ni wajinga, bali wamekusudia kuwa ni Umma wa Kiislamu mzima kuwa ni wajinga.

 

Hata hivyo, habari hizi tumezinukuu hapa kwa kuwa zimeenea sana miongoni wa Waislam, lakini kama tulivyotangulia kueleza, ni kuwa, uhakika na ukweli wake una mashaka kwa sababu kuna wanaosema kuwa wakati huo sigara na uvutaji tumbaku ulikuwa haujaanza hadi baada ya kushindwa Waislamu huko Hispania. 

 

Wahahistoria wanasema sababu za kushindwa Waislamu zilikuwa ni wenyewe kujiingiza zaidi kwenye mapenzi ya kidunia na starehe, pamoja na kuacha mafundisho sahihi ya Uislam na badala yake kuchanganya zaidi na falsafa ya Kigiriki na kutegemea zaidi fikra za kirumi katika kuendesha mambo yao badala ya mwongozo imara wa Kiislam. Kadhalika kuna Waislamu waliokuwa wakishirikiana na makafiri katika kupambana na makundi mengine ya Kiislam waliyokuwa hawaelewani nayo kama tunavyoona leo hii.

 

 

Baadhi Ya Udanganyifu Wanaodanganyana Watu Katika Siku Hii Ya April Fool

 

Wengine wanapewa habari ya mmoja wa kipenzi chake katika familia kama mtoto, mke au mume kwamba amefariki na kwa wengine taarifa hizo husababisha hata kifo chao kutokana na kutokustahamili kupata mshtuko huo. Wengine wanapewa habari ya kufukuzwa kazi, au kuwashtua kwa habari mbaya kama kuunguliwa moto nyumba yake, au familia yake kupata ajali, na husababisha aathirike mtu kwa mshtuko huo hadi apate maradhi ya moyo, au maradhi ya kupooza au hata kifo cha ghafla. 

 

Wengine wadanganywe kuwa wake zao wameonana na wanaume wengine, jambo ambalo husababisha mauaji au talaka ya wake. 

 

Kuna visa visivyokuwa na mwisho na matukio yanayotokea kutokana na uongo huu. Uongo ambao umeharamishwa katika Uislamu na ambao haukubaliwi katika tabia za kiungwana.

 

 

Hukumu Ya Uongo Katika Uislamu 

 

Uongo ni tabia ovu kabisa ambao dini zote na mfumo wa elimu za maadili zimeonya dhidi yake, na pia asili ya kimaumbile ya binaadamu (fitrah) inakubaliana kuwa ni uovu.

 

Ukweli ni moja wa nguzo ambayo maadili ya maisha ya kidunia yanategemea ili yahifadhike. Ni asasi ya tabia za kustahili kusifiwa, ni msingi wa Utume na matokeo ya Taqwa. Isingelikuwa ni ukweli, hukumu za shariy'ah za kufunuliwa kutoka mbinguni zingeliporomoka. Kuwa na tabia ya uongo ni ujamaa wa kupukusa tabia pekee ya ubinaadamu, kwani kuzungumza uongo ni uangamizaji wa hali ya kibinaadamu. 

 

Shariy'ah ya Kiislamu; Qur-aan na Sunnah inatuonya kusema uongo na kwa makubaliano ya wanachuoni kwamba ni haramu. Mtu muongo atachuma malipo mabaya duniani na Aakhirah.

 

Katika shariy'ah, kuongopa hakuruhusiwi ila katika hali fulani ambazo hazipotezi haki za mtu, au kumwaga damu au kufedhehesha, au kumvunjia mtu heshima yake. Bali katika mas-alah ya kuokoa maisha, kusuluhisha baina ya watu au kujenga mapenzi baina ya mume na mke umeruhusiwa uongo. Wala shariy'ah haikumruhusu mtu aseme uongo wa utani usio na maana kama huu wa April Fool.

 

 

Makatazo Ya Kusema Uongo 

 

Allaah (Subhaanahu wa Ta'aala) Anasema:

إِنَّمَا يَفْتَرِي الْكَذِبَ الَّذِينَ لاَ يُؤْمِنُونَ بِآيَاتِ اللّهِ وَأُوْلئِكَ هُمُ الْكَاذِبُونَ﴿١٠٥﴾

Hakika wanaotunga uongo ni wale ambao hawaamini Aayaat za Allaah. Na hao ndio waongo. [An-Nahl: 105]

 

Ibn Kathiyr amesema kuhusu Aayah hiyo:

"Allaah Anatuambia kwamba Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) sio mzushi au muongo, kwa sababu ni watu waovu tu ambao hawaamini alama za Allaah, makafiri na wanafiki wanaojulikana baina ya watu kwa uongo wao, uongo kuhusu Allaah na Nabiy Wake (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam).

 

Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa ni mkweli kabisa miongoni mwa watu, mchaji Allaah, mwenye elimu bora kabisa, mwenye matendo mema, tabia njema. Hakuna aliyekuwa na shaka naye hadi kwamba aliitwa 'Al-Amiyn' (Mkweli). Hivyo Hercules, mfalme wa Rome alipomuuliza Abu Sufyaan kuhusu tabia za Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam), jambo moja alilouliza lilikuwa ni: "Je, mmepata kumtuhumu kwa uongo kabla ya kusema aliyoyasema?". Alijibu: "Hapana". Hercules akasema: "Ikiwa alijiepusha kusema uongo kwa watu basi hawezi kusema uongo kuhusu Allaah". [Tafsiyr Ibn Kathiyr, 2/588].

 

Imetoka kwa Abuu Hurayrah (Radhwiya Allaahu 'anhu) kwamba Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Alama za munaafiq ni tatu; akizungumza husema uongo, akitoa ahadi huivunja, akiaminishwa kwa kitu hufanya khiyana" [Al-Bukhaariy na Muslim]

 

 

Uongo Ulio Muovu Kabisa 

 

1. Uongo Kuhusu Allaah Na Nabiy Wake (Swalla Allaahu 'Alayhi Wa aalihi Wa Sallam)

Huu ni uongo wa hatari kabisa na anayezua hivyo basi hupewa onyo kali. Baadhi wa 'Ulamaa wamesema kwamba anayezua uongo kama huu basi ashutumiwe kuwa kafiri.

 

Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Anasema:

قُلْ إِنَّ الَّذِينَ يَفْتَرُونَ عَلَى اللّهِ الْكَذِبَ لاَ يُفْلِحُونَ﴿٦٩﴾

Sema: Hakika wale wanaomtungia uongo Allaah hawatofaulu.[Yuwnus: 69]

 

Imetoka kwa 'Aliy (Radhwiya Allaahu 'anhu) kwamba Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Msinizulie uongo. Yeyote atakayezua uongo kuhusu mimi basi ataingia motoni)) [Al-Bukhaariy]

 

Imetoka kwa Abuu Hurayrah (Radhwiya Allaahu 'anhu) kwamba Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Yeyote atakayenizulia uongo basi ajitayarishie makazi yake motoni)) [Al-Bukhaariy na Muslim]

 

Ibnu Al-Qayyim amesema kuhusu maana ya Hadiyth hii kwamba:  "Yeyote atakayezua uongo kuhusu mimi basi ajitayarishie makazi yake motoni ambako ataishi milele, na sio kama kambi ambayo mtu huishi kwa muda kisha akahamia kwengine" [Twariyqul-Hijratayn ukurasa 169]

 

 

2. Uongo Katika Kununua Na Kuuza

Uongo mwengine ni wakati mtu anapofanya biashara na katika kununua huzua na kuuza pia hudanganya.

 

Imetoka kwa Abuu Dharr (Radhwiya Allaahu 'anhu) kwamba Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Watu watatu ambao Allaah Hatosema nao siku ya Qiyaamah na wala Hatowatazama wala kuwatukuza, na watapata adhabu iumizayo)) Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alisema mara tatu. Abu Dharr akasema: "Waangamizwe na wapotezwe, ni nani hao ewe Rasuli wa Allaah?" Akasema: (([mwanaume] Mwenye kuachia nguo yake ivuke kiwiko cha mguu, mwenye kujisifu, na mwenye kufanya biashara yake kwa kuapa uongo)). [Muslim] 

 

Imesimuliwa na Hakiym bin Hizaam (Radhwiya Allaahu 'anhu) kwamba "Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Watu wawili wanaohusika na makubaliano ya biashara wanayo khiyari (ya kuvunja makubaliano) hadi watakapofarikiana. Ikiwa waaminifu makubaliano yao yatabarikiwa na wakikhini kitu na kusema uongo, baraka itafutwa katika makubaliano yao)) [Al-Bukhaariy na Muslim]

 

Shaykhul-Islaam Ibn Taymiyyah amesema:

Allaah Ameusia ukweli na uaminifu, na Ameharamisha uongo na khiana katika mambo yapasayo kujulikana na kufunuliwa kwa watu kama alivyosema Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ((Watu wawili wanaohusika na makubaliano ya biashara wanayo khiari (ya kuvunja makubaliano) hadi watakapofarikiana. Ikiwa waaminifu makubaliano yao yatabarikiwa na wakikhini kitu na kusema uongo, baraka itafutwa katika makubaliano yao)) na Allaah (Subhaanahu wa Ta'aala) Anasema:

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُواْ كُونُواْ قَوَّامِينَ لِلّهِ شُهَدَاء بِالْقِسْطِ وَلاَ يَجْرِمَنَّكُمْ شَنَآنُ قَوْمٍ عَلَى أَلاَّ تَعْدِلُواْ اعْدِلُواْ هُوَ أَقْرَبُ لِلتَّقْوَى  

Enyi walioamini!  Kuweni wasimamizi madhubuti kwa ajili ya Allaah mkitoa ushahidi kwa uadilifu. Na wala chuki ya watu isikuchocheeni kutokufanya uadilifu. Fanyeni uadilifu; hivyo ni karibu zaidi na taqwa. [Al-Maaidah: 8] [Minhaajus-Sunnah 1/16]

 

3. Kuharamishwa Uongo Kuhusu Njozi Na Ndoto

Hii ni kuhusu baadhi ya watu wanaodai kuwa wameona ndoto kadhaa kisha asubuhi wanawasimulia watu mambo ambayo wala hawakuyaona.

 

Imetoka kwa Ibn 'Abbaas (Radhwiya Allaahu 'anhuma) kwamba Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Yeyote atakayesimulia ndoto ambayo hakuiona, ataamrishwa (Siku ya Qiyaamah) aunganishe pamoja chembe mbili za shayiri, lakini hatoweza. Yeyote atakayetega masikio (kwa umbea) kusikiliza mazungumzo ya watu ambao wasingelipenda (yeye asikilize), au ambao wanamuepuka atamiminiwa shaba ya moto iliyoyeyushwa katika masikio yake siku ya Qiyaamah. Na Yeyote atakayetengeneza (kuchora au kuchonga) picha ataadhibiwa na ataambiwa aitie uhai (roho) na wala hatoweza)) [Al-Bukhaariy] 

 

Katika kufafanua Hadiyth hiyo, Wanachuoni wanasema: "Kuunganisha shayiri mbili, lakini hatoweza kufanya hivyo" kwa sababu kuiunga moja kwa mwenziwe haiwezekani kikawaida. Ataadhibiwa mpaka aweze kuziunga, na wala hataweza kuziunga. Kama kwamba anasema, ameshurutishwa kufanya jambo asiloliweza na anaadhibiwa kwa hilo. Hii ni sitiari ya adhabu inayoendelea. Sababu ya kutajwa shayiri hasa, ni kwamba ndoto zina uhusiano na hisia (Kwa Kiarabu hisia ni shu'uur), maneno ya shayiri na shu'uur yanatokana na mzizi (asili ya neno) mmoja katika Kiarabu.

 

Adhabu ya aina hii ya uongo ni kali sana ingawa anapokuwa macho huenda akasababisha madhara zaidi, kwa sababu huenda yakahusiana na kutoa ushahidi na huenda yakampelekea kuuliwa au kupewa adhabu ya hadd. Hii ni kwa sababu kusema uongo kuhusu ndoto ni kumzulia Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) kwani ndoto ni sehemu ya Utume, hivyo zinatoka Kwake. Na kumzulia Muumba ni khatari zaidi kuliko kuwazulia viumbe.

 

 

4. Kuharamishwa Kusema Kila Anachokisikia Mtu

Imesimuliwa kwamba Hafsw bin 'Aaswim amesema: Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Inatosheleza kuwa ni uongo kwa mtu anayesema kila anachokisikia)) [Muslim]

 

"Kutokana na maana ya Hadiyth kuhusu maudhui hii, tunaona kwamba inakatazwa kutaja au kuhadithia kila jambo analolisikia mtu, kwa sababu kawaida mtu anasikia yote ya kweli na uongo. Kwa hiyo ikiwa atasema kila anachokisikia atakuwa anasema uongo kwa kusema jambo lisilotokea. Tumetaja juu rai za watu wakweli, kwamba uongo una maana kwamba kusema au kuelezea jambo katika hali dhidi ya lilivyotokea. Sio sharti juu yake ikiwa limefanyika makusudi lakini kufanyika kwake makusudi kunashurutisha kuwa ni dhambi. Na Allaah Anajua zaidi" [Sharh Muslim, 1/75]

 

 

5. Uongo Wa Utani

Watu wengine wanadhania kwamba inaruhusiwa kusema uongo wakati wa utani. Na huu ndio udhuru wanaoutoa katika kuongopa siku ya terehe 1 Aprili au siku nyinginezo. Hayo ni makosa. Hakuna msingi wa jambo hili katika sharia safi. Kuongopa ni haraam ikiwa ni kwa kutania au kwa dhati. Kuongopa kwa kutania ni haramu sawa sawa na kuongopa kwa aina yoyote nyingine.

 

Imesimuliwa kwamba 'Umar (Radhwiya Allaahu 'anhu) amesema: Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Mimi hutania lakini sisemi ila ni ya kweli)) [At-Twabaraaniy katika 'Al-Mu'jam Al-Kabiyr 12/391 – Hadiyth hii imepewa daraja ya hasan na Al-Haythamiy katika Majma' Az-Zawaaid 8/89 na Shaykh Al-Albaaniy ameipa daraja ya sahihi katika Swahiyh Al-Jaami' 2394]]

 

Imesimuliwa kwamba amesema: "Walisema, ee Rasuli wa Allaah, unafanya utani na sisi". Akasema: ((Lakini nnayoyasema ni ukweli tu)) [At-Tirmidhiy]

 

'Abdur-Rahmaan bin Abiy Laylaa amesema: "Swahaba wa Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) wametuambia kuwa walikuwa safarini pamoja na Rasuli wa Allaah. Mtu mmoja miongoni mwao alilala na baadhi yao walikwenda kuchukua mishale yake. Alipoamka alishtuka (alipoona mishale yake haipo). Watu wakacheka. Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akasema: ((Mnacheka nini?)) Wakasema: "Hakuna kitu isipokuwa tumechukua mishale yake na ameshtuka". Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akasema: ((Haimpasi Muislamu kumtisha Muislamu mwingine)) [Abuu Daawuwd, Ahmad na Shaykh Al-Albaaniy ameipa daraja ya Swahiyh katika Swahiyh Al-Jaami']

 

Imesimuliwa kutoka kwa 'Abdullaah bin As-Saa'ib bin Yaziyd kutoka kwa baba yake, kutoka kwa babu yake kwamba amemsikia Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akisema: ((Haimpasi yeyote katika nyinyi kuchukua kitu cha ndugu yake, ikiwa ni kwa utani au kwa vyovyote. Yeyote aliyechukua kijiti cha ndugu yake basi akirudishe)) [Abuu Daawuwd, At-Tirmidhiy na Shaykh Al-Albaaniy ameipa daraja ya hasan katika Swahiyh Al-Jaami']

 

 

6.    Kuongopa Wakati Wa Kucheza Na Watoto

Lazima tutahadhari na kusema uongo tunapocheza na watoto kwa sababu itaandikwa katika kitabu cha hesabu. Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ameonya jambo hili.

 

Imesimuliwa kwamba 'Abdullaah bin 'Aamir (Radhwiya Allaahu 'anhu) alisema: "Siku moja mama yangu aliniita wakati alipokuwa Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ameketi nyumbani kwetu. Akasema: Njoo hapa nikupe (kitu). Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akasema: ((Je, unataka kumpa nini?)) Akasema: 'Nitampa tende'. Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akasema: ((Kama usingelimpa basi ungelikuwa unasema uongo)).

 

Na imesimuliwa kwamba Abuu Hurayrah (Radhwiya Allaahu 'anhu) amesema: Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Yeyote atakayemuambia mtoto 'njoo hapa uchukue hii' kisha asimpe kitu basi itahesabiwa ni uongo)) [Abuu Daawuwd na Shaykh Al-Albaaniy ameipa daraja ya hasan katika Swahiyh Al-Jaami']

 

 

7.    Uongo Ili Kuchekesha Watu

Imesimuliwa kwamba Mu'aawiyah bin Hadah amesema: "Nimemsikia Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akisema: ((Ole wake mtu anayezungumza kwa ajili ya kuwachekesha watu na akasema uongo, ole wake, ole wake)) [At-Trimidhiy akisema ni hadiyth hasan na Abuu Daawuwd]

 

 

Adhabu Kwa Ajili Ya Kusema Uongo

 

Mwenye kusema uongo amepewa onyo kali la adhabu ya hizaya duniani na adhabu kali Aakhirah nazo ni kama zifuatazo:

 

Unafiki Katika Moyo

Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Anasema:

فَأَعْقَبَهُمْ نِفَاقًا فِي قُلُوبِهِمْ إِلَى يَوْمِ يَلْقَوْنَهُ بِمَا أَخْلَفُواْ اللّهَ مَا وَعَدُوهُ وَبِمَا كَانُواْ يَكْذِبُونَ﴿٧٧﴾

Basi Akawapatilizia unafiki katika nyoyo zao mpaka Siku watakayokutana Naye kwa vile walivyomkhalifu kwao Allaah kwa waliyomuahidi, na kwa yale waliyokuwa wakikadhibisha. [At-Tawbah: 77]

 

'Abdullaah bin Mas'uwd (Radhwiya Allaahu 'anhu) amesema: "Unaweza kumjua mtu mnafiki kwa mambo matatu; anaposema anaongopa, anapotoa ahadi anaivunja, anapoaminiwa na amana hufanya khiyana". Akasema: "Someni aya hizi:

وَمِنْهُم مَّنْ عَاهَدَ اللّهَ لَئِنْ آتَانَا مِن فَضْلِهِ لَنَصَّدَّقَنَّ وَلَنَكُونَنَّ مِنَ الصَّالِحِينَ﴿٧٥﴾فَلَمَّا آتَاهُم مِّن فَضْلِهِ بَخِلُواْ بِهِ وَتَوَلَّواْ وَّهُم مُّعْرِضُونَ﴿٧٦﴾فَأَعْقَبَهُمْ نِفَاقًا فِي قُلُوبِهِمْ إِلَى يَوْمِ يَلْقَوْنَهُ بِمَا أَخْلَفُواْ اللّهَ مَا وَعَدُوهُ وَبِمَا كَانُواْ  يَكْذِبُونَ﴿٧٧﴾  

Basi Akawapatilizia unafiki katika nyoyo zao mpaka Siku watakayokutana Naye kwa vile walivyomkhalifu kwao Allaah kwa waliyomuahidi, na kwa yale waliyokuwa wakikadhibisha.

Alipowapa katika fadhila Zake; walizifanyia ubakhili, na wakakengeuka huku wakipuuza.

Basi Akawapatilizia unafiki katika nyoyo zao mpaka Siku watakayokutana Naye kwa vile walivyomkhalifu kwao Allaah kwa waliyomuahidi, na kwa yale waliyokuwa wakikadhibisha. [At-Tawbah: 75-77]

[Muswanaf Ibn Abiy Shaybah, 6/125] 

 

 

Uongo Humpeleka Mtu Motoni

Imesimuliwa kwamba 'Abdullaah bin Mas'uwd (Radhwiya Allaahu 'anhu) amesema: Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Ukweli ni utiifu, na utiifu huelekeza Jannah. Mtu ataendelea kusema ukweli hadi Ataandikiwa na Allaah kuwa ni mkweli. Uongo ni uovu, na uovu huelekeza motoni. Mtu ataendelea kusema uongo hadi Ataandikiwa kuwa ni muongo)) [Al-Bukhaariy na Muslim]

 

As-Swan'aaniy amesema:

"Hadiyth hii inaonyesha kwamba yeyote anayeendelea kusema ukweli, itakuwa ni wasifu wake, na yeyote anayesema uongo makusudi na kuendelea, itakuwa ni wasifu wake. Hii ni sawa kama kitendo chochote kingine chema au kiovu. Mtu akiendelea nacho kinakuwa ndio sifa yake.

 

Vile vile Hadiyth hii inaonyesha jinsi gani ilivyo muhimu kusema ukweli hadi kwamba unampeleka mtu Peponi na imeonyesha vipi ubaya wa kusema uongo hadi unampeleka mtu motoni. Juu ya hivyo, bado kuna matokeo ya adhabu za duniya kwani anayesema ukweli atakuwa anakubaliwa usemi wake na watu na ushahidi wake utakubaliwa na jaji na atapendwa kwa yale anayoyasema. Ama mtu muongo ni dhidi ya hayo." [Subul-As-Salaam 2/687]

 

 

Ushahidi Wake Utakanushwa

Ibnul-Qayyim amesema kuhusu sababu ya ushahidi wa mtu muongo kukanushwa:

"Sababu ya nguvu kabisa kwa nini katika kutoa ushahidi, fatwa na ripoti zikanushwe ni kusema uongo, kwa sababu inafisidi asili ya ushahidi, fatwa au taarifa. Ni kama ushahidi wa kipofu kuona mwezi mpya, au ushahidi wa kiziwi kuhusu kusikia kuruhusiwa kuingia mtu mahali. Ulimi unaoongopa ni kama baadhi ya uelekevu ambao haufanyi kazi tena. Hakika ni mbaya zaidi kuliko hivyo, kwani kitendo kiovu kabisa mtu kumiliki ni ulimi muongo." [I’ilaam Al-Muwaqqi'iyn 1/95]

 

 

Nyuso Kuwa Nyeusi Duniani Na Aakhirah           

Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Anasema:

وَيَوْمَ الْقِيَامَةِ تَرَى الَّذِينَ كَذَبُواْ عَلَى اللَّهِ وُجُوهُهُم مُّسْوَدَّةٌ أَلَيْسَ فِي جَهَنَّمَ مَثْوًى لِّلْمُتَكَبِّرِينَ﴿٦٠﴾

((Na Siku ya Qiyaamah utawaona waliomsingizia uongo Allaah nyuso zao zimesawijika (zimekuwa nyeusi). Je! Si katika Jahannamu makaazi ya wanaotakabari?)) [Az-Zumar: 60]

 

Ibnul-Qayyim amesema: "Hivyo siku ya Qiyaamah Allaah (Subhaanahu Wa Ta'aala) Atazifanya nyuso ziwe alama za waliosema uongo kuhusu Allaah na Mjumbe Wake. Kusema uongo kunaleta taathira kubwa ya kufanya nyuso ziwe nyeusi na kuzifunika na kitambaa cha hizaya na kila mtu mkweli ataziona nyuso hizo. Wasifu wa mtu muongo utatambulikana dhahiri kabisa usoni na kila mtu aliye na macho ataweza kumuona. Lakini Allaah (Subhaanahu wa Ta'aala) Anambariki mtu mkweli kwa hadhi na heshima ili yeyote atakayemuona atamuheshimu na kumpenda. Na Atampa muongo fedheha na aibu ili yeyote atakayemuona atamchukia na kumdharau. Na Allaah Ni Mwenye Chanzo cha Nguvu" [I'laam Al-Muwaqi'iyn 1/95]

 

 

Mtu Muongo Atachanwa Mashavu Yake Kutoka Kisogoni

Imesimuliwa kwamba Samurah ibn Jundub (Radhwiya Allaahu 'anhu) amesema"Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akiwaambia mara kwa mara Maswahaba zake: ((Je, kuna yeyote miongoni mwenu aliyeona ndoto?)). Kisha yeyote aliyejaaliwa na Allaah ataelezea ndoto yake. Siku moja alituambia: (([Malaika] Wawili walinijia jana usiku na kuniamsha, kisha wakaniambia: 'Twende…' Tukatoka na kwenda hadi tukafika kwa mtu aliyelala chali na mwengine amesimama juu ya kichwa chake akiwa na ndoana ya chuma. (Akashtuka aliyoyaona na kusema) Na kitu gani cha kutazama! Alikuwa akitia ndoana katika upande mmoja mdomoni mwa mwenzake (aliyelala) akimchana kutoka upande mmoja wa uso hadi nyuma (ya shingo) na hivyo hivyo akiichana pua kutoka mbele hadi nyuma ya macho yake kisha akiendelea kufanya hivyo hivyo kama alivyofanya kwa upande mwingine. Hawahi kumaliza kumchana upande mmoja ila upande mwingine unarudishwa hali yake (ya mwanzo). Kisha hurudia kufanya hivyo hivyo upya tena. Nikasema kwa Swahaba zangu (Malaika) wawili, 'Subhaanahu Allaah! Ni watu gani hawa wawili?' Wakaniambia: 'Endelea kwenda, endelea kwenda!' (kisha akasema akielezea vipi Malaika wawili wakielezea mambo aliyokuwa akiyaona): 'Ama yule mtu uliyemuona kuwa anachanwa mdomo, pua na macho yake, ni alama ya mtu anayetoka nyumbani kwake asubuhi na kusema uongo mwingi hadi unasambaa duniani kote')) [Al-Bukhaariy]        

 

 

Kauli Za Swahab Kuhusu Uongo 

 

Abuu Bakr As-Swiddiyq (Radhwiya Allaahu 'anhu):   

"Tahadharini na uongo kwani hauna uhusiano na Iymaan".

 

'Umar Ibnul-Khatwaab (Radhwiya Allaahu 'anhu):  

"Iymaan ya dhaati haiwezi kupatikana hadi mtu aache uongo wa utani"

 

'Abdullaah bin Mas'uwd (Radhwiya Allaahu 'anhu):  

"Mtu atasema ukweli na kuendelea kufanya hivyo hadi hakutakuwa na nafasi ya uovu katika moyo wake japo kama ni wa kiasi cha sindano. Au mtu atasema uongo na kuendelea kufanya hivyo hadi hakutakuwa na nafasi ya ukweli katika moyo wake japo kama ni wa kiasi cha sindano".

 

Vile vile amesema:  "Haimpasi mtu kusema uongo ikiwa ni kwa kutania au kikweli". Kisha Ibn Mas'uud akasoma Ayah:

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُواْ اتَّقُواْ اللّهَ وَكُونُواْ مَعَ الصَّادِقِينَ﴿١١٩﴾

Enyi walioamini! Mcheni Allaah na kuweni pamoja na wakweli.[At-Tawbah: 119]

 

 Sa'ad bin Abi Waqqaasw (Radhwiya Allaahu 'anhu)    

"Muumini anaweza kuwa na sifa zote isipokuwa usaliti na uongo"

[Muswannaf Ibn Abi Shaybah, 5/235, 236] 

 

 

Aina Ya Uongo  Unaoruhusiwa

 

Uongo unaruhusiwa katika hali tatu; kwenye vita, kusuluhisha baina ya watu wawili waliogombana, mume kumuongopea mkewe au kinyume chake kwa ajili ya mapenzi na maelewano.

 

Imesimuliwa kutoka kwa Ummu Kulthuwm bint 'Uqbah (Radhwiya Allaahu 'anhaa) kwamba amemsikia Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akisema: ((Sio muongo mwenye kupatanisha baina ya watu na akasimulia jambo zuri au akasema maneno mazuri)) [Al-Bukhaariy, Muslim]  

 

Imesimuliwa kwamba Asmaa bin Yaziyd amesema: Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Hairuhusiwi kusema uongo isipokuwa katika hali tatu; mtu anapozungumza na mkewe katika njia ya kumfurahisha, kusema uongo katika vita, na uongo kwa ajili ya kusuluhisha baina ya watu)) [At-Tirmidhiy na Shaykh Al-Albaaniy ameipa daraja ya Swahiyh katika Swahiyh Al-Jaami']

 

 

Khitimisho

 

Baada ya kutambua chanzo cha siku hiyo ya April Fool, uongo na madhara yake, basi tujitahidi nafsi zetu kutosherehekea siku hiyo kabisa, ili tubakie katika tabia ya ukweli daima. Hata kama si muhimu kujua chanzo cha siku hii, bali lililo muhimu ni kujua hukumu ya kusema uongo na khofu ya adhabu zake kama tulivyopata mafundisho katika Aayah na Hadiyth zilizotangulia.

 

Hiyo ni shariy'ah ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) ambayo ina Hikma inayorekebisha nafsi za binaadamu kubakia katika hali ya fitrah (asili ya maumbile) ili abakie binaadamu daima ni mwenye kuishi salama na amani katika jamii, na vile vile ajiepushe na adhabu kali Alizoziandaa Mola Mtukufu kwa maovu kama hayo.

 

Mafundisho muhimu na yatakayoonekana mapya kwa wengi wetu tunayoyapata katika makala haya ni kujihadhari na matani yaliyojaa uongo; tukitazama matani mengi hadi yawe matani basi kutakuwepo na uongo ndani yake, na utani haufurahishi kwa wengi hadi uwe na udanganyifu na hila ndani yake, hivyo tujihadhari sana Waislam na uongo kwenye matani. Vilevile tujiepushe na tabia mbaya ambayo baadhi yetu wanaipenda, nayo ni kuleta matani watu wacheke, au kuwafurahisha watu kwa matani. Kuna watu kazi yao kukaa vijiweni na kumwaga matani hadi wakawa wanajulikana kwa sifa hiyo na wasipoonekana siku moja ni pengo kwenye kijiwe! Hadi inafika mtu jina lake kubadilishwa na kuitwa Fulani Matani! Na kuna wengine ambao tabia yao ni kupenda kuwa katika mwangaza daima (kuonekana) na kuwa na tabia ya kujipendekeza na haswa kwa watu wa jinsia tofauti ili akusanye sifa au kupendeka, mwisho akawa anajulikana kwa kufanya sifa hizo na vituko ambavyo vimejaa uongo, matusi, kuigiza wenzake, kebehi n.k.

 

Kadhaalika, tuifuate Hadiyth isemayo: ((Mwenye kumuamini Allaah na siku ya mwisho, aseme khayr (maneno mazuri/ukweli) au anyamaze...)) [Hadiyth kutoka kwa Abu Hurayrah iliyosimuliwa na Al-Bukhaariy na Muslim]

 

Tunamuomba Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Aturuzuku ukweli daima na Ajaalie ndimi zetu ziseme yanayopasa tu kusema na Atujaalie miongoni mwa walioamini na wasemao kweli (Asw-Swiddiyqiyn). Aamiyn.

 

 

Share