Mfugaji Wanyama Vipi Achinje Idadi Kubwa Ya Wanyama Kama Kuku?

Mfugaji Wanyama Vipi Achinje Idadi Kubwa Ya Wanyama Kama Kuku?

 

Alhidaaya.com

 

 

SWALI:

 

 

Assalam alaykum

Mimi ni mfugaji wa kuku wa kizungu naomba nifahamiswe taratibu za kisheria za kuchinja kuku idadi nyingi kama zaidi ya 200 nimeambiwa nisipoosha kisu kwa maji baada ya kila kuku, kuku hao watakuwa ni haraam kuwala, vipi pia kuhusu kuku  kuwakusanya pamoja wakati wa kuwachinja?

 

 

JIBU:

 

 

Hakika hatujapata chochote kuhusu kuosha kisu baada ya kuchinja kuku mmoja na kabla ya kumchinja mwingine. Kile ambacho kinahitajika katika Sunnah ni kukinoa kisu ili uondoe usumbufu kwa mnyama. Hii ni kwa mujibu wa kauli ya Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): “Hakika Allaah Ameamrisha ihsaan (wema) kwa kila kitu. Kwa hivyo, mkiua ueni vizuri, na mkichinja chinjeni vizuri. Kila mmoja wenu na akitie makali kisu chake na akipunguzie uchungu kichinjwa chake” [Muslim, Abu Daawuwd, at-Tirmidhiy, an-Nasaa’iy, Ibn Maajah na ad-Daarimiy].

 

 

Kuchinja vizuri ni kwa kutumia ala ya kuchinjia yenye makali na kumchinja mnyama upesi upesi. Haifai mnyama kupigwa ovyo kabla ya kuchinjwa wala kumburuza. Achinjaye aseme

 

بِسْمِ اللَّهِ

 

BismiLlaahi

 

amuelekeze Qiblah, amkate gorombo (koo) na mishipa miwili ya damu (jugular veins) ili afe upesi na damu yote itoke. Pia ni vyema kuwa wanyama (kuku kwa kesi yako) wawe hawapo sehemu moja ya kuchinjwa.

 

 

Kuwakusanya pamoja kuku wote pamoja na wakawa wanaona wenzao wanaochinjwa haipendezi, ni bora kuwaweka sehemu na ukamtoa mmoja mmojabila wengine kuona. Likiwa haliwezekani hilo na ikawa inabidi lazima wawe pamoja, hapo ni masuala ya dharura na haitokatazwa kwa dharura hiyo, lakini kama inawezekana ni bora kutokufanya hivyo.

 

Bonyeza viungo vifuatavyo upate maelezo zaidi

 

Nyama Ya Halaal Uchinjaji Wake

  

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share