Mirungi -1: Aina Zake

Mirungi - 1 (Na Aina Zake)

 

Abuu 'Abdillaah

 

www.alhidaaya.com

بسم الله الرحمن الرحيم

 

 

MIRUNGI, QAAT, KHAT, GHAT, GATI, MIRAA, GOMBA, MBAGA, VEVE, MTI, KIJITI, MAJANI, MAUA …

 

 

    

 

 

Mirungi au kama inavyojulikana kama Qaat au Qaadka huko Somalia, na Yemen huitwa au Al-Qaat القات; ingawa kwa matamshi ya huko hutamkwa ‘Gaat’, Kadhalika Kenya kulingana na miji yake hujulikana kama; Miraa, Veve, Kijiti, Gomba n.k., na Tanzania ni maarufu kwa majina; Mirungi, Gomba, Gati, Miti, Majani n.k. kulingana na kila eneo na jina lake.

 

Mirungi au (Catha edulis) Ni mmea au mti unaoota au kuoteshwa kwa wingi sana huko Ethiopia, Yemen na Kenya.

 

Jani hilo ambalo Maulamaa wameeleza kuwa ni Haraam kutafuna kama tutakavyoona mbele ya makala hii, ni jani lenye madhara mengi katika siha ya mwana Aadam na lenye kusababisha mengi katika madhara na maangamizi ya kimaadili na kijamii.

 

Matumizi ya mmea huo ambao hakika kwa masikitiko makubwa, yameenea zaidi katika jamii za Kiislam na haswa maeneo ya mijini na zaidi kwa wanaojulikana kama ‘Waswahili.’

 

Ingawa neno ‘Waswahili’ asli yake ni neno la Kiarabu ‘Saahil’ ساحل pwani, mwambao na ‘Saahiliy’ -ya pwani, au mkaazi wa pwani au mwambao, ila neno hilo au jina hilo hivi sasa limegeuka kimatumizi na kuashiria zaidi kwa wale watu zaidi wa mtaani, wasiopenda kutumika; kufanya kazi, wasio wakweli, wapenda starehe, wasio na elimu, wazembe n.k. Kwa wasio Waislam wao wanatumia jina hilo kuwaita nalo Waislam, na zaidi wakikusudia sifa hizo tulizozitaja hapo nyuma. Na kadhalika Waislam kadhaa huwaita wenzao hivyo wakimaanisha, wasio na ahadi, wasemao uongo, wasioaminika, wajanja wajanja, wajuaji, na wenye maneno mengi wasioshindika.

 

Mirungi inakusanya ndani yake alkaloid iitwayo cathinone, amphetamine kama kichangamsho (stimulant) ambayo inasemekana husababisha msisimko, uchangamfu, kuwa na aina ya furaha ya kuwazika –kuhandasika- na huondosha hamu ya kula na kusababisha ukosefu wa usingizi.

 

Mnamo mwaka 1980 WHO (Shirika la Afya Duniani) liliiweka Mirungi katika fungu la madawa ya kulevya ambayo inasababisha nafsi kutawaliwa nayo au kuwa na uraibu (addiction) kwa daraja ya kati hadi ile yenye nguvu.

 

Mti huo umekuwa ukiandamwa na mashirika yenye kupinga madawa ya kulevya kama shirika liitwalo DEA (Drug Enforcement Administration). Shirika hilo katika mwaka 2006 Julai tarehe 26, shirika hilo katika operesheni iliyokuwa ikijulikana kama ‘Somalia Express’ ambayo katika upelelezi wake uliodumu kwa muda wa mwaka mmoja na nusu ambao ulihusisha wanachama 44 wa kundi lililokuwa likisafirisha tani 25 za Mirungi ambazo zilikuwa na thamani ya Dola milioni 10 za Kimarekani kutoka Somalia kupelekwa Marekani. Shitaka (Kosa) hilo lilihusisha utoroshaji mkubwa kabisa wa Mirungi katika Historia ya Marekani.

 

Biashara hiyo ambayo imeshamiri nchi za Afrika Mashariki ambapo hivi sasa Tanzania imepigwa marufuku, na pia kuenea katika nchi za Ulaya na Marekani. Mirungi imepigwa marufuku katika nchi mbalimbali za Scandinavia, lakini bado inajadiliwa Uingereza kama ni katika kifungu cha madawa ya kulevya au hapana!

 

Ni mmea ambao umewekewa sheria kali au kupigwa marufuku nchi nyingi duniani.

 

Mirungi imekuwa ni sehemu muhimu ya maisha ya watu wengi kuanzia Yemen, Ethiopia, Kenya, Tanzania na nchi ambazo watu wa nchi hizi wanaishi. Uingereza ambapo bado ulaji wa Mirungi haujapigwa marufuku; kila siku ndege inateremsha Mirungi kutoka Ethiopia na Kenya kwa wingi, na biashara yake imekuwa na nguvu kwa jamii ya Wasomali, Wayemen, Waethiopia na Watanzania wanaoishi katika nchi hiyo. Utagundua haraka sehemu au maeneo na nyumba zinazouzwa au kuliwa Mirungi kwa athari za uchafu wa vijiti vya Mirungi na majani yake yanayotupwa ovyo ovyo kila pahali na kuwa kero kubwa kwa wakazi wa jirani wa maeneo hayo na hata Manispaa au Serikali za Mitaa (Borough Councils) za maeneo hayo Uingereza.

 

Kadhalika, kwa unafuu wake wa usafirishaji kwa ndege, majani hayo husafirishwa kuelekea sehemu zingine kama Wales, Rome, Amsterdam, Canada, Australia, New Zealand na Marekani.

 

 

 

Ulaji wa Mirungi umekuwa ukiongezeka sana katika jamii mbalimbali hususan Yemen, Kenya na Tanzania na haswa walaji wa kiada –wakiwemo wanawake na hata watoto- na kusababisha kuongezeka mahitajio yake. Hii ni kwa sababu Mirungi ni kilevi cha kawaida katika jamii kama ilivyokuwa sigara ni kilevi kikubwa cha jamii ya Ulaya na Marekani hadi hivi karibuni baada ya kampeni za kila siku za kupiga vita. Ni kilewesho na uraibu ambao haujafikia daraja na uzito wa pombe. Haki ya uraibu huu umewatatiza Wanachuoni wengi wa Yemen na jamii zingine kufikia ufumbuzi wa kukata katika kuzima balaa hilo. Hata hivyo, kama tutakavyoona mbele ya makala hii, Wanachuoni wengi wakubwa wa nchi mbalimbali duniani, wameeleza uharamu wake.

 

Kwa kujitetea, walaji Mirungi wanaamini kuwa majani hayo huwapatia nguvu, na uchangamfu na mliwazo wa furaha ‘Handasi au Nakhwa’ kwa lugha yao. “Hakuna Mirungi, hakuna nguvu, na hivyo hakuna kufanya kazi, jimaa, kusoma, au chochote,” hivyo ndivyo wanavyodai.

 

Pamoja na madhara yake na maonyo makali ya taasisi za tiba na mashirika ya Afya duniani, lakini inaelekea kumalizika matumizi ya Mirungi moja kwa moja, ni jambo linaloonekana litachukua miaka mingi sana na vizazi vingi huko Yemen na hata Afrika Mashariki. Yemen ni nchi ambayo uraibu huo umetawala hadi kufikia watu kulazimika kuwekea ‘nyakati maalumu’ za ulaji.

 

Miaka kadhaa nyuma, Raisi wa nchi hiyo ‘Aliy ‘Abdullaah Swaalih aliwahi kueleza hadharani kuwa naye ni mlaji wa Mirungi lakini mwisho wa wiki; ingawa siku za mbeleni akaja kutangaza hadharani anajaribu kuachana nayo moja kwa moja. Mwaka 2002, wafanyakazi wote wa serikali ambao mwanzoni walikuwa wakila Mirungi kazini, walipigwa marufuku kuila kazini. Lakini leo hii, ulaji umeongezeka sana kuliko ulivyokuwa huko nyuma.

 

Anasema mwandishi maarufu Yemen, ‘Abdul-Kariym Ar-Razihi: “Mirungi (Qaat)… ni kileo cha watu wetu. Ni Imamu wa kijani anayeongoza nchi yetu. Ni ufunguo wa kila kitu na ni makutano ya vikao na minasabati yote ya kijamii. Ni kitu kisichoelezeka kinachoeleza kila kitu”

 

Vitabu kadhaa vimeandikwa na watu wa Magharibi kuhusu uraibu huo unaotisha, watengenezaji vipindi vya Televisheni vya Ulaya wamekuwa wakizuru nchi hiyo kuchukua maisha ya kila siku ya Wayemen ambayo yameeathiriwa kiasi kikubwa na ulaji huo hadi kuonekana watoto wadogo ambao hawajafikia baleghe kuwa ni walaji na wauzaji wakubwa.

 

Hali hii kwa mtazamo wa Kiislam, ikiwa inaashiria jambo, basi inaashiria uporomokaji na uozo wa jamii ya Kiislam na mustaqbali wa kizazi cha jamii hii ya Kiislam.

 

Itaendelea…/2

 

Mirungi - 2 (Historia, Madhara Na Mikasa)

 

 

Share