Anaomba Toba Kisha Anarudia Tena Kufanya Kosa Kila Mara. Vipi Aweze Kuimarika Bila Kurudi Makosani?
SWALI:
assalaam alykum swala ni mambo gani ambayo natakiwa kufanya ila nisirudie kosa baada ya kutubu, kwani huwa najitahidi kutubu huwenda isipite hata miezi mitatu hurirejea kosa lile lile nililotubu najitahidi kujizuia kwa kubadilsha mazingara lakini bado shetani hunizidi nguvu naomba msaada kuhusiana na hili
JIBU
Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho
.
Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu kurudia katika kosa baada ya kutubia.
Yapo mambo mengi ambayo unaweza kufanya ili kujitenga na maasiya na makosa hayo ambayo unayarudia.
Hakika ni maumbile ya mwanaadamu kurudia kosa baada ya muda. Hata hivyo, inatakiwa ufanye juhudi nyingi za kuweza kutorudia lakini ukikosa inabidi urudi utake msamaha kwake. Ikiwa utaweza kutimiza yale masharti ya kusamehewa basi InshaAllaah Allaah Aliyetukuka Atakusamehe. Jaribu sana utimize masharti yafuatayo:
- Kuacha maasiya.
- Kujuta katika kufanya hayo maasiya.
- Kuazimia kutorudia makosa hayo.
- Ukiwa umemkosea mwanaadamu mwenzako basi uombe msamaha kutoka kwake.
Baada ya kurudia kosa basi utarudia mfumo huo ulio juu katika kuomba msamaha. Ama mambo ambayo yanaweza kukusaidia ili kukupatia kinga ili usirudie makosa hayo kwa kiasi ulicho nacho sasa ni kama yafuatayo:
- Kuifanya Qur-aan kuwa rafiki yako wa karibu sana. Na haitakiwi kuisoma peke yake bali unatakiwa uisome pamoja na kufahamu na kujua maana yake. Na baada ya kujua maana yake kufanya juhudi kutekeleza yaliyo ndani kwa kiasi kikubwa sana.
- Kuifahamu Sunnah ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na kujaribu sana kufuata yale tuliyofundishwa ndani yake.
- Kuyafahamu majina ya Allaah Aliyetukuka na kujua maana ya kila jina pamoja na sifa Zake.
- Kuleta adhkaar za asubuhi na jioni pamoja na adhkaar nyingine ambazo zinapatikana katika viungo vifuatavyo:
Hiswnul-Muslim: Du’aa Na Adhkaar Kusoma Na Kwa Kusikiliza (Toleo Lilohaririwa)
027-Hiswnul-Muslim: Nyiradi Za Asubuhi Na Jioni
- Kufanya urafiki na watu walio Waumini ili kuweza kusaidiana katika kufanya mema na kuacha mabaya.
Kufanya hayo kutatusaidia sana katika kujiepusha na makosa ambayo unayarudia rudia kila wakati.
Na Allaah Anajua zaidi