Kubadilisha Pombe Kuwa Siki Na Siki Iliyobadilishwa Kutoka Pombe Inayouzwa Madukani Nini Hukmu Yake?

SWALI:

Katika kitabu bulughul maram Hadiyth ya 22 mlango wa kuondosha najisi na kuibainisha ……… yasema: 'Mtume s.a.w. aliulizwa kuhusu tembo linapobadilishwa kuwa siki. Akajibu la.' Katika maf-humu yangu ama maelezo zaidi katika subulu salaam (sherhe ya bulugh) yaelezea kwa kirefu na kuna kila aina za maoni. Kwa mfano:


1. Riwaya yakwanza yasema HINI HARAMU KULIBADILISHA TEMBO LIKAWA SIKI.


2. SI HARAMU KUBALIKA LENYEWE IKIWA MHUSIKA HAKUKUSUDIA.
3. MHUSIKA AKIKUSUDIA KUBADILISHA TEMBO LIKAWA SIKI ATAPATA DHAMBI KWA KITENDO LAKINI ILE SIKI HAITAKUWA NAJISI AMA HARAMU KUTUMIWA.

 
Je swala langu liko hapa......?

 
1. IKIWA KWA MUJIBU WA HADIYTH HINI HAIFAI KUBADILISHA TEMBO KUWA SIKI ISIPOKUWA LIBADILIKE LENYEWE. JE HIZI SIKI (MALT VINEGAR) TUNAYONUNUA SUPERMARKET, BILA YA SHAKA ZIMETENGENEZWA KUWA SIKI KWA SABABU YA KUUZWA MADUKANI. JE HUKMU YAKE ITAKUWA VIPI?

 
 NA PILI NIKUWA:

 
2. IKIWA YARUHUSIWA JE MTUME S.A.W. HAKULAANI WATU SAMPULI KADHA (8/ 10 KAMA SIJAKOSA) WANAOSHUHULIKIA TEMBO KUTOKA MNUNUZI MPAKA MTUMIAJI? SASA YULE MWENYE KULI TRANSFORM INTO VINEGAR PIA NAYE ATAKUWA KWENYE KUNDI LA MUEKAJI (PRESERVER)?

 



 

 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu utengenezaji wa siki kutoka kuwa pombe.

 

Kwanza

tunamkumbusha ndugu yetu kuwa na mazoea ya kumswalia Mtume wetu kwa kirefu kikamilifu hata kwenye maandishi, badala ya kutosheka na kufupisha (S.A.W.) kwa kulinda le hadhi na kupata ujira kamili kwa kuitekeleza 'Ibaadah hiyo inavyotakikana.

 

Sasa tuliangalie suala hilo la siki kutoka kwenye Hadiyth na maoni ya wanachuoni.

 

Mwanzo, pombe likibadilika kuwa siki peke yake bila ya mtu kukusudia, siki hiyo itakuwa halali bila tofauti yoyote baina ya wanachuoni wa Fiqhi. Hii ni kauli ya kijumla ya Mtume (Swalla Allaahu ‘Alayhi wa aalihi wa sallam):Kiungo bora ni siki(Muslim, at-Tirmidhiy, Abu Daawuud na an-Nasaa’iy).

 

Ama inapokusudiwa kuibadilisha pombe kuwa siki kwa ima kutia siki yenyewe, kitunguu, chumvi, kuwashia moto au kutia kitu chengine chochote, wanachuoni wametofautiana kuhusu hukmu yake kwa kauli mbili. Nazo ni kama zifuatazo:

 

1-Haifai kubadilisha pombe kuwa siki, na siki hiyo itakuwa haramu: Hii ni kauli ya ‘Umar bin al-Khatwtwaab (Radhiya Allaahu ‘anhu), nayo ndio rai ya wanachuoni wa Imaam ash-Shaafi‘iy na Ahmad bin Hanbal na riwaya ya Imaam Maalik. Hoja zao ni kama zifuatazo:

 

Imepokewa na Anas bn Maalik (Radhiya Allaahu ‘anhuma) kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliulizwa kuhusu utumiaji wa pombe (khamr) kulifanya kuwa siki. Akasema: “Haifai (ni haramu)” (Muslim)..

Anas (Radhiya Allaahu ‘anhu) amemnukuu Abu Twalhah (Radhiya Allaahu ‘anhu) akisema kuwa alimwambia Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘Alayhi wa aalihi wa sallam) amenunua pombe kwa ajili ya mayatima waliokuwa chini ya uangalizi wake, naye akamjibu, “Imwage pombe na yavunje mitungi ya pombe” (at-Tirmidhiy, lakini akasema ni dhaifu).

Katika riwaya ya Abu Daawuud inasema, alimuuliza Mtume (Swalla Allaahu ‘Alayhi wa aalihi wa sallam) kuhusu mayatima waliorithi pombe, naye akasema: “Imwage chini”. Aliuliza kama anaweza kutengeneza siki kutoka kwayo (hiyo pombe). Naye alimjibu: Usifanye hivyo”. Katazo hilo linaashiria kuharamisha...

 

Imepokewa kuwa ‘Umar (Radhiya Allaahu ‘anhu) alipanda Minbar akasema: “Msile siki iliyobadilishwa kutoka pombe mpaka Allaah Aliyetukuka Aibadilishe na hiyo ni pindi inapokuwa siki tamu. Na hakuna tatizo kwa mtu aliyekula siki kutoka kwa watu waliopewa Kitabu maadamu atakuwa hajui kuwa walikusudia kufanya hivyo” (Abu ‘Ubayd).

 

2-Inafaa kubadilisha pombe kuwa siki na siki hiyo inakuwa halali: Na hii ni rai ya wanachuoni wa Hanafiyyah, na rai yenye nguvu kwa wanachuoni wa Maalikiyah. Nayo ni kauli ya Abu Muhammad bin Hazm. Na dalili zao ni:

 

 

Hiyo ni kutengeneza, na kutengeneza kunaruhusiwa kwa kulinganisha (Qiyaas) na kutia rangi ngozi. Kutia rangi ngozi kunaitwaharisha, hivyo kuruhusiwa kuitumia ngozi hiyo.

Hadiyth iliyopokewa marfu‘ kuhusu ngozi ya kondoo aliyekufa:Hakika kuitia rangi kunaihalalisha kama inavyokuwa halali pombe inayogeuzwa kuwa siki(ad-Daraqutwniy, nayo ni dhaifu).

 

Hadiyth iliyopokewa marfu‘: Bora ya siki yenu ni siki iliyogeuzwa kutoka kwa pombe(al-Bayhaqiy, nayo ni dhaifu).

 

Kwa ujumla wa kauli yake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):Kiungo bora ni siki(Muslim, at-Tirmidhiy, Abu Daawuud na an-Nasaa’iy). Hakutofautisha baina ya kuwa siki peke yake na kufanya siki kutoka kwa pombe.  

 

Kutokana na dalili zilizo juu ni wazi kuwa dalili za wenye kuharamisha kubadilisha pombe kuwa siki ni za nguvu zaidi.

 

Hata hivyo, ikiwa mtu atapatiwa hadiya ya siki iliyotengenezwa hakuna tatizo kuitumia kwa sababu ya kuondoka sifa yake mbaya. Pamoja na hilo haifai kwake kununua, kwani kufanya hivyo ni kusaidia uovu. Hakika Allaah Aliyetukuka Amesema:

Na saidianeni katika wema na kumcha Allaah. Wala msisaidiane katika dhambi na uadui. Na mcheni Allaah. Hakika Allaah ni Mkali wa kuadhibu(al-Maaidah [5]: 2).

Na lau itabadilika peke yake hakuna ubaya kununua au kuila kama tulivyotangulia kueleza hilo hapo juu.

 

Ama waliolaaniwa kuhusiana na kulishughulikia pombe/ tembo si 8 bali ni kumi (10). Na kuhusu yule mwenye kuliweka ikiwa ni pombe hasa bila shaka atakuwa na makosa kwani analiwekea kulifanyia nini nalo ni haramu. Hata hivyo, inatakiwa tufahamu kuwa pombe hili hutokana na vitu ambavyo ni tamu navyo vikivunda hubadilika na kuwa pombe. Kwa mfano, pombe tamu la mnazi ni halali lakini ukiliweka huwa pombe kali ambalo ni haramu, nalo hugeuka kwa kuwekwa na kuwa siki. Huenda mtu bila kukusudia kulifanya pombe, hilo lililokuwa tamu likabadilika na kwa hali hiyo huyo hatokuwa amekusudia kulifanya.

Na kadhalika mfano wa zabibu au maji yake ambayo si haramu kuitumia, lakini mtu akaliacha likae hadi ligeuke pombe,hapo itakuwa haramu kuitumia.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

 

Share