Zingatio: Unapotenda Dhambi Omba Tawbah

 

Zingatio: Unapotenda Dhambi Omba Tawbah

 

Naaswir Haamid

 

Alhidaaya.com

 

 

Tawbah ni kuwacha madhambi yote na kujuta kwa kila dhambi Muislamu aliyoifanya, pamoja na kuwa na azma ya kutorudia tena kutenda dhambi hiyo. Wala Muislamu aliyeamini Siku ya Qiyaamah asitosheke na hayo tu, bali aelewe kwamba hana uhakika wa 100% kwamba tawbah yake imekubaliwa ama laa. Hivyo, ni wajibu wake kuendelea kuwa na matarajio tu na unyenyekevu wa hali ya juu.

 

Rabb wetu Mwenye kusamehe madhambi makubwa makubwa na madogo Anatuambia:

 

 يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا تُوبُوا إِلَى اللَّـهِ تَوْبَةً نَّصُوحًا عَسَىٰ رَبُّكُمْ أَن يُكَفِّرَ عَنكُمْ سَيِّئَاتِكُمْ وَيُدْخِلَكُمْ جَنَّاتٍ تَجْرِي مِن تَحْتِهَا الْأَنْهَارُ يَوْمَ لَا يُخْزِي اللَّـهُ النَّبِيَّ وَالَّذِينَ آمَنُوا مَعَهُ ۖ نُورُهُمْ يَسْعَىٰ بَيْنَ أَيْدِيهِمْ وَبِأَيْمَانِهِمْ يَقُولُونَ رَبَّنَا أَتْمِمْ لَنَا نُورَنَا وَاغْفِرْ لَنَا ۖ إِنَّكَ عَلَىٰ كُلِّ شَيْءٍ قَدِيرٌ﴿٨﴾

Enyi walioamini! Tubieni kwa Allaah tawbah ya nasuha (kwelikweli); asaa Rabb   wenu Akakufutieni maovu yenu, na Akakuingizeni Jannaat zipitazo chini yake mito. Siku ambayo Allaah Hatomfedhehesha Nabiy (Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم) na wale walioamini pamoja naye. Nuru yao itatembea mbele yao na kuliani mwao, watasema: Rabb wetu! Tutimizie Nuru yetu, na Tughufurie, hakika Wewe juu ya kila kitu ni Muweza. [At-Tahriym: 8]

 

Hakuna shaka yoyote kwamba nafsi ya mwanaadamu ni yenye kumshawishi mja kuingia kwenye upotofu kwa lengo la kumuasi Rabb wake. Na iwapo mja anajitahidi kutenda mema, basi Ibilisi mkosefu wa Rahmah za Allaah humletea wasi wasi mbaya na kumharibia Ibada zake. Ndio sababu Muislamu anahitajika milele kuwa na hadhari dhidi ya adui yake Ibilisi Maluuni.

 

Kutubia kwa Allaah ni katika sifa njema za Waislamu. Halikadhalika, kwa kuwa Rahmah Zake Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) zipo juu basi Anawakubalia tawbah za waja Wake madhali bado hawajafikia katika mauti:

 وَتُوبُوا إِلَى اللَّـهِ جَمِيعًا أَيُّهَ الْمُؤْمِنُونَ لَعَلَّكُمْ تُفْلِحُونَ ﴿٣١﴾

Na tubuni kwa Allaah nyote, enyi Waumini mpate kufaulu. [An-Nuwr: 31]

 

Pia Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) anasema:

 

"Kwa hakika Allaah Anakubali tawbah ya mja (Wake) madhali bado hajawa katika Sakaratul-Mawt." [Imesimuliwa na Ibn 'Umar na kupokelewa na Imaam At-Tirmidhiy, Ibn Maajah na Ahmad]

 

Tuache ujinga na turudie kwa Allaah(Subhaanahu wa Ta'aalaa). Na kwa sababu gani kiumbe dhaifu umuasi Rabb Aliyekuumba, Alikunyima kitu gani Allaah? Huna shukurani kwa mola wako? Na kama wewe unajiona una nguvu za kumuasi Allaah basi usikae katika Ardhi wala usitembee katika Mbingu Yake, nenda katafute pahala ukae peke yako, au hata usile neema Zake, tafuta riziki yako mwenyewe ule. Hayo yote hutoyaweza, tena WaLlaahi utashindwa, ni muhali kuwa hivyo.

 

Enyi wenye kuchelewesha tawbah kwa kusubiri uzee, mumeweka ahadi gani kwa Rabb wenu kwamba Atawafikisha umri huo? Nini mnachokipata katika kumuasi Allaah?

 

Basi kama unamuhitajia Allaah na unahitajia Rahmah Zake, usimuasi na wala usikate tamaa. Atakaeteleza kisha akarudi kwa Rabb wake kweli kweli na akatenda mema kwa kutaka kulipiza ule wakati alioupoteza katika mambo mabaya, basi huyo hupokelewa tawbah yake.

 

 

Share