Mashairi 1: Inakuja Ramadhani, Viumbe Tuwe Tayari
Mashairi 1: Inakuja Ramadhani, Viumbe Tuwe Tayari
‘Abdallah Bin Eifan (Rahimahu-Allaah)
Bismillahi naanza, salaamu zipokeeni,
Mola Atatuongoza, Atutoe mashakani,
Azidi Kutuongoza, Atunawiri machoni,
Inakuja Ramadhani, viumbe tuwe tayari.
Viumbe tuwe tayari, inakuja Ramadhani,
Tukae tukifikiri, ikija tufanye nini?
Tufanye mengi ya kheri, na tusome Qur-ani,
Inakuja Ramadhani, viumbe tuwe tayari.
Tusipoteze wakati, kuzurura mitaani,
Au kusoma gazeti, asubuhi na jioni,
Au nyumbani kuketi, kuona televisheni,
Inakuja Ramadhani, viumbe tuwe tayari.
Tusibaki kukoroma, kujibwaga vitandani,
Au kwenda kwenye ngoma, mchezo wa mashetani,
Au kwenye masenema, kwenye picha za kigeni,
Inakuja Ramadhani, viumbe tuwe tayari.
Mwezi huo mtukufu, tayari upo njiani,
Kula chakula khafifu, acha nafasi tumboni,
Hapana ubadhirifu, Anaupinga Manani,
Inakuja Ramadhani, viumbe tuwe tayari.
Omba dua omba sana, mwezi huu wa imani,
Fursa kupata tena, hiyo haijulikani,
Leo upo twakuona, kesho upo kaburini,
Inakuja Ramadhani, viumbe tuwe tayari.
Kwenda kucheza karata, ni madhambi ikhwani,
Faida hautopata, ni upuuzi kwa yakini,
Mwisho wake ni matata, na ugomvi barazani,
Inakuja Ramadhani, viumbe tuwe tayari.
Kwenda kufuata mpira, mpaka kule uwanjani,
Jambo hili linakera, zindukeni Waumini,
Wakati unatupora, majuto huja mwishoni,
Inakuja Ramadhani, viumbe tuwe tayari.
Tusigombane na watu, kwa matusi hadharani,
Tazama Mtume wetu, ifikapo Ramadhani,
Huwa mpole wa watu, na mwingi wa ihsani,
Inakuja Ramadhani, viumbe tuwe tayari.
Mwezi mmoja sio mwingi, ndugu zangu kumbukeni,
Mema tufanye kwa wingi, iwe akiba mbeleni,
Tarawihi ni msingi, wa mwezi wa Ramadhani,
Inakuja Ramadhani, viumbe tuwe tayari.
Mola Atupe subira, asitushinde shetani,
Mola Atupe sitara, akhera na duniani,
Tunaomba maghfira, na ridha Za Rahmani,
Inakuja Ramadhani, viumbe tuwe tayari.