Zingatio: Ewe Nafsi Mche Mola Wako

 

Naaswir Haamid


Ewe nafsi mche Mola wako kabla ya kufika mbele ya Hisabu. Utataka ardhi ipasuke ujifukie wala hutaweza, utahitaji kuitenganisha nafsi na umbo lako hutapatiwa nafasi hiyo na wala hutaonja mauti wala uhai. Ni adhabu juu ya adhabu.

 

Nafsi huwezi kuhimili vishindo vya siku hiyo, basi ni kwanini unamuasi Mola wako? Ni kwa neema gani ambayo Mola wako kakunyima? Nafsi tubu kabla ya siku isiyoshikika wala isiyo na msamaha haijakufikia.

 

Nafsi unahadaika na dunia? Ni kwa kipi ambacho kinakuhadaa ndani ya dunia hii? Vyote hivyo ni pumba zitakazokuja kupeperushwa, sio mali wala watoto wako. Nafsi mukhofu Mwenye Kiburi Ambaye Hana kimshindacho. Muogope Mwenye Enzi Ambaye Alikuwepo kabla Yako na Atakuwepo milele kukuchunga wewe na nafsi nyengine. Naye Ndie Ajuaye kuadhibu hakuna mwengine mfano wake. Basi ni kwanini umuasi Mola wako?

 

Ewe nafsi, utakuja kulaumu siku ambayo haitafaa lawama, umshike Ibilisi na akakuruka mita alfu juu. Nafsi tubia kwa Mola wako kabla ya kaburi halijakubinya, mbavu zako za kushoto na kulia zikakutanishwa pamoja!

 

Rehema za Mola zisizo na kifani kutwa zakumurika, nazo ndizo zinazokupelekea kutomuasi Mola wake. Ewe nafsi unapojiweka mbali na rehema hizi, naye Muumbaji Anajiweka mbali na wewe, ni hasara iliyoje kujiweka mbali na rehema za Yule Ambaye nafsi yako imo Mikononi Mwake.

 

Ndani ya Suratu-Yuusuf tunakutana na kisa maarufu cha mke wa Mheshimiwa kumhadaa Nabii Yuusuf, naye mwisho alikiri kwamba nafsi ndiyo iliyompotosha isipokuwa ile ambayo Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Ameirehemu. Tafsiri ya aya hiyo ni kama ifuatavyo:

{{Kwa hakika nafsi ni mno kuamrisha maovu, isipokuwa ile ambayo Mola wangu Aliyoirehemu.}} [Suratu-Yuusuf: 53]

 

Nafsi zote ni zenye kukosa, na mbora wa mwenye kukosa ni yule ambaye atarudi kwa Mola wake. Ikamate nafsi yako na uzungumze nayo asubuhi, mchana na usiku. Hiyo ni nafsi ambayo itakuja kuwa ni adui yako namba moja Siku ya Qiyaamah.

 

Basi elekea kwa Mola wako na muombe msamaha wa makosa ya nafsi yako kama Alivyokufunza kupitia ndani ya Qur-aan na Sunnah ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):

{{Mola wetu! Usituchukulie tukisahau au tukikosea. Mola wetu! Usitubebeshe mzigo kama ulio wabebesha wale waliokuwa kabla yetu. Mola wetu Usitutwike tusiyoyaweza, na Utusamehe, na Utughufirie, na Uturehemu. Wewe Ndiye Mlinzi wetu...}} [Al-Baqarah: 286]

 

((Ee Allaah! Wewe ni Mola wangu, hapana mola Apasaye kuabudiwa kwa haki ila Wewe, Umeniumba mimi na mimi ni mja Wako, nami niko juu ya  ahadi Yako, na agano Lako, kiasi cha uwezo wangu, najilinda Kwako kutokana  na shari ya nilichokifanya, nakiri  Kwako kwa Kunineemesha, na nakiri kwa madhambi yangu, basi nakuomba Unisamehe kwani hasamehe madhambi ila Wewe.))

 

 

Share