Siku Kumi Bora Kabisa Za Allaah - 01 - 10 Dhul-Hijjah

 

Siku Kumi Bora Kabisa Za Allaah:  1 - 10 Dhul-Hijjah

 

Alhidaaya.com

 

Inatupasa tumshukuru Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) kwa neema Aliyotujaalia ya kutuwekea miezi mitukufu, au siku tukufu au nyakati tukufu ambazo ‘amali njema huwa na thawabu nyingi mno. Na hivi tunakaribia kabisa kuingia katika mwezi mwingine mtukufu wa Dhul-Hijjah. Katika mwezi huu, siku kumi za mwanzo ni siku bora kabisa mbele ya Allaah ambazo 'amali yoyote inayotendwa humo ni yenye kupendwa mno na Allaah:     

        

عن ابن عباس رضي الله عنهما، أن النبي صلى الله عليه وسلم قال: ((مَا مِنْ أَيَّامٍ الْعَمَلُ الصَّالِحُ فِيهَا أَحَبُّ إِلَى اللَّهِ مِنْ هَذِهِ الْأَيَّامِ)) يَعْنِي أَيَّامَ الْعَشْرِ قَاُوا:  يَا رَسُولَ اللَّهِ وَلَا الْجِهَادُ فِي سَبِيلِ اللَّهِ؟  قَالَ: ((وَلَا الْجِهَادُ فِي سَبِيلِ اللَّهِ إِلَّا رَجُلٌ خَرَجَ بِنَفْسِهِ وَمَالِهِ فَلَمْ يَرْجِعْ مِنْ ذَلِكَ بِشَيْ)) البخاري

Ibn 'Abbaas (Radhwiya Allaahu 'anhumaa) ameahadithia kwamba Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Hakuna siku ambazo ‘amali njema zinazotendwa humo, zinapendwa mno na Allaah kama (‘amali zinazotendwa katika) siku kumi hizi.” Yaani: Siku kumi za mwanzo wa mwezi wa Dhul-Hijjah. Wakauliza: Ee Rasuli wa Allaah! Je, hata kuliko jihaad katika njia ya Allaah? Akajibu: “Hata Jihaad katika njia ya Allaah isipokuwa mtu aliyetoka (kwenda kupigana jihaad) mwenyewe na mali yake kisha kisirudi chochote katika hivyo.” [Al-Bukhaariy]

 

 

Ee ndugu Muislamu! Usiache fursa hii kukupita kujichumia thawabu tele kutokana na uzito wa malipo katika masiku haya. Hivyo basi tunawanasihi kusoma yafuatayo kuhusu fadhila za masiku haya kumi ya Dhul-Hijjah pamoja na amali za kutenda katika masiku haya matukufu kabisa mbele ya Allaah ('Azza wa Jalla).

 

 

I-Allaah Ameziapia Siku Kumi Hizi:

 

Kwa jinsi zilivyokuwa na umuhimu mkubwa siku hizo kumi, hadi kwamba Allaah (Subhaanah wa Ta'aalaa) Ameziapia katika Qur-aan Anaposema:

بِسْمِ اللّهِ الرَّحْمَنِ الرَّحِيمِ ((وَالْفَجْرِ)) ((وَلَيَالٍ عَشْرٍ))

Kwa Jina la Allaah, Mwingi wa rahmah, Mwenye kurehemu. ((Naapa kwa Alfajiri)) ((Na kwa masiku kumi)) [Al-Fajr: 1-2]

 

Wanachuoni wafasiri wa Qur-aan wamekubaliana kwamba zilokusudiwa hapo ni siku kumi za Dhul-Hijjah.

 

II-Siku Za Manufaa Na Kumdhukuru Allaah:

 

Inapasa kumdhukuru mno Allaah (Subhaanah wa Ta’alaa) kwa kukumbuka neema Zake zisizohesabika kama Anavyosema:

 

((لِيَشْهَدُوا مَنَافِعَ لَهُمْ وَيَذْكُرُوا اسْمَ اللَّهِ فِي أَيَّامٍ مَّعْلُومَاتٍ))

((Ili washuhudie manufaa yao na kulitaja Jina la Allaah katika siku zinazojulikana)) [Al-Hajj: 28]

 

Ibn ‘Abbaas (Radhwiya Allaahu 'anhumaa) kasema: “Hizo ni siku kumi za Dhul-Hijjah.” Na Amesema: “Manufaa ya dunia hii na ya Aakhirah.”  Manufaa ya Aakhirah yanajumuisha kupata radhi za Allaah. Manufaa ya vitu vya dunia inajumuisha wanyama wa kuchinjwa na biashara. [Tafsiyr Ibn Kathiyr]

 

 

III-'Amali Zake Ni Bora Kuliko Kwenda Katika Jihaad Fiy SabiliLLaah:

 

Kutokana na ilivyotajwa katika usimulizi wa Hadiyth ifuatayo, kwamba amali yoyote utendayo katika masiku kumi hayo, ni bora kuliko kwenda kupigana jihaad vitani. Ukizingatia kwenda kupigana jihaad ni jambo zito mtu kuliitikia, kwani huko kuna mashaka mbali mbali, ikiwemo kupoteza mali, khofu ya kujeruhiwa na kupoteza viungo vya mwili, kufariki, n.k. Ila hilo si zito kwa mwenye iymaan ya hali ya juu kabisa kutaka kuyakabili mashaka hayo na kutamani kufa shahidi. Kwa hiyo usidharau ‘amali yoyote hata iwe ndogo vipi itekeleze kwani Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) ni Al-Jawwaad (Mwingi wa Ukarimu), Al-Kariym (Mkarimu), Al-Wahhaab (Mwingi wa kutunuku, Mpaji wa yote), Al-Majiyd (Mwingi mno wa vipawa na ukarimu).

 

عن ابن عباس رضي الله عنهما، أن النبي صلى الله عليه وسلم قال: ((مَا مِنْ أَيَّامٍ الْعَمَلُ الصَّالِحُ فِيهَا أَحَبُّ إِلَى اللَّهِ مِنْ هَذِهِ الْأَيَّامِ)) يَعْنِي أَيَّامَ الْعَشْرِ قَاُوا:  يَا رَسُولَ اللَّهِ وَلَا الْجِهَادُ فِي سَبِيلِ اللَّهِ؟  قَالَ: ((وَلَا الْجِهَادُ فِي سَبِيلِ اللَّهِ إِلَّا رَجُلٌ خَرَجَ بِنَفْسِهِ وَمَالِهِ فَلَمْ يَرْجِعْ مِنْ ذَلِكَ بِشَيْ)) البخاري

Ibn 'Abbaas (Radhwiya Allaahu 'anhumaa) ameahadithia kwamba Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Hakuna siku ambazo ‘amali njema zinazotendwa humo, zinapendwa mno na Allaah kama (‘amali zinazotendwa katika) siku kumi hizi.” Yaani: Siku kumi za mwanzo wa mwezi wa Dhul-Hijjah. Wakauliza: Yaa Rasula-Allaah! Je hata kuliko jihaad katika njia ya Allaah? Akajibu: “Hata Jihaad katika njia ya Allaah isipokuwa mtu aliyetoka (kwenda kupigana jihaad) mwenyewe na mali yake kisha kisirudi chochote katika hivyo.” [Al-Bukhaariy]

 

 

IV-'Ibaadah Zote Zimejumuika Katika Siku Hizi

 

'Ibaadah zote zimejumuika katika siku kumi hizi nazo ni Swalaah, kufunga Swiyaam, Swadaqah, Hajj, wala hazijumuiki pamoja wakati mwingine.

 

 

 

V-‘Amali Za Kutenda Katika Siku Kumi Hizi:

 

 

 

1- Kutekeleza Hajj na 'Umrah (kwa mwenye uwezo):

 

عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ رضي الله عنه أَنَّ رَسُولَ اللهِ صلى الله عليه وسلم قَالَ: ((العُمْرَةُ إِلَى العُمْرَةِ كَفَّارَةٌ لِمَا بَيْنَهُمَا، وَالحَجُّ الـمَبْرُورُ لَيْسَ لَهُ جَزَاءٌ إِلَّا الجَنَّةُ))

Abuu Hurayrah (Radhwiya Allaahu 'anhu) amehadithia kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kasema: “'Umrah hadi 'Umrah hufuta (madhambi) baina yake, na Hajjum-Mabruwr haina jazaa ila Jannah) [Al-Bukhaariy na Muslim]

 

عن أبي هريرة رضي الله عنه قال: "سئل رسول الله صلى الله عليه وسلم: أي الأعمال أفضل؟ قال: ((إيمان بالله ورسـوله)). قيل: ثم مـاذا؟ قال: ((الجهاد في سبيل الله)) قيل: ثم ماذا؟ قال: ((حج مبـرور)) متفق علية

Abuu Hurayrah (Radhwiya Allaahu 'anhu) amehadithia kwamba aliulizwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ‘Amali gani ni bora kabisa? Akasema: “Kumuamini Allaah na Rasuli Wake.” Akaulizwa: Kisha nini? Akasema: “Jihaad katika njia ya Allaah.” Akaulizwa: Kisha nini? Akasema: “Hajj Mabruwr.” [Al-Bukhaariy na Muslim]

 

Bonyeza viungo vifuatavyo upate faida ziyada:

 

Umuhimu Wa Kukimbilia Kutekeleza Nguzo Ya Hajj

 

Fadhila Za ‘Umrah Na Hajj - Kutoka Kitabu: Alhidaaya Katika Manaasik Za Hajj Na 'Umrah

 

 

 

2- Kuomba Tawbah ya kweli na kujiepusha na maasi:

 

Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

(( يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا تُوبُوا إِلَى اللَّهِ تَوْبَةً نَّصُوحًا))

((Enyi walioamini! Tubuni kwa Allaah tawbah iliyo ya kweli!)) [At-Tahriym: 8]

 

Na Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ametupa matumaini makubwa ya kufutiwa madhambi na makosa yetu katika usimulizi ufuatao:

 

 عن أَنَسُ بْنُ مَالِكٍ قَالَ: سَمِعْتُ رَسُولَ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ يَقُولُ: ((قَالَ اللَّهُ تَبَارَكَ وَتَعَالَى يَا ابْنَ آدَمَ،  إِنَّكَ مَا دَعَوْتَنِي وَرَجَوْتَنِي غَفَرْتُ لَكَ عَلَى مَا كَانَ فِيكَ وَلَا أُبَالِي، يَا ابْنَ آدَمَ لَوْ بَلَغَتْ ذُنُوبُكَ عَنَانَ السَّمَاءِ ثُمَّ اسْتَغْفَرْتَنِي غَفَرْتُ لَكَ وَلَا أُبَالِي، يَا ابْنَ آدَمَ إِنَّكَ لَوْ أَتَيْتَنِي بِقُرَابِ الْأَرْضِ خَطَايَا ثُمَّ لَقِيتَنِي لَا تُشْرِكُ بِي شَيْئًا لَأَتَيْتُكَ بِقُرَابِهَا مَغْفِرَةً))    

Anas (Radhwiya Allaahu 'anhu) amehadithia kwamba: Nimemsikia Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akisema: “Allaah (Tabaaraka wa Ta’aalaa) Amesema: Ee bin-Aadam! Hakika ukiniomba na ukanitaraji (kwa malipo) Nitakughufuria yale yote uliyonayo na wala Sijali, Ee bin-Aadam! Lau zingefikia dhambi zako ukubwa wa mbingu, kisha ukaniomba maghfirah, Ningekughufuria bila ya kujali (kiasi cha madhambi uliyoyafanya). Ee bin-Aadam! Hakika ungenijia na madhambi yakaribiayo ukubwa wa ardhi, kisha ukakutana nami na hali hukunishirikisha chochote, basi Nami Nitakujia na maghfirah yanayolinga nayo.” [At-Tirmidhiy na Shaykh Al-Albaaniy kaipa daraja ya Hasan]

 

Bonyeza kiungo kifuatacho upate faida ziyada:

 

Tawbah: Hukmu Na Fadhila Zake

 

 

3-Kumdhukuru Mno Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

Kwa kuleta Takbiyrah  kuanzia unapoandama mwezi wa dhul-Hijjah mpaka mwisho wa Ayyaamut-Tashriyq (Yaani tarehe 13 Dhul-Hijjah) baada ya Swalaatul-'Asr ndio kumalizika kwake. Dalili ni zifuatazo:  Kauli ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

لِّيَشْهَدُوا مَنَافِعَ لَهُمْ وَيَذْكُرُوا اسْمَ اللَّـهِ فِي أَيَّامٍ مَّعْلُومَاتٍ عَلَىٰ مَا رَزَقَهُم مِّن بَهِيمَةِ الْأَنْعَامِ ۖ

 ((Ili washuhudie manufaa yao; na walitaje Jina la Allaah katika siku maalumu kwa yale Aliyowaruzuku kati ya wanyama wenye miguu minne wa mifugo.    [Al-Hajj  28]

 

Na pia Hadiyth:

 

كَانَ إبْن عَمَر وَأبُو هُرَيْرَةَ رَضِيَ اللَّه عَنْهُما يَخْرُجَانِ إِلَى السُّوقِ فِي أَيَّامِ العَشْرِ يُكَبِّرَانِ، وَيُكَبِّرُ النَّاسُ بِتَكْبِيرِهِمَا

Ibn 'Umar na Abuu Hurayrah (Radhwiya Allaahu 'anhumaa) walikuwa wakienda sokoni katika siku kumi (za Dhul-Hijjah) na kutamka Takbiyr kwa sauti na watu wakiwaigiza. [Al-Bukhaariy]

 

Na Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

وَاذْكُرُوا اللَّـهَ فِي أَيَّامٍ مَّعْدُودَاتٍ ۚ

Na mdhukuruni Allaah katika siku za kuhesabika.  [Al-Baqarah: 203]

 

Ibn 'Abbaas (Radhwiya Allaahu 'anhumaa) amesema: "Siku za kuhesabika ni siku za tashriyq (11, 12, 13 Dhul-Hijjah) na siku maalumu ni siku za kumi za mwanzo za Dhul-Hijjah." [Al-Qurtwubiy: 3.3]

 

Mdhukuru Allaah Ta'aalaa zaidi kwa Tasbiyh, Tahmiyd, Tahliyl, Takbiyr: Maana yake ni: kusema: Subhaana Allaah, AlhamduliLLaah, laa Ilaaha illa Allaah, Allaahu Akbar.

 

Takbiyr katika masiku haya matukufu ni aina mbili:[1]

 

 

A)  Takbiyr Al-Mutwlaq: Za Nyakati Zote:

 

Takbiyr wakati wote mchana na usiku, mahali popote ulipo, tokea unapoingia mwezi wa Dhul-Hijjah na inaendelea mpaka siku ya mwisho ya Tashriyq (tarehe 13 Dhul-Hijjah) na kumalizika baada ya kuingia Magharibi.

 

B)  Takbiyr Al-Muqayyad: Za Kuthibitika Mahali Maalumu Na Nyakati Maalumu, Za Kukadirika:

 

Takbiyr baada ya kila Swalaah za fardhi na huanza baada ya Swalaah ya Alfajiri Siku ya 'Arafah mpaka mpaka baada ya Swalaah ya Alasiri siku ya mwisho ya Tashriyq (tarehe 13 Dhul-Hijjah).

 

 

Inavyopasa kufanya Takbiyr:

 

 اللَّهُ أَكْبَرُ، اللَّهُ أَكْبَرُ،  لاَ إِلَهَ إِلاَّ اللَّهُ، اللَّهُ أَكْبَرُ، اللَّهُ أَكْبَرُ، وَلِلَّهِ الْحَمْد

Allaahu Akbar, Allaahu Akbar, laa Ilaaha illa Allaah, Allaahu Akbar Allaahu Akbar WaliLLaahil-Hamd

 

 

Bonyeza Upate Takbiyrah Ya Sauti:

 

 

 

4- Kufufua Sunnah ya Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam):

 

Wanaume wanatakiwa waseme kwa sauti ili kuwakumbusha wengine na wanawake waseme kimya kimya isipokuwa wakiwa na mahaarim wao. Kufufua Sunnah ya Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ni muhimu kwa sababu bila ya kufanya hivyo ni kukosa fadhila zake, na pia ni kupoteza Sunnah za kipenzi chetu Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam).

 

مَنْ سَنَّ فِي الْإِسْلَامِ سُنَّةً حَسَنَةً فَعُمِلَ بِهَا بَعْدَهُ كُتِبَ لَهُ مِثْلُ أَجْرِ مَنْ عَمِلَ بِهَا ، وَلَا يَنْقُصُ مِنْ أُجُورِهِمْ شَيْءٌ .

Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kasema: “Atakayefufua tendo jema katika Uislaam na watu wakalitenda baada yake, basi ataandikiwa ujira sawa na yule atakayelitenda, na hakipungui chochote katika ujira wao.  [Muslim]

 

 

 

5- Kufunga Swiyaam siku hizi khaswa siku ya 'Arafah:

 

Kufunga Swiyaam siku hii ni kufutiwa madhambi ya miaka miwili:

 

 عَنْ أَبِي قَتَادَةَ رضي الله عنه أن النَّبِيَّ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ قَالَ: ((صِيَامُ يَوْمِ عَرَفَةَ أَحْتَسِبُ عَلَى اللَّهِ أَنْ يُكَفِّرَ السَّنَةَ الَّتِي قَبْلَهُ وَالسَّنَةَ الَّتِي بَعْدَهُ )) أخرجه مسلم

Abuu Qataadah (Radhwiya Allaahu 'anhu) amehadithia kwamba: Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kasema: “Swawm ya 'Arafah nataraji (kwa Allaah) kufuta madhambi ya mwaka uliopita na wa baada yake.” [Muslim]

 

Swawm inamweka mtu mbali na Moto.

 عَنْ أَبِي سَعِيدٍ الْخُدْرِيِّ رضي الله عنه قَالَ : قَالَ رَسُو

لُ اللَّهِ صلى الله عليه وسلم : مَنْ صَامَ يَوْماً فِي سَبِيلِ اللَّهِ بَعَّدَ اللَّهُ وَجْهَهُ عَنْ النَّارِ سَبْعِينَ خَرِيفًا.

Abuu Sa'iyd Al-Khudhwriyy (Radhwiya Allaahu 'anhu) amehadithia kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Atakayefunga Swiyaam siku moja kwa ajili ya Allaah, Allaah Atauweka  uso wake mbali na moto masafa ya miaka sabiini.” [Al-Bukhaariy na Muslim]

 

 

Na Swawm ina thawabu maradufu.

 

عنْ أَبِي هُرَيْرَةَ رَضِيَ اللَّهُ عَنْهُ قَالَ: قَالَ رَسُولُ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ: ((كُلُّ عَمَلِ ابْنِ آدَمَ يُضَاعَفُ الْحَسَنَةُ عَشْرُ أَمْثَالِهَا إِلَى سَبْعمِائَة ضِعْفٍ قَالَ اللَّهُ عَزَّ وَجَلَّ إِلَّا الصَّوْمَ فَإِنَّهُ لِي وَأَنَا أَجْزِي بِهِ يَدَعُ شَهْوَتَهُ وَطَعَامَهُ مِنْ أَجْلِي لِلصَّائِمِ فَرْحَتَانِ فَرْحَةٌ عِنْدَ فِطْرِهِ وَفَرْحَةٌ عِنْدَ لِقَاءِ رَبِّهِ وَلَخُلُوفُ فِيهِ أَطْيَبُ عِنْدَ اللَّهِ مِنْ رِيحِ الْمِسْكِ))

Abuu Hurayrah (Radhwiya Allaahu ‘anhu) amehadithia kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam): “Kila 'amali njema ya mwanaadamu inalipwa mara kumi na inaongezewa thawabu kutoka kumi hadi mia saba, na Allaah (‘Azza wa Jalla) Anasema: Isipokuwa Swawm, kwani hiyo ni kwa ajili Yangu na Mimi Ndiye Nitakayemlipa. Ameacha matamanio yake na chakula chake kwa ajili Yangu. Kwa aliyefunga Swawm atapata furaha mbili; furaha anapofuturu na furaha atakapoonana na Rabb wake, harufu inayotoka kinywani mwa aliyefunga ni nzuri mbele ya Allaah kuliko harufu ya misk.” [Muslim na Ahmad]

 

Bonyeza kiungo kifuatacho upate fadhila za Swiyaam:

 

Fadhila Za Swiyaam Za Fardhi Na Za Sunnah

 

 

6- Kuzidisha ‘amali njema mbali mbali:

 

Kuanzia kuswali Swalaah za fardhi kwa wakati wake kisha kuswali Swalaah za Sunnah, kusoma Qur-aan, kutoa swadaqah, kuomba du’aa kwa wingi, kutii wazazi na kuwafanyia wema, kuwasiliana na jamaa (kuunga undugu), kuwafanyia wema jirani, kuamrishana mema na kukatazana maovu, kufanyiana wema na ihsani na kadhalika.

 

 

 

7- Kuchinja baada ya Swalaah ya 'Iyd:

 

Anasema Allaah (Subhaanahu Wa Ta'aalaa):

((فَصَلِّ لِرَبِّكَ وَانْحَرْ))

((Basi Swali kwa ajili ya Rabb wako na uchinje)) [Al-Kawthar: 2]

 

 

Na usimulizi ufuatao tunapata maelezo ya aina ya mnyama wa kuchinja na uchinjaji wake. 

 

 

فعَنْ أَنَسٍ رضي الله عنه قَالَ: ضَحَّى النَّبِيُّ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ بِكَبْشَيْنِ أَمْلَحَيْنِ أَقْرَنَيْنِ ذَبَحَهُمَا بِيَدِهِ وَسَمَّى وَكَبَّرَ وَوَضَعَ رِجْلَهُ عَلَى صِفَاحِهِمَا  متفق عليه

Anas (Radhwiya Allaahu 'anhu) amehadithia kwamba: Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alichinja kondoo wawili weupe* wenye pembe, amewachinja kwa mikono yake, akasema BismiLLaah na Allaahu Akbar na akaweka mguu wake upande wa nyuma yao. [Al-Bukhaariy na Muslim]

 

*Baadhi ya Wanachuoni wamesema kuwa ni weupe ulio na alama nyeusi, wengine wamesema uliochanganyika na wekundu.

 

‘Amali hii ya kuchinja ni 'ibaadah tukufu na ni Sunnah iliyosisitizwa hata wanachuoni wameona kuwa ni waajib kwa kila aliyekuwa na uwezo wa kuchinja.

 

 

Yanayompasa kufanya mwenye kutaka kuchinja:

 

Baada ya kutia niyyah ya kuchinja, asikate mtu nywele wala kucha mpaka amalize kuchinja kama tulivyoamrishwa katika Hadiyth ifuatayo:

 

 

 عن أم سلمة رضي الله عنها، أن النبي صلى الله عليه وسلم قال: (((ِذَا رَأَيْتُمْ هِلَالَ ذِي الْحِجَّةِ وَأَرَادَ أَحَدُكُمْ أَنْ يُضَحِّيَ ، فَلْيُمْسِكْ عَنْ شَعْرِهِ وَأَظْفَارِهِ))) وفي راوية: ((فَلَا يَأْخُذْ مِنْ شَعْرِهِ وَلَا مِنْ أَظْفَارِهِ شَيْئًا، حَتَّى يُضَحِّيَ)) مسلم

Ummu Salamah (Radhwiya Allaahu 'anhaa) amehadithia kwamba Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Mtakapoona mwezi umeandama wa Dhul-Hijjah na ikiwa yuko anayetaka kuchinja basi azuie (asikate) nywele zake na kucha zake).” [Muslim na wengineo] Na katika riwaayah nyengine: "Asikate nywele wala kucha mpaka akimaliza kuchinja."

 

Hii ni fadhila na neema kwetu maana tunakuwa kama vile tumo katika ihraam ndogo kama vile wanavyokuwa Mahujaji katika ihraam zao, ingawa ihraam zao zimeshurutishwa kwa kuharamishwa mambo mengineyo.  Ikiwa amesahau mtu, mfano akakata kucha basi aendelee tu na niyyah yake mpaka amalize kuchinja.

 

Bonyeza kiungo kifuatacho upate faida ziyada:

 

Kuchinja - Fadhila, Hikmah Na Hukmu Zake

 

 

8- Kuhudhuria Swalaah ya 'Iyd:

 

Kwenda kuswali Swalaah ya ‘Iyd ni jambo lilosisitizwa mno na Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam). Lakini Waislaam wengi wamepuuza ‘amali hii na hali Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amehimiza mpaka wanawake walio katika hedhi na wazee waende kusikiliza khutbah ya Swalaah. Wakati wa Swalah ukifika, wanawake hao wenye hedhi wajitenge kando hadi itakapomalizika Swalaah na kisha wajiunge na wenzao kusikiliza khutbah.

 

 

 

9-‘Amali za Kutenda Siku Ya ‘Arafah Ambayo Ni Siku  Ya Tisa Dhul-Hijjah

 

a) Mwenye kufunga Swawm, atafutiwa madhambi ya miaka miwili!  

 

Siku hii tukufu ni siku iliyokamilika Dini yetu. Thawabu za kufunga siku hii ni kufutiwa madhambi ya miaka miwili.

عَنْ أَبِي قَتَادَةَ رضي الله عنه أن النَّبِيَّ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ قَالَ: ((صِيَامُ يَوْمِ عَرَفَةَ أَحْتَسِبُ عَلَى اللَّهِ أَنْ يُكَفِّرَ السَّنَةَ الَّتِي قَبْلَهُ وَالسَّنَةَ الَّتِي بَعْدَهُ )) أخرجه مسلم

Abuu Qataadah (Radhwiya Allaahu 'anhu) amehadithia kwamba Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Swawm ya 'Arafah, nataraji kwa Allaah kuwa afute madhambi ya mwaka uliopita na wa baada yake.” [Muslim]

 

b) Siku ambayo huachiliwa watu wengi huru kutokana na moto

 

 عَنْ عَائِشَةَ (رضي الله عنها)  أَنَّ رَسُولَ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ قَالَ: ((مَا عَمِلَ آدَمِيٌّ مِنْ عَمَلٍ يَوْمَ النَّحْرِ أَحَبَّ إِلَى اللَّهِ مِنْ إِهْرَاقِ الدَّمِ, إِنَّهَا لَتَأْتِي يَوْمَ الْقِيَامَةِ بِقُرُونِهَا, وَأَشْعَارِهَا, وَأَظْلَافِهَا وَأَنَّ الدَّمَ لَيَقَعُ مِنْ اللَّهِ بِمَكَانٍ قَبْلَ أَنْ يَقَعَ مِنْ الْأَرْضِ فَطِيبُوا بِهَا نَفْسًا))

Mama wa Waumini, 'Aaishah (Radhwiya Allaahu 'anhaa) amehadithia kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Hakuna kitendo cha bin Aadam kilichokuwa ni kipenzi kabisa kwa Allaah siku ya kuchinja kama kumwaga damu. Atakuja (huyo mnyama) siku ya Qiyaamah na pembe zake, kucha zake na nywele zake. Damu yake itamwagika mahali fulani Allaah Anapajua kabla ya kumwagika katika ardhi. Hivyo zipendezesheni nafsi kwayo.” [At-Tirmidhiy, Sunan Ibn Maajah]

 

Na alipoulizwa Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam):

 

مَا هَذِهِ الْأَضَاحِيُّ؟  قَالَ: ((سُنَّةُ أَبِيكُمْ إِبْرَاهِيمَ)) قَالُوا: فَمَا لَنَا فِيهَا يَا رَسُولَ اللَّهِ؟ قَالَ: ((بِكُلِّ شَعَرَةٍ حَسَنَةٌ)) قَالُوا: فَالصُّوفُ يَا رَسُولَ اللَّهِ؟  قَالَ: ((بِكُلِّ شَعَرَةٍ مِنْ الصُّوفِ حَسَنَةٌ))

Nini hivi vichinjo? Akajibu: “Ni Sunnah ya baba yenu Ibraahiym.”. Wakasema, "Nini umuhimu wake kwetu?” Akasema: “Katika kila unywele kuna jema moja.” Wakasema: Na sufi? Akasema: “Katika kila unywele wa sufi kuna jema moja.” [Ahmad, Ibn Maajah]

 

 

c) Du'aa bora kabisa ni Du'aa katika siku ya 'Arafah

 

 

Inapasa kumdhukuru mno Allaah siku hii kama alivyosema Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kuwa:

 

((خَيْرُ الدُّعَاءِ دُعَاءُ يَوْمِ عَرَفَةَ، وخَيْرُ مَا قُلْتُ أنَا وَالنَّبيُّونَ مِنْ قَبْـلِي: لَا إِلَهَ إِلاَّ اللهُ وَحْدَهُ لا شَرِيْكَ لَهُ، لَهُ الـمُلْكُ، ولَهُ الـحَمْدُ، وَهُوَ عَلَى كُلِّ شَيءٍ قَدِير)) روى الترمذي

“Du’aa bora kabisa ni du’aa katika siku ya 'Arafah, na yaliyo bora kabisa niliyosema mimi na Manabii kabla yangu ni:

 

 

Laa Ilaaha illa Allaah Wahdahu laa shariyka Lahu, Lahul-Mulku Walahul-Hamdu wa Huwa 'alaa kulli shay-in Qadiyr. [At-Tirmidhiy]

 

Bonyeza kiungo kifuatacho upate faida ziyada:

 

Fadhila Za Siku Ya 'Arafah Na Yawmun-Nahr (Siku Ya Kuchinja)

 

 

10-Amali Za Kutenda Siku Ya Kuchinja Ambayo Ni Sikukuu Ya ‘Iyd

 

Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

((إِنَّ أعظمَ الأيامِ عندَ اللهِ تباركَ وتعالى يومُ النَّحْرِ ، ثمَّ يَومُ القَّرِّ)) سنن أبي داود

“Siku iliyo tukufu kabisa kwa Allaah ni siku ya kuchinja, kisha siku ya kutulia.” (yaani siku ya kukaa Minaa) [Sunan Abi  Daawuwd]

 

Kadhalika hii ni Sikukuu ya pili ya Waislamu, inapaswa siku hii kwenda kuswali Swalaah ya 'Iyd, kuamkiana na Waislamu, kuunga undugu kwa kuwatembelea na kuwasiliana nao kwa njia mbalimbali, kupeana zawadi khasa kuwapa watoto,  kula na kunywa na kufurahi kwa kila aina za starehe zinazoruhusika kishariy'ah. 

 

 

Pia bonyeza viungo vifuatavyo upate faida nyenginezo za 'amali za kutenda katika Siku hii tukufu ya 'Iydul-Adhwhaa na mambo ya kujiepusha nayo:

 

'Iyd Al-Fitwr: Yaliyo Sunnah Kutekelezwa

 

 

'Iyd - Yaliyo Ya Sunnah Na Yaliyo Bid'ah Katika Sherehe Za 'Iyd

 

 

 

Wa biLLaahi At-Tawfiyq

 

 

[1] Takbiyr hizo za masiku haya matukufu zimetekelezwa na baadhi ya Maswahaba watukufu na ni Mustahabb (imependekezwa) na wengi katika Salaf wa madhehebu ya Hanbaliy, Ash-Shaafi’iyy, Hanafiy na wengineo kama ifuatavyo:  

Imaam An-Nawawiy - Al-Majmuw’ (5/32).

Ibn Rajab - Fat-hul-Baariy (6/125, 130).

Ibn Taymiyyah - Majmuw’ Al-Fataawaa (24/220. 222).

Imaam Ibn Baaz - Fataawaa Nuwr ‘Alad-Darb (13/355).

Imaam Ibn ‘Uthaymiyn - Ash-Sharh Al-Mumti’ (5/166), Majmuw’ Fataawaa wa Rasaail Al-‘Uthyamiyn (16/262, 265).

 

 

Share