Kuchukua Video Kwenye Maharusi

 

Kuchukua Video Kwenye Maharusi

 

Alhidaaya.com 

 

 

Swali:

 

Assalaam Aleikum,

Je inafaa kufanya kazi ya kupiga video maharusi au sherehe zinazo husisha wanawake kuto kujisitiri kulingana na sheria ya kislamu. Naomba Muongozo.

 

 

Jibu:

 

AlhamduliLLaah - Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

 

Asli katika upigaji picha iwe ya kawaida au hata ya video ni haramu isipokuwa picha za dharura kama vile picha za passport na zenye kufanana na hilo kulingana na dharura iliyopo au itakayokuwepo; na harusi si jambo la dharura wala haliwezi kuingia katika dharura kwa hali yoyote ile na pia maziko ambayo yamekuwa yakichukuliwa kwa video.

 

Ingia kwenye viungo vifuatavyo uweze kusoma kuhusu hukmu ya picha:

 

Hukmu Ya Kuchora Au Kupiga Picha Za Viumbe Vyenye Roho

 

Malaika Hawaingii Nyumba Iliyotundikwa Picha Za Familia?

 

Kuweka Picha Katika Album

 

Muislamu hatarajiwi kuwa kazi yake ya kumpatia riziki ya halali kuwa ni kazi yenye uharamu zaidi kuliko uhalali.

 

Haijuzu kwa hali yoyote ile kuwachukua video au kuwapiga picha maharusi au kumfunua biharusi mbele ya waliohudhuria sherehe ya harusi hata akiwa na mumewe pamoja naye; bali inalazimika kwa biharusi kujisitiri na kuwa mbali na wanaume wasiokuwa maharimu wake na hasa hasa ‘masheikh’ wenye kudai kuwa wanaingia chumbani kumsomea du’aa na wale wenye kujipachika jina la ‘best man’.

 

Pia haijuzu kuwachukua picha wanawake waliohudhuria sherehe ya harusi au nyenginezo wawe wamejisitiri au vyenginevyo hali zote ni sawa sawa.

 

Ikiwa hali ndio kama hii basi mchukuaji picha au video huwa yuko hatarini kwa kazi yake kwani huwa bila ya shaka yoyote ile anafanya haramu; haramu yenyewe ina vipengele vingi baadhi yake ni kama hivi:

 

Uharamu wa kumuangalia mwanamke/wanawake asiye/wasiokuwa maharimu wake kwa macho yako ya kawaida tena kwa makusudi achilia mbali wakati huo huwa anatumia kifaa chenye uwezo wa kumvuta karibu na kumuona mengi zaidi usiyoweza kuyaona kwa macho yako.

 

Na isitoshe wenye kufanya hivyo, huenda kwenye studio zao, au majumbani kwao na kuzitengeneza na kuziunganisha hizo video, huku wakizitazama na wanaume wengine wasio Mahram wa hao wanaotazamwa, na zaidi pia, huenezwa video hizo sehemu mbalimbali wakaona wengi na fitna ikatapakaa na uovu kuzidi.

 

Qur-aan inasema:

قُل لِّلْمُؤْمِنِينَ يَغُضُّوا مِنْ أَبْصَارِهِمْ وَيَحْفَظُوا فُرُوجَهُمْ ۚ

Waambie Waumini wanaume wainamishe macho yao na wahifadhi tupu zao. Hivyo ni utakaso zaidi kwao. [An-Nuwr: 30]. 

 

Uharamu wa kuchanganyika yeye na wanawake wasio maharimu zake hata kama mchukuaji atakuwa ni baradhuli basi huyo ni hatari zaidi.

 

Uharamu wa kuwa utakuwa unafanya yaliyokatazwa wazi na kujichumia majidhambi bila ya wewe kuelewa na kufanya tendo hilo; kwani hata kama utakuwa umemaliza kazi basi dhambi huwa zinaendelea bila ya kusita na huenda mpaka utubie au hiyo video iharibike; kwani utakuwa kama huyu aliyetajwa katika Hadiyth hii ya Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

“Atakayefufua tendo jema katika Uislaam na watu wakalitenda baada yake, basi ataandikiwa ujira sawa na yule atakayelitenda, na hakipungui chochote katika ujira wao. Na atakayebuni kitendo kibaya katika Uislamu na watu wakakifanya baada yake, basi ataandikiwa dhambi sawa na yule atakayekifanya, na wala hakipungui chochote katika madhambi yao.” [Muslim]  

 

Uharamu wa kujichukulia nasibu yako -sehemu- yako katika zinaa; kwani Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

"Hakika Allaah (‘Azza wa Jalla) amemuandikia mtoto wa Aadam fungu lake katika zinaa ambalo halikwepeki, jicho linazini na zinaa yake ni kuangalia, na ulimi unazini zinaa yake ni kutamka, na nafsi zinaa yake ni kutamani, na kadhalika utupu husadikisha au hukanusha...)) [Imepokelewa na Al-Bukhaariy, kitabu cha ‘Idhni’. Mlango wa ‘Zinaa ya viungo visivyokuwa utupu/uchi.’]

 

Ameanza na zinaa ya jicho na wewe ndio kazi yako ya kila siku au karibu kila pakiwa na harusi au sherehe ze mchanganyiko; na wewe huwa katika makuwadi -samahani sio neno zuri lakini hakuna jengine zaidi ya hilo kwani wanaume wenye kutazama hiyo/hizo video huwa ushawafanyia kazi kubwa na kuwafanyia wepesi wa kuwaangalia wanawake; bila ya video yako wasingepata wepesi huo kwani wengine huwa hawaonekani isipokuwa katika video zako.

 

Hivyo, hiyo sio kazi ya kufanya, ni kazi yenye uharamu na ufisadi mwingi, jaribu kujiepusha nayo na kuomba maghfirah kwa yaliyopita na kutafuta kazi nzuri ya halali kuifanya.

 

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share