Khawaarij

 

 

Khawaarij

 

Muhammad Faraj Saalim As-Sa'iy (Rahimahu Allaah)

 

Alhidaaya.com

 

 

 

Yaliyomo:

 

 

Nani Khawaarij

 

Mwanzo Wao

 

‘Uthmaan Anabashiriwa Jannah

 

Kundi La Khawaarij

 

Mapatano

 

Baada Ya Makubaliano

 

Hapana Hukmu Isipokuwa Ya Allaah

 

Kisa Cha Kuuliwa Kwa ‘Abdullaah Bin Khubaab

 

Kisa Cha Waasil Bin ‘Atwaa

 

Nahraawan

 

Vita Vya Nahrawaan

 

Kuuliwa Kwa ‘Aliy (Radhwiya Allaahu ‘anhu)

 

Itikadi (‘Aqiydah) Ya Khawaarij

 

Makundi Ya Khawaarij

 

Ibadhi

 

 

 

Mwanzo Wao

Kundi hili lilianza pamoja na Shia, na makundi yote mawili yalijitokeza kwa nguvu wakati wa vita vya wenyewe kwa wenyewe baina ya majeshi ya ‘Aliy na Mu'aawiyah (Radhwiya Allaahu ‘anhum) katika mji wa Swiffiyn, na wengi kati ya wafuasi wa makundi haya walijiunga na majeshi ya ‘Aliy (Radhwiya Allaahu ‘anhu), baada ya kumuuua ‘Uthmaan bin ‘Affaan (Radhwiya Allaahu ‘anhu) Khalifa wa tatu wa Waislamu kisha wakakimbilia Basra na huko wakajiunga na jeshi la ‘Aliy (Radhwiya Allaahu ‘anhu).

 

 

Wakati wa utawala wa ‘Uthmaan bin ‘Affaan (Radhwiya Allaahu ‘anhu) watu hawa walikuwa wakimtuhumu kuwa alikuwa akiwapa vyeo watu wa kabila lake na jamaa zake, kisha wakawa wanamlaumu kuwa anawakinga baadhi ya jamaa zake wenye kutenda makosa, kisha wakawa wanamtuhumu yeye mwenyewe juu ya Uislamu wake, kisha watu hawa hawa wakamuua ‘Uthmaan kwa dhulma na uadui, na hapo ndipo ulipofunguka mlango wa fitna, na uadui mkubwa baina ya Waislamu wenyewe kwa wenyewe ukaanza.

 

 

 ‘Uthmaan Anabashiriwa Jannah

‘Uthmaan (Radhwiya Allaahu ‘anhu) alikuwa Khalifa wa tatu muongofu wa Waislamu ‘Aliyebashiriwa mara nyingi na Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) kuwa ataingia Peponi.

 

 

Nitazitaja hapa chini hadithi mbili tu:

Katika hadithi ndefu iliyosimuliwa na Abu Muwsaa Al-Ash’ariy (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kuwa siku moja Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) aliingia katika bustani yenye kisima kilichozungushiwa ukuta. na Abu Muusa alikuwa mlinzi, akasema:

 

 

"‘Uthmaan bin ‘Affaan akagonga mlango. Nikamwambia; “Subiri hapo ulipo, usiingie mpaka kwanza nimjulishe Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam)”.

 

 

Nilipomjulisha, Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) akanyamaza muda kidogo, kisha akaniambia:

 

 

“Mruhusu aingie na mpe biashara ya kuingia Peponi baada ya kupambana na mtihani mkubwa”.

 

 

‘Uthmaan akasema:

AAllaahul Musta’aan”, (na katika riwaya nyingine alisema: “Tutakuwa wenye subira In shaa Allaah”).[Al-Bukhaariy]

 

 

Kutoka kwa Murrah bin Ka’ab (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kuwa amesema:

"Nilimsikia Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akihadithia juu ya fitan, akapita mtu mbele yake ‘Aliyejifunika uso. Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) akasema:

 

 

"Mtu huyu siku hiyo atakuwa juu ya uongofu."

 

 

Nikainuka na kumfuata na mtu yule alikuwa ‘Uthmaan bin ‘Affaan. Nikamgeuza uso wake na kumuuliza: "Ni huyu?" akaniambia. "Ndiye."

Imaam Ahmad na At-Tirmidhiy na An-Nasaaiy na Al-Haakim katika Mustadrak na wengine.

 

 

Kundi La Khawaarij

Kundi la Khawaarij lilianza pale vita vya Swiffiyn vilipozidi ukali na Mu’aawiyah (Radhwiya Allaahu ‘anhu) akawataka watu wake wanyanyue juu Misahafu na kulitaka jeshi la ‘Aliy (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kuacha vita na badala yake wahukumiane kwa mujibu wa Qur-aan Tukufu.

 

 

‘Aliy (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kwanza alikataa na kushikilia kuwa jeshi lake liendelee kupigana mpaka ushindi upatikane, lakini ndani ya jeshi lake kundi moja lilitishia kujitenga na kumtaka ‘Aliy akubali hukumu ya mujibu wa Qur-aan, na hatimaye baada ya kushikiliwa sana, ‘Aliy akakubali kwa kulazimika siyo kwa kuridhika, baada ya kuambiwa:

 

 

"Ee ‘Aliy, unapoitwa katika kitabu cha Allaah itikia, ama sivyo tutakufanyia yale yale tuliyomfanyia ‘Uthmaan bin ‘Affaan, kwa sababu yeye pia alikataa kuitikia alipotakiwa ahukumu kwa kitabu cha Allaah na sisi tukamuuwa".

 

 

Baada ya vita kusimama, pande zote mbili zilikubaliana kuwa hukumu itolewe na watu wawili watakaochaguliwa moja kutoka katika kundi la ‘Aliy na mwengine kutoka kundi la Mu'aawiyah.

 

 

Upande wa Mu'aawiyah alichaguliwa ‘Amr bin al-’Aas, na ‘Aliy alitaka kumchagua Ibn ‘Abbaas lakini wale waliojitenga walikataa wakataka achaguliwe Abu Muwsaa al Ash' ary (Radhwiya Allaahu ‘anhum jamiyan).

 

 

Abu Muwsaa alijitoa katika vita hivyo tokea mwanzo baada ya kuwakataza sana watu wasiingie katika mapambano hayo ya wenyewe kwa wenyewe ambayo mwisho wake utaleta mtengano mkubwa baina ya Waislamu. Na kwa vile hawakutaka kumsikiliza, alijiuzulu hata ugavana aliopewa, na kuuhama mji.

 

 

‘Aliy bin Abi Twaalib (Radhwiya Allaahu ‘anhu) hakuridhika kuchaguliwa kwa Abu Muwsaa si kwa sababu hakuwa akimuamini, bali alikuwa akielewa vizuri kuwa Abu Muwsaa (Radhwiya Allaahu ‘anhu) ni mtu mwema na mchaji Allaah sana, na alikuwa akijua kuwa alikuwa akimpenda sana ‘Aliy, isipokuwa kwa vile upande wa Mu'aawiyah (Radhwiya Allaahu ‘anhu) unawakilishwa na ‘Amr bin al-’Aas (Radhwiya Allaahu ‘anhu) anayejulikana sana kwa umahiri wake katika kujadiliana na uhodari wake wa kupanga maneno na wepesi wake wa kufikiri na kutoa uamuzi unaosibu. Kwa hivyo ‘Aliy (Radhwiya Allaahu ‘anhu) naye akataka upande wake pia uwakilishwe na mtu wa kadiri yake ambaye ni Ibn ‘Abbaas (Radhwiya Allaahu ‘anhu) ‘Aliyekuwa akijulikana kuwa ni kufu yake ‘Amr bin al-’Aas (Radhwiya Allaahu ‘anhu).

 

 

Lakini Al Ash'ath bin Qays ‘Aliyekuwa upande wa ‘Aliy alipinga sana jambo hilo na kushikilia kuwa lazima upande wao uwakilishwe na Abu Muwsaa, ama sivyo watajitenga, na Sayiduna ‘Aliy kwa sababu hakutaka utokee mfarakano akakubali.

 

 

 

Mapatano

Katika hadithi sahihi iliyosimuliwa na Ad-Daaraqutniy pamoja na Khalifa bin Khayyaat [huyu ni mwalimu wa Imaam Al-Bukhaariy] juu ya kisa hiki, wanasema:

 

 

"Katika mkutano ule, Abu Muwsaa alipendekeza ‘Aliy na Mu'awiyah wasimamishwe na achaguliwe ‘Abdullaah bin ‘Umar bin Khatwaab (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kuwa Khalifa wa Waislamu kwa ajili ya heshima   aliyonayo mbele ya Waislamu, pamoja na elimu yake na ucha wake, na hasa kwa vile tokea mwanzo alikataa kujiingiza katika mgogoro huu.

‘Amr bin al-’Aas (Radhwiya Allaahu ‘anhu) akasema:

"Kwa nini hatumchagui Mu'awiyah?"

 

 

Baada ya kukataliwa pendekezo lake hilo, ‘Amr bin al-’Aas (Radhwiya Allaahu ‘anhu) akampendekeza ‘Abdullaah bin ‘Amr (mwanawe) ‘Aliyekuwa mchaji Allaah na akiheshimiwa sana na Swahaba wa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) pamoja na Waislamu wengine.

 

 

Abu Muwsaa akamwambia:

"Mwanao ni mwanamume kweli kweli na mchaji Allaah, lakini kwa vile wewe umo ndani ya mgogoro huu, haitawezekana kumchagua yeye akakubalika. Sikiliza ewe ‘Amr! Waislamu wametubebesha sisi jukumu hili baada ya kushindwa kulimaliza kwa panga zao na mikuki, kwa hivyo usizidi kuwaingiza katika mitihani".

 

 

‘Amr bin al-’Aas (Radhwiya Allaahu ‘anhu) akasema:

"Sasa wewe unaonaje?"

Abu Muwsaa akasema:

 

'Mimi naona bora tuwaondoe wote wawili na tuwaachie uamuzi Swahaba wa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) wamchague wanayemuona kuwa anafaa katika jambo hili".

 

‘Amr (Radhwiya Allaahu ‘anhu) akauliza:

'Mimi na Mu'awiyah tutakuwa na msimamo gani?'

 

Abu Muwsaa akasema:

 

"Mkihitajiwa mtaitwa, la ikiwa hamkuhitajiwa, nyinyi hamtakuwa watu wa mwanzo wasiohitajiwa".

 

 

Walikubaliana kuwaachia uamuzi Swahaba wakubwa kulitatua tatizo hilo kwa kumchagua yule wanayemuona kuwa atafaa.

 

 

Walikubaliana pia kuwa, kwa wakati ule mambo yabaki kama yalivyo, ‘Aliy (Radhwiya Allaahu ‘anhu) ambaye alichaguliwa kuwa Khalifa baada ya watu wote kufungamana naye abaki katika utawala wake, na Mu'awiyah (Radhwiya Allaahu ‘anhu) abaki kuwa gavana wa Shaam mpaka pale Swahaba waliochaguliwa na wajumbe hao wawili watakapofikia uamuzi wa mwisho juu ya Khalifa mpya wa Waislamu.

 

 

Walihudhuria mazungumzo hayo pia Swahaba wakubwa kama vile, ‘Abdullaah bin ‘Umar, ‘Abdullaah bin ‘Abbaas, ‘Abdullaah bin Zubayr, Al Mughiyra bin Shuuba na wengineo (Radhwiya Allaahu ‘anhum).

 

 

Kisa kama hiki pia kimeelezwa katika Taariykh ya Al-Bukhaariy kama alivyoelezea Shaykh ‘Uthmaan Al-Khamiys katika 'Hiqbah minat Taariykh – uk. 84.

 

 

 

Baada Ya Makubaliano

Haujapita muda mrefu baada ya makubaliano hayo baina ya Abu Muwsaa na ‘Amr (Radhwiya Allaahu ‘anhu), zikasikika sauti kutoka kwenye kambi ya ‘Aliy(Radhwiya Allaahu ‘anhu) zikisema:

 

 

"Tulikosea tulipokubali kuhukumiwa na watu, na sasa tunarudia tena makosa yetu yale yale. Hatukubali kuhukumiwa isipokuwa kwa Kitabu cha Allaah".

 

 

‘Aliy (Radhwiya Allaahu ‘anhu) ambaye tokea mwanzo alikwishawaonya watu wake kuwa madai ya upande wa Mu'awiyah (Radhwiya Allaahu ‘anhu) ya kutaka kuhukumu kwa Qur-aan yalikuwa ni katika mbinu za kivita akawajibu watu wake kwa kuwaambia:

 

 

"Sasa hivi tena, baada ya kutoa ahadi zetu na baada ya makubaliano ndiyo mnasema maneno haya.?"

 

 

‘Aliy (Radhwiya Allaahu ‘anhu) aliondoka hapo akiwa pamoja na watu wachache aliobaki nao na kuelekea mji wa Al-Kuufa.

 

 

Wengi kati ya wafuasi wake walijitenga naye kwa hoja kuwa eti alikubali kuhukumiwa na watu badala ya kuhukumiwa na Kitabu cha Allaah, jambo lililokuwa likimuudhi sana ‘Aliy (Radhwiya Allaahu ‘anhu) aliyekuwa akielewa kuwa maana ya kuhukumiwa na kitabu cha Allaah ni kuwa ‘Ulamaa wahukumu kutokana na dalili zilizomo ndani ya Kitabu cha Allaah.

 

 

Wengine waliamua kujitenga baada ya kuchoshwa tu na vita virefu vya wenyewe kwa wenyewe visivyokwisha.

 

 

Inasemekana kuwa ‘Aliy (Radhwiya Allaahu ‘anhu) alijikuta amebakiwa na watu wasiozidi elfu kumi na sita, na riwaya nyingine zinasema kuwa alibakiwa na watu wapatao elfu kumi na mbili na nyengine zinasema kuwa waliobaki walikuwa wachache zaidi kuliko idadi hiyo.

 

 

Kuanzia hapo ‘Aliy (Radhwiya Allaahu ‘anhu) akawa anakabiliwa na makundi mawili - Moja lipo Shaam likidai kisasi cha kuuliwa kwa ‘Uthmaan (Radhwiya Allaahu ‘anhu), na kundi la pili lipo Iraaq, limepiga kambi katika mji unaoitwa Naharawaan, ulio kando kando ya mto Tigris. Kundi hili lilipewa jina la Khawaarij, na lilikuwa likimlaumu ‘Aliy (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kwa kukubali kwake kuhukumiwa na watu badala ya kuhukumiwa na Qur-aan.

 

 

 

Hapana Hukmu Isipokuwa Ya Allaah

 

Walikuwa wakisema:

 

"Hapana hukmu isipokuwa ile ya Allaah".

 

 

Khawaarij walikuwa wakilitumia neno hili kama nguzo yao kubwa ya dini, na walikuwa kila wanapomuona ‘Aliy (Radhwiya Allaahu ‘anhu) akihutubia wakipiga kelele:

 

 

"Hapana hukmu isipokuwa ile ya Allaah!".

 

 

Walikuwa wakiowaona ‘Aliy na ‘Uthmaan (Radhwiya Allaahu ‘anhum) kuwa ni makafiri, kwa sababu kutokana na itikadi yao, mtu yeyote anayekosea katika kuhukumu, huyo anakuwa kafiri. Na kwa vile wanaona kuwa ‘Uthmaan na ‘Aliy (Radhwiya Allaahu ‘anhum) walikosea, basi walikuwa makafiri na damu yao ilikuwa halali kumwagika.

 

 

Si hao tu, bali hata Swahaba wengine kama vile Twalhah au Az-Zubayr (Radhwiya Allaahu ‘anhum) walikuwa wakiwaona kuwa ni makafiri pia na Ilikuwa vigumu kuwafahamisha lolote katika mambo ya dini, kwa sababu walikuwa watu wabishi sana na wakati huo huo walikuwa wacha sana.

 

 

Linalosikitisha ni kuwa wakati wanawakufurisha Waislamu wenzao kwa sababu ya kukhitilafiana kwa rai na kuhalalisha damu yao, wakati huo huo mkiristo au mshirikina kwa rai yao hakuwa akistahiki kuuliwa kwa sababu hao ni watu wa dhimma.

 

 

Walikuwa pia wakimkufurisha kila mwenye kuwaunga mkono watawala wa Banu Umayyah.

 

 

Wakati huo huo yeyote atakayejitenga na ‘Aliy na ‘Uthmaan na Twalhah na Az-Zubayr na watawala wa Banu Umayyah, basi hata awe na makosa makubwa namna gani, walikuwa wakiyakubali makosa hayo na kumfanya kuwa sahibu yao.

 

 

Walimfanyia uadui Khalifa muadilifu ‘Umar bin ‘Abdil-Aziyz (Radhwiya Allaahu ‘anhu) anayetokana na kabila la Banu Umayyah, juu ya kuwa Khalifa huyo aliwarudishia haki zao wote waliodhulumiwa na watawala wa Banu Umayyah, na alikuwa mtu mwema, muadilifu, mchaji Allaah na mpenda haki, lakini kwa vile hakuwakufurisha jamaa zake watu wa Banu Umayyah, kwa ajili hiyo Khawaarij hawakumtambua khalifa huyo kuwa ni muadilifu na hawajakubali kumtii.

 

 

Hawakuwa wakimfanyia zogo ‘Aliy (Radhwiya Allaahu ‘anhu) katika hotuba zake tu, bali wengi wao walikuwa wakimkata Swalah yake na walikuwa wakiutilia shaka Uislamu wa mtu yeyote mwenye kuwaunga mkono ‘Aliy na ‘Uthmaan (Radhwiya Allaahu ‘anhum).

 

 

 

Kisa Cha Kuuliwa Kwa ‘Abdullaah Bin Khubaab

Walimuuwa ‘Abdullaah bin Khubaab bin Al-Arat na kutumbua matumbo ya mke wake, kwa sababu alikataa kusema kuwa ‘Aliy (Radhwiya Allaahu ‘anhu) alikuwa mshirikina.

 

 

Wakati huo huo imepokelewa kuwa hawajakubali kula tende za mkiristo mmoja bila ya kulipa thamani yake kwa sababu alikuwa katika watu wa dhimmah. Walishikilia lazima walipe thamani ya tende hizo.

 

 

Walimuacha mkristo huru na wakamuua Muislamu huku wakisema:

 

 

"Hifadhini dhimah ya Rasuli wenu."

 

 

Walimkuta ‘Abdullaah bin Khubaab bin Al-Art akiwa na Msahafu shingoni pake na wakati huo alikuwa na mkewe mja mzito. Wakamuambia:

 

 

"Hicho ulichovaa shingoni kinatuamrisha tukuuwe. Nini rai yako juu ya ‘Aliy baada ya mapatano?" Akasema: "Nasema kuwa ‘Aliy anakijua zaidi kitabu cha Allaah kupita nyinyi, na anaipenda zaidi dini yake kupita nyinyi na ana hekima zaidi." Wakasema: "Wewe unawafuata watu kwa majina yao."

 

 

Wakamchukuwa kwa nguvu mpaka kandokando ya mto na kumchinja hapo.

Na ‘Aliy (Radhwiya Allaahu ‘anhu) alipowaendea na kuwaambia: "Mleteni waliomuuwa ‘Abdullaah bin Khubaab," wakasema: "Sisi sote tumemuua."

 

 

 

Kisa Cha Waasil Bin ‘Atwaa

Imepokelewa kuwa siku moja Waasil bin ‘Atwaa ambaye ndiye alikuja kuwa mwanzilishi wa kundi la Mu'tazilah hapo baadaye, alipokuwa safarini pamoja na wenzake, walikutana na majeshi ya Khawaarij waliopiga kambi katika mojawapo ya njia kuu. ‘Atwaa akawaambia wenzake: "Niachieni mimi ninajua namna ya kuzungumza nao." Kisha akawakaribia, na walipomuuliza: "Nani nyinyi?"

 

 

‘Atwaa akasema: "Sisi ni washirikina tumekuja kuomba ulinzi na kusikiliza maneno ya Allaah kutoka kwenu, si Allaah katika kitabu chenu Amesema:

 

وَإِنْ أَحَدٌ مِّنَ الْمُشْرِكِينَ اسْتَجَارَكَ فَأَجِرْهُ حَتَّىٰ يَسْمَعَ كَلَامَ اللَّـهِ

Na ikiwa mmoja wa washirikina akikuomba umlinde, basi mlinde mpaka asikie Maneno ya Allaah (Qur-aan). [At-Tawbah: 6]

 

 

Wakamuambia: "Ulinzi mtaupata kutoka kwetu."

Kisha ‘Atwaa akawaambia: "Basi tufundisheni."

 

 

Wakaanza kuwasomea aya za Qur-aan na wao wakawa wanasikiliza, kisha ‘Atwaa akawaambia: "Tushasikiliza maneno ya Allaah na sasa tunataka kurudi makwetu." Wakawaambia: "Rudini makwenu kwa amani." ‘Atwaa akawaambia: "Bali tunataka nyinyi mtufikishe pahali petu pa amani kwa sababu Allaah Amesema:

 

ثُمَّ أَبْلِغْهُ مَأْمَنَهُ 

Kisha mfikishe pahala pake pa amani. [At-Tawbah: 6]

 

 

Wakatizamana muda kidogo kisha wakasema: "Hiyo ni haki yenu."

Wakawasindikiza na kuwafikisha pahala pa amani.

Al-Kaamil fil Lughah wal adab – Juz. 2 uk. 112

 

 

Hivyo ndivyo walivyokuwa wakiifasiri Qur-aan Tukufu. Walikuwa wakiifasiri juu juu na siyo kwa maana yake hasa, na hawakuwa wakifasiri kutokana na sababu zilizoteremshwa aya.

 

 

Lau kama ‘Atwaa angelisema kuwa wao ni Waislamu basi wangelimuuwa kwa sababu asingelikubali kumlaani ‘Aliy na ‘Uthmaan (Radhwiya Allaahu ‘anhum), lakini aliposema kuwa wao ni washirikina wakasalimika.

 

 

 

 

Nahrawaan

Siku moja Ibn ‘Abbaas alimuomba ‘Aliy amkubalie aende kujadiliana nao, na ‘Aliy (Radhwiya Allaahu ‘anhu) akamuamiba:

 

"Mimi nakuogopea."

 

Ibn ‘Abbaas (Radhwiya Allaahu ‘anhu) akasema:

 

"Hapana hofu yoyote In Shaa Allaah".

 

 

Ibn ‘Abbaas (Radhwiya Allaahu ‘anhu) alipowaendea akawakuta kuwa ni watu wenye kufanya ibada sana, na walipomuona wakamwambia:

 

Akasema:

"Nimekuja kuzungumza nanyi".

Wengine kati yao wakasema:

"Msizungumze naye".

Wengine wakamwambia:

"Sema tutakusikiliza".

Akasema:

"Hebu niambieni, mnamlaumu ‘Aliy bin ‘ammi yake Rasuli wa Allaah kwa kosa gani? Huyu ambaye ni mume wa binti yake na wa mwanzo kumuamini?"

Wakasema:

"Mambo matatu".

"Yepi hayo?"

Wakasema:

"La mwanzo ni kukubali kwake kufuata hukmu ya wanaadamu katika dini ya Allaah. La pili, amepigana vita na ‘Aaishah na Mu'awiyah bila kuchukuwa ngawira wala kuwateka, na la tatu amekubali kujiondolea mwenyewe cheo chake cha Ukhalifa juu ya kuwa Waislamu wamefungamana naye na kumkubali kuwa yeye ni Khalifa wao".

 

Ibn ‘Abbaas (Radhwiya Allaahu ‘anhu) akawauliza:

"Mnaonaje nikikupeni dalili kutoka katika kitabu cha Allaah na kutoka katika mafundisho ya Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) juu ya haya mnayomlaumu, mtarudi kwake na kuyaacha haya mliyo ndani yake?"

 

Wakasema:

"Ndiyo".

Akasema:

"Ama ile kauli yenu katika kumlaumu kukubali kwake kuhukumiwa na watu katika dini ya Allaah, basi Allaah Anasema:

 

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا لَا تَقْتُلُوا الصَّيْدَ وَأَنتُمْ حُرُمٌ ۚ وَمَن قَتَلَهُ مِنكُم مُّتَعَمِّدًا فَجَزَاءٌ مِّثْلُ مَا قَتَلَ مِنَ النَّعَمِ يَحْكُمُ بِهِ ذَوَا عَدْلٍ مِّنكُمْ..

Enyi walioamini! Msiue mawindo na hali mko katika ihraam. Na atakayemuua (mnyama) miongoni mwenu kwa kusudi, basi malipo yake itakuwa ni kilicho sawa na alichokiua katika wanyama wa mifugo. Kama wanavyohukumu wawili wenye uadilifu miongoni mwenu. [Al-Maaidah: 95]

 

 

Semeni ukweli wenu! hivyo kuhukumiwa na wanaadamu katika kusimamisha umwagaji wa damu na kupoteza nafsi zenu na kupatanisha baina yenu ni bora, au kuhukumiwa na wanadamu juu ya sungura (‘Aliyeuliwa na mtu anayehiji) ambaye thamani yake ni sawa na robo Dirham?"

 

Wakasema:

"Bali katika kusimamisha umwagaji wa damu na kupatanisha baina ya watu".

Akasema:

"Hilo tushalimaliza?'

Wakasema:

"Ndiyo".

 

Akasema:

"Ama ile kauli yenu kuwa ‘Aliy alipigana vita na hakuwateka ngawira wanawake kama vile Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alivyofanya. Hivyo nyinyi mlikuwa mkitaka amteke ngawira mama yenu Bibi ‘Aaishah na awe halali kwenu kama wanavyohalalishwa wanawake wanaotekwa katika vita? Mkijibu 'ndiyo', mtakuwa mumekufuru, na mkisema kuwa yeye si mama yenu, pia mtakuwa mumekufuru, kwa sababu Allaah Anasema:

 

 ۖ وَأَزْوَاجُهُ أُمَّهَاتُهُمْ ۗ 

Na wake zenu ni mama zao… [Al-Ahzaab: 6]

 

 

Kwa hivyo jichagulieni mnachotaka".

Wakasema:

"Na hili pia tushalimaliza".

Ibn ‘Abbaas (Radhiya Allaahu ‘anhu) akasema:

 

"Ama kauli yenu kuwa ‘Aliy alijifutia mwenyewe cheo chake cha Ukhalifa, basi hata Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) alifanya hivyo siku ya mapatano ya Hudaybiyah, pale washirikina walipomtaka aandike mkataba, na yeye akaandika; “Haya ni makubaliano baina ya Muhammad Rasuli wa Allaah." Na makafiri wakasema; "Tungelikuwa tunaamini kuwa wewe ni Rasuli wa Allaah, tusingelikuzuia kwenda kutufu Al-Ka’abah, na wala tusingekupiga vita, lakini andika:

 

 

"Muhammad bin ‘Abdillaah".

Na Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) akalikubali sharti lao huku akisema:

"Wa-Allaahi mimi ni Rasuli wa Allaah hata mkinikadhibisha".

Khawaarij wakasema:

"Na hili pia nalo tushalimaliza."

 

 

Ikawa katika matunda ya majadiliano hayo yenye hoja zilizo wazi, watu wapatao elfu tano walirudi katika kambi ya ‘Aliy bin Abi Twaalib (Radhwiya Allaahu ‘anhu) na riwaya nyingine zinasema kuwa idadi kubwa kuliko hiyo walirudi.

 

 

 

 

Vita Vya Nahrawaan

:Anasema Imaam Ahmad bin Hanbal

Nimehadithiwa na Is-haaq bin ‘Iysa At-Taba'a ‘Aliyehadithiwa na Yahya bin Sulaym kutoka kwa ‘Abdullaah bin ‘Uthmaan bin Khaytham kutoka kwa ‘Ubaydullaah bin ‘Iyaadh bin ‘Amr al-Qaariy kuwa amesema:

 

 

"‘Abdullaah bin Shaddaad alikuja kwa Bibi ‘Aaishah (Radhwiya Allaahu ‘anhaa) wakati sisi tupo kwake tumekaa na wakati huo alikuwa anarudi kutoka ‘Iraaq katika siku za kuuliwa kwa ‘Aliy, na bibi ‘Aaishah akamwambia: "Ewe ‘Abdullaah bin Shaddaad utanielezea ukweli kwa nitakayokuuliza? Nihadithie juu ya hawa waliomuua ‘Aliy", ‘Abdullaah akasema: "Na kwa nini nisikuelezee ukweli." Akasema: "Haya nihadithie juu ya kisa chao."

 

 

Akasema: "Hakika ‘Aliy alipokubali mkataba na Mu'awiyah na waamuzi wawili walipotoa uamuzi wao, wakajitoa kutoka katika jeshi lake watu elfu nane miongoni mwa wasomi na kuelekea mahali panapoitwa Hururaa pembezoni mwa mji wa Al-Kuufa huku wakimwambia: "Umejivua nguo ‘Aliyokuvisha Allaah na (umelikataa) jina alilokupa Allaah kisha ukakubali hukmu ya watu katika dini ya Allaah wakati hapana hukmu isipokuwa ya Allaah."

 

 

Zilipomfikia habari hizo ‘Aliy akaamrisha patangazwe kuwa kila mtu aje kwake na asiingie kwake mtu isipokuwa awe amebeba Qur-aan (au amehifadhi Qur-aan). Na nyumba ilipojaa watu wenye elimu, ‘Aliy (Radhwiya Allaahu ‘anhu) akataka aletewe Msahafu. Akauweka mbele yake na kuushika huku akiuambia; "Ewe Msahafu! Zungumza na watu!"

 

 

Watu wakamwambia: "Ewe Amiri wa Waislamu unazungumza na nani? Hizi ni karatasi na uwino tu, sisi ndio tunaozungumza kama kitabu kinavyotutaka. Unataka nini?"

 

 

Akasema: "Sahibu zenu hawa waliojitenga. Baina yangu na wao ni Kitabu cha Allaah. Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) katika Kitabu chake anasema:

 

وَإِنْ خِفْتُمْ شِقَاقَ بَيْنِهِمَا فَابْعَثُوا حَكَمًا مِّنْ أَهْلِهِ وَحَكَمًا مِّنْ أَهْلِهَا إِن يُرِيدَا إِصْلَاحًا يُوَفِّقِ اللَّـهُ بَيْنَهُمَا ۗ إِنَّ اللَّـهَ كَانَ عَلِيمًا خَبِيرًا ﴿٣٥﴾

Na mkikhofu mafarikiano baina yao wawili, basi pelekeni mwamuzi kutoka watu wa mume na mwamuzi kutoka watu mke. Wakitaka sulhu Allaah Atawawafikisha baina yao.  Hakika Allaah daima ni Mjuzi wa yote, Mwenye upeo wa khabari za dhahiri na za kufichika. [An-Nisaa: 35]

 

 

Na damu ya umati wa Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) ni adhimu zaidi na tukufu zaidi kupita ugomvi baina ya mume na mke. Kisha wananilaumu kuwa nimekubali kufanya kama alivyotaka Mu'awiyah kuliandika jina langu ‘Aliy bin Abi Twaalib (bila kuandika kuwa mimi ni Khalifa wa Waislamu), wakati Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) kwa ajili ya kutaka sulhu, alikubali katika sulhu ya Hudaybiyah kuliandika jina lake Muhammad bin ‘Abdillaah bila ya kuandika 'Muhammad RasuuluAllaah'."

 

 

Na hapo ndipo ‘Aliy (Radhwiya Allaahu ‘anhu) alipokubali Ibn ‘Abbaas (Radhwiya Allaahu ‘anhu) awaendee waliojitenga naye, na baada ya kujadiliana nao walitubu waliotubu na kurudi katika jeshi la ‘Aliy."

 

 

Bibi ‘Aaishah (Radhwiya Allaahu ‘anha) akaendelea kumuuliza ‘Abdullaah bin Shaddaad:

 

 

"Kisha ‘Aliy akapigana vita nao?"

 

 

Akasema: Ndiyo Wa-Allaahi, na ‘Aliy aliwashinda, na ndani ya kundi hilo alikuwemo Dhu Thadiy, na ikawa kama alivyosema Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) kuwa; wakati Waislamu watakapokhitalifiana (wakawa makundi mawili) litatokea kundi la tatu litakalopigwa vita na kundi la haki baina ya mawili hayo, na ndani ya kundi hilo (la tatu) atakuwemo Dhu Thadiy. Na vita vilipomalizika ‘Aliy akawa anatafuta baina ya waliouliwa mpaka alipomuona Dhu Thadiy ndipo aliposujudu kumshukuru Allaah maana alielewa kuwa yupo upande wa haki.

 

 

Muslim - mlango wa Zakaah juu ya kundi hilo. Imaam Ahmad - katika Musnad ya ‘Aliy bin Abi Twaalib, nambari 656 kilichofanyiwa tahakiki na Shaykh Ahmad Shaakir na akasema kuwa ni hadithi sahihi.

 

 

‘Aliy (Radhwiya Allaahu ‘anhu) hajawahi kusujudu baada ya kushinda vita vyovyote isipokuwa katika vita hivyo.

 

 

Alishinda katika vita vya Al-Jamal na alishinda vita vya Swiffiyn baina ya majeshi yake na ya Mu'awiyah, na kabla ya hapo alishinda katika vita vya Khaybar n.k., lakini siku ya Nahrawaan alisujudu kumshukuru Allaah.

 

 

Vita vilianza baada ya habari nyingi kumfikia ‘Aliy (Radhwiya Allaahu ‘anhu) juu ya mauaji ya kila siku yanayofanywa na Khawaarij, ndipo alipoamua kuwafuata huko na kuwapiga vita.

 

 

‘Aliy (Radhwiya Allaahu ‘anhu) aliwapiga vita Khawaarij katika mji wa Nahrawaan na alikaribia kuwamaliza, lakini waliobaki waliendelea na mwenendo ule ule wa uasi na mapambano ya chini kwa chini na hatimaye walifanikiwa kumuua ‘Aliy (Radhwiya Allaahu ‘anhu).

 

 

 

 

Kuuliwa Kwa ‘Aliy (Radhiya Allaahu ‘Anhu)

‘Aliy (Radhwiya Allaahu ‘anhu) aliuliwa wakati wa Alfajiri baada ya kupita kiasi cha miaka miwili tokea vita vya Nahrawaan kumalizika alipokuwa katika jukumu lake la kila siku la kuwaamsha watu Swalah ya Alfajiri. Alishambuliwa na mtu aliyekuwa katika kundi la Khawaarij aitwaye ‘Abdur-Rahmaan bin Muljim Al-Muraadiy huku akimchoma kwa panga na visu vilivyojazwa sumu.

 

 

Aliuliwa alipokuwa akiamsha watu akisema kwa sauti kubwa:

 

 

"Asw-Swalaatu enyi watu, amkeni Mwenyeezi Akurehemuni!".

 

 

Muuaji huyo alikuwa keshapangana na wenzake wawili, Brayk bin ‘Abdillaah At-Tamimiy na ‘Amr bin Bakr At-Tamimiy. Mmoja wao aende Shaam na kumuua Mu'awiyah na mwengine aende Misri kumuua ‘Amr bin al-‘Aas katika siku moja na wakati mmoja waliokwisha kubaliana baina yao, ili wawapumzishe watu na matatizo yao!

 

 

Wakakubaliana wote kuwa watimize ukatili wao huo siku ya Ijumaa, Ramadhaan ya kumi na saba, mwaka wa arubaini baada ya Hijra Sayiduna ‘Aliy (Radhwiya Allaahu ‘anhu) alikuwa na kawaida ya kutoka peke yake bila ya ulinzi kabla ya Swalah ya Alfajiri kwa ajili ya kuwaamsha watu, na kwa ajili hiyo ilikuwa rahisi kwa muuaji kumshambulia kwa upanga wake alioulaza ndani ya sumu kwa muda wa mwezi mzima.

 

 

Ama Brayk, aliyekwenda kumuua Mu'awiyah (Radhwiya Allaahu ‘anhu), alimkosea na kumjeruhi pajani, na watu wa Mu'awiyah waliwahi kumkamata mtu huyo, na alipokamatwa alisema:

 

 

"Usuniue ewe Mu'awiyah, maana nataka kukupa habari njema".

Mu'awiyah akamuuliza:

"Habari gani hizo?"

Akasema:

"Mwenzangu tuliyepangana naye keshamuua ‘Aliy bin Abi Twaalib siku hii ya leo".

Mu'awiyah akamuuliza:

"Unajuaje pengine naye pia hakufanikiwa?"

Akasema:

"Lazima atafanikiwa kwa sababu ‘Aliy hatoki na walinzi kama wewe".

Mu'awiyah (Radhwiya Allaahu ‘anhu) akaamrisha auliwe, akauliwa.

 

 

‘Amr bin al-‘Aas (Radhwiya Allaahu ‘anhu) naye siku hiyo kwa bahati alishikwa na tumbo la kuharisha akachelewa kutoka, na badala yake akatoka mmoja katika majemadari wa jeshi lake aitwaye Khaarijah bin Abi Hubaybah, na yule aliyepewa jukumu la kumuua ‘Amr ambaye jina lake pia ni ‘Amr bin Bakr alimshambulia Khaarijah na kumuua akidhania kuwa ndiye aliyemkusudia.

 

 

 

 

 tikadi (‘Aqiydah) Ya Khawaarij

 

 

1-Khawaarij hawaamini kuwa Qur-aan ni maneno ya Allaah, bali wao wanasema kuwa Qur-aan ni kiumbe kwa sababu Allaah Ameumba kila kitu, na Qur-aan ni kitu.

 

 

2-Wanajitenga na ‘Aliy na ‘Uthmaan na Mu'aawiyah na wengi kati ya Swahaba wa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).

 

 

3-Wanazikanusha sifa na majina ya Allaah Alizojinasibisha nazo, wakati Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Anasema:

 

وَلِلَّـهِ الْأَسْمَاءُ الْحُسْنَىٰ فَادْعُوهُ بِهَا ۖ وَذَرُوا الَّذِينَ يُلْحِدُونَ فِي أَسْمَائِهِ ۚ سَيُجْزَوْنَ مَا كَانُوا يَعْمَلُونَ ﴿١٨٠﴾

Na Allaah Ana Majina Mazuri kabisa, basi muombeni kwayo. Na waacheni wale wanamili katika kukadhibisha Majina Yake, watalipwa yale waliyokuwa wakiyatenda. [Al-A’araaf: 180]

 

 

4-Wanakanusha kumuona Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) siku ya Qiyaamah, juu ya kuwa Allaah katika Qur-aan Tukufu Amesema:

 

وُجُوهٌ يَوْمَئِذٍ نَّاضِرَةٌ﴿٢٢﴾ إِلَىٰ رَبِّهَا نَاظِرَةٌ﴿٢٣﴾

22. Nyuso siku hiyo zitanawiri. 23. Zikimtazama Rabb wake. [Al-Qiyaamah: 22-23]

 

 

5-Wanabadilisha maana ya maneno na kusema kuwa hayo ni majazi tu. Na maana yake ni kuwa Allaah Anaposema kuwa Anao Wajihi hakusudii kuwa Anao Wajihi kikweli, bali hayo ni majazi tu, na Anaposema kuwa Anayo macho, hakusudii kuwa Anayo macho kikweli, bali hayo ni majazi tu, na Anaposema kuwa Anayo mikono hakusudii kuwa Anayo mikono bali hayo ni majazi tu, nk.

 

 

6-Hawaamini kuwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) atawaombea Shafa’ah Waislamu walioasi, bali watakaopata Shafa’ah ni wacha peke yao.

 

 

7-Wanaamini kuwa mfanya madhambi, hata kama ni Muislamu, huyo ataingia Motoni na kubaki humo milele sawa na makafiri.

 

 

8-Wanamkufurisha kila asiyekubaliana na rai yao na wanaamini kuwa mtu wa aina hiyo anastahiki kuuliwa, kama walivyowauwa ‘Uthmaan na ‘Aliy na ‘Abdullaah bin Khubaab na wengine, wakati huo huo wanaamini kuwa kafiri au mshirikina hastahiki kuuliwa kama walivyomfanyia Waasil bin ‘Atwaa alivyowadanganya kuwa alikuwa mshirikina wakamuacha huru na kumpa ulinzi wa amani.

 

 

9-Ni wajibu kwao kumpiga vita kiongozi wanayemuona kuwa ni mtenda dhambi hata kama kiongozi huyo ni mtu mwenye uwezo mkubwa wa kuongoza, na kwa ajili hiyo walimsaidia ‘Abdullaah bin Zubayr alipokataa kufungamana na Yaziyd juu ya kuwa ‘Abdullaah hakuwa pamoja nao.

 

 

10-Na hii ndiyo sababu wakati wao wote walikuwa wakiutumia katika kuwapiga vita Waislamu wenzao badala ya kujishughulisha na kuwapiga vita makafiri na kufungua nchi za kikafiri pamoja na Waislamu wenzao.

 

 

Kwa sababu hii Khawaarij hawakuweza kudumu, walitoweka isipokuwa wachache sana waliobaki baada ya kubadili nyingi katika fikra zao.

 

 

 

Makundi Ya Khawaarij

Khawaarij wamegawika makundi yapatayo ishirini, kila moja anamkufurisha mwenzake, na yafuatayo ni baadhi ya majina ya makundi yao:

 

 

  • Al-Mahkamah al-Uwlaa- na hawa ni wale waliojitoa katika jeshi la Sayiduna ‘Aliy (Radhwiya Allaahu ‘anhu), baada ya kukubali mapatano na Mu’aawiyah (Radhwiya Allaahu ‘anhu), wakiongozwa na ‘Abdullaah bin Al-Kawaa na ‘Utaab bin al Aawar na ‘Abdullaah bin Wahab Ar-Raasibiy na ‘Urwah bin Jariyr na Yaziyd bin Abi ‘Aasim Al-Muhariby na Harquus bin Zuhayr Al-Bajiliy anayejulikana kwa jina la Dhu Thadiy.

 

  • Al-Azaariq – hawa ni wafuasi na Naafi’ bin Al-Azraq waliokuwa wengi kupita wenzao.

 

  • An-Najdaat - wafuasi wa Najdah bin ‘Aamir Al-Hanafiy

 

  • As-Safriyah - wafuasi wa Ziyaad bin Al-Asfar

 

  • Al- Ajaaridah - wafuasi wa ‘Abdul-Kariym bin Ajrad

 

  • Al-Khaazimiyah

 

  • Ash-Shu’aybiyah

 

  • Al-Ma’alumiyah

 

  • Al-Majhuliyah

 

  • Asw-Swaltiyah – wafuasi wa Swalt bin ‘Uthmaan

 

  • Ash-Shubaybiyah

 

  • Al-Maaadiyah

 

  • Ar-Rushaydiyah

 

  • Al-Hamziyah

 

  • Ash-Shamrakhiyah

 

  • Al-Makramiyah

 

  • Al-Hamziyah

 

  • Al-Ibraahimiyah

 

  • Al-Waaqifah

 

  • Al-Abaadhiyah – na haw ani wafuasi wa ‘Abdullaah bin Abaadh, na hawa waligawika makundi mawili nayo ni Hafswiyah na Haarithiyah.

 

 

 

Ibadhi

Tunamshukuru Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) kuwa makundi yote ya Khawaarij hivi sasa yamekwishatoweka duniani, na hapana lilillobaki isipokuwa hili la Al-Abaadhiyah - 'Ibadhi,' wasiopenda kunasibishwa na Khawaarij.

 

 

Wao wameweza kubaki hadi leo kwa sababu wamebadilisha na kukataa nyingi kati ya itikadi zenye kupindukia mipaka za Khawaarij waliotangulia, isipokuwa wanazikubali Itikadi za Khawaarij zote zenye kuhusiana na sifa na majina ya Allaah. Kwani wao wanakanusha pia kumuona Allaah siku ya Qiyaamah na wanakanusha adhabu ya kaburi na wanakanusha sifa za kuona na kusikia na wajihi na macho na mikono Alizojinasibisha nazo Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) n.k.

 

 

Ibadhi badala ya kuwaita Waislamu wenzao wenye kukhitalifiana nao kwa rai kuwa ni makafiri, kama walivyofanya Khawaarij, wao wanasema kuwa ni makafiri wa neema, na si makafiri wa Itikadi, isipokuwa wanaitakidi kuwa ni Waislamu waliopunguza katika haki ya Allaah.

 

 

Abadhiyah ambao jina lao linatokana na ‘Abdullaah bin Abaadh Al-Murriy anayetokana na kabila la Bani Tamiym ambaye ni Taabi'iy aliyewaona Swahaba kama vile Mu'aawiyah na ‘Abdullaah bin Zubayr (Radhwiya Allaahu ‘anhum).

 

 

Wafuasi wa madhehebu ya Ibadhi wapo Algeria na Tunisia na Libya na Oman na Zanzibar - Tanzania hivi sasa.

 

 

Hapana Swahaba yeyote aliyejiunga na Khawaarij, juu ya kuwa wao wanadai kuwa ‘Abdullaah bin Wahab Ar-Raasibiy alikuwa Swahaba.

 

 

Anasema Imaam Ibn Hazm:

"Hawajapata wa kumchagua isipokuwa ‘Abdullaah bin Wahab Ar-Raasibiy, beduwi asiyekuwa na kheri yoyote wala hakuwa Swahaba wala hakuwa na Fiqhi..."

Al-Milal wal Ahwaa wan An-Nihal – Imaam Ibn Hazm Adh-Dhwaahiry

 

 

 

 

 

Share