Kuvaa Shanga Kwa Ajili Ya Itikadi Ya Kuzuia Mimba Ni Shirki?

 

SWALI:

 

Assalam Alaykum. Ama baady, Mimi niko ndani ya ndoa na Mungu ametujaalia na mume wangu tumepata binti mmoja, lakini katika kuzuia mimba ninatumia dawa ambayo nilienda kupewa ni dawa ya kienyeji ni kama kijiti kidogo kinachanganywa na kijiwe halafu natengenezewa kwenye ushanga naivaa!!! Je nauliza kufanya hivyo ni dhambi au ni shirki? Tafadhali naomba mnijibu swali langu na Inshaalah ALLAH awajaze kheri nyingi AMIYN.

 


 

 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu kuzuia mimba kwa njia ya kuvaa shangaa.

 

Hujatoa nyudhuru za kishari’ah za wewe kuzuia mimba. Bila udhuru au sababu za kisiha hairuhusiwi mtu kuzuia mimba kabisa. Mtume wetu katupendezeshea sisi kuwa na kizazi kingi na amesema yeye atajifakharisha kwa wingi wa Ummah wake siku ya Qiyaamah. Sasa ikiwa ndugu yetu wewe motto mmoja tu unaanza kuzuia mamba, itakuwaje kwa wale wanaopata watoto sita au saba? Na, je, ungekuwa hukujaaliwa motto labda leo ungekuwa unalalamika na kwenda kwa waganga wa uongo wenye kukupa vitu vya ajabu ajabu kama hivyo vya kuvaa ili upate mtoto! Huoni ndugu yetu kila jambo utakuwa unafanya mambo ya kishirikina?

 

Hakuna dawa kutokana na vitu vya kuvaa kama shanga. Ushanga huo ni kama hirizi ambayo inavaliwa kwa sababu nyingi ambao watu wanapatiwa na wachawi kwa majina ya dawa za kienyeji. Uvaaji wa hirizi ni shirki, kwa mujibu wa kauli ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): “Mwenye kutundika hirizi, hakika amefanya shirki” (Ahmad). Na pia: “Aliyetundika hirizi basi Allaah hamtimizii (hamuondolei shida yake)” (Al-Haakim).

 

Kwa hivyo, kutungika na kuvaa ushanga huo ni shirki na ni madhambi. Itabidi uuvue haraka sana na umuombe Allaah Maghfirah na msamaha kwa makosa hayo uliyoyafanya. Naye ni Mwingi wa Kusamehe kwa wale waliofanya mambo wasiyoyajua.

 

Na daima tunakushauri, uwe unauliza jambo kwa wenye elimu kabla hujaamua kulifanya, na sio kulifanya kasha unakuja kuuliza hukumu yake baada ya kuwa tayari ushafanya! Na hilo ni tatizo sugu katika jamii yetu, watu huenda kwenye matatizo na madhambi kasha huja kuuliza hukumu baada ya kuwa tayari washavuruga na kufanya maovu.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share