Nini Kazi Au Majukmu Ya Imaam Katika Uislamu

SWALI:

 

 

Nataka nijuwe mtu anayeitwa imam ana kazi gani katika Uislam, ni hayo tuu.

 


 

 

 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

 

 

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu kazi au majukumu ya Imaam.

Hakika majukumu ya Imaam yamebadika sana kwa kupitia na wakati na hasa kuwa hakuna dola ya Kiislamu kwa sasa. Wakati wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Makhalifa wake waongofu (Abu Bakr Asw-Swiddiyq, ‘Umar bin al-Khatwtwaab, ‘Uthmaan bin ‘Affaan na ‘Aliy bin Abi Twaalib {Radhiya Allaahu ‘anhum}) walikuwa wao ni Maimaam wa kila kitu kwa Uislamu. Uimaam wao ulikuwa ni wa uongozi wa juu wa kijumla.

 

Wakati huo walikuwa wao wana Uimaam wa kuongoza watu katika Swalah zote katika Msikiti mkuu wa makao yao makuu (mji mkuu wa dola). Na pia walikuwa viongozi wa mambo yote ya wananchi wao ya kidunia. Kwa hiyo, kwa muhtasari walikuwa wakifanya yafuatayo:

 

 1. Kuongoza katika Swalah.

 2. Kuendesha Dola na siasa yake.

 3. Kuhakikisha ukusanyaji wa Zakaah umekwenda sawa na mali iliyo patikana imewekwa katika Baytul Maal.

 4. Kuhakikisha biashara inakwenda kulingana na shari’ah.

 5. Kuhukumu kesi.

 6. Kuwa Amiri wa jeshi linalokwenda katika Jihaad.

 7. Kuwa kiongozi katika Shuura iliyokuwa ikifanyika.

 8. Na mengineyo.

 

Haya takriban yote yalikuwa zaidi wakati wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Ama wakati wa Makhalifa waongofu dola ilikuwa imepanuka kwa kiasi kikubwa na ujemadari wa majeshi walikuwa wakiachiwa watu wengine. Na majukumu ya hukumu na uliwali katika miji iliyokuwa mbali na mji mkuu yakaachiwa mahakimu na maliwali waliochaguliwa na Khaliyfah.

 

Ama kwa sasa, kwa kuwa Imaam anasaidiwa na kamati ya Msikiti, Imaam amekuwa na majukumu yafuatayo:

 

 1. Kuongoza Waumini katika Swalah.

 2. Kutoa Khutbah Siku ya Ijumaa.

 3. Kuandaa darsa na mihadhara ndani ya Msikiti ili kuwaelewesha maamuma wake kuhusu Dini yao.

 4. Kufanya suluhu baina ya watesi wawili au makundi mawili au wanandoa.

 5. Kuishauri kamati kuhusiana na kuendesha mambo kulingana na mfumo wa Kiislamu.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share