Kuchangia Chakula Katika Sherehe Za Makafiri
Kuchangia Chakula Katika Sherehe Za Makafiri
SWALI:
Kazini wakati wa kipindi cha chakula wako wasio waislamu wataleta chakula kusheherekia mwaka mpya kikwao je inaruhusiwa kula. Pia wafanya kazi wameamua kushirikiana kuchangishana ili kutayarisha chakula kabla ya siku kuu ya easter nao wanasema hii haihusiani na dini isipokuwa wanataka kufanya get together na kuenjoy chakula je inaruhusiwa.
JIBU:
AlhamduliLLaah - Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na Salaam zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho
Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu kuchangia chakula katika sherehe za makafiri. Inafahamika kuwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alipohamia Madiynah aliwakuta watu wa huko wanasherehekea siku mbili. Hapo Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akawaambia:
"Hakika Allaah Aliyetukuka Amewabadilishia kwayo siku zilizo bora kuliko hizo: Siku ya Fitwr (‘Iyd baada ya Ramadhaan) na Siku ya kuchinja" [An-Nasaaiy].
Kwa ajili hiyo haifai kwa Muislamu kusherehekea wala kushirikiana na wasio Waislamu kwa sikukuu nyingine yoyote. Haifai kwa Muislamu kushirikiana na wasiokuwa Waislamu katika kuchangia kwa ajili ya kula pamoja wakati wa mwaka mpya au pasaka. Ikiwa ni kweli jambo hilo halihusiani na Dini hawangekuwa ni wenye kulipatia umuhimu mkubwa. Kadhalika haifai kwa nyinyi Waislamu kushiriki katika mambo kama hayo na wasio Waislam. Mjue pia kuwa katika vyakula vyao, wataleta vyakula vya haraam na hata vinywaji, na nyie mtakuwa mnashiriki katika kukaa nao ambapo mtakuwa mnafanya makosa kwa kuwepo sehemu yenye kuliwa na kunywewa haraam.
Isitoshe, mambo kama hayo hayahusiani na kazi wala sheria zake, na hayawezi kukuharibia kazi yako wala mahusiano yako na zaidi ni kuweka misimamo yenu wazi ili ipate kuheshimiwa na siku za mbele muwe ni wenye kutobughudhiwa kushiriki katika shughuli kama hizo.
Muwe wawazi na wakweli kwa kuwafahamisha kuwa hayo hayahusiani na hayakubaliani na Diyn yenu. Ama kukwepa na kutoa udhuru wa uongo hakutawasaidia na kutawafanya muzidi kuandamwa kila wakati.
Tukumbuke kauli ya Allaah aliyetukuka:
وَتَعَاوَنُوا عَلَى الْبِرِّ وَالتَّقْوَىٰ ۖ وَلَا تَعَاوَنُوا عَلَى الْإِثْمِ وَالْعُدْوَانِ ۚ وَاتَّقُوا اللَّـهَ ۖ
Na shirikianeni katika wema na taqwa, na wala msishirikiane katika dhambi na uadui. Na Mcheni Allaah;.. [Al-Maaidah: 2].
Na Allaah Anajua zaidi