Kupewa Gari Kazini Ambayo Imenunuliwa Kwa Mkopo Wa Riba – Kisha Analipia Kwa Installments Inayojumuisha Gharama Na Riba

 

SWALI:

 

Ni hukuma ya mtu kupewa gari kwa mkopo (mfano wa yale yanayoolewa makazini) halafu katika malipo ya gari hiyo analipa kwa awamu (installments) na kila instalment inajumuisha gharama halisi na riba (principal and interest). Aina hii ya malipo ni ipi hukmu yake katika Uislam?

 


 

 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘Alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu mkopo wa riba kazini. Hakika ni kuwa Uislamu umekataza mikopo aina yoyote ikiwa ni kazini au sehemu nyengine ambayo itahitajiwa kulipwa na riba. Kukopesha au kukopeshwa kwa riba kumekatazwa na Uislamu.

 

Allaah Aliyetukuka Anasema yafuatayo kuhusu riba: “Wale walao riba hawasimami ila kama anavyo simama aliye zugwa na Shetani kwa kumgusa. Hayo ni kwa kuwa wamesema: Biashara ni kama riba. Lakini Allaah Ameihalalisha biashara na Ameiharimisha riba” (al-Baqarah [2]: 275). Baada ya aayah hiyo Allaah Aliyetukuka Ametoa onyo kali kwa wenye kuendelea na riba: “Enyi mlioamini! Mcheni Allaah, na acheni riba zilizo bakia, ikiwa nyinyi ni Waumini. Basi mkitofanya jitangazieni vita na Allaah na Mtume wake. Na mkitubu, basi haki yenu ni rasilmali zenu. Msidhulumu wala msidhulumiwe” (al-Baqarah [2]: 278 – 279).

 

Kwa hiyo, mkopo kama huo haufai kisheria na unatakiwa ukae mbali nao kabisa.

 

Na Allaah Anajua zaidi.

 

 

Share