005-Kutoa Zakaah: Umuhimu Wake (Katika Qur-aan)
Kutoa Zakaah: Umuhimu Wake (Katika Qur-aan)
Katika Qur-aan tukufu na katika Mafundisho ya Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), yamo mafunzo mengi yanayopendekeza Kutoa Zakaah na yanayowakemea wale wasioitoa.
Katika Qur-aan Allaah Anasema:
خُذْ مِنْ أَمْوَالِهِمْ صَدَقَةً تُطَهِّرُهُمْ وَتُزَكِّيهِم بِهَا
Chukua (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم) katika mali zao Swadaqah, uwatakase na ziwazidishie kwazo. [At-Tawbah: 103]
Na maana yake ni "Chukua ee Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) Swadaqah maalum kutoka katika mali za Waislam na uwape wanaostahiki ili wenye mali 'wasafike' kutokana na uchafu wa ubakhili na tamaa, na kutokana na ubaya wa kuwanyima masikini haki zao na pia 'uwatakase' nafsi zao kwa Swadaqah hizo na wapate baraka za Rabb wao ili waweze kupata furaha za hapa duniani na za huko Aakhirah.
Na Akasema:
إِنَّ الْمُتَّقِينَ فِي جَنَّاتٍ وَعُيُونٍ. آخِذِينَ مَا آتَاهُمْ رَبُّهُمْ إِنَّهُمْ كَانُوا قَبْلَ ذَلِكَ مُحْسِنِينَ. كَانُوا قَلِيلًا مِّنَ اللَّيْلِ مَا يَهْجَعُونَ. وَبِالْأَسْحَارِ هُمْ يَسْتَغْفِرُونَ. وَفِي أَمْوَالِهِمْ حَقٌّ لِّلسَّائِلِ وَالْمَحْرُومِ
Hakika wenye taqwa watakuwa katika Jannaat na chemchemu. Wakichukua yale Atakayowapa Rabb wao. Hakika wao walikuwa kabla ya hapo ni wahisani. Walikuwa kidogo tu katika usiku wakilala kwa raha. Na kabla ya Alfajiri wakiomba maghfirah. Na katika mali zao kuna haki maalumu kwa mwenye kuomba na asiyeomba. [Adh-Dhaariyaat: 15-19]
Katika Aayah hii Allaah Anatuelezea juu ya wale atakaowaingiza katika bustani Zake na chemchem, kwa sababu walipokuwa huko duniani walikuwa wenye kulala muda mfupi sana nyakati za usiku, na sehemu kubwa ya usiku, walikuwa wakiswali, na nyakati za kabla ya kuingia alfajiri walikuwa wakiomba maghfira huku wakijikurubisha kwake Subhanaahu wa Ta’aalaa.
Walikuwa pia watu wenye kutoa katika mali zao kuwapa fakiri na maskini, wenye kuomba na wasiyo omba huku wakiwaonea huruma.
Na Allaah Akasema pia:
وَالْمُؤْمِنُونَ وَالْمُؤْمِنَاتُ بَعْضُهُمْ أَوْلِيَاء بَعْضٍ يَأْمُرُونَ بِالْمَعْرُوفِ وَيَنْهَوْنَ عَنِ الْمُنكَرِ وَيُقِيمُونَ الصَّلاَةَ وَيُؤْتُونَ الزَّكَاةَ وَيُطِيعُونَ اللّهَ وَرَسُولَهُ أُوْلَـئِكَ سَيَرْحَمُهُمُ اللّهُ إِنَّ اللّهَ عَزِيزٌ حَكِيمٌ
"Na Waumini wanaume na Waumini wanawake ni marafiki wandani wao kwa wao, wanaamrisha mema na wanakataza munkari na wanasimamisha Swalaah na wanatoa Zakaah na wanamtii Allaah na Rasuli Wake. Hao Allaah Atawarehemu. Hakika Allaah ni Mwenye enzi ya nguvu Asiyeshindika, Mwenye hikmah wa yote". [At-Tawbah - 71]