008-Kutoa Zakaah: Wasiotoa Zakaah (Katika Sunnah)
Kutoa Zakaah: Wasiotoa Zakaah (Katika Sunnah)
Imepokelewa kutoka kwa Abuu Hurayrah (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kuwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:
"Atakayepewa mali kisha asitoe Zakaah yake, basi mali hiyo Siku ya Qiyaamah itageuzwa kuwa joka dume lenye upara, mwenye madoa mawili machoni (kutokana na wingi wa sumu aliyonayo), atajizungusha katika mwili wa mtu huyo, kisha atamkaba shingoni huku akimwambia:
"Mimi ndiyo hazina yako uliyokuwa ukiikusanya, mimi ndiyo mali yako", kisha Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akaisoma Aayah hii:
وَلاَ يَحْسَبَنَّ الَّذِينَ يَبْخَلُونَ بِمَا آتَاهُمُ اللّهُ مِن فَضْلِهِ هُوَ خَيْرًا لَّهُمْ
Wala wasidhani kabisa wale wanaofanya ubakhili kwa yale Aliyowapa Allaah katika fadhila Zake kwamba hayo ni khayr kwao. [Aal-‘Imraan: 180]
[Al-Bukhaariy na Muslim]
Na kutoka kwa ‘Abdullaah bin ‘Umar bin Al-Khatwaab (Radhwiya Allaahu 'anhumaa) amesema kuwa; Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:
"Enyi watu wa Madina, mambo matano mkija mkapewa mtihani juu yake na kuteremshiwa - Najikinga kwa Allaah yasije yakakukuteni - Hautoenea uzinzi katika kaumu mpaka wakafikia kujitangazia, (isipokuwa) yatakuja kuenea kwao maradhi (aina mpya) ambayo hayajakuwepo kwa waliowatangulia, na hawatopunjwa watu katika vipimo na katika mezani isipokuwa wataletewa umasikini na shida ya kupatikana vitu, na dhulma ya ufalme. Na watakapoacha (watu) kutoka Zakaah ya mali zao, watanyimwa mvua, na lau kama si kwa ajili ya wanyama, basi isingenyesha mvua. Na watakapovunja ahadi ya Allaah na ahadi ya Rasuli wake, watasalitishiwa adui asiyekuwa mwenzao achukuwe baadhi ya vilivyo mikononi mwao. Na ikiwa viongozi wao hawatahukumu kwa kitabu cha Allaah, basi vitafanywa vita vyao viwe baina yao" [Ibn Maajah – Al-Bazaar na Al-Bayhaqiy]