019-Kutoa Zakaah: Dhahabu Na Fedha
Kuota Zakaah: Dhahabu Na Fedha
Allaah Anasema:
هُوَ الَّذِي أَرْسَلَ رَسُولَهُ بِالْهُدَىٰ وَدِينِ الْحَقِّ لِيُظْهِرَهُ عَلَى الدِّينِ كُلِّهِ وَلَوْ كَرِهَ الْمُشْرِكُونَ﴿٣٣﴾ وَالَّذِينَ يَكْنِزُونَ الذَّهَبَ وَالْفِضَّةَ وَلاَ يُنفِقُونَهَا فِي سَبِيلِ اللّهِ فَبَشِّرْهُم بِعَذَابٍ أَلِيمٍ. يَوْمَ يُحْمَى عَلَيْهَا فِي نَارِ جَهَنَّمَ فَتُكْوَى بِهَا جِبَاهُهُمْ وَجُنوبُهُمْ وَظُهُورُهُمْ هَـذَا مَا كَنَزْتُمْ لأَنفُسِكُمْ فَذُوقُواْ مَا كُنتُمْ تَكْنِزُونَ. يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا إِنَّ كَثِيرًا مِّنَ الْأَحْبَارِ وَالرُّهْبَانِ لَيَأْكُلُونَ أَمْوَالَ النَّاسِ بِالْبَاطِلِ وَيَصُدُّونَ عَن سَبِيلِ اللَّـهِ ۗ وَالَّذِينَ يَكْنِزُونَ الذَّهَبَ وَالْفِضَّةَ وَلَا يُنفِقُونَهَا فِي سَبِيلِ اللَّـهِ فَبَشِّرْهُم بِعَذَابٍ أَلِيمٍ﴿٣٤﴾
Yeye Ndiye Aliyemtuma Rasuli Wake (Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم) kwa mwongozo na Dini ya haki ili Aishindishe juu ya dini zote, japo watakirihika washirikina. Enyi walioamini! Hakika wengi katika Wanazuoni Marabai wa dini (zao) na Wamonaki wanakula mali za watu kwa batili, na wanazuia njia ya Allaah. Na wale wanaorundika dhahabu na fedha na wala hawazitoi katika njia ya Allaah, basi wabashirie adhabu iumizayo. [ At-Tawbah: 33-34]
Kwa hivyo mwenye kumiliki viwili hivyo (Dhahabu au Fedha) ikiwa ni katika mfumo wa pesa au mikufu au vipande (vinoo), ikitimia Niswaab yake na kukamilisha mwaka na akawa hana deni, wala shida yoyote inayokubalika, anawajibika kuitolea Zakaah yake.
Wakati Wa Nabiy(Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa Sallam)
Wakati wa Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), watu wa Bara Arabu walikuwa wakifanya biashara zao kwa njia ya kubadilishana bidhaa, na hawakuwa wakitumia pesa isipokuwa wachache sana walioweza kumiliki pesa za dhahabu na za fedha zilizokuwa zikitumika katika nchi za jirani.
Pesa zilizotengenezwa kwa dhahabu zilikuwa zikiitwa Dinari, na zilikuwa zikiletwa kutoka nchi za Warumi kama vile Byzantine na nyenginezo, na walikuwa pia wakitumia pesa zilizotengenezwa kwa fedha zilizokuwa zikiitwa Dirham.
Kwa vile pesa hizo zilikuwa zikiwafikia zikiwa na uzito mbali mbali, na kiasi mbali mbali, nyengine ndogo ndogo na nyengine kubwa kubwa, na hazikuwa na kiasi maalum wala uzito maalum, kwa hivyo watu wa Makkah hawakuwa wakizitumia kama zinavyotumiwa pesa za kawaida, bali walikuwa wakizipima na kuzipa thamani maalum waliyokubaliana.
Miongoni mwa vipimo walivyokuwa wakitumia ilikuwa ratili, ambayo wakati huo ilikuwa na uzito wa wakia kumi na mbili na walikuwa pia wakitumia vipimo vya Mithqaal.
Kutokana na kipimo cha Mithqaal, Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akasema:
"Haitolewi Zakaah ikiwa dhahabu haikutimia Mithqaal ishirini."
Karatasi za benki (Bank notes) zinazopigwa chapa na serikali tofauti ulimwenguni, hupigwa chapa kulingana na Dhahabu na Fedha inayomiliki serikali hizo, ama sivyo serikali yoyote masikini au yenye madeni ingelipiga chapa idadi ya noti yenye thamani kubwa kuliko dhahabu waliyo nayo na kuweza kulipa madeni yao na kujitajirisha.
Niswaab Yake
Dhahabu hailipiwi kitu mpaka ifikie Niswaab yake na imilikiwe (Niswaab hiyo) kwa muda wa mwaka (Mwaka wa Kiislam).
Niswaab ya dhahabu ni mithqaal 20 au gramu 92 au Tola71/2 au wakia 3. (Baadhi ya Wanachuoniwanasema kuwa Niswaab yake ni gramu 85 au Tola 5 au wakia 2), na hii inatokana na ugumu wa kuweza kukisia bei ya vipimo vilivyokuwa vikitumika wakati wa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na vinavyotumika wakati wetu huu. Hapana hitilafu juu ya kiwango cha Mithqaal 20 isipokuwa hitilafu ipo katika kuifasiri Mithqaal katika vipimo vya kisasa.
Inapofikia kiwango hicho, na kubaki muda wa mwaka, unaichukua na kuipeleka kuipima kwa sonara au kwa wajuzi, na baada ya kuijua thamani yake unailipia 2.5% (mbili unusu katika mia) ya thamani ya dhahabu yote.
Niswaab Ya Dhahabu Ndiyo Niswaab Ya Pesa Za Kawaida.
Kwa mfano katika nchi ya UAE, bei ya gramu tisini na mbili ya dhahabu ni Dh. 2575/-
Kwa hivyo hicho ndicho kiwango cha kuanzia kulipia Zakaah. Na dhahabu yako inapofikia kiwango hicho unailipia Dh. 64/- ambayo ni mbili unusu katika mia ya thamani hiyo. Dhahabu inapozidi, na Zakaah yake inaongezeka.
Unailipia thamani ya dhahabu tu bila kuhesabu ujira wa mfuo au kazi ya mkono au thamani ya nakshi zake. (Gharama za ufulishaji hazimo).
Fedha
Niswaab ya fedha ni mithqaal 140 au Tola 36 au wakia 141/2.
Ikifikia kiwango hicho na ikamilikiwa muda wa mwaka, inalipiwa moja katika arubaini au mbili unusu katika mia ya thamani yake.