Mwanamke Kupata Laylatul-Qadr Akiwa katika Hedhi

 Mwanamke Kupata Laylatul Qadr Akiwa katika Hedhi

 

 www.alhidaaya.com

 

SWALI:

 

Assalam aleykum,

 

Kwanza natoa pongezi kwa uzinduzi wa Alhidaaya na ninawaombea wazidi kutuelimisha na kutukumbusha mengi zaidi. 

Swali langu linahusu juu ya mwanamke mwenye hedhi katika masiku ya mwisho ili apate laylatul-Qadar. Kulingana na maelezo mulieleza kuwa mwanamke anaweza kufanya ibada isipokuwa swala. Anaweza kusema Subhaan-Allah, la ilaaha illa-Allah nakadhalika, na kusoma Qur'an. Jee pindi atakapokuwa akisema ataruhusiwa kushika Tasbihi ili kupata hesabu kamili? Jee ataruhusiwa kushika Quran apate kusoma vizuri? Mbali na hayo ningependa munielezee baadhi za ibada zenginezo ambazo mwanamke anaweza kufanya ili apate Laytul-Qadar. 

Shukran.

 

 

JIBU: 

 

AlhamduliLLaah Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho. 

 

 

 

Hakika tayari wewe umeelezea kama ulivyosoma mambo ambayo mwanamke anaweza kuyafanya na kupata fadhila kubwa wakati yuko katika hedhi yake ya mwezi.

 

Jibu la swali kama hili linapatikana katika kiungo hiki hapa chini:

 

Mwanamke Mwenye Hedhi Afanye Nini Masiku Ya Mwisho Kupata Laylatul-Qadr?

 

Anaweza kuleta Adhkaar zote kama SubhaanaAllaah, AlhamduliLlaah, Allaahu Akbar, Laa ilaaha Illa Allaah na nyiradi nyingenezo za usiku.  

 

Katika kuleta hizi nyiradi haifai yeye kushika tasbihi kwani kufanya hivyo ni uzushi bali atumie vidole vyake kwa ajili ya kuweka hesabu anayotaka. Hilo halitofautiani ikiwa mwanamke akiwa na hedhi au hana. Na mwanamme wakati wote hafai kutumia tasbihi kwa kuleta Adhkaar tofauti. 

Soma zaidi kuhusu masuala ya kutumia tasbihi kwenye viungo vifuatavyo:

 

Kutumia Tasbihi Katika Kumdhukuru Allaah Inafaa?

 

Kutumia Vidole Vya Mikono Miwili Kuleta Tasbihi Inafaa? 

 

Ama Qur-aan pia hakuna makatazo ya kuushika Msahafu kutoka katika Qur-aan wala Hadiyth, lakini Maulamaa wengine wanaonelea ni bora kutofanya hivyo na ikibidi ni bora atumie ule wenye Kiarabu na tafsiri ima kwa Kiingereza, Kiswahili au lugha nyingine yoyote ile ambapo ataweza kushika kufungua n.k.  

Kwa majibu yaliyokamilika kwa dalili, soma katika kiungo hiki:

 

Kushika Na Kusoma Qur-aan Katika Hedhi, Nifaas Na Janaba

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share