Je, Umenilinganisha Mimi Kuwa Sawa Na Allaah?
Je, Umenilinganisha Mimi Kuwa Sawa Na Allaah?
Kuandika Na Kutundika Jina La Allaah Na Muhammad Pamoja.
للعلم والحذر
Kwa Ufahamu Wako, Na Kwa Tahadhari
Usije Kutumbukia Katika Shirk
Je, Una Picha Au Maandishi Kama Haya Nyumbani Kwako? Ondosha Na Uzifutilie mbali, Allaah Atakulipa Ujira Wako Na Watambulishe Wenzio Kuhusu Madhara Yake!
Hukumu Ya Kuandika (Allaah … Muhammad) Katika Karatasi Au Ubao Au Vinavyofanana Na Hivyo
حكم كتابة ( الله ... محمد ) في ورقة أو لوحة ونحوها
Sifa Njema zote ni Za Allaah Pekee, Rahma na amani zimifike kwa Rasuli wa Allaah.
Na baada ya hayo,
Kutoka kwa ibn ‘Abbaas (Radhwiya Allaahu ‘anhumaa) kwamba mtu mmoja alimwambia Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): “Atakavyotaka Allaah na ukataka wewe” Akamjibu: ((Je umenilinganisha mimi kuwa sawa na Allaah? Bali sema: Akipenda Allaah [In shaa Allaah] pekee)) [Ahmad].
Ee Muislamu mwenye wivu na Dini yake! Ee mwenye mapenzi na Allaah na Nabiy Wake! Hakika Allaah Ametuonya katika Kitabu Chake Kitukufu kutokufuata hatua za Shaytwaan:
يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا لَا تَتَّبِعُوا خُطُوَاتِ الشَّيْطَانِ ۚ
Enyi walioamini! Msifuate nyayo za shaytwaan; [An-Nuwr: 21]
Na hatua za Shaytwaan ovu kabisa ni kuwaingiza watu kwenye shirki katika njia za uvukaji wao mipaka kwa kuwatukuza Rusuli na waja wema. Na Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ameonya: ((Tahadharini na upindukiaji mipaka ya Dini, kwani waliokuwa kabla yenu wameangamizwa kwa ajili ya uvukaji mipaka ya Dini)) [Ahmad, An-Nasaaiy na Ibn Maajah].
Na hakika siku hizi imeenea baina ya watu kutundika picha zenye muundo na sura mbali mbali lakini zikiwa na hali moja; nayo ni kumlinganisha sawa Allaah (Tabaaraka Wa Ta’ala) na Nabiy Wake Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Nayo ni kuandika Jina la Allaah ( الله) upande wa kulia na jina la Mtume wetu (محمد) upande wa pili yake sambamba. Tazama picha hapo chini.
Na bila ya shaka yaliyotajwa kabla kuhusu haya yanaonyesha wazi kuwa mambo hayo ni kumlinganisha sawa Muumba [Allaah] na aliyeumbwa [Nabiy Muhammad Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam], na huu ni upindukiaji wa mipaka katika Dini alioutahadharisha Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ambaye amesema: ((Msinitukuze Kama Manaswara [Wakristo] walivyomtukuza Masiyh mwana wa Maryam, hakika mimi na mja kwa hiyo semeni mja wa Allaah na Rasuli Wake)) [Al-Bukhaariy na Muslim]
Na kutoka kwa Anas (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kwamba watu walisema: “Ee Rasuli wa Allaah! Ee mbora wetu, ee mwana wa mbora wetu, na Bwana wetu, na mwana wa bwana wetu” Akasema: ((Enyi watu! Shikamaneni na Kumcha Allaah wenu na msimuache Shaytwaan akawafanyia wepesi [kukutumbukizeni kwenye shirki] Mimi ni Muhammad mja wa Allaah na Rasuli Wake, Sipendi mnipandishe cheo zaidi/ juu ya cheo changu Alichoniteremshia Allaah ‘Azza wa Jalla) [Ahmad].
Basi alichukizwa Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kukabiliwa na kusifiwa na watu hadi ikawapelekea kupindukia mipaka. Na kwa Hadiyth hii Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amefanya hima kuzuia kila njia ya kupelekea katika shirki.
Hakika haki ya Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ni kumsadikisha [kauli zake] na kumfuata kwa udhahiri na siri, na mapenzi yake kwetu yawe ni makubwa mno kuliko mapenzi ya wazazi na watoto na watu wote, lakini yasifikie mapenzi haya yakawa sawa na daraja ya mapenzi kwa Allaah.
Amesema Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):
((Je, Umenilinganisha mimi kuwa sawa na Allaah))
فتوى اللجنة الدائمة
Fatwa Ya Baraza Kuu La Kudumu La Fatwa
Sifa Njema zote ni Za Allaah Pekee, Rahma na amani zimifike kwa ambaye hakuna mwenye utume baada yake.
Ammaa baa’d,
Fataawa al-Lajnah ad-Daaimah lil-Buhuuth al-'Ilmiyyah wal-Iftaa imepitia yaliyofikishwa kwa Mufti Mkuu kutoka kwa muulizaji Humuud ‘Abdul-Aziyz As-Saayigh kwa marejeo Nambari 6860 9/11/1421H ambayo muulizaji ameuliza swali na haya hapa maelezo yake: (Allaah Akuhifadhini, na kukhofia yanayojiri katika Dini hii na kutikilia mkazo yanayofisidi ‘Aqiydah na ambayo yanaenea kwa Ummah huu kutoka kwa maadui wa Allaah na wa Dini Yake na wepesi wa watu kufuata mambo wanayodhania ni madogo mno lakini kumbe ni makubwa mno na ikawa kuondosha madhara yake ni vigumu. Kama ilivyokuwa hali katika watu wa Nuuh na masaamu yao [walivyoanza kuweka masanamu/picha za waja wema wakaanza kuwaabudu wakidhania ni jambo jema kumbe ni shirki iliyowasababisha watu waliofuata kuabudu masanamu]. Tunadhihirisha mbele yenu aina mbali mbali za picha zilizotayarishwa/zilizofikia hadi kwamba zimewekwa katika pande mbili; upande kuna Jina la Allaah ’Azza wa Jalla na upande wa jina la Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Wala sijui lipi bado litakalojiri baada ya haya! Na baadhi ya ndugu wamewaandikia Baraza La Fatwa maombi haya ili kufuatilia maovu ya ‘Aqiydah wakitaraji mtoe maoni yenu ambayo huenda ikiwa ni sababu ya ufumbuzi na tiba ya kuondosha uovu huu, Allaah Awathibitishieni na Akulipeni kwa kuiwanufaisha waja Wake Katika utiifu Wake.
Na baada ya utafiti wa Baraza La Fatwa, Limejibu kwamba “Haijuzu kuandika Jina la Allaah Mtukufu [Allaah] pamoja na [Muhammad] jina la Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) sambaba katika karatasi au kwenye ubao [au vitambaa], au kutundika ukutani [kwa hali yoyote]. Huko ni kupindukia mipaka kwa haki yake Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), na kumlinganisha yeye sawa na Allaah. Haya ni mas-ala miongoni mwa mas-ala ya shirki na hali yeye mwenyewe amekataza katika kauli yake, aliposema: ((Msinitukuze Kama Manaswara walivyomtukuza Masiyh mwana wa Maryam, hakika mimi ni mja kwa hiyo semeni mja wa Allaah na Rasuli Wake)).
Na hivyo ni wajibu kuondosha picha hizo au karatasi na kufutilia mbali maandishi kama hayo katika kuta au popote penye aina hizo za picha, ili tuilinde ‘Aqiydah na kufuata wasia wa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Wa biLlaahi tawfiyq. Wa Swalla Allaahu ‘alaa Nabiyyinaa wa ‘alaa aalihi wa swahbihi wa sallam.
Fataawa al-Lajnah ad-Daaimah lil-Buhuuth al-'Ilmiyyah wal-Iftaa
‘Abdullaahi bin ‘Abdur-Rahmaan Al-‘Adh-baan
‘Abdul-Aziyz bin ‘Abdullaah bin Muhammad Aal Shaykh
Swaalih bin Fawzaan Aal Fawzaan
فتوى الشيخ ابن عثيمين رحمه الله
Fatwa Ya Shaykh Ibn ‘Uthyamiyn (Rahimahu Allaah)
Hakika kuandikwa Jina la Allaah (الله) upande mmoja na jina la (محمد) upande wa pili, yakiwa majina hayo yako sambamba na kama hivi:
(الله) *** (محمد) yanamfanya anayetazama kuona kwamba wako katika cheo kimoja na hali Nabiy alimjibu mtu mmoja aliyemwambia Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) “Atakavyotaka/Akipenda Allaah [In shaa Allaah) na ukataka wewe” Akamjibu: ((Je umenilinganisha mimi kuwa sawa Allaah? Bali sema: Akipenda Allaah [In Shaa Allaah] pekee)).
Na ikiwa maandishi kama hayo yamewekwa hivyo mbele ya wanaoswali, yatakuwa ni sababu ya kuwashughulisha watu na Swalah zao. Pia 'Ulamaa wakubwa wamechukizwa [na kukataza] kuandikwa kitu mbele ya Qiblah kwa ajili ya kumshughulisha na kumshawishi mwenye kuswali. Hivyo, haipasi kuandikwa hivyo; naamanisha (الله) *** (محمد) Na popote palipoandikwa hivyo panapaswa kufutiliwa mbali!
Na katika sharh yake ya Kitabu cha Buluughul-Maraam, Kitabu cha Swalah, Mlango wa Misikiti, Mkanda namba 16 upande wa pili, anasema Shaykh kuwa, kwa uchache maandishi kama haya ni shirk ndogo.
Ameandika: Muhammad Asw-Swaalih Al-‘Uthaymiyn 9/1/1420H