Makaburi Misikitini

 

Makaburi Misikitini

 

Imekusanywa Na: Muhammad Faraj Saalim As-Sa’aiy (Rahimahu Allaah)

 

Alhidaaya.com

 

 

 

Kuna baadhi ya kauli zilizotolewa na baadhi ya watu kuwa Haajar na baadhi ya Manabii (‘Alayhimus Salaam) wamezikwa ndani ya Msikiti wa Makkah, na kwamba maneno hayo yameandikwa katika vitabu vya historia.

 

 

Bila shaka yoyote mwenye hoja hii anaelewa wazi kabisa kuwa waandishi wa historia hawajiwekea shuruti za usahihi wa Hadiyth zao, pamoja na kufanya tahakiki juu ya mlolongo wa wapokezi wa Hadiyth hizo (narrators), kwani wao hukusanya tu habari na kuziandika. Ama vitabu vilivyo sahihi na vinavyojiwekea shuruti za kuandika Hadiyth sahihi hapana hata kimoja kilichoandika juu ya jambo hilo.

 

 

Katika kitabu cha Al-Jaami’ as-Swaghiyr mwandishi wake Al-Manaar anasema;

 

"Hakuna hata moja katika makaburi ya Manabii yaliyo na uhakika kuwa wamezikwa hapo isipokuwa kaburi la Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) peke yake, ama kaburi la Nabiy Muusa na Ibraahiym (‘Alayhimas Salaam) ni dhanna tu, na wala hapana uhakika juu yake".

Kwa hivyo kauli hizo haziwezi kuchukuliwa kuwa ni hoja, hasa katika mambo yanayohusu itikadi za dini.

 

 

Ama kuhusu kauli kuwa katika kisa cha Asw-haabul Kahf, baada ya kufa kwa watu hao, palisemwa kuwa; ‘Watawajengea Msikiti’, hiyo pia si hoja, kwa sababu katika Aayah hiyo hiyo imeandikwa kuwa; wenzao walisema;

 

  فَقَالُوا ابْنُوا عَلَيْهِم بُنْيَانًا ۖ رَّبُّهُمْ أَعْلَمُ بِهِمْ ۚ قَالَ الَّذِينَ غَلَبُوا عَلَىٰ أَمْرِهِمْ لَنَتَّخِذَنَّ عَلَيْهِم مَّسْجِدًا ﴿٢١﴾

 “Jengeni jengo juu yao; Rabb wao Anawajua vyema.” Wakasema wale walioshinda katika shauri lao: “Bila shaka tutajenga msikiti juu yao.” [Al-Kahf: 21]

 

 

Ukichunguza utaona kuwa waliotaka wajengewe jengo, ndio waliotoa hoja ya Uchaji Allaah kuliko hao walioshinda, na Allaah hakueleza lolote katika hali zote mbili, na maneno haya ndiyo yanayokubaliwa na maulamaa wengi, wa zamani na wa sasa.

 

Isitoshe, hata ikiwa tutakubali kwa ajili ya mjadala tu, basi kauli hii haileti maana yoyote ya kututaka sisi tufuate maneno yao, kwani Allaah Ametuletea Rasuli wetu (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na akatufundisha yale anayotaka kutoka kwetu, na miongoni mwa aliyotufundisha ni kauli yake (Subhaanahu wa Ta’aalaa) katika hiyo Suwrah Al-Maaidah, Suwrah  ambayo ni ya mwisho kuteremshwa, kauli isemayo

 

  لِكُلٍّ جَعَلْنَا مِنكُمْ شِرْعَةً وَمِنْهَاجًا ۚ  

 Kwa kila (ummah) katika nyinyi Tumeujaalia shariy’ah na manhaj.  [Al-Maaidah: 48]

 

Kwa hivyo wao walikuwa na shariy’ah zao na njia zao, na sisi tuna shariy’ah zetu na njia zetu. Kama vile wao walivyokuwa wakiruhusiwa kumsujudia kiumbe mwenzao (Soma Suwrat Yuwsuf) na waliharamishiwa kula baadhi ya nyama na shahamu, wakati sisi tumeruhusiwa kula vyakula hivyo na tumeharamishiwa kumsujudia yeyote mwengine asiyekuwa Allaah.

 

Na kwa vile Suwra hii ya Al-Maaidah inajulikana kuwa ni Suwrah ya mwisho kuteremshwa na kwa ajili hiyo kila kilichoandikwa ndani yake kinahesabiwa kuwa ni hukmu ya mwisho kabisa.

 

Tukirudia katika maudhui yetu ya Kaburi la Nabiy  (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam), nilikwishanukuu hapo mwanzo kauli mbali mbali za ‘Ulamaa zinazotofautisha hali baina ya kaburi la Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na yale wanayozikwa watu ndani ya Misikiti au kujengewa juu yake Misikiti.

 

Ndugu zangu Waislam, Hadiyth sahihi ziko nyingi sana na zinaeleza kwa uwazi kabisa kuhusu maudhui yetu haya;

 

Kutoka kwa Mama Wa Waumini ‘Aaishah (Radhwiya Allaahu ‘anhaa) kuwa Ummu Habiybah na Ummu Salamah (Radhwiya Allaahu ‘anhumaa) walimhadithia juu ya kanisa waliloliona walipokuwa katika nchi ya uhabeshi, ndani yake mna picha nyingi, na bibi ‘Aaishah (Radhwiya Allaahu ‘anhaa) akamhadithia Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam), na Nabiyt (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akamwambia;

“Watu wale anapokuwa nao mtu mwema baina yao, basi anapokufa mtu huyo wanajenga juu ya kaburi lake Msikiti (mahala pa ‘ibaadah), wanachora juu yake picha hizo, hao ni watu wabaya kabisa kwa Allaah.” [Al-Bukhaariy na Muslim]

 

Hadiyth nyingine;

Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema;

“Ghadhabu ya Allaah imekuwa kali sana juu ya watu wanaoyageuza makaburi ya Manabii wao na watu wema wao kuwa misikiti.” [Al-Bukhaariy na Muslim]

 

 

Na akasema;

"Rabb wangu usilijaalie kaburi langu likawa sanamu linaloabudiwa."  [Muslim]

 

Na akasema;

"Msiswali kuyaelekea makaburi wala msikae juu yake.” [Muslim]

 

 

Na akasema

"Allaah Amewalaani Mayahudi na Manaswara wamegeuza makaburi ya Manabii wao kuwa Misikiti". [Imepokelewa na Maimamu wa Sunnah wote]

 

Imesimuliwa na Abdur-Razaaq katika Musanaf yake kuwa;

"Kauli ya mwisho kabiisa aliyoitamka  Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kabla ya kuirudisha roho yake iliyotwaharika kwa Rabb wake aliyeiumba, alisema;

"Allaah Awaangamize Mayahudi na Manaswara, wameyageuza makaburi ya Manabii wao kuwa mahali pa ‘ibaadah, pasibaki na dini mbili katika bara ya Arabuni". [Hadiyth hii pia imo katika Muwatwaa ya Imaam Maalik]

 

 

Kutokana na Hadiyth zote hizi, ndiyo maana ‘Ulamaa wetu wakatuambia kuwa ni haramu kuswali ndani ya Misikiti iliyo na makaburi ndani yake, yote haya kwa ajili ya kuogopa laana za Allaah zisije zikatusibu kama zilivyowasibu Mayahudi na Manaswara kwa ajili ya kuyageuza makaburi ya Manabii wao kuwa ni mahali pa ‘ibaadah.

 

Hadiyth za aina hii zilizo sahihi ziko nyingi sana, na tukiendelea kuzitaja tunaweza kujaza kurasa nyingi, isipokuwa ningependa kuongezea jambo moja, nalo ni kuwa, Imam An-Nawawiy amezielezea Hadiyth hizi katika kitabu cha Adhkaar katika mlango wa kutujulisha juu ya watu wanaostahiki kulaaniwa, akawataja hawa wanaotenda mambo haya kuwa ni miongoni mwa watu hao wanaostahiki kulaaniwa.

 

Kwa hivyo ni bora mtu ayakimbie mambo kama haya yenye kutatanisha na yanyomuingiza mtu katika kundi la wanaostahiki kulaaniwa na badala yake kufuata yale yaliyo dahiri na sahihi, yale yanayomkaribisha mja na radhi za Rabb wake

 

Watu hawa, wanasema ‘Ulamaa kuwa wanayajengea makaburi hayo kwa niyyah njema ya kutaka kuwaigiza katika juhudi zao za kufanya ‘ibaadah, lakini baada ya kupita miaka mingi wakaja vizazi wasiotambua kusudi la kujengewa, Shaytwaan ataanza kuwatia wasiwasi wake na kuwaambia kuwa wazee wao na babu zao walikuwa wakiwaabudu, kisha na wao wakawaabudu. Na hii ndiyo sababu Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akatukataza kufanya hivyo ili kuufunga mlango wa fitina tokea mwanzo wake"

 

Allaah Anasema;

 

اتَّخَذُوا أَحْبَارَهُمْ وَرُهْبَانَهُمْ أَرْبَابًا مِّن دُونِ اللَّـهِ وَالْمَسِيحَ ابْنَ مَرْيَمَ وَمَا أُمِرُوا إِلَّا لِيَعْبُدُوا إِلَـٰهًا وَاحِدًا ۖ لَّا إِلَـٰهَ إِلَّا هُوَ ۚ سُبْحَانَهُ عَمَّا يُشْرِكُونَ﴿٣١﴾

Wamewafanya Wanachuoni Marabai wao wa dini na Wamonaki wao kuwa ni miola badala ya Allaah, na (pia) Al-Masiyh mwana wa Maryam na hali hawakuamrishwa isipokuwa kumwabudu Ilaah Mmoja Pekee. Hapana mwabudiwa wa haki ila Yeye. Utakasifu ni Wake kutokana na yale yote wanayomshirkisha nayo.   [At-Tawbah: 31]

 

 

Imepokelewa kutoka kwa Imaam Ahmad na At-Tirmidhiy kuwa ‘Uday bin Haatim Atw-Twaaiy (Radhwiya Allaahu ‘anhu) aliyekuwa mkubwa wa kabila la Atw-Twaaiy, kwamba aliposikia juu ya kuja kwa Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Dini ya Kiislam, alikimbilia nchi ya Shaam, na hii ni kwa sababu kabila lake liliingia katika dini ya Manaswara tokea wakati wa Jahilia (kabla ya kuja kwa Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam).

Katika mapambano baina ya watu wake ‘Uday bin Haatim Atw-Twaaiy, na majeshi ya Waislam, dada yake aitwae Savanah alikuwa miongoni mwa mateka waliotekwa na Waislam.

Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alipojua kuwa Savanah ni binti wa Haatim Atw-Twaaiy aliyekuwa akijulikana sana na akipigiwa mifano kwa ukarimu wake, akamuacha huru. Aliporudi kwa kaka yake ambaye ni mkuu wa kabila hilo kubwa, alimshikilia sana aingie katika Dini ya Kiislam.

 

Wakatoka pamoja kwenda Madiynah ili ‘Uday amuone Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam). Alipokuwa amekaa chumbani kwa Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na msalaba wake alouvaa shingoni pake ukiwa unaning’inia kifuani pake, ikateremshwa Aaayah hiyo hapo juu;

 

Wamewafanya Wanachuoni Marabai wao wa dini na Wamonaki wao kuwa ni miola badala ya Allaah,…”

 

 

‘Uday akasema kumwambia Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam);

“Lakini hatukuwa tukiwaabudu ee Rasuli wa Allaah.”

 

‘Uday masikini alikuwa akdhania kuwa ‘Ibaadah  ni kumsujudia mtu au kumswalia.

Lakini Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akamsahihisha na kumfundisha nini hasa maana ya ibada, akamuuliza;

“Si (hawa wanavyuoni wao na watawa wao) walikuwa wakiharamisha yale Aliyohalalisha Allaah na wakihalalisha yale Aliyoharamisha Allaah na wao wanawafuata?”

Akasema;

“Ndiyo walikuwa wakifanya hivyo”.

Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akasema;

“Basi huko ndiko kuwaabudu .”

 

Hapa Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) anatufundisha kuwa kuabudu, si lazima kuwe kwa kusujudu au kuswali tu, bali hata kumfuata mwenye kuhalalisha haramu na kuharamisha halali pia hiyo ni ‘ibaadah.

Kisha Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akamwambia ‘Uday (Radhwiya Allaahu ‘anhu);

“Ee ‘Uday! Unasemaje, kwani unadhurika kitu wewe panaposemwa ‘Allaahu Akbar? Kwani unakijua chochote kingine kilichokuwa kikubwa kuliko Allaah?

Kwani unadhurika wewe panaposemwa: laa ilaaha illa Allaah.”   

 

 

Katika mafundisho ya Nabiye (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam), tutaona anatukataza kuyaabudu makaburi ya watu wema (wachaji Allaah – au kama wanavyoitwa sasa Mawalii).

 

Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema;

“Ghadhabu ya Allaah imezidi kwa wale wanaogeuza makaburi ya Manabii wao na wachaji Allaah wao kuwa mahala pa ‘Ibaadah, Rabb wangu usijaalie kaburi langu likawa mahali pa ‘ibaadah.”  [Muslim]

 

Na katika riwaayah nyingine;

“Uslijaalie kaburi langu likawa sanamu linaloabudiwa”.

 

Juu ya kuwa imeshapita karne nyingi tokea alipofariki Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam), inasikitisha kuona kuwa mpaka leo katika nchi nyingi za Waislam bado wapo watu wanaojishughulisha na ibada hizo za makaburi.

 

Ama kuhusu kaburi la Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) , hali yake inakhitililafiana kabisa na maudhui haya, kwa sababu kwanza Msikiti huo haukujengwa juu ya kaburi hilo, wala Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) hakuzikwa ndani ya Msikiti, isipokuwa katika upanuzi wa Msikiti wakati wa utawala wa Banu Umayyah, kwa vile Nabiy  (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alizikwa ndani ya nyumba yake iliyoambatana na Msikiti, ikabidi kaburi hilo liwe ndani yake, na ‘Ulamaa wakafanya kila njia na kuweza kuuzungushia ukuta na kuutenga mbali na watu wanaoswali.

 

Hili ndilo waliloweza, pamoja na kujenga viti vya saruji mahali ambapo watu wangesimama kwa ajili ya kuswali, na kwa ajili hiyo haiwezekani mtu kusimama na kuswali hapo, na wanaweza kukaa tu na kumswalia Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) pamoja na kumuombea du’aa.

 

 

Share