08-Swabrun Jamiyl: Subira Njema Ilivyo Na Daraja Za Subira

Subira njema

 

08 - Subira Njema Ilivyo Na Daraja Za Subira

 

 

 

Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Alimwamrisha Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)  kuvumilia subira njema kama Anavyosema:

 

 فَاصْبِرْ صَبْرًا جَمِيلًا﴿٥﴾

Basi subiri, subira njema (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم). [Al-Ma’aarij:  5]

 

Aayah hii tukufu imeteremka kumliwaza Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kutokana na maudhi ya makafiri wa Makkah; maudhi ambayo yalimhuzunisha kupita kiasi, yakamtia dhiki. Na alipofariki ‘ammi yake Abuu Twaalib na mkewe Mama wa Waumini Khadiyjah (Radhwiya Allaahu ‘anhaa)  huzuni juu ya huzuni ikamzidi ndipo Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)  Akamteremshia Suwrat Yuwsuf ambayo ilikuwa ni ukumbusho kwake kwamba si pekee aliyefikwa na mitihani bali Manabii wenzake pia walifikwa na masaibu. Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)  kuhusu kauli ya Nabiy Ya’quwb katika Suwrah hiyo:

فَصَبْرٌ جَمِيلٌ﴿١٨﴾

Basi subira njema [Yuwsuf: 18, 83]

 

 Kwa hiyo nini hasa maana ya ‘Swabrun Jamiyl (subira njema)?’ Na je, kuna subira nyinginezo zisizokuwa ni njema? Subira zote zina malipo mema, lakini subira zinakhitilafiana kwa daraja. Salafus-Swaalih (Wema waliotangulia) wamesema: “Hakika subira ni nusu ya iymaan”. Na Ibnul Qayyim amesema katika ‘Madaarijus-Saalikiyn’: “Daraja za subira ni tatu:

 

 

Ya Kwanza: Swabrun biLLaah (Subira kwa Allaah): 

 

Nayo ni subira ya kutaka msaada Kwake Subhaanahu wa Ta’aalaa, na mwenye kuikusudia subira atambue kwamba Allaah Ndiye Mwenye kumpa uwezo wa kusubiri. Na kwamba subira ya mja ni kwa ajili ya Rabb wake na si kwa ajili ya nafsi yake kama Anavyosema Jalla wa ‘Alaa:

 وَاصْبِرْ وَمَا صَبْرُكَ إِلَّا بِاللَّـهِ ﴿١٢٧﴾

Na subiri (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم), na haiwi subira yako isipokuwa kupitia kwa Allaah.  [An-Nahl: 127]

 

 

Kwa maana ikiwa Allaah Hatakupa uwezo wa kusubiri hutaweza kusibiri.

 

 

Ya Pili:  Swabrun liLLaah (Subira kwa ajili ya Allaah):

 

Nayo iwe sababu ya subira yako ni mahaba ya Allaah, na kutaka radhi Zake, na kujikurubisha Kwake na si kudhihirisha uwezo wa nafsi, wala kwa kusifiwa na watu kuhusu subira yako n.k., kwa ajili ya manufaa ya kidunia, bali kuvuta subira kwa ajili ya kupata mahaba ya Allaah na kutaka radhi Zake na kujikurubisha Kwake.

 

 

Ya Tatu:  Swabrun Ma’a-Allaah (Subira Pamoja Na Allaah):

 

Iwe hima ya mja ni matakwa na malengo yake ni ya kidini kwa Allaah. Na hukmu zake za kidini, akijisubirisha nafsi yake pamoja na yote hayo, yaani aiweke nafsi yake katika kuthibiti katika amri Zake na mahaba Yake Subhaanahu wa Ta’aalaa. Na subira ya aina hii ndiyo iliyo ngumu kabisa, nayo ndio subira ya Asw-Swswiddiqiyn.

 

 

Na subira ni kubakia katika utiifu, kuacha maasi na kuridhika na majaaliwa. Na hiyo ndio uthibitisho wa iymaan. Inapomfikia mtu neema hushukuru, na unapomsibu msiba husubiri. Hivyo ndivyo inavyopasa kumwabudu Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)  katika furaha na misiba, na ndipo Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)  Akajumuisha hayo katika kauli Yake:

 

 إِنَّ فِي ذَٰلِكَ لَآيَاتٍ لِّكُلِّ صَبَّارٍ شَكُورٍ﴿٥﴾

Hakika katika hayo kuna Aayaat (ishara, zingatio, mafunzo) kwa kila mwingi wa kusubiri na kushukuru. [Ibraahiym: 5, Luqmaan: 31, Sabaa: 19, Ash-Shuwraa:  33]

 

 

Hizo ndizo sifa za mwenye subira njema, aliyekuwa ni mwingi wa kushukuru katika kila hali. Kwa hiyo, maana ya subira njema ni kuvumilia mitihani na masaibu bila ya kulalamika kwa watu, kuhamanika, kuweweseka, kutokuridhika na majaaliwa, au kukata tamaa hata afikie mtu kutaka kujiangamiza. Ni bora aache moyo wake uumie na uhuzunike, jicho lake litoke chozi la kiasi, ulimi wake ujizuie usije kutamka yasiyopasa, lakini abakie mtu katika subira akitegemea malipo mema.

 

 

 Hivyo ndivyo alivyosubiri Nabiy Ya’quwb ('Alayhis-Salaam)   walipomjia wanawe kumpa habari ya mwanawe Yuwsuf kwamba kaliwa na mbwa mwitu na pia alipozuiliwa mwanawe Bin-Yamiyn Misr na wakampasha habari hiyo waliporudi   msafara, hapo   akasema Nabiy Ya’quwb ('Alayhis-Salaam):

 

 فَصَبْرٌ جَمِيلٌ ۖ وَاللَّـهُ الْمُسْتَعَانُ عَلَىٰ مَا تَصِفُونَ﴿١٨﴾

Basi subira njema, na Allaah ni Mwenye kuombwa msaada juu ya mnayoyavumisha.” [Yuwsuf: 18]

 فَصَبْرٌ جَمِيلٌ ۖ عَسَى اللَّـهُ أَن يَأْتِيَنِي بِهِمْ جَمِيعًا ۚ إِنَّهُ هُوَ الْعَلِيمُ الْحَكِيمُ ﴿٨٣﴾

Basi subira ni njema. Asaa Allaah Aniletee wote pamoja. Hakika Yeye Ndiye Mjuzi wa yote, Mwenye hikmah wa yote.” [Yuwsuf: 83]

 

 

Subira njema pia ni pale Nabiy Yuwsuf ('Alayhis-Salaam) alipotupwa kisimani na nduguze, akapitishiwa mbele ya wanawake wa mji ili iwadhihirikie uzuri wake wa ajabu hata wakajikata vidole vyao. Kisha akasingiziwa kuwa amemtaka mke wa al-'Aziyz akatiwa jela. Kisha walipokuja ndugu zake kutaka chakula katika hazina iliyoko chini ya milki yake, wakatambuana nao wakakiri makosa yao wakasema:

 

 تَاللَّـهِ لَقَدْ آثَرَكَ اللَّـهُ عَلَيْنَا وَإِن كُنَّا لَخَاطِئِينَ ﴿٩١﴾

 “Tunaapa Allaah! Kwa yakini Allaah Amekustahabu kuliko sisi, nasi bila shaka tulikuwa wakosa.” [Yuwsuf: 91]

 

Naye akawajibu:

 لَا تَثْرِيبَ عَلَيْكُمُ الْيَوْمَ ۖ يَغْفِرُ اللَّـهُ لَكُمْ ۖ وَهُوَ أَرْحَمُ الرَّاحِمِينَ ﴿٩٢﴾

 “Hakuna lawama juu yenu leo. Allaah Atakughufurieni. Naye ni Mbora zaidi wa kurehemu kuliko wengine wote wenye kurehemu.” [Yuwsuf: 92]

 

 

Na pale Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) aliporudi Twaaif baada ya kufukuzwa kwa kupigwa mawe akamjia Malaika kumuuliza kama anataka awaangushie majabali mawili watu wa Twaaif waangamizwe. Lakini yeye alikataa akajibu: ((Bali nataraji Allaah Atoe katika migongo yao mwenye kumuabudu Allaah peke Yake bila ya kumshirikisha na chochote)) [Al-Bukhaariy, Muslim]

 

 Pia subira ya Nabiy Ayyuwb ('Alayhis-Salaam) aliyefikwa na mitihani ya kila aina; maradhi aliyouguwa miaka kumi na nane, msiba wa kuondokewa na watoto na mali yake yote, lakini juu ya hivyo alivumilia bila ya kulalamika, bali aliendelea bila ya kusita na ‘ibaadah zake na huku akimshukuru Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) hadi mwishowe aliomba ni:

 

 أَنِّي مَسَّنِيَ الضُّرُّ وَأَنتَ أَرْحَمُ الرَّاحِمِينَ ﴿٨٣﴾

 “Hakika mimi imenigusa dhara, Nawe Ndiye Mbora zaidi wa kurehemu kuliko wengine wote wenye kurehemu”. [Al-Anbiyaa: 83]

 

 

Nabiy Ibraahiym pia watu wake walipoumuingiza katika moto akavumilia na kutawakali kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Ambaye Aliubadilisha moto kuwa baridi. Na pindi alipomlingania baba yake kwa maneno mazuri ya adabu, heshima, hikma na ujuzi aache kuabudu masanamu [Maryam: 41-45]  lakini jibu la baba yake likawa:

 

 أَرَاغِبٌ أَنتَ عَنْ آلِهَتِي يَا إِبْرَاهِيمُ ۖ لَئِن لَّمْ تَنتَهِ لَأَرْجُمَنَّكَ ۖ وَاهْجُرْنِي مَلِيًّا ﴿٤٦﴾

 “Unachukia waabudiwa wangu ee Ibraahiym? Usipokoma, bila shaka nitakupiga mawe; na niondokelee mbali kwa muda mrefu!” [Maryam: 46]

 

 

Juu ya ujeuri na tisho la baba yake, Ibraahiym ('Alayhis-Salaam)  hakulipiza ujeuri bali alivumilia na akamjibu kwa upole kabisa na kumtakia amani:

 

 سَلَامٌ عَلَيْكَ ۖ سَأَسْتَغْفِرُ لَكَ رَبِّي ۖ إِنَّهُ كَانَ بِي حَفِيًّا ﴿٤٧﴾

 “Amani iwe juu yako. Nitakuombea maghfirah kwa Rabb wangu. Hakika Yeye daima kwangu ni Mwenye huruma sana.”

 

 وَأَعْتَزِلُكُمْ وَمَا تَدْعُونَ مِن دُونِ اللَّـهِ وَأَدْعُو رَبِّي عَسَىٰ أَلَّا أَكُونَ بِدُعَاءِ رَبِّي شَقِيًّا ﴿٤٨﴾

 “Na natengana nanyi na mnavyoviomba pasi na Allaah; na namuomba Rabb wangu asaa nisijekuwa kwa kumwomba Rabb wangu, mwenye kukosa baraka.” [Maryam: 47-48]

 

 

 Subira Njema Katika Utiifu

 

Subira katika utiifu ni bora zaidi mbele ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)  kuliko subira katika misiba na mitihani kwa sababu subira ya misiba na mitihani ni subira ya kulazimika mtu kutokana na majaaliwa, kwa maana hana budi nayo wala hana khiari ya kuyakataa. Ama subira katika utiifu na kujiepusha na maasi ni subira ya khiari yake mtu, na hiyo inahitaji azimio la nguvu. Mfano Nabiy Yuwsuf ('Alayhis-Salaam) alipomkataa mke wa al-‘aziyz pale alipomtongoza ilhali mwanamke huyo alikuwa ni mwenye uzuri na mali na kisha walikuwa peke yao wawili chumbani. Hali kama hiyo ni nyepesi kabisa kumpeleka mtu katika maasi, lakini pale mtu anapomlaani shaytwaan na akaacha kuiendekeza nafsi na matamanio, basi hiyo ndio aina ya subira njema.

 

 

Pia, Siku ya Fat-h (ushindi wa) Makkah walipokamatwa makafiri mbele ya Ka’bah baada ya kuwa walimfanyia Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kila aina ya maudhi na kila njia za kumzuia asilinganie risala ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa), na wakamfukuza Makkah – basi siku hiyo walidhania kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) atalipiza kisasi, lakini aliwaambia: ((Nendeni, nyinyi mmeachiwa huru)) Yaani nimekusameheni [Ar-Rahiyq Al-Makhtuwm] 

 

 Hali kadhalika, kijana anapokuwa hana uwezo wa kuoa, akazuia matamanio yake kwa kufuata amri ya Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam):

 

 عن عبد الله بن مسعود (رضي الله عنه) قال: كُنَّا مَعَ رَسُول اللَّه صَلَّى اللَّه عَلَيْهِ وَسَلَّمَ  شباباً لا نجد شيئا   فَقَالَ لَنَا: ((يَا مَعْشَرَ الشَّبَابِ مَنِ اسْتَطَاعَ مِنْكُمُ البَاءَةَ فَلْيَتَزَوَّجْ، فَإِنَّهُ أَغَضُّ لِلْبَصَرِ، وَأَحْصَنُ لِلْفَرجِ، وَمَنْ لَمْ يَسْتَطِيعْ فَعَلَيْهِ بِالصَّوْمِ، فَإِنَّهُ لَهُ وَجَاءٌ.)) رواه البخاري ومسلم .

Imepokelewa kutoka kwa ‘Abdullaah bin Mas’uwd   (Radhwiya Allaahu 'anhu)  “Tulikuwa na Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na hali bado ni vijana na hatuna uwezo wa mali. Basi akatuambia: ((Enyi vijana! Mwenye kuweza kuoa na aoe, kwani kuoa kunamsaidia yeye kuinamisha macho yake [kutotazama ya haraam] na kuhifadhi tupu yake [kutofanya zinaa na uchafu mwingine], na yule asiye na uwezo wa kuoa, afunge, maana swawm hupunguza matamanio ya kimwili)) [Al-Bukhaariy, Muslim]

 

 Zaidi ya hayo ni kwamba  Subira Njema ni pale mwanzo tu pindi mtu anapopata habari ya msiba kama ilivyothibiti katika kisa cha mwanamke aliyekuwa akilia mbele ya kaburi la kipenzi chake.  Rejea Mlango wa ‘Subira Katika Mitihani Kwa Ujumla’

 

 Kauli za Salaf Kuhusu Subira:

 

 ‘Umar (Radhwiya Allaahu 'anhu):  “Maisha yaliyokuwa bora kabisa kwetu ni yale tuliyokumbana  na subira”

 

Hasan Al-Baswry: “Subira ni hazina miongoni mwa hazina. Lakini Allaah Hampi mtu isipokuwa mja karimu mbele Yake”

 

 ‘Umar bin ‘Abdil-‘Aziyz: “Hakuna neema yoyote Anayomneemsha Allaah mja Wake kisha akaiondoa na badala yake Akambadilishia kwa subira, ila huwa ile Aliyoibadilisha (mtihani na misiba) huwa ni kheri kuliko Aliyoiondoa (neema)”

 

Ibnul-Qayyim katika Madaarij As-Saalikiyn: “Subira imehusishwa na  yakini, iymaan, taqwa, kutawakali, shukurani, ‘amali njema na rahmah. Na ndio maana subira ikawa kama sehemu ya kichwa na iymaan ikawa kama mwili, na hivyo hakuna iymaan kwa asiyekuwa na subira kama vile haiwezekani kuweko mwili bila ya kichwa”

 

 

Share