Allaah Huteremka Kwenye Mbingu Ya Dunia Theluthi Ya Mwisho Ya Usiku

 

 

Allaah Huteremka Kwenye Mbingu Ya Dunia Theluthi Ya Mwisho Ya Usiku

 

Alhidaaya.com

 

 

 

Imaam Maalik (Rahimahu Allaah) anaeleza kuhusu kushuka kwa Allaah jwa maelezo yenye vipengele vinne:

 

1. Kushuka ni jambo lenye kufahamika vizuri.

 

2. Namna halisi ya kushuka kwa Allaah haijulikani kwetu.

 

3.  Imani ya jambo hilo ni jambo la Waajib.

 

4. Kutafuta undani wake ni hambo la uzushi (bid’ah).

 

Shaykh Al-Islaam Ibn Taymiyyah (Rahimahu Allaah) amezungumzia maelezo kwa kirefu - kuhusu shubuhaat za watu wa Jahmiyyah - kwenye kitabu chake “Sharh Hadiyth an-Nuzuwl” karibu na mwisho wa kitabu hicho (uk. 320 na kuendelea mbele) na katika msingi wa jambo hili ni kuwa swali kama hilo huja pale wakati mtu anapofikiria na kuoanisha namna au aina ya kushuka kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)  na kuufananisha na kule kushuka au kuteremka kiumbe. Na wakati mtu anapoanza kufikiria hivyo ndipo mashaka na utata unapoanza. Kama alivyosema Imaam Maalik (Rahimahu Allaah) kuhusiana na Istiwaa (Yuko juu kwa namna inayolingana na Utukufu Wake Yeye Mwenyewe Allaah. .) na alivyosema Abua Ja’afar At-Tirmidhiy (Faqiyh wa Baghdaad) kama alivyonukuliwa na Imaam Adh-Dhahabiy katika ‘Al-‘Uluww’ (uk. 231), kuhusiana na ‘kushuka’:

“Kushuka (nuzuwl) ni jambo lenye kufahamika (ma’aquwl), na namna yake (kayf) haifahamiki (majhuwl), na kuamini jambo hilo ni Waajib, na kuliulizia ni uzushi (bid’ah).”

 

Na kifupi, tunajua ya kwamba:

 

- Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)  huteremka bila ya kuondoka kutoka kwenye

‘Arshi, yeye hubakia juu ya ‘Arshi.

 

 

- Allaah huteremka bila ya kuwa chini ya Pepo zake, kama watangu wema waliotangulia (Salaf) mbele ya Allaah waliwaambia Majahmiyyah waliotilia shaka jambo hili la Allaah kuteremka: “Tunamuamini Rabb Ambaye Anafanya Atakalo.”

 

- Kwa watu wote ulimwenguni na pembe zote za dunia, juu ya kuwa na tafauti za masaa mchana na usiku, kuteremka kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)  ni katika robo ya tatu ya usiku wao na hatuwezi kujua jambo hili Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)  Analifanya vipi -kama ambavyo hatujui namna Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)  Atawafanyia hesabu wanaadamu wote siku ya Qiyaamah kwa wakati mmoja.

 

Ibn Taymiyyah akasema tena:

“Ama huko kuteremka kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)  si kama kuteremka kwa waja wa Allaah yaani binaadamu, kwa hivyo si kwamba haiwezekani kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)  kufanyika hilo (la kushuka) kwa wakati mmoja kwa viumbe wengi… na hili ni kama vile wakati wa Hesabu Atakapowahesabia waja Wake Siku ya Hesabu. Atawahesabia wote kwa muda na wakati mmoja, na wote watakuwa pekee na Yeye tu, kama ambavyo mtu anapokuwa Mwenyewe Pekee na mwezi katika usiku unaong’aa, na Atathibitisha Aayah Zake, na kila mmoja atakapokuwa anafanyiwa Hesabu, mwenziwe aliye pembeni yake hatojua hilo. [uk. 334].

 

Kisha Ibn Taymiyyah akatoa Hadiyth kadhaa kuhusiana na hilo, mojawapo ni Hadiyth inayozungumzia Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)  Anapomjibu mja Wake pale anaposoma Suwratul Faatihah akiwa katika Swalaah. Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)  Anasema, “Mja Wangu ananisifu Mimi’’ na kuendelea… na jambo hili ni kwa kila mtu ambaye yuko kwenye Swalaah (Allaah Anamjibu), kwa wakati mmoja, na hivyo ndivyo Allaah Anawaona watu wote kwa mara moja na akawakidhia haja zao wote  kwa mara moja. Na ndio hivyo hivyo hali ya kushuka Kwake Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)  - basi ikiwa tutaondosha ile shaka ya vipi (namna) Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)  huteremka ambayo tumekatazwa nayo, nayo ni ile ya kutaka kufananisha ushukaji Wake Allaah na ule ushukaji au uteremkaji wa kiumbe - basi tutakuwa hatuna tena shaka ya kuteremka huko kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)  hivyo tutakuwa tumethibitisha bila ya tashbiyh wala tamthiyl na bila ya shaka yoyote  juu ya hilo.

 

Na yote haya yanamtosheleza Muumin ambaye amezikubali sifa zote za Allaah Alizojipa Mwenyewe Allaah bila takyif wala ta’atwiyl wala tamthiyl.

 

Hapa Tutaona Athar Ya Imaam Maalik (Rahimahu Allaah) Kuhusiana Na Haya

 

Ametuhadithia Yahya bin Yahya At-Tamiymiy na Ja’afar bin ‘Abdillaah na wengine miongoni mwao walisema:

 

Tulikuwa pamoja na Imaam Maalik akatokea mtu mmoja akamuuliza? Yaa Aba-Abdillaah! Allaah aliyetukuka ‘Istawaa’ (yuko juu) kwenye ‘Arshi Yake (kwa namna inayolingana na Utukufu Wake Yeye mwenyewe Allaah) (Twaahaa 20: 5). Je, vipi Yeye Allaah Istawaa? Imaam Maalik aliinamisha kichwa chake chini kwa muda mrefu mpaka akalowa na jasho. Kisha akasema:

 

 “Al-Istiwaa (kuwa Kwake juu ya ‘Arshi) ni jambo ma’aquwl (linajulikana); ‘Vipi’ ni majhuwl (hakujulikani, hakuwaziki); na kuamini hilo ni Waajib (lazima); na kuuliza au kuhoji hilo ni bid’ah (uzushi); na nina hofu kuwa wewe si zaidi ila mzushi.”   Kisha akaamrisha mtu huyo atolewe kwenye darsa lake.

[Shaykh Al-Albaaniy (Rahimahu Allaah) amesema Hadiyth hii ni sahihi.

(Tazama Mukhthasar Al-Uluww cha Imaam Adh-Dhahabiy (Rahimahu ALlaah) iliyopitiwa na Shaykh Naaswir (Rahimahu Allaah). Uk. 131]

 

 

Yafuatayo Ni Maelezo Kutoka Kitabu ‘Kitaabul ‘Ilm Cha Shaykh Ibn ‘Uthaymiyn (Rahimahu Allaah) Uk. 47-48

 

 

 “Rabb wetu Huteremka (kwa namna inavyolingana na utukufu Wake) kila siku katika mbingu ya dunia inapobakia thuluthi ya mwisho ya usiku na Husema: Nani ananiomba du’aa Nimuitike? Nani Ananiomba jambo Nimpe? Nani ananiomba maghfirah Nimghufurie?)) [Al-Bukhaariy, M

 

 

Hadiyth ya Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na inajulikana wazi. Hakuna katika Maswahaba wake Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)  hata mmoja aliyehoji au kuleta kipingamizi kwa kumwambia Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam): “Vipi Allaah huteremka na je huacha ‘Arshi Yake au hapana? Na wala hakukuwa na maswali mfano wa hayo kutoka kwa Maswahaba. Hata hivyo, tunaona watu wakizungumza na kuuliza maswali kama, “Iweje Yuko juu ya ‘Arshi na kisha tena Ashuke chini kwenye mbingu ya chini kabisa? Na maswali ya upinzani mfano wa hilo! Lakini hapo hapo utawaona watu hao wakiwa wanaikubali Hadiyth hiyo na wanakubali kuwa Allaah Yuko juu ya ‘Arsh, na kupanda au kuwa juu ni kule kunakolingana na Utukufu Wake, na hushuka Yeye (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Anavyotaka Mwenyewe, na hayo yanavunja na kuondosha mashaka yao ambayo yanawachanganya na kuwatatiza kwa yale ambayo Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amewafahamisha wao kumhusu Rabb wao.

 

Kwa hivyo ndugu Muislamu ni wajibu wetu kukubali yale Allaah (‘Azza wa Jallah) na Rasuli Wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) waliyotujulisha nayo yanayotokana na yale tusiyokuwa na ujuzi nayo (Ghayb) kwa moyo wetu wote na kuyatii kikamilifu, na kisha tusiwe ni wenye kupinga kwa kuendekeza yale ya kutokana na akili zetu yaliyotawaliwa na hisia zetu na ufahamu wetu wa kifalsafa. Kwani mas-alah ya Ghayb, yako mbali na upeo wa fahamu zetu. Na mifano kuhusiana na haya ni mingi, na sihitajii kurefusha kuitaja.

 

Kwa nafasi ya Muumin anapoletewa Hadiyth kama hii ni kuikubali kikamilifu kwa kusema Allaah na Rasuli Wake (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) wamesema kweli, kama Allaah Anavyosema:

 

آمَنَ الرَّسُولُ بِمَا أُنزِلَ إِلَيْهِ مِن رَّبِّهِ وَالْمُؤْمِنُونَ ۚ كُلٌّ آمَنَ بِاللَّـهِ وَمَلَائِكَتِهِ وَكُتُبِهِ وَرُسُلِهِ لَا نُفَرِّقُ بَيْنَ أَحَدٍ مِّن رُّسُلِهِ ۚ وَقَالُوا سَمِعْنَا وَأَطَعْنَا ۖ غُفْرَانَكَ رَبَّنَا وَإِلَيْكَ الْمَصِيرُ ﴿٢٨٥﴾

Rasuli ameamini yaliyoteremshwa kwake kutoka kwa Rabb wake na Waumini (pia). Wote wamemwamini Allaah, na Malaika Wake, na Vitabu Vyake, na Rusuli Wake. (Nao husema): “Hatutofautishi baina ya yeyote kati ya Rusuli Wake.” Na wakasema: “Tumesikia na tumetii, tunakuomba maghfirah Rabb wetu na Kwako ni mahali pa kuishia.  [Al-Baqarah: 285]

 

 

 

 

Share