Shukurani Kwa Allaah - Kisa Katika Hadiyth Kuhusu Mkoma, Kipara Na Kipofu

Shukurani Kwa Allaah - Kisa Katika Hadiyth Kuhusu Mkoma, Kipara Na Kipofu

 

Alhidaaya.com

 

 

Hakika neema za Allaah (سبحانه وتعالى) ni nyingi mno hazihesabiki kama Anavyotaja Mwenyewe katika Qur-aan. Yeye Ndiye mtoaji rizki zote na Mwenye kudabiri (kuendesha) mambo yote. Lakini wengi miongoni mwa waja Wake hawashukuru, sababu; kuna baadhi ya watu hujaaliwa neema lakini hawatafakari wala kutambua kwamba inatoka kwa Allaah Pekee. Ikiwa ni neema ya mali, watoto, chakula, uhai, siha, hata kubakia katika usalama, amani na furaha ya nafsi nayo pia ni neema. Wengine hujaaliwa neema kadhaa na kadhaa lakini humshukuru mwengine. Wengine wanakanusha kabisa kwamba neema waliyojaaliwa ni kutoka kwa Allaah (سبحانه وتعالى). Bali wengine hujaaliwa neema Zake lakini wanamshirikisha Allaah (سبحانه وتعالى).   Anasema hivyo katika kauli Yake:

 

 ((وَمَا بِكُم مِّن نِّعْمَةٍ فَمِنَ اللّهِ ثُمَّ إِذَا مَسَّكُمُ الضُّرُّ فَإِلَيْهِ تَجْأَرُونَ  ((((ثُمَّ إِذَا كَشَفَ الضُّرَّ عَنكُمْ إِذَا فَرِيقٌ مِّنكُم بِرَبِّهِمْ يُشْرِكُونَ)) ((لِيَكْفُرُواْ بِمَا آتَيْنَاهُمْ فَتَمَتَّعُواْ فَسَوْفَ تَعْلَمُون))  

 

((Na neema yoyote mliyonayo basi imetoka kwa Allaah [na nyinyi hamumshukuru]. Kisha inapokuguseni dhara mara Yeye mnamlilia [mnamlalamikia])). Kisha Anapokuondeleeni hiyo dhara, mara kundi moja miongoni mwenu linamshirikisha [tena] Rabb wao)) ((Wanazikanusha zile neema Tulizowapa, basi stareheni kidogo, karibuni mtajua [malipo yenu ya ubaya wenu])) [An-Nahl 16: 53-55]

 

Kisa kifuatacho cha watu watatu waliojaaliwa neema za Allaah (سبحانه وتعالى) kinatupa mfano na mafunzo kuhusu kukanusha au kushukuru neema Zake Ta’aalaa. Nacho ni kisa katika Hadiyth ya Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم):

 

عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ أَنَّهُ سَمِعَ رَسُولَ اللَّهِ (صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ) يَقُولُ: ((إِنَّ ثَلاثَةً مِنْ بَنِي إِسْرَائِيلَ أَبْرَصَ وَأَقْرَعَ وَأَعْمَى، فَأَرَادَ اللَّهُ أَنَّ يَبْتَلِيَهُمْ،  فَبَعَثَ إِلَيْهِمْ مَلَكًا. فَأَتَى الأَبْرَصَ فَقَالَ: أَيُّ شَيْءٍ أَحَبُّ إِلَيْكَ؟ قَالَ: لَوْنٌ حَسَنٌ وَجِلْدٌ حَسَنٌ وَيَذْهَبُ عَنِّي الَّذِي قَدْ قَذَرَنِي النَّاسُ بِهِ. قَالَ: فَمَسَحَهُ، فَذَهَبَ عَنْهُ قَذَرَهُ، فَأُعْطِيَ لَوْنًا حَسَنًا وَجِلْدًا حَسَنًا. قَالَ: فَأَيُّ الْمَالِ أَحَبُّ إِلَيْكَ؟ قَالَ الإِبِلُ أَوْ الْبَقَرُ (شَكَّ إِسْحَاقُ)، فَأُعْطِيَ نَاقَةً عُشَرَاءَ، وَقَالَ بَارِكَ اللَّهُ لَكَ فِيهَا.

قَالَ: فَأَتَى الأَقْرَعَ فَقَالَ: أَيُّ شَيْءٍ أَحَبُّ إِلَيْكَ؟ قَالَ: شَعْرٌ حَسَنٌ ، وَيَذْهَبُ عَنِّي الَّذِي قَدْ قَذَرَنِي النَّاسُ بِهِ. فَمَسَحَهُ فَذَهَبَ عَنْهُ، وَأُعْطِيَ شَعْرًا حَسَنًا. فَقَالَ: أَيُّ الْمَالِ أَحَبُّ إِلَيْكَ؟ قَالَ: الْبَقَرُ أَوْ الإِبِلُ. فَأُعْطِيَ بَقَرَةً حَامِلاً، قَالَ: بَارِكَ اللَّهُ لَكَ فِيهَا .

فَأَتَى الأَعْمَى، فَقَالَ: أَيُّ شَيْءٍ أَحَبُّ إِلَيْكَ؟ قَالَ: أَنْ يَرُدَّ اللَّهُ إِلَيَّ بَصَرِي فَأُبْصِرُ بِهِ النَّاسَ، فَمَسَحَهُ فَرَدَّ اللَّهُ إِلَيْهِ بَصَرَهُ، قَالَ: فَأَيُّ الْمَالِ أَحَبُّ إِلَيْكَ؟ قَالَ: الْغَنَمُ،  فَأُعْطِيَ شَاةً وَالِدًا، فَأُنْتَجَ هَذَانِ وَوَلَّدَ هَذَا، فَكَانَ لِهَذَا وَادٍ مِنَ الإِبِلِ وَلِهَذَا وَادٍ مِنَ الْبَقَرِ، وَلِهَذَا وَادٍ مِنَ الْغَنَمِ.

قَالَ:  ثُمَّ إِنَّهُ أَتَى الأَبْرَصَ فِي صُورَتِهِ وَهَيْئَتِهِ، فَقَالَ: رَجُلٌ مِسْكِينٌ وَابْنُ سَبِيلٍ قَدْ اِنْقَطَعَتْ بِيَ الْحِبَالُ فِي سَفَرِي; فَلا بَلاغَ لِيَ الْيَوْمَ إِلاَّ بِاللَّهِ ثُمَّ بِكَ، أَسْأَلُكَ بِالَّذِي أَعْطَاكَ اللَّوْنَ الْحَسَنَ وَالْجِلْدَ الْحَسَنَ وَالْمَالَ،  بَعِيرًا أَتَبَلَّغُ بِهِ فِي سَفَرِي، فَقَالَ: الْحُقُوقُ كَثِيرَةٌ. فَقَالَ لَهُ كَأَنِّي أَعْرِفُكَ! أَلَمْ تَكُنْ أَبْرَصَ يَقْذَرُكَ النَّاسُ، فَقِيرًا، فَأَعْطَاكَ اللَّهُ عَزَّ وَجَلَّ الْمَالَ؟ فَقَالَ: إِنَّمَا وَرِثْتُ هَذَا الْمَالَ كَابِرًا عَنْ كَابِرٍ. فَقَالَ: إِنْ كُنْتَ كَاذِبًا فَصَيَّرَكَ اللَّهُ إِلَى مَا كُنْتَ.

قَالَ:ثُمَّ إِنَّهُ أَتَى الأَقْرَعَ فِي صُورَتِهِ، فَقَالَ لَهُ مِثْلَ مَا قَالَ لِهَذَا، وَرَدَّ عَلَيْهِ مِثْلَ مَا رَدَّ عَلَيْهِ هَذَا، فَقَالَ إِنْ كُنْتَ كَاذِبًا، فَصَيَّرَكَ اللَّهُ إِلَى مَا كُنْتَ.

 قَالَ "وَأَتَى الأَعْمَى فِي صُورَتِهِ فَقَالَ: رَجُلٌ مِسْكِينٌ وَابْنُ سَبِيلٍ قَدْ اِنْقَطَعَتْ بِيَ الْحِبَالُ فِي سَفَرِي ; فَلا بَلاغَ لِيَ الْيَوْمَ إِلاَّ بِاللَّهِ ثُمَّ بِكَ، أَسْأَلُكَ بالَّذِي رَدَّ عَلَيْكَ بَصَرَكَ; شَاةً أَتَبَلَّغُ بِهَا فِي سَفَرِي. فَقَالَ قَدْ كُنْتُ أَعْمَى فَرَدَّ اللَّهُ إِلَيَّ بَصَرِي، فَخُذْ مَا شِئْتَ، وَدَعْ مَا شِئْتَ فَوَاللَّهِ لاَ أَجْهَدُكَ الْيَوْمَ بِشَيْءٍ أَخَذْتَهُ لِلَّهِ. فَقَالَ: أَمْسِكْ مَالَكَ، فَإِنَّمَا ابْتُلِيتُمْ،  فَقَدْ رَضِيَ اللَّهُ عَنْكَ، وَسَخِطَ عَلَى صَاحِبَيْكَ))

 

Na imepokewa toka kwa Abu Hurayrah (رضي الله عنه) kwamba kamsikia Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) akisema: ((Allaah alitaka kuwajaribu watu watatu katika wana wa Israaiyl; mkoma, kipofu na kipara Akawatumia Malaika. Akamwendea mkoma akamuuliza: Kitu gani ukipendacho mno? Akajibu: Rangi na ngozi nzuri [ya mwili], na uniondokee [ukoma] niliokuwa nao unaowakera watu. Akasema: [Malaika] Akamgusa ukamuondokea ugonjwa akapewa rangi na ngozi nzuri. Akamuuliza: Mali ipi upendayo zaidi? Akajibu: Ngamia au ng’ombe. [Msimuliaji Is-haaq hana uhakika ni yupi] Basi mwenye ukoma akapewa ngamia jike mwenye mimba. [Malaika] Akasema [kumuombea]: “Allaah Akubarikie navyo.

Kisha Malaika akaenda kwa kipara akamuuliza: Kitu gani ukipendacho mno? Akajibu: Nywele nzuri na kiniondokee [kipara] kinachowakera watu. Akamgusa, kikamuondoka [kipara] akapewa nywele nzuri. Akamuuliza: Mali ipi upendayo zaidi? Akajibu: Ng’ombe au ngamia. Akapewa ng’ombe jike mwenye mimba. Akasema [kumuombea]: Allaah Akubarikie navyo.

Akamwendea kipofu: Akamuuliza: Kitu gani ukipendacho mno? Akajibu: Allaah Anirudishie macho yangu nipate kuwaona watu. Akamgusa, Allaah Akamrudishia macho yake. Akamuuliza: Mali ipi uipendayo zaidi? Akajibu: Mbuzi. Akapewa mbuzi mwenye mimba. Baada ya hapo, wanyama wote watatu wakazaa na kuzaliana hadi kwamba kila mmoja alikuwa na bonde la ngamia, na mwengine bonde la ng’ombe na mwengine bonde la mbuzi.

Akasema: Kisha [Malaika] akamrudia mkoma akiwa katika hali kama yake ya mtu mwenye ukoma. Akasema: Mimi ni masikini, nimekatikiwa na nyenzo zangu safarini, kwa hiyo sina leo wa kunitimizia isipokuwa Allaah kisha wewe. Nakuomba kwa Ambaye Amekupa rangi na ngozi nzuri, na mali, unigawie ngamia ili anifikishe katika safari yangu. Akajibu: Nina majukumu mengi [kwa hiyo siwezi kukupa kitu!]. [Malaika] Akasema: Kana kwamba nakujua? Si wewe uliyekuwa na ukoma wakikereka watu, na ulikuwa masikini kisha Allaah (عز وجل) [Aliyetukuka na Mwenye Ujalali] Akakupa mali [yote hii]? Akajibu: [Hapana ni uongo!] Hakika nimerithi yote hayo kwa mababu zangu. [Malaika] akasema: Ikiwa unasema uongo, basi Allaah Akurudishe kama ulivyokuwa awali.

 

Akamwendea aliyenyonyoka nywele (kipara) akiwa katika hali kama yake ya mtu mwenye kipara. Akamuuliza kama alivyomuuliza huyu [mwenye ukoma], naye akamjibu kama alivyojibu naye. Akamwambia: Ikiwa unasema uongo, basi Allaah Akurudishe kama ulivyokuwa awali. 

 

Akasema: Akamwendea kipofu akiwa katika hali kama yake ya mtu kipofu. Akamwambia: Mimi ni masikini na msafiri, nimekatikiwa na nyenzo zangu safarini, kwa hiyo sina leo wa kunitimizia isipokuwa Allaah kisha wewe. Nakuomba kwa Ambaye Amekupa macho yako, unigawie mbuzi ili anifikishe katika safari yangu. Akajibu: Bila shaka! Nilikuwa kipofu na Allaah Akanirudishia macho yangu [na nilikuwa masikini Allaah Akanitajirisha]. Chukua utakacho, na acha utakacho, kwani wa-Allaahi sitakuzuia chochote [unachohitaji] kuchukua kwa ajili ya Allaah. Akasema [kumuombea]: Weka mali yako, kwani hakika mmejaribiwa, na hakika Allaah Ameridhika nawe na Amewaghadhibikia wenzako))[Al-Bukhaariy na Muslim]

 

Basi nasi tujiulize kama tunamshukuru Allaah (سبحانه وتعالى) kwa neema Zake zote, hata ya neema ya kuvuta pumzi moja ya uhai ambayo ni kubwa mno!  Tujitahidi kumshukuru kwa wingi kwani ni wachache mno wanaotafakari neema za Muumba wao kama Anavyosema Mwenyewe katika kauli Yake:

((وَقَلِيلٌ مِّنْ عِبَادِيَ الشَّكُورُ))

((Na ni wachache wanaoshukuru katika waja Wangu)) [Sabaa 34: 13]

 

 

 

Share