Fadhila Za Mwezi Wa Ramadhwaan

 

Fadhila Za Mwezi Wa Ramadhwaan

 

 Ummu Faraj

  

  Alhidaaya.com

 

 

 

Sifa njema zote Anastahiki Allaah Rabb wa viumbe vyote na Swalah na salamu zimfikie Nabiy wetu na kipenzi chetu Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na aali zake na sahaba zake wote.

  

Ama kwa hakika katika mwezi wa Ramadhwaan kuna fadhila nyingi ambazo mimi nitazitaja kwa uchache namuomba Allaah Aniwafikishe 'asaa yawe na manufaa katika Duniya na Akhera.

 

 

1)-  Ni Mwezi Wa Qur-aan

 

Kama Alivyosema Allaah Mtukufu:

  

شَهْرُ رَمَضَانَ الَّذِي أُنزِلَ فِيهِ الْقُرْآنُ هُدًى لِّلنَّاسِ وَبَيِّنَاتٍ مِّنَ الْهُدَىٰ وَالْفُرْقَانِ ۚ 

Mwezi wa Ramadhwaan ambao imeteremshwa humo Qur-aan ili iwe mwongozo kwa watu na hoja bayana za mwongozo na pambanuo (la haki na batili). [Al-Baqarah:185]

 

Vilevile kama ilivyopokewa na Ibn 'Abbaas (Radhwiya Allaahu 'anhu) kuwa  makusudiyo yake   kwa hakika kuteremshiwa Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi aalihi wa sallam) Qur-aan mwanzo ni katika mwezi wa Ramadhwaan na vilevile Qur-aan mwanzo wa kuteremka ni usiku wa Laylatul-Qadir na Laylatul-Qadir iko katika mwezi wa Ramadhwaan.

 

Hivyo basi ni juu yetu kufanya juhudi katika mwezi huu kukithirisha sana kusoma Qur-aan.  Walikua Salafus-Swaalih (Wema Waliotangulia) wakikilinda kitabu cha Allaah kwa kukisoma na kuyafanyia kazi yaliyokuwemo kwa mazingatiyo. Pia Tunaambiwa kuwa Sayyidnaa Jibriyl (‘Alayhis-salaam) akimfundisha Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) Qur-aan katika mwezi wa Ramadhwaan, na alikuwa 'Uthmaan bin 'Afaan (Radhwiya Allaahu 'anhu)  kila siku akisoma Qur-aan yote yaani anakhitimisha mara moja kwa siku,  kwa maana,  msahafu mzima anausoma kwa siku moja. Na walikuwa baadhi yao katika wema wakisoma Qur-aan yote kwa siku tatu, wengine kwa wiki moja na wengine kwa siku kumi. Walikuwa wakisoma Qur-aan ndani ya Swalah na nje ya Swalah.

 

Allaah Atuwafiqishe mimi na wewe tuisome Qur-aan na kwa mazingatio khasa katika mwezi huu tufanye juhudi sana ili tuweze kupata fadhila za mwezi huu mtukufu.

 

 

2)-   Ni Mwezi Wa Subira

 

Subira ni katika jambo gumu na halipati ila kwa mtu mchaji Allaah na mnyenyekevu kwa Allaah. Na katika kufunga kunatakiwa subira pale mtu anapojizuilia kutokana na kutokula, kunywa, matamanio na mengineyo. Imekua Swawm ni nusu ya subira na subira malipo yake ni pepo kama alivyosema Allaah Mtukufu:

ۗ إِنَّمَا يُوَفَّى الصَّابِرُونَ أَجْرَهُم بِغَيْرِ حِسَابٍ ﴿١٠﴾

Hakika wanaosubiri watalipwa kikamilifu ujira wao bila ya hesabu. [Qur-aan 39:10]

 

 

3)- Milango Ya Moto Inafungwa, Milango Ya Jannah Inafunguliwa Na Mashetani Wanafungwa

 

 

Kama ilivyokuja katika Hadiyth iliyopokelewa na Imamu wawili:

 

Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam) amesema, "Pindi inapokuja Ramadhwaan inafunguliwa milango ya jannah, na hufungwa milango ya moto, na mashetani wanafungwa kwa Minyororo." [Imesimuliwa na Al-Bukhaariy na Muslim]

 

 

Kwa hakika utaona katika mwezi huu watu wengi wanajitahidi kujiepusha na maasi, watu wanajaa misikitini kwa kufanya ibada ya mwezi huu hii ni kwa sababu mashetani wamefungwa na shetani juu ya uasi wake lakini anauogopa mwezi wa Ramadhwaan na vitimbi vyake vinakuwa dhaifu ndio mana wengi nyoyo zinabadilika wanaswali  na kujitahidi kufanya kheri.  Lakini ikimalizika Ramadhwaan tu basi Swalah imekwisha kama vile Allaah yupo Ramadhwaan tu. Huu ni msiba ndugu zangu Waislamu Allaah Asitujaalie katika hao.

 

 

4)-   Laylatul Qadr

 

Katika mwezi huu kuna siku ya Laylatul-Qadr siku ambayo ni bora kuliko miezi elfu kama Alivyosema Allaah:

 

لَيْلَةُ الْقَدْرِ خَيْرٌ مِّنْ أَلْفِ شَهْرٍ ﴿٣﴾ تَنَزَّلُ الْمَلَائِكَةُ وَالرُّوحُ فِيهَا بِإِذْنِ رَبِّهِم مِّن كُلِّ أَمْرٍ ﴿٤﴾ سَلَامٌ هِيَ حَتَّىٰ مَطْلَعِ الْفَجْرِ ﴿٥﴾

Laylatul-Qadr ni mbora kuliko miezi elfu. Wanateremka humo Malaika na Ar-Ruwh (Jibriyl) kwa idhini ya Rabb wao kwa kila jambo. Amani mpaka kuchomoza Alfajiri. [Al-Qadr: 3-5]

 

 

Imehisabiwa mtu atakapofanya ibada katika usiku huo mmoja ni kama amefanya ibada sawa na miaka 83 na hii ni katika fadhila kubwa kabisa. Na katika kitabu Muwatwaa, Imamu Maalik amesema:

 

 

Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam) ameona umri wa ummah za mwanzo ni mrefu, na umri wa ummah wake ni mfupi akapewa usiku wa Laylatul-Qadr uwe ni bora kuliko miezi elfu. [Muwatwaa, 1/321]

 

 

Hakuna siku tukufu na kubwa kama siku hii ni wajibu kwetu kuutafuta usiku huu katika kumi la mwisho kufanya ibada ili tupate fadhila hizo. Ninamuomba Allaah atuwezeshe kwa hilo, Aamiyn.

 

 

5)-     Du'aa Ni Zenye Kukubaliwa

 

Katika hadiyth iliyopokewa na Imaam Ahmad: Kutoka kwa Jaabir (Radhwiya Allaahu 'anhu) kwa isnadi iliyo nzuri.

 

 

Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam) Amesema: "Kila Muislam du'aa zake ni zenye kukubaliwa atapomuomba katika mwezi wa Ramadhwaan".

 

 

Na imepokewa katika Hadiyth kuwa du'aa ya mwenye kufunga pia ni yenye kukubaliwa. Basi mtu ajipinde katika kumuelekea Allaah kumuomba mambo ya kheri ya dunia na aakhirah aombe jannah ya Jannaatul Firdaus na alete maombi mengine, Allaah Atayapokea maombi yetu, Aamiyn.

 

La mwisho ambalo nitakua nimekamilisha maudhui yangu:

 

 

6)-  Mwezi Huu Ni Mwezi Wa Kutoa

 

Na alikua Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam) akizidisha kheri nyingi katika mwezi wa Ramadhwaan.

 

Imepokewa na At-Tirmidhiy kutoka kwa Anas (Radhwiya Allaahu 'anhu) Kasema Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam) "Bora ya (wakati wa) kutoa sadaqa ni kutoa katika mwezi wa Ramadhwaan".

 

Na imepokewa na Zayd bin Aslam kutoka kwa babake, amesema nimemsikia 'Umar bin Al-Khatwaab (Radhwiya Allaahu 'anhu) anasema, "Ametuamrisha Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam) tutoe sadaqa nikatoa mali yangu nikasema leo nimemtangulia Abu Bakr nimekwenda na nusu ya mali, akasema Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam) kuniambia, "Umewabakishia nini watu wako?" Nikasema, nusu kama hii, na akaja Abu Bakr na kila mali yake Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam) akamuuliza, "Umewabakishia nini watu wako? Akasema, nimewabakishia Allaah na Nabiy wake. Nikasema huyu Abu Bakr hapitiki na kitu chochote abadan"

 

Kuonyesha wema waliotangulia walikua wakishindana katika kheri lakini tofauti kubwa katika zama zetu hizi watu wanashindana katika mambo ya kidunia na kujifakharisha nayo. 

 

 

Tunamuomba Allaah Atuonyeshe mema tuyafuate na mabaya tuyawache na tushindane katika kila kheri ili tuwe ni wenye kufuzu na kupata daraja ya juu ya Jannah.

 

 

Aamiyn.

 

Share