Zingatio 4: Ramadhwaan Alhidaaya Imefika

 

 

Zingatio 4: Ramadhwaan Alhidaaya Imefika

 

Naaswir Haamid

 

 

Alhidaaya.com

 

 

Kutoka Mashariki, Magharibi, Kusini hadi Kaskazini, Ramadhwaan imeshaingia na Alhidaaya imeikaribisha kwa mikono miwili. Kwenu ni kujihimu kuzichuma fadhila za mwezi huu kupitia Alhidaaya kwa kuchukua mafunzo Swahiyh kwa mujibu wa Qur-aan na Sunnah.

 

Yamo mengi ndani ya mtandao huu ambayo utaweza kunufaika nayo, lengo sio jengine bali kusaidiana kuweza kuzipata radhi za Allaah     (Subhaanahu wa Ta’aalaa), kwani Waislamu wote ni ndugu, na lile analolipenda Muislamu ndani ya moyo wake, basi ampendelee hilo hilo kwa Muislamu mwenziwe.

 

Ni mapenzi haya ndiyo yamewafanya ndugu zenu wa Alhidaaya, walio fakiri wa radhi za Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa), kuwasaidia ndugu zao wa jamii ya Kiswahili kuweza kunufaika na Ramadhwaan kupitia mtandao huu.

 

Kuna faida za kusikiliza, kuna orodha ya makala na vitabu vingi mno vya wewe kuweza kunufaika navyo. Usiiache nafasi hii adhimu na duni kabisa. Hakuna shaka yoyote kwamba tumezungukwa na mitandao ambayo imejaa uchafu wa kila aina, na kwa uchungu zaidi ni kwamba hata tovuti za baadhi ya Waislamu, zimeshtadi kwa mambo ya upotofu na uzushi. Hivyo, kaa kitako unufaike kwa mtandao wako wenye kujitahidi kuchunga vipimo vya Uislamu kwa mujibu wa Qur-aan na Sunnah.

 

Hivyo, hakikisha hayakupiti masiku haya matukufu ya Ramadhwaan kwa kuzuru kurasa zilizo humu, kuanzia ukurasa wa mbele hadi wa ndani. Kuwa ni mtundu wa kutaka kuelewa fadhila za Ramadhwaan, kuwa mbunifu wa kujibu Chemsha Bongo; lakini lililo muhimu zaidi ni kuyachukua mafunzo haya kwa vitendo na kwenda kuyafanyia kazi katika kila dakika na siku yako ya Ramadhwaan. Jitengee muda usiku, asubuhi, mchana na jioni kwa kumuomba Rabb wako maghfirah kwa dhati ya moyo wako:

 

Kutoka kwa Jaabir (Radhwiya Allaahu ‘Anhu) amesema Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Kila Muislam du'aa zake ni zenye kukubaliwa atakapomuomba katika mwezi wa Ramadhwaan.)) [Imepokewa na Imaam Ahmad]

 

Basi ndugu zangu, hukumbuki yale uliyoyatenda miezi kumi na moja iliyopita? Kama hujamuomba Rabb wako tawbah wakati huu ambao milango ipo wazi hata kuliko milango ya bahari, utaomba wakati gani mwengine?

 

Muombe maghfirah Rabb wako, kwani Yeye ni mwenye kusikia vilio vyetu na muhimu zaidi ni kwamba Yeye Anayapokea maombi zaidi. Na kwa hakika Rabb wetu Ar-Rahiym, Al-Ghafuwr Anafurahika mno mja Anapotubu mbele Yake.

 

 

Share