Zingatio: Hijjah Wajibu Wetu

 

Zingatio: Hijjah Wajibu Wetu

 

Naaswir Haamid

 

 

Alhidaaya.com

 

 

Rabb wetu Mtukufu, Mwenye hikmah na Mwenye maarifa ya kupambanua, Ametuwekea amali ya Hijjah kuwa ni nguzo ya tano ya Uislamu na Akaifanya juu yetu kuwa ni faradhi, isipokuwa tu kwa yule asiyekuwa na uwezo. Hivyo, mbali ya nguzo nyengine nne, Hijjah inatakiwa kukamilishwa na kwa kila mwenye uwezo, na asipoitekeleza basi atakuwa ni mwenye makosa.

 

 

Nguzo hii imefaradhishwa kwetu kupitia amri ya Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) ndani ya Qur-aan:

 وَلِلَّـهِ عَلَى النَّاسِ حِجُّ الْبَيْتِ مَنِ اسْتَطَاعَ إِلَيْهِ سَبِيلًا ۚ وَمَن كَفَرَ فَإِنَّ اللَّـهَ غَنِيٌّ عَنِ الْعَالَمِينَ ﴿٩٧﴾ 

Na kwa ajili ya Allaah imewajibika watu watekeleze Hajj katika Nyumba hiyo kwa mwenye uwezo. Na atakayekufuru, basi hakika Allaah ni Mkwasi kwa walimwengu. [Aali ‘Imraan–97]

 

 

Naye Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ameeleza:

 

“Fanyeni haraka mukahiji, maana hajui mmoja wenu atapatwa na nini.” [Imepokewa na Ahmad, Al-Bayhaqiy, At-Twahaawiy na Ibn Maajah]

 

 

Hijjah yenye kukubaliwa haina malipo mengine isipokuwa ni kupatiwa Jannah. Na kwa hakika Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Ameiweka Hijjah kuwa ni nguzo ya Uislamu kutokana na umuhimu wake kwa Waislamu na Uislamu kwa ujumla wake. Hijjah tokea maandalizi yake hadi utekelezaji wake, imejaa mambo ambayo Muislamu humpatia ‘ibrah na ukakamavu juu ya umoja wa Waislamu.

 

 

Halikadhalika, ibadah ya Hijjah humrejesha Muislamu katika fikra asili za Uislamu, akautambua namna ulivyoasisiwa Uislamu kupitia kwa Manabii wetu, haswa Nabiy Ibraahiym (‘Alayhis-salaam) na Nabiy wetu Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).

 

 

Ndani ya viwanja vya kufanya tawaaf na ‘Arafah, hakuna tofauti tunayoiona kimavazi kati ya mweusi na mweupe, mtawala na mtawaliwa au tajiri na masikini.

 

 

Basi ni wapi tutaipata fursa ya kushikamana kiudugu wa Uislamu zaidi ya amali ya Hijjah? Ni hasara iliyoje yule ambaye amepatiwa uwezo wa kuhijji akakatisha umri wake, pengine hadi kufa kwake, asiitekeleze amri hii.

 

 

Zile zama ambazo zimejaa fikra kwamba Hijjah ni kwa wazee, ni lazima zifutwe moja kwa moja ndani ya akili za Waislamu. Kwani hata hao vijana wenye kuporomosha majumba ya ghorofa, wakanunua magari ya kifakhari, hawaelewi fika ni lini roho zao zitatolewa.

 

 

Kila mmoja wetu, na zaidi kwa wale waliokuwa hawajaifanya amali hii, ni lazima wajiwekee mikakati madhubuti ya kumuwezesha kumfanikisha kuitekeleza. Inaweza kumbainikia Muislamu kwamba hata mwenye kipato kidogo akaweza kuitekeleza kutokana na akiba anayoiweka awamu baada ya awamu. Basi ni aibu iliyoje kwa yule tajiri kushindwa kuitekeleza amali hii, huku akitoa sababu zisizo na msingi, kwamba mali yake haijafikia kiwango, biashara zake zitaporomoka au familia yake hajaiweka sawa na nyenginezo.

 

 

Twamuomba Rabb Awakubalie Hijjah zao wale waliohijji miaka iliyopita, na kwa mwaka huu, na kwa miaka inayokuja. Na kwa wale waliokuwa hawajaenda kuhijji, Rabb Awajaalie kuwapatia uwezo na kuwapatia nia yenye kuthibiti – Aamiyn.

 

 

 

Share