Ndoa Ya Wazinifu

 

SWALI:

Eti mtu akitembeya na mwanamme yaani boy friend halafu akamuowa, je, ndoa inafaa? Na akizaliwa mtoto inakuwaje ni halali yao mtoto huyo? Insha’Allaah nasubiri majibu.

 


JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Tunamshukuru ndugu yetu ambaye ana thiqah (imani) na sisi kwa kuuliza swali hili na tunaomba tawfiki ya Allaah katika kulijibu swali hili ili lipate kueleweka.

Suala hili ni nyeti sana kwa jamii yetu hasa wakati wa sasa, jamii ambazo zinaishi pamoja na jamii nyinginezo ambazo zina maadili na mila na desturi zinazokwenda kinyume na sisi. Hivyo ni muhimu mwanzo kusikia kauli ya Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) kuwa Mayahudi na Manasara hawataridhika nasi mpaka tufuate mila zao.

}}وَلَن تَرْضَى عَنكَ الْيَهُودُ وَلاَ النَّصَارَى حَتَّى تَتَّبِعَ مِلَّتَهُمْ{{

{{“Mayahudi hawatokuwa radhi nawe, wala Wakristo, mpaka ufuate mila yao”}} (2: 120).

Na ((Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) anasema: “Mtafuata desturi (mwenendo) za waliokuwa kabla yenu shibri kwa shibri na pima kwa pima hata wakiingia katika shimo la mburukenge (yaani ndani ya shimo lenye mnyama anayeweza kukudhuru) mutaingia nao”. Wakauliza: “Je, unakusudia Mayahudi na Manasara?” Akasema: “Ni nani wengine ikiwa si wao”)) (Imesimuliwa na Al Bukhaariy na Muslim kutoka kwa Abu Sa‘iyd al-Khudriy).

Lakini kwa sababu ya udhaifu wa Imani na kuonekana kuwa maaruf imekuwa munkar na munkar imekuwa maaruf na pia ile nadharia ya kwamba mambo yote ya kutoka magharibi ni mazuri tumeanza kuiga bila kuangalia mafundisho ya Dini ya Kiislamu.

Kwa ajili hii Uislamu umefanya ndoa kuwa rahisi na ikafunga milango yote ya kuiendea zina. Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Anasema:

}}وَلاَ تَقْرَبُواْ الزِّنَى إِنَّهُ كَانَ فَاحِشَةً وَسَاء سَبِيلاً{{

{{“Wala msikaribie uzinzi. Hakika huo ni uchafu na njia mbaya”}} ().

Wafasiri wanachambua hivi:

"Amri hii ni kwa mtu binafsi na jamii. Hii haimlindi mtu tu asikaribie uzinifu, lakini pia vitu vinavyopelekea au kuhamasisha hisia. Jamii ina jukumu la kufanya mipango ili kuzuia zinaa na kuondosha zile njia na vishawishi ambazo vinampelekea mtu katika jambo hilo. Katika jambo hili Uislamu kama kawaida umefunga mlango na kufanya haramu zile njia zote ambazo zitampelekea kwayo”.

"Allaah amesema wa laa Taqrabuu ambayo ni kali na ina nguvu zaidi kuliko Laa Taznuu. Kukataa huku ni kwa nguvu zaidi kwa inaharamisha hata vile vianzilishi vya zinaa yenyewe kwa mfano kugusa, kukutana, kuangalia, kuchang’anyikana, na kadhalika”.

Ndio Uislamu ukaweka masharti ambayo yanazuia kuja karibu na uzinzi. Kwa mfano:

1.    Kuinamisha macho chini kwa wanaume na wanawake (Q 24: 30 – 31). Ndio mshairi wa hivi karibuni alisema: “A look, then a smile, then a nod of the head, then a talk, then a promise, then the warmth of the bed – Kutizama, kisha tabasamu, kisha kutingisha kichwa, kisha ni mazungumzo, baadae ni ahadi na mwisho uharara wa kitanda”.

2.    Kuweka vikwazo katika mas’ala ya muziki, dansi ambazo ni vishawishi vya zinaa.

3.    Kukataza vileo na picha za pono (za kuonyesha uchi wa binadamu).

4.    Kukataza khulwah (upweke) baina ya mwanamume na mwanamke ambao si maharimu wako.

((Amesema Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): “Tahadharini na kuingia katika nyumba ambazo wanawake wapo peke yao”. Akasema mtu miongoni mwa Answaar: “Je, unaonaje kuhusu Hamwa (jamaa wa karibu wa mume kama ndugu [shemeji])?” Akasema: “Hamwa ni mauti”)) (al-Bukhaariy, Muslim na at-Tirmidhiy kutoka kwa ‘Uqbah bin ‘Aamir [Radhiya Allaahu ‘anhu]).

Yaani huyu hamwu ni hatari zaidi kwa sababu akiachiwa anakuwa na faragha zaidi. Na matukio mbalimbali yameonekana kwa wingi katika sehemu zetu kutokana na mashemeji.

((Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) anasema tena: “Asikae mmoja wenu peke yake na mwanamke isipokuwa awepo maharimu yake”)) (al-Bukhaariy, Muslim kutoka kwa Ibn ‘Abbaas [Radhiya Allaahu ‘anhuma])

Na katika Hadiyth nyingine: 

((“Hakai mwanamume na mwanamke isipokuwa wa tatu wao ni shetani. Na shetani hutembea katika mwili wa mwanadamu kama vile damu (kwenye mshipa)”.))

5.    Kuvaa nguo za heshima ili kuondoa matamanio pindi munapokutana na mtu wa jinsia nyingine.

Njia hizi zote zikifungwa basi inakuwa shida sana kupatikana tatizo la zinaa na watoto randaranda mitaani na wanawake peke yao (single mothers) ambao hakuna wa kuwasaidia katika jukumu la malezi.

Baada ya yote yaliyotangulia tunaona ya kwamba mas’ala ya girl au boy friend kwa jinsia ya pili yake haikubaliwi. Ule wakati ambao msichana atakuwa anakaa na mvulana katika nyumba au wanakutana watakuwa wana madhambi kwani watakuwa wamekiuka sheria na pia wapo katika zina ya macho, kushika wanaposalimia, kuzungumza, na kadhalika. Mara nyingi wasichana wanadanganywa na wavulana kuwa watawaoa hivyo wanawachezea kisha wanawatupa. Hili linamharibia sifa kabisa msichana na huenda wakati mwingine ikawa vigumu kupata mume mwengine baada ya yale yaliyopita. Nasaha zetu kwa wasichana ni kuwa, ikiwa mtu anamuahidi kuwa atamuoa amwambie mvulana atumie njia ya sawa ya kwenda kumposa kwa wazazi kwa njia ya heshima sio kuzunguka naye tu.

Ama kuhusu Swali lenyewe uliloliuliza lina utata lakini ikiwa ni kama tulivyofahamu ndivyo basi tunasema hivi, ndoa katika Uislamu ina masharti yake. Na lau masharti haya yatapatikana basi ndoa itaswihi lakini ikiwa wamefanya zinaa kabla ya ndoa yenyewe watakuwa na dhambi hilo la tendo lenyewe na itabidi wafanye toba ya kikweli kweli ili wasamehewe na Allaah. Nguzo za kuswihi Ndoa ni kama zifuatazo:

1.     Walii: Awepo baba wa muolewaji, ndugu wa karibu zaidi, muwakilishi, au watu wenye rai/ busara njema katika jamaa au mtawala/ sultani wakikosekana hawa wote, kwa mujibu wa kauli yake Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):

“Hakuna ndoa bila walii” (Abu Daawuud, at-Tirmidhiy na al-Haakim).

Ili mtu kuwa walii (msimamizi) anatakiwa atimize mambo yafuatayo:

i.                    Awe ni mwanaume, baleghe, mwenye akili timamu, muungwana na mwenye busara.

ii.                   Kumtaka idhini yule anayemtawalia juu ya yule anayetaka kumuoza, kama mtawaliwa ni bikra, na walii akawa ni baba mzazi, na atamtaka amri yake na kukubali kwake ni kunyamaza na mke mkuu ana haki haki zaidi ya nafsi yake.

iii.                 Walii wa aliye karibu hautasihi pamoja na kuwepo kwa wa karibu zaidi.

iv.                Mwanamke atakapotoa idhini kwa watu wawili miongoni mwa nduguze ili kumuozesha, na kila mtu akamuozesha kwa mtu, basi yeye ni wa yule wa kwanza (Abu Bakr al-Jazairiy, Minhajul Muslim).

2. Mashahidi Wawili: Ni kuwepo kwa watu wawili au zaidi katika fungisho la ndoa, miongoni mwa wanaume waadilifu. Allaah anasema:

}}وَأَشْهِدُوا ذَوَيْ عَدْلٍ مِّنكُمْ{{   

{{Na washuhudisheni watu wenye uadilifu miongoni mwenu}} (65: 2).

Na kwa kauli ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): ((“Hapana ndoa isipokuwa kwa walii na mashahidi wawili waadilifu")) (ad-Daaraqutniy na al-Bayhaqiy).

3.  Tamko la Kufungisha Ndoa: Hii ni kauli ya mume au wakili wake katika kufunga ndoa: “Niozeshe binti yako, au muusiwa wako Fulani …” Na kauli ya walii: “Nimekuoza binti yangu Fulani…”, na kauli ya mume: “Nimeikubali ndoa yake kwa nafsi yangu”.

4.  Mahari: Au Swadaaq ni kile anachopewa mwanamke ili kuhalalika kustarehe nae. Nayo ni wajibu kwa kauli ya Allaah Aliyetukuka:

}}وَآتُواْ النَّسَاء صَدُقَاتِهِنَّ نِحْلَةً{{

Na wapeni wanawake mahari zao hali ya kuwa ni kitu kama tuzo (4: 4).

Na kauli yake Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):

((“Tafuta  japokuwa ni pete ya chuma”)) (al-Bukhaariy na Muslim).

Ikiwa masharti haya yatatimizwa basi ndoa itakuwa ni halali baina ya watu hao wawili, hivyo akizaliwa mtoto atakuwa ni mtoto wao wa halali. Ikiwa labda wamekutana kimwili kabla ya ndoa chochote kitakachozaliwa kitakuwa si halali, na mtoto atakuwa ni mwana wa mama naye ataweza kumrithi mama tu na wala sio baba. Hivyo, tuachane na mila na desturi zisizokuwa zetu ili tuishi na kuzaa watoto ambao ni halali hivyo kujenga jamii nzuri zaidi kwa siku zijazo.

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share