Kutengukwa Na Wudhuu Katika Swalaah Ya Jamaa

Kutengukwa Na Wudhuu Katika Swalaah Ya Jamaa

 

www.alhidaaya.com

 

 

 

SWALI: 

 

 

Kama unasali jamaa kati kati ukatengukwa na udhu utahitajika kuondoka pale pale au usubiri umalize then utie udhu usali tena? ukizingatia jamii yetu wengi hatujui namna ya kupishana katika sala ukitokewa na udhuru.

 

 

JIBU:

 

AlhamduliLLaah - Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

   

Swala hili ni muhimu  na linahitaji kuonyeshwa kimatendo kwani huenda lisifahamike katika waraka. Hivyo, itabidi katika Misikiti watu wafundishwe ili kusiwe na utata aina yoyote baada ya hapo. Kwani hili ni tatizo kubwa katika jamii zetu kujua namna ya kutoka pindi mtu anapotengukwa na wudhuu. Lakini tujaribu na tunamuomba Allaah atupatie tawfiyq katika hilo.

 

 

Pindi wudhuu unapovunjika inakuwa huwezi tena kuendelea na Swalaah na inabidi uondoke ili ukachukue wudhuu na urudi uanze Swalaah ile kuanzia mwanzo.

 

Wudhuu unapomtenguka mmoja wetu inabidi akate Swalaah na aanze harakati za kutoka ili aende kuchukua wudhuu mpya. Hapo atasimama nyuma ya mtu wa upande wa kushoto au kuumeni katika wale waliokuwa naye msitari mmoja. Na anaweza kumuashiria yule aliye katika msitari wa nyuma ili ajongee katika nafasi yake. yeye naye atapiga hatua katika ile nafasi iliyoachwa wazi kwa yule wa nyuma kujongea mbele. Atasimama tena nyuma ya mtu wa msitari huu wa nyuma. Huyu wa msitari wa tatu atakuja kuziba ule mwanya na ataendelea hivyo mpaka afike sehemu ya kuchukua wudhuu. Akiona kuwa kutoka kwake kunaweza kuleta shida zaidi na vurugu kwa wengine au kuleta tashwishi ya kuwaondolea khushuu wengine, itakuwa ni afadhali abakie amekaa katika sehemu yake mpaka jamaa imalizike kisha atoke kwenda kuchukua wudhuu mpya kwa ajili ya kuanza Swalaah upya.

 

Lakini pia kuna ushahidi mwengine uuoneshao kuwa mtu anaweza kupita mbele ya safu nyuma ya Imaam na hatokuwa amewakata wenzake Swalaah, kwani   imethibiti:

 

(( سترة الإمام سترة من خلفه))  البخاري

((Sutra ya Imaam ni Sutra ya walio nyuma yake)) [Al-Bukhariy]

 

 

Na maadam Maamuma kizuizi chao ni kile kizuizi cha Imaam, basi haikatwi Swalaah yao kwa kupita mtu mbele yaokama tunavyoona katika tukio la Ibn ‘Abbaas رضي الله عنهما:

 

عَنْ عَبْدِ اللَّهِ بْنِ عَبَّاسٍ رضي الله عنهما قَالَ : أَقْبَلْتُ رَاكِباً عَلَى حِمَارٍ أَتَانٍ , وَأَنَا يَوْمَئِذٍ قَدْ نَاهَزْتُ الاحْتِلامَ , وَرَسُولُ اللَّهِ صلى الله عليه وسلم يُصَلِّي بِالنَّاسِ بِمِنًى إلَى غَيْرِ جِدَارٍ، فمَرَرْتُ بَيْنَ يَدَيْ بَعْضِ الصَّفِّ فَنَزَلْتُ, فَأَرْسَلْتُ الأَتَانَ تَرْتَعُ، وَدَخَلْتُ فِي الصَّفِّ  فَلَمْ يُنْكِرْ ذَلِكَ عَلَيَّ أَحَدٌ .

 

Imetoka kwa Ibn ‘Abbaas (Radhwiya Allaahu ‘anhumaa)    ambaye kasema: “Nilikuja siku moja huku nimepanda punda mwanamke na nilikuwa ndio kwanza nafikia umri wa kubaleghe, Na Nabiy (Swalla-Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) anaswalisha watu huko Minaa bila ya kuweko ukuta mbele yake. Nikapita baina ya baadhi ya safu, kisha nikateremka, nikampeleka punda (sehemu ya ) kumlisha, na nikaingia katika safu, wala hakuniambia mtu lolote kuhusu hivyo nilivyofanya”  [Al-Bukhariy]

 

 

Na katika Hadiyth nyingine:   

 

من طريق عبيد الله بن عبد الله بن عتبة أن عبد الله بن عباس أخبره أنه أقبل يسير على حمار ورسول الله صلى الله عليه وسلم قائم يصلي بِمِنى في حجة الوداع، يُصلي بالناس.  قال : فَسَارَ الحمار بين يدي بعض الصف، ثم نزل عنه ، فَصَفّ مع الناس.

 

Kutoka kwa 'Ubaydullaah bin Abdillaah bin 'Utbah kwamba Abdullaah bin 'Abbaas kamjulisha kuwa alifika huku kapanda punda na  Nabiy (Swalla-Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kasimama anaswalisha watu alipokuwa Minaa katika Hijjatul-Widaa. Akasema:  Akawa anapita na punda baina ya safu, kisha akateremka akaingia katika safu (kuswali) pamoja na watu”   [Muslim] 

 

 

Hadiyth hizi zinatujulisha kuwa mtu anaweza kupita mbele ya safu za Maamuma kama kuna haja ya kufanya hivyo, na bila ya kuwa na makatazo yoyote juu ya hilo. Pia kuna Hadiyth ambayo:

 

Ibn ‘Abbaas (Radhwiya-Allaahu ‘anhumaa) anasimulia kuwa alikuwa na nduguye juu ya kipando na wakapita mbele ya safu na Nabiy (Swalla-Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) hakuwaambia chochote. [Muslim]

 

 

Pia tunaona katika Hadiyth hizi kuwa Nabiy (Swalla-Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliswali bila ya kuweko na ukuta mbele yake, kwa hiyo Swalaah ya Maamuma ni kumfuata Imaam hata kama Imaam hana sutra mbele yake, na haidhuru ikiwa mtu atapita baina ya safu, kwa maana kuwa huyo mtu haikati Swalaah za wanaoswali.

 

Vile vile ingawa katika Hadiyth nyingine ya Swahiyh inayosema kuwa miongoni mwa vitu vinavyoharibu Swalaah ni kupita kwa punda ikiwa atapita mbele ya Imaam au mtu anayeswali pekee, lakini hapa haikuharibu Swalaah kupita punda baina ya safu.  

 

Kwa faida zaidi bonyeza viungo vifuatavyo:

 

 

040-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Mlango Wa Swalaah: Uimamu Na Hukmu Zake

 

 

041-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Mlango Wa Swalaah: Mahala Pa Kusimama Imamu Na Maamuma

 

 

042-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Mlango Wa Swalaah: Safu Na Hukmu Zake

 

044-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Mlango Wa Swalaah: Hukmu Za Aliyetanguliwa

 

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share