12-Swabrun Jamiyl: Subira Za Wanawake Wema Wa Awali - Mama Yake Nabiy Muwsaa

 

Swabrun Jamiyl (Subira njema)

 

12 - Subira Za Wanawake Wema Wa Awali -

 

Mama Yake Nabiy Muwsaa

 

 

 

 

Fir’awn alipoota ndoto kuwa atazaliwa mtoto katika wana wa Israaiyl atakayekuwa ni sababu ya kutoweka milki yake na kuangamia kwake, aliamrisha kuua kila mtoto mwanamume anayezaliwa. Mwishowe walikhofia kwamba utafika wakati kutakuweko na wanawake wengi na hakutakuwa na wanaume wa kufanya kazi za kiume. Akaamrisha mwaka mmoja wauliwe watoto wa kiume wote, na mwaka mwengine waachiwe hai. Mwaka aliozaliwa Nabiy Muwsa ('Alayhis-Salaam) ulikuwa ni mwaka wa kuuliwa watoto wanaozaliwa. Mama yake Muwsa alipoibeba mimba yake, tumbo halikutokeza kama mimba za wanawake wengine. Kwa hiyo alisalimika kwani walikuwa wakiingiliwa majumbani kuchunguzwa kama kuna mwanamke mwenye mimba, kisha husubiriwa anapozaa huuliwa mtoto huyo. Mama yake Muwsa alipojifungua alianza kuingiwa na khofu kubwa na huzuni ya kuwa mwanawe atauliwa. Ilipomzidi khofu, Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Alimpoza moyo wake na Akamtia ilhamu na kumuongoza la kufanya. Kisha Akamuahidi kwamba Atamrudisha mwanawe kwake na juu ya hivyo atarudi akiwa ni Rasuli wa Allaah:

 

 

 وَأَوْحَيْنَا إِلَىٰ أُمِّ مُوسَىٰ أَنْ أَرْضِعِيهِ ۖ فَإِذَا خِفْتِ عَلَيْهِ فَأَلْقِيهِ فِي الْيَمِّ وَلَا تَخَافِي وَلَا تَحْزَنِي ۖ إِنَّا رَادُّوهُ إِلَيْكِ وَجَاعِلُوهُ مِنَ الْمُرْسَلِينَ ﴿٧﴾

Na Tukamtia ilhamu mama yake Muwsaa kwamba: “Mnyonyeshe. Lakini utakapomkhofia, basi mtupe katika mto na wala usikhofu wala usihuzunike. Hakika Sisi Tutamrudisha kwako, na Tutamfanya miongoni mwa Rusuli”. [Al-Qaswasw: 7]

 

 

Mama yake Muwsa alikuwa akiishi karibu na mto wa Nile. Alichukua kisanduku akamfanyia kama susu la kulalia mtoto. Akalifunga na kamba akawa anamnyonyesha kwa uficho. Ikawa kila anapomjia mtu anayemuogopa humtia mtoto wake katika kisanduku na kumweka katika mto huku akilifunga kamba. Siku moja alisahau kulifunga kamba. Maji yakachukua kisanduku   yakipita nalo mbele ya nyumba ya Fir’awn. Wajakazi wa Fir’awn wakaliona susu wakalibeba mpaka kwa Aasiyah mke wa Fir’awn. Hawakujua kilichomo ndani yake na walikhofu kufungua kwani wangeliingia matatani kufanya hivyo bila ya kupata amri. Kisanduku kilipofunguliwa walimwona mtoto mchanga mzuri ajabu! Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Akaujaza moyo wa Aasiyah, mapenzi ya mtoto huyo kwa vile Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)  ni Mjuzi wa ya ghaibu, Alijua kuwa Aasiyah ni atakuwa ni Muumini, hivyo Alitaka mtoto huyo awe ni sababu yake ya kutoka katika shirki ya mumewe aingie katika Tawhiyd apate maisha mema ya milele. Na mtoto huyo awe sababu ya kuangamia kwa Fir’awn bila ya yeye kuhisi. Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

فَالْتَقَطَهُ آلُ فِرْعَوْنَ لِيَكُونَ لَهُمْ عَدُوًّا وَحَزَنًا ۗ إِنَّ فِرْعَوْنَ وَهَامَانَ وَجُنُودَهُمَا كَانُوا خَاطِئِينَ ﴿٨﴾

Basi wakamwokota watu wa Fir’awn ili awe adui kwao na (sababu ya) huzuni. Hakika Fir’awn na Haamaan na majeshi yao walikuwa wenye makosa. [Al-Qaswasw: 8]

 

 

Kwa maana, Fir’awn alipomuona, alitaka kumuua akikhofu kuwa atakuwa ni yule mtoto aliyemuota ndotoni. Lakini mkewe Aasiyah bint Muzaahim alimkinga na akamwambia mumewe:

 

 قُرَّتُ عَيْنٍ لِّي وَلَكَ ۖ لَا تَقْتُلُوهُ عَسَىٰ أَن يَنفَعَنَا أَوْ نَتَّخِذَهُ وَلَدًا وَهُمْ لَا يَشْعُرُونَ ﴿٩﴾

 “Kiburudisho cha macho kwangu na kwako; usimuue, asaa akatufaa, au tumfanye mwana.” Nao hawatambui. [Al-Qaswasw: 9]

 

Subira ya mama yake Muwsa iliendelea kama Anavyosema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) katika Kauli Yake:

 

وَأَصْبَحَ فُؤَادُ أُمِّ مُوسَىٰ فَارِغًا ۖ إِن كَادَتْ لَتُبْدِي بِهِ لَوْلَا أَن رَّبَطْنَا عَلَىٰ قَلْبِهَا لِتَكُونَ مِنَ الْمُؤْمِنِينَ ﴿١٠﴾

Na ukawa moyo uliojaa hisia wa mama yake Muwsaa mtupu! Alikaribia kumdhihirisha (kuwa ni mwanawe) lau kama Tusingeutia nguvu moyo wake ili awe miongoni mwa Waumini.

 

 

وَقَالَتْ لِأُخْتِهِ قُصِّيهِ ۖ فَبَصُرَتْ بِهِ عَن جُنُبٍ وَهُمْ لَا يَشْعُرُونَ ﴿١١﴾

Akamwambia dada yake (Muwsaa): “Mfuatilie!”  Akamtazama kwa mbali nao hawatambui.

 

وَحَرَّمْنَا عَلَيْهِ الْمَرَاضِعَ مِن قَبْلُ فَقَالَتْ هَلْ أَدُلُّكُمْ عَلَىٰ أَهْلِ بَيْتٍ يَكْفُلُونَهُ لَكُمْ وَهُمْ لَهُ نَاصِحُونَ ﴿١٢﴾

Na Tulimharamishia akatae kabisa wanyonyeshaji tangu mwanzo, mpaka akasema: “Je, nikuelekezeni kwa watu wa nyumba watakaomlea kwa ajili yenu, nao watakuwa wenye kumweka vyema kidhati?

 

 

فَرَدَدْنَاهُ إِلَىٰ أُمِّهِ كَيْ تَقَرَّ عَيْنُهَا وَلَا تَحْزَنَ وَلِتَعْلَمَ أَنَّ وَعْدَ اللَّـهِ حَقٌّ وَلَـٰكِنَّ أَكْثَرَهُمْ لَا يَعْلَمُونَ ﴿١٣﴾

Basi Tukamrudisha kwa mama yake ili yaburudike macho yake na wala asihuzunike, na ili ajue kwamba ahadi ya Allaah ni kweli, lakini wengi wao hawajui. [Al-Qaswasw: 10-13]

 

 

 Hiyo ndivyo alivyovumilia mama yake Muwsa kufuata amri ya Rabb wake na matokeo yake akatimiziwa ahadi ya kurudishiwa mwanawe ili amnyonyeshe na kisha akapata fadhila kubwa zaidi kwa  kujaaliwa mtoto wake kuwa Nabiy na Rasuli  wa wana wa  Israaiyl. 

 

 

Share