Mashairi: Swalah Ni Nguzo Muhimu: Sababu Ya Israa Na Mi'iraaj

Swalah Ni Nguzo Muhimu: Sababu Ya Israa Na Mi'iraaj

‘Abdallaah Bin Eifan (Rahimahu Allaah)

Alhidaaya.com

Bismillahi  naanza, salaam kwa ikhwani

nalifungua  baraza, nitowe yangu maoni,
tupate kulisambaza, liende kila makani,
Swalah Ni Nguzo Muhimu, Sababu ya Mi’iraaj.

Sote sasa tunajuwa, Mtume kwenda mbinguni

usiku kachukuliwa, Makkah Msikitini,
safari hakuchelewa, alirudi ardhini,
Swalah Ni Nguzo Muhimu, Sababu ya Mi’iraaj.

Mitume wakaswalishwa, Al-Aqsa tunaamini,
halafu kaondolewa, akapazishwa angani,
mbinguni kapokelewa, kwa heshima ya mgeni,
Swalah Ni Nguzo Muhimu, Sababu ya Mi’iraaj.

Mengi alieyaona, kwa ushahidi machoni,
kwa marefu na mapana, kayaona kwa yakini,
kaitwa na Subhana, kuzungumza kileleni,
Swalah Ni Nguzo Muhimu, Sababu ya Mi’iraaj.

Kaitwa kupewa amri, Swalah ziwe khamsini,
Musa akamshauri, arudi kwa Rahmani,
zikapunguzwa nambari, Swalah tano sio duni,
Swalah Ni Nguzo Muhimu, Sababu ya Mi’iraaj.

Swalah tano ndio nguzo, muhimu katika dini,
hizo hazina mchezo, wala hazina utani,
ukipunguza kigezo, hakuna cha samahani,
Swalah Ni Nguzo Muhimu, Sababu ya Mi’iraaj.

Swalah tano kila siku, tuziswali kwa makini,
kusujudu, kurukuu, tuzifanye kwa imani,
bila kufanya makuu, kila kitu wastani,
Swalah Ni Nguzo Muhimu, Sababu ya Mi’iraaj.

Akhera kitu cha kwanza, huulizwa muumini,
kama amezitimiza, Swalah tano kwa mizani,
na kama amepunguza, sunnah ziwe hisabuni,
Swalah Ni Nguzo Muhimu, Sababu ya Mi’iraaj.

Swalah jama'ah ni bora, bora kuliko nyumbani,

upate malipo bora, ukiswali hadharani,
au waimbe ngonjera, ukifeli mtihani,
Swalah Ni Nguzo Muhimu, Sababu ya Mi’iraaj.

Binadamu kurupuka, pale anapoadhini,
fanya uende haraka, uwe mbele ya foleni,
kuwa mbele ni baraka, ni safu yenye thamani,
Swalah Ni Nguzo Muhimu, Sababu ya Mi’iraaj.

Lazima kunyenyekea, swali kwa matumaini,
makinika na tulia, utulivu wa mwilini,
Swalah kuiizingatia, kwa utulivu moyoni,
Swalah Ni Nguzo Muhimu, Sababu ya Mi’iraaj.

Swali bila wasiwasi, tahadhari na shetani,
usimwachie nafasi, apenyeze akilini,
usiihusishe nafsi, na mambo ya duniani,
Swalah Ni Nguzo Muhimu, Sababu ya Mi’iraaj.

Kwenye sijda mkifika, kwa Mola sana ombeni

Yupo karibu Rabuka, hapo dua zisomeni,
dua zenu zitafika, kwa haraka kwa Manani,
Swalah Ni Nguzo Muhimu, Sababu ya Mi’iraaj.

Mkishatoa salaamu, dhikiri zikumbukeni,
mzitimize muhimu, dhikri zote mwishoni,
Kwa pamoja si timamu, kinyume na yetu Dini,
Swalah Ni Nguzo Muhimu, Sababu ya Mi’iraaj.

Bila Swalah ndugu zangu, mtakuwa mashakani,
bila Swalah walimwengu, vyote havina thamani,
vitendo vyote wenzangu, Swalah ni ya mbeleni,
Swalah Ni Nguzo Muhimu, Sababu ya Mi’iraaj.

Ujuwe unakufuru, Swalah kutupa pembeni,
mwenyewe utajidhuru, utakufa masikini,
nani atakunusuru, ukiingia motoni?
Swalah Ni Nguzo Muhimu, Sababu ya Mi’iraaj.

Mziswali kwa wakati, msichelewe jamani,
nawaombea umati, salaama-u-salimini,
na hapa ndio tamati, nawaaga kwaherini,
Swalah Ni Nguzo Muhimu, Sababu ya Mi’iraaj.

Share