Kumlazimisha Mtoto Aoelewe Kwa Ajili Ya Mali Inajuzu?

 

SWALI:

Asalamu Alaikum

mimi nataka kujua

kama inajuzu kumuozesha mtoto wakike mtu yeye hamtaki  kwasababu mwanamume ana pesa na yuko nchi za nje?

 

 


JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Kwanza wazazi wa Kiislamu watambue kwamba haifai kuwalazimisha watoto kuolewa au kuoa ikiwa wenyewe watoto hawakuridhika na mume aliyekuja kumposa mtoto wa kike au mke watakayemposea mtoto wao wa kiume. Na kutokuridhika huko kuwe ni kutokana na sababu fulani labda kukosekana uzuri wa hao wachumba hivyo huenda ikaleta ukosefu wa mapenzi katika ndoa kisha ndoa iharibike, jambo ambalo hakuna apendaye litokee.

Lakini muhimu katika kuposa au kuposwa anapotokea mchumba mwenye kushika dini na khuluq (tabia) njema na ikiwa ni mwenye kumridhisha aliyeposwa basi haifai kukataa posa hiyo kwani Mtume صلى الله عليه وآله وسلم ametupa onyo kwa kufanya hivyo:

 

))   إِذَا خَطَبَ إِلَيْكُمْ مَنْ تَرْضَوْنَ دِينَهُ وَخُلُقَهُ فَزَوِّجُوهُ إِلَّا تَفْعَلُوا تَكُنْ فِتْنَةٌ فِي الْأَرْضِ وَفَسَادٌ عَرِيضٌ   ( رواه الترمذي   وقال الألباني : حسن

((Atakapoposa kwenu yule mtakaeridhika na dini yake, na tabia yake, basi muozesheni, kwani kutokufanya hivyo itakuwa fitna katika ardhi (duniani) na ufisadi mpana (mkubwa) )) [At-Tirmidhiy na Sh Albaaniy amesema ni Hadiyth Hasan]

 

Vile vile Mtume صلى الله عليه وآله وسلم ametupa sifa nne za kuchagua katika kuposa au kuposwa nazo ni:

 

((تنكح المرأة لأربع: لمالها ولحسبها ولجمالها ولدينها فاظفر بذات الدين تربت يداك ))البخاري و مسلم

((Mwanamke huolewa kwa mambo (sifa) manne; mali yake, nasabu (ukoo) yake, uzuri wake, na dini yake, basi shikilia (chagua) mwenye sifa za dini utasalimika)) [Al-Bukharriy na Muslim]

 

Kama tunavyoona katika hadiyth hiyo kuwa sifa mojawapo ya kuchagua kuposa au kuposwa ni mali, lakini haina maana kwamba alazimishwe mtoto kuoa au kuolewa kwa ajili ya mali tu, bali hadi aridhike mwenyewe. Na ikiwa mwenye kuposa au kuposwa ana sifa ya dini ambayo ndio aliyotuonyesha Mtume صلى الله عليه وآله وسلم kuwa ndio tuitazame zaidi, basi watoto wapewe nasiha na kuelezwa umuhimu wa kuwa na mke au mume mwenye dini na ikiwa hayakumchukiza mengine basi afikirie kukubali posa hiyo.

Ama kumlazimisha tu kwa hali hiyo uliyoitaja bila ya kuridhika mwenyewe haifai.

Nini faida ya kumlazimisha mwanao kuolewa na mtu asiyempenda kisha baada ya muda anakurejelea kaachika au kadai talaka yake? 

 

Lakini pia kuna nyakati ambazo mtoto wa kike anaweza kuozeshwa bila khiyari yake, ikiwa kuna khofu au madhara ya zinaa. Mathalan bint akawa na uhusiano wa haramu na kukakhofiwa kusipatikane madhara ya zinaa na uchafu kuendelea, hapo bint anaweza kuozeshwa haraka ili kumlinda na kumuepusha na machafu hayo.

 

 Na Allah Anajua zaidi.

 

 

Share