001 - Al-Faatihah

 

 

الْفَأتِحَة

001-Al-Faatihah

 

001-Al-Faatihah: Utangulizi Wa Suwrah

 

Alhidaaya.com

 

 

 

 

 بِسْمِ اللَّـهِ الرَّحْمَـٰنِ الرَّحِيمِ ﴿١﴾

1. Kwa Jina la Allaah Ar-Rahmaan (Mwingi wa Rehma), Ar-Rahiym (Mwenye Kurehemu)[1].

 

  

 الْحَمْدُ لِلَّـهِ رَبِّ الْعَالَمِينَ ﴿٢﴾

2. AlhamduliLLaah (Himdi Anastahiki) Allaah Rabb wa walimwengu.

 

 

الرَّحْمَـٰنِ الرَّحِيمِ ﴿٣﴾

3. Mwingi wa Rehma, Mwenye Kurehemu.  

 

 مَالِكِ يَوْمِ الدِّينِ ﴿٤﴾

4. Mfalme wa Siku ya Malipo.

 

 

 إِيَّاكَ نَعْبُدُ وَإِيَّاكَ نَسْتَعِينُ ﴿٥﴾

5. Wewe Pekee tunakuabudu na Wewe Pekee tunakuomba msaada.[2]

 

اهْدِنَا الصِّرَاطَ الْمُسْتَقِيمَ ﴿٦﴾

6. Tuongoze njia iliyonyooka.[3]

 

 

صِرَاطَ الَّذِينَ أَنْعَمْتَ عَلَيْهِمْ غَيْرِ الْمَغْضُوبِ عَلَيْهِمْ وَلَا الضَّالِّينَ ﴿٧﴾

7. Njia ya wale Uliowaneemesha, si ya walioghadhibikiwa wala waliopotea.[4]

 

[1] Tofauti Ya Jina Na Sifa Ya Ar-Rahmaan (Mwingi wa Rehma), Ar-Rahiym (Mwenye Kurehemu). 

 

Ar-Rahmaan: Sifa ya Jina hili ni pana zaidi na ni Sifa yenye kuenea zaidi kuliko Ar-Rahiym (Mwenye Kurehemu). Sifa hii inakusanya maana zote za Rehma, huruma n.k. Allaah Ndiye Mwenye Rehma iliyokusanya kila kitu, iliyoenea kwa viumbe Vyake vyote duniani; wanaadamu, majini, Waumini, makafiri, wanyama, mimea na kadhaalika. Hakuna yeyote au chochote katika kuwepo kwake ila Rehma Yake imemuenea. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

الرَّحْمَـٰنُ عَلَى الْعَرْشِ اسْتَوَىٰ ﴿٥﴾

Ar-Rahmaan (Mwingi wa Rehma), Yuko juu ya ‘Arshi. [Twaahaa (20:50]

 

Na Sifa ya Majina mawili ya Ar-Rahmaan na Ar-Rahiym yanatokana na herufi tatu za asili, hivyo basi asili yake ni maana moja, isipokuwa tu kama ilivyobainishwa katika Sifa ya Rahmaan kuwa ni Rehma inayowafikia viumbe wote. Ama Rahiym ni Sifa khaswa kwa ajili ya Waumini pekee kama Anavyosema Allaah (سبحانه وتعالى):

وَكَانَ بِالْمُؤْمِنِينَ رَحِيمًا ﴿٤٣﴾

Naye daima Ni Mwenye Kurehemu Waumini. [Al-Ahzaab: (33:43)]

 

 

[2] Isti’aanah (Kuomba Msaada):

 

Rejea makala ifuatayo kupata faida:

 

18-Hakika Shirki Ni Dhulma Kubwa Mno! - Isti’aanah (Kuomba Msaada) Kwa Asiyekuwa Allaah

 

Rejea pia Al-Anfaal (8:9), Al-Qaswasw (28:15) kupata maana ya Istighaathah (Kuomba Uokozi).

 

[3] Maana Ya Swiraatw Al-Mustaqiym (Njia Iliyonyooka):

 

Hadiyth Ya Kwanza:

Amesimulia An-Nawaas bin Sam’aan  (رضي الله عنه): Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Allaah (تعالى)  Amepiga mfano Swiraatw (njia) iliyonyooka, imezungukwa pande zote na kuta mbili na kila ukuta una milango iliyo wazi na imefunikwa na mapazia. Na katika lango la Swiraatw kuna mlinganiaji akiita: “Enyi watu! Ingieni nyote katika swiraatw na msipite pembeni.” Na juu ya Swiraatw, kuna mlinganiaji mwengine anamuonya mtu yeyote anayetaka kufungua hiyo milango akiwaambia: Ole wenu! Msiufungue! Kwani mkifungua mtapita ndani! Kwani Asw-Swiraatw ni Uislaam, na kuta mbili ni mipaka Aliyoiweka Allaah. Na milango iliyofunguliwa ni yaliyoharamishwa na Allaah. Na huyo mlinganiaji juu ya lango la Swiraatw ni Kitabu cha Allaah, na mlinganiaji juu ya Swiraatw ni Maonyo ya Allaah yaliyo ndani ya kila nafsi ya Muislamu.”  [Ahmad, ameisahihisha Al-Albaaniy; Swahiyh Al-Jaami’ (3887)]

 

Hadiyth Ya Pili:

Amesimulia Jaabir (رضي الله عنه): Tulikuwa tumekaa pamoja na Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم), akachora mstari mbele yake, kisha akachora mistari miwili kuliani, na mistari miwili kushotoni, kisha akaweka mkono wake katika njia ya katikati akasema: “Hii Njia ya Allaah.” Kisha akasoma:

 

وَأَنَّ هَـٰذَا صِرَاطِي مُسْتَقِيمًا فَاتَّبِعُوهُ ۖ  وَلَا تَتَّبِعُوا السُّبُلَ فَتَفَرَّقَ بِكُمْ عَن سَبِيلِهِ ۚ

Na kwamba hii ndiyo njia Yangu iliyonyooka, basi ifuateni. Na wala msifuate njia nyinginezo zitakufarikisheni na Njia Yake. [Al-An’aam (6:153)]

[Ahmad, Swahiyh Ibn Maajah (11)] 

 

Rejea pia (Aal-‘Imraan (3:103) (3:105), Al-An’aam (6:153).

 

[4] Nani Walioghadhibikiwa Na Waliopotea:

 

Amesimulia ‘Adiy bin Haatim (رضي الله عنه): Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Walioghadhibikiwa ni Mayahudi, na waliopotea ni Manaswara.” [At-Tirmidhiy Hadiyth Hasan Ghariyb na taz. Silsilah Asw-Swahiyhah (363)]

 

 

 

Share