022-Lu-ulu-un-Manthuwrun: Kuhifadhi Undugu Wa Kiislamu, Haki, Heshima, Kutokufanyiana Uadui, Chuki Na Kudharauliana
Lu-ulu-un-Manthuwrun
(Mkusanyiko Wa Hadiyth Mbali Mbali Na Mafunzo Yake)
Hadiyth Ya 22
Kuhifadhi Undugu Wa Kiislamu, Haki, Heshima,
Kutokufanyiana Uadui, Chuki Na Kudharauliana
عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ (رضي الله عنه) قَالَ: قَالَ رَسُولُ اللَّه (صلى الله عليه و آله وسلم) ((لاَ تَحَاسَدُوا وَلاَ تَنَاجَشُوا وَلاَ تَبَاغَضُوا وَلاَ تَدَابَرُوا ولاَ يَبِعْ بَعْضُكُمْ عَلَى بَيْعِ بَعْضٍ، وَكُونُوا عِبَادَ اللَّهِ إِخْوَانًا. الْمُسْلِمُ أَخُو الْمُسْلِمِ لاَ يَظْلِمُهُ وَلاَ يَخْذُلُهُ وَلاَ يكذبه ولاَ يَحْقِرُهُ. التَّقْوَى هَاهُنَا)) وَيُشِيرُ إِلَى صَدْرِهِ ثَلاَثَ مَرَّاتٍ ((بِحَسْبِ امْرِئٍ مِنْ الشَّرِّ أَنْ يَحْقِرَ أَخَاهُ الْمُسْلِمَ. كُلُّ الْمُسْلِمِ عَلَى الْمُسْلِمِ حَرَامٌ دَمُهُ وَمَالُهُ وَعِرْضُهُ)) رواه مسلم
Imepokelewa kutoka kwa Abuu Hurayrah (رضي الله عنه) amesema: Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: ((Msihusudiane, wala msipandishiane bei wala msibughudhiane, wala msikatane, wala msiingie katika biashara waliyokwishaingia wenzenu, nyote kuweni ni waja wa Allaah ndugu moja. Muislamu ni ndugu wa Muislamu, hamdhulumu, wala haachi kumsaidia, wala hamdanganyi, wala hamdharau. Taqwa ipo hapa)) Akaashiria kifuani mwake mara tatu. ((Yatosha kuwa shari mtu kumdharau nduguye Muislamu. Kila Muislamu juu ya Muislamu mwenziwe ni haraam damu yake, mali yake, na heshima yake)).[Muslim]
Mafunzo Na Mwongozo:
1. Uislamu unasisitiza kuchunga haki na heshima baina ya watu, na unatahadharisha kudharauliana.
Rejea Hadiyth namba (87), (88), (89), (96) (97), (126).
Na Allaah (سبحانه وتعالى) Anaonya:
يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا لَا يَسْخَرْ قَوْمٌ مِّن قَوْمٍ عَسَىٰ أَن يَكُونُوا خَيْرًا مِّنْهُمْ وَلَا نِسَاءٌ مِّن نِّسَاءٍ عَسَىٰ أَن يَكُنَّ خَيْرًا مِّنْهُنَّ ۖ وَلَا تَلْمِزُوا أَنفُسَكُمْ وَلَا تَنَابَزُوا بِالْأَلْقَابِ ۖ بِئْسَ الِاسْمُ الْفُسُوقُ بَعْدَ الْإِيمَانِ ۚ وَمَن لَّمْ يَتُبْ فَأُولَـٰئِكَ هُمُ الظَّالِمُونَ﴿١١﴾
Enyi walioamini! Wanaume wasiwafanyie dhihaka na kudharau wanaume wengineo asaa wakawa bora kuliko wao, wala wanawake kwa wanawake wengineo, asaa wakawa bora kuliko wao. Na wala msifedheheshane kwa kutukanana na wala msiitane majina (mabaya) ya utani. Ubaya ulioje kuita jina la ufasiki baada ya iymaan. Na yeyote asiyetubu, basi hao ndio madhalimu. [Al-Hujuraat (49: 11)]
2. Uislamu unakataza kuudhiana.
Rejea: Al-Ahzaab (33: 58) na pia imeharamishwa kutendeana uadui bali imeamrishwa kushirikiana kwa wema. Rejea: Al-Maaidah (5: 2).
3. Waislamu wote ni ndugu Rejea: Al-Hujuraat: (49: 10).
4. Uhasidi, bughudha na chuki, ni miongoni mwa maradhi ya moyo yanayomhatarisha Muislamu siku ya Qiyaamah kufika mbele ya Allaah (سبحانه وتعالى) akiwa na moyo usiosalimika na ndio maana Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) akasema katika Hadiyth hiyo ya maudhui: “Taqwa ipo hapa.” (akiashiria moyo mara tatu). Na Allaah (سبحانه وتعالى) Anasema:
يَوْمَ لَا يَنفَعُ مَالٌ وَلَا بَنُونَ ﴿٨٨﴾
“Siku hayatofaa mali wa watoto.
إِلَّا مَنْ أَتَى اللَّـهَ بِقَلْبٍ سَلِيمٍ ﴿٨٩﴾
“Isipokuwa yule atakayemfikia Allaah na moyo uliosalimika. [Ash-Shu’araa (26: 88-89)]
5. Uislamu unasisitiza kuungana si kutengana au kukatana undugu.
Rejea: Muhammad (47: 22-23).
6. Kuuana ni miongoni mwa madhambi makubwa, nayo yanahusiana na haki ya mtu.
Rejea: An-Nisaa: (92-93).
7. Taqwa ipo moyoni, na inadhihirishwa kwa vitendo vyake, kukhofu kutenda uovu au kutenda mema.
8. Muislamu anafaa achunge sana asije kuingia katika haraam kwa kuvunja heshima ya nduguye, kumwaga damu yake au kula mali yake.
9. Hii ni Hadiyth ‘adhimu yenye kutufunza mahusiano mema na maingiliano mazuri baina ya Waislamu wao kwa wao na wana Aadam wote.