Nimempa Talaka Mke Wa Mwanzo Lakini Bado Nampenda

SWALI: 

Assalaam aleikum,

Kila sifa njema ni zake Allah SW, rehma na Amani zimuendee Mtume SAW. Mimi ni kijana mwenye umri wa miaka 30, nilikuwa na mke  na baadae nikaoa mke mwingine lakini baada ya kuoa mke mwingine uadilifu ukaanza kunishinda nikawa nampenda sana huyu wa pili hasa kutokana na umbile! Japo nakiri huo ni udhaifu mkubwa niliouonesha. Sasa mwishowe nikaamua kumwacha yule wa kwanza lakini kipindi nilichomuacha ni katika mwezi ambao nimeshamwingilia, sasa nimesoma ktk Quran nimekuta Allah Anataka tuwape talaka wake zetu katika eda zao yaani katika twahara. Sasa nauliza, je talaka yangu ile imesihi na pia hawakuwepo mashahidi kipindi nampa talaka yake huyo mke wangu wa awali, Hata hivyo bado nampenda.


 

JIBU:

Sifa zote njema anastahiki Allah Aliyetukuka Mola  wa walimwengu wote, Salah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allahu 'Alayhi Wa Aalihi Wasallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'Anhum)  na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho

 Shukran kwa muulizaji kuhusu swali hili nyeti kuhusu mas-ala ya talaka. Talaka imekuwa ni tatizo kubwa katika jamii yetu. Katika halali iliyoruhusiwa talaka ni jambo lisilopendeza. Lakini kunatokea wakati ambapo inabidi mume na mke waachane na huenda kila mmoja akapata mwenzi katika unyumba ambaye wataelewana vyema zaidi.

Kuhusu talaka mwanzo zipo aina mbili, nazo ni:

1- Talaka ya Ki-Sunnah: Nayo ni kumuacha mkeo talaka moja wakati yuko katika twahara ambayo hajamuingilia kwayo.

 2- Talaka ya Ki-Bid‘ah: Hii ni talaka ambayo imetolewa kwa njia iliyo kinyume na sheria. Kwa mfano, kumpatia talaka wakati wa ada yake ya mwezi, au akiwa katika damu ya uzazi au katika twahara ambayo amejamiiana naye.

Talaka yako ni aina ya pili kwani ulimuacha wakati wa twahara uliyokutana naye kimwili. Wanazuoni wamejumuika katika kusema kuwa talaka aina hii ni haramu, na anayefanya hivyo ana dhambi. Hivyo, inabidi urudi kwa Allah (Subhaanahu wa Ta'ala) na uombe toba na ufanye mema. Wanazuoni wametofautiana kuhusu talaka kama hii kama inapita au haipiti. Jamhuur ya wanazuoni wanasema kuwa talaka hiyo inapita kwa kuwa:

a-   Aayah za talaka ni za kijumla, hivyo zinajumlisha talaka  aina yoyote.

b- Uwazi wa Hadiyth ya Ibn 'Umar (Radhiya Allaahu ‘anhu) ambaye amesema alipomtaliki mkewe naye yu katika hedhi na Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akamuamuru kumrudia, talaka hiyo ilihesabiwa.

Baadhi ya wanazuoni (kama Twaawus, Sa‘iyd ibn al-Musayyab, ‘Abullah ibn Ma‘mar, Ibn Taymiyah, Ibn Hazm na Ibn Qayyim, na wengineo) wanasema talaka hiyo haipiti kwa sababu si aina ile iliyoidhinishwa na Allah (Subhaanahu wa Ta'ala), ambaye Amesema: “Basi wapeni talaka katika wakati wa eda zao” (65: 1).  

Na Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alimwambia Ibn ‘Umar (Radhiya Allaahu ‘anhu) kwa kumwambia: “Mwamrisheni amrudie”, na imeswihi kutoka kwake kuwa alikasirika pindi alipopata habari hiyo, naye haghadhibiki kwa alichohalalisha Allah (Subhaanahu wa Ta'ala). Na ama kauli ya Ibn ‘Umar (Radhiya Allaahu  ‘anhu) kuwa ilihesabiwa, haijabainika nani aliyehesabu. Bali amepokea Ahmad, Abu Daawuud na an-Nasaa’iy: “Kuwa alimtaliki mkewe katika hedhi na Mtume wa Allah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akawarudisha pamoja na hakuona kuwa ni chochote”.

Kwa kifupi inajulikana kuwa talaka inayokwenda kinyume na Sunnah ni Talaka ya Bid‘ah na imethubutu kwa Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kuwa, “Kila Bid‘ah ni upotevu”. Na hapa tofauti pia ya kwamba talaka inayokwenda kinyume na sheria ya Allah (Subhaanahu wa Ta'ala) katika Kitabu chake na kubainishwa na Mtume wa Allah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) katika Hadithi ya Ibn ‘Umar, na chochote ambacho kitakwenda kinyume na sheria ya Allah (Subhaanahu wa Ta'ala) na Mtume Wake (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) litakataliwa, kwa ushahidi wa Hadiythi ya Bibi ‘Aa’ishah (Radhiya Allaahu  ‘anha) kuwa Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Mwenye kufanya amali isiyokuwa na hukumu yetu, itakataliwa” (Muslim).

Kwa hivyo, hizo juu ni rai mbili ambazo zimetolewa na wanazuoni na hii ya pili ina nguvu zaidi katika dalili. Lakini hata ukichukulia ile rai ya kwanza kuwa talaka imepita bado una nafasi ya kuwa unaweza kurudiana naye ikiwa hiyo ni talaka ya kwanza au ya pili.

Kuhusu mas-ala ya kumtaliki mke haihitaji mashahidi kwani huo ni uwezo aliopatiwa mwanamume. Mafakihi wengi wa kale na wa sasa wana msimamo huo, na haikupatikana kwa Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) wala Maswahaba inayotoa dalili kwa hilo. Kuhusu hili Allah (Subhaanahu wa Ta'ala) Anasema: “Basi wanapofikia muda wao, ima warejeeni muwaweke kwa wema, au farikianeni nao kwa wema. Na mshuhudishe mashahidi wawili waadilifu miongoni mwenu. Na simamisheni ushahidi kwa ajili ya Allaah” (65: 2). Ukiitizama hii aayah inatuelezea kuwa wakati eda yao inamalizika na mumeamua kurudiana au hamutaki tena kuwa pamoja wakati huo ndio kunatakiwa kuwe na mashahidi. Lakini wakati unamwambia au umemwandikia huwa si lazima kuwe na mashahidi.

Kulingana na ushahidi tulioutaja ni kuwa talaka haijapita na kama tulivyosema ikiwa imepita pia bado unaweza kurudiana naye.

Jambo muhimu na nasaha zetu kwako ni kuwa rudiana na mkeo na ufanye bidii ufanye uadilifu kwani bila ya kufanya uadilifu basi utakuwa pabaya kesho Akhera.

Tunamuomba Allah (Subhaanahu wa Ta'ala) Awatilie tawfiki murudiane na Akupe hima ya kuweza kufanya uadilifu baina ya wake zako.

Na Allah Anajua zaidi

 

Share