02-Sifa Kumi Na Fadhila Zake: Waumini Wanaume Na Wanawake

 

 Sifa Kumi Na Fadhila Zake

 

02 - Waumini Wanaume Na Wanawake

 

 

Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa):

 

((إِنَّ الْمُسْلِمِينَ وَالْمُسْلِمَاتِ وَالْمُؤْمِنِينَ وَالْمُؤْمِنَاتِ…..))

Hakika Waislamu wanaume na wanawake, na Waumini wanaume na wanawake, [Al-Ahzaab: 35]

 

 

Katika Aayah hiyo tukufu, Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Ametaja sifa ya pili ambayo ni Waumini baada ya kutaja Waislamu. Kwa hivyo kuna tofuati hapo baina ya Muislamu na Muumini, na dalili ya kutofuatiana inapatikana pia katika Hadiyth ifuatayo:

 

 

 عن عامر بن سعد عن أبيه قال: أعطى النبيّ صَلَّى الله عَلَيْهِ وَسَلَّم رجالا ولم يعط رجلا منهم شيئا ، فقال سعد: يا رسول الله أعطيت فلانا وفلانا  ولم تعط فلانا شيئا وهو مؤمن ، فقال النبيّ صَلَّى الله عَلَيْهِ وَسَلَّم: أو مُسْلِمٌ؟ حتى أعادها سعد ثلاثا ، والنبيّ صَلَّى الله عَلَيْهِ وَسَلَّم يقول: أوْ مُسْلِمٌ ، ثم قال النبي صَلَّى الله عَلَيْهِ وَسَلَّم إني أُعْطِي رِجالا وأَدَعُ مَنْ هُوَ أحَبُّ إليَّ مِنْهُمْ ، لا أُعْطِيه شَيْئا مَخافَةَ أنْ يُكَبُّوا فِي النَّارِ عَلى وُجُوهِهِمْ"  أحمد وأخرجاه في الصحيحين من حديث الزهري .

 

Imetoka kwa 'Aamir bin Sa'ad bin Abi Waqqaasw (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kutoka kwa baba yake ambaye amesema: Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alitoa (baadhi ya vitu) na kuwapa baadhi ya watu na akaacha kuwapa baadhi yao. Sa'ad akasema: "Ee Rasuli wa Allah, umempa fulani na fulani na fulani na fulani, lakini hukumpa chochote fulani ingawa naye ni Muumini." Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akasema: ((Au Muislamu)). Sa'ad akarudia kusema kauli hiyo mara tatu kila mara Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alijibu: ((Au Muislamu)). Kisha Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)

akasema: ((Huenda nikawapa baadhi ya watu na nisiwape chochote wengine, ingawa wa mwisho ni kipenzi kwangu kuliko wa mwanzo. Siwapi vitu (hao) kwa khofu kwamba huenda wakatupwa katika moto)) [Ahmad na Al-Bukhaariy na Muslim wamesimulia kutoka kwa Az-Zuhriy]

 

 

Dalili nyengineyo ya kutofautisha baina ya Uislamu na Muumini ni katika zama za Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) Mabedui walipoingia Uislamu walimjia Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na kumwambia kuwa wao wameamini. Lakini Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Anawajulisha kuwa kuna tofauti ya kusilimu na kuamini:

 

 قَالَتِ الْأَعْرَابُ آمَنَّا ۖ قُل لَّمْ تُؤْمِنُوا وَلَـٰكِن قُولُوا أَسْلَمْنَا وَلَمَّا يَدْخُلِ الْإِيمَانُ فِي قُلُوبِكُمْ ۖ وَإِن تُطِيعُوا اللَّـهَ وَرَسُولَهُ لَا يَلِتْكُم مِّنْ أَعْمَالِكُمْ شَيْئًا ۚ إِنَّ اللَّـهَ غَفُورٌ رَّحِيمٌ﴿١٤﴾

Mabedui walisema: “Tumeamini!” Sema (ee Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)): “Hamkuamini, lakini semeni: “Tumesilimu.” Kwani iymaan haijaingia bado nyoyoni mwenu. Na mtakapomtii Allaah na Rasuli Wake, Hatokupunguzieni katika ‘amali zenu kitu chochote. Hakika Allaah ni Mwingi wa kughufuria, Mwenye kurehemu. [Al-Hujuraat: 14]

 

Aayah hii inathibitisha kuwa daraja ya Muumini ni ya juu kuliko ya Muislamu, na hii ni rai ya ‘Ulamaa wa Ahlus-Sunnah wal-Jamaa'ah. Na Aayah hii imeonyesha kwamba kuamini ni kumtii Allaah ('Azza wa Jalla)  kufuata yale yote Aliyotuamrisha na kujiepusha na yale Aliyotuharamisha katika Qur-aan.

 

Na kumtii Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ni kufuata amri zake na mafunzo yote aliyotuletea katika Sunnah zake, hapo ndipo Iymaan itakuwa imeingia moyoni mwa Muislamu.

 

Mfano kutofanya maasi yaliyotajwa katika Hadiyth ifuatayo ya Abuu    Hurayrah (Radhwiya Allaahu ‘anhu):

 

((لا يزني الزاني حين يزني وهو مؤمن ، ولا يشرب الخمر حين يشربها وهو مؤمن ، ولا يسرق السارق حين يسرق وهو مؤمن)) البخاري

((Hazini mzinifu  anapozini  hali ya kuwa ni Muumini, wala hanywi pombe   anapokunywa hali ya kuwa ni  Muumini, wala haibi mwizi  anapoiba hali ya kuwa ni Muumini)) [Al-Bukhaariy]

 

 

Kisa cha Julaybiyb na Swahaabiyah aliyemtii Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)

 

Swahaba aliyeitwa Julaybiyb alijulikana sana kuwa alikuwa ni mtu duni asiyemiliki mali na hakuwa ni mzuri kwa sura na umbo, na alikuwa ni mtu wa kuchekesha watu. Kwa hivyo hakuna aliyetaka kumuozesha binti yake. Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)  alimuuliza Julaybib kama anataka kuoa, naye akamjibu: "Ee Rasuli wa Allaah, nani atakayekubali nimuoe mimi? Sina nyumba wala wala mali wala chochote katika mapambo ya dunia."

 

 

Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akamtuma mtu mmoja aende nyumba ya Answaariy fulani ambao walikuwa ni familia yenye kujulikana kwa kabila lao maarufu kubwa lenye kujulikana kwa heshima na wenye hali nzuri. Alipopiga hodi, alifungua mlango mama wa binti huyo. Swahaba akamjulisha kuwa ametumwa na Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kuleta posa kwa binti yake. Mama huyo alifurahi sana kudhania kwamba Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ndiye anayetaka kumposa binti yake.

Swahaba Alipomjulisha kuwa sio kwa ajili ya Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)  bali ni kwa ajili ya Julaybiyb, mama huyo alisema: "Nani? Julaybib? Hapana! Hatumuozeshi yeye binti yetu!" Mara yule binti alisikia mazungumzo hayo akaja kuuliza vizuri: "Nani anayetaka kuniposa?" Mama mtu akamuelezea kuwa Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amemtuma mtu aje kumposa yeye kwa ajili ya Julaybiyb. Binti huyo alimwambia mama yake: "Vipi mama unakataa amri ya Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)? Fuata amri yake kwani hakuna kitakachonidhuru.” (Katika usemi mmoja ni kwamba hapo hapo Aayah ifuatayo iliteremshwa [Ibnu Kathiyr 7:692-694]) na katika usemi mwingine aliwaambia wazazi wake: "Hamkusikia kauli ya Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa):

 

 وَمَا كَانَ لِمُؤْمِنٍ وَلَا مُؤْمِنَةٍ إِذَا قَضَى اللَّـهُ وَرَسُولُهُ أَمْرًا أَن يَكُونَ لَهُمُ الْخِيَرَةُ مِنْ أَمْرِهِمْ ۗ وَمَن يَعْصِ اللَّـهَ وَرَسُولَهُ فَقَدْ ضَلَّ ضَلَالًا مُّبِينًا ﴿٣٦﴾

Na haiwi kwa Muumini mwanamme na wala kwa Muumini mwanamke, Anapohukumu Allaah na Rasuli Wake jambo lolote, iwe wana hiari katika jambo lao.  Na anayemuasi Allaah na Rasuli Wake, basi kwa yakini amepotoka upotofu bayana. [Al-Ahzaab: 36]

 

Ikabidi wamuozeshe binti yao kwa Julaybiyb. Kisha katika vita fulani alitoka Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Maswahaba miongoni mwao ni Julaybiyb na baada ya ushindi wa vita hivyo, Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)  aliwauliza Maswahaba kabla ya kurudi:  ((Je, kuna mtu aliyekosekana?)) Wakataja baadhi ya Maswahaba waliokosekana kisha Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akawauliza tena wakasema: "Hakuna mtu mwingine aliyekosekana.” Lakini Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akasema: ((Lakini mimi naona kwamba Julaybiyb amekosekana)) yaani hayupo na sisi.  (Nendeni mkamtafute miongoni mwa waliouliwa)). Wakaenda Maswahaba kumtafuta wakamkuta ameuawa akiwa karibu yake makafiri saba ambao aliwahi kuwaua yeye Julaybiyb. Maswahaba wakamjulisha Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)  ambaye alikwenda na kusimama karibu naye kisha akasema: ((Ameua saba kisha wakamuua. Yeye ni wangu na mimi ni wake)).

 

Alisema hivyo mara mbili au tatu, kisha Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akambeba kwa mikono yake na kwenda kumzika. Na akamuombea Du'aa mke wake:

 

 

((الَّلهُمَّ، صَبَّ عَلَيْهَا [الخير] صَبَّا، وَلاَ تَجْعَل عَيْشَها كَدَّا))

((Ee Allah, Mjaze kheri (nyingi) zilizojaa na Usimjaaliye maisha yake kuwa ni ya shida [tabu na mashaka]))

 

Imesemekana kwamba hakuweko mjane aliyekuwa ana maisha mema kama maisha ya mke wa Julaybiy (Radhwiya Allaahu ‘anhaa).

 

[Kisa kimesimuliwa na Imaam Ahmad Muslim na An-Nasaaiy]

 

 

Baada ya Aayah hiyo katika Suratul-Hujuraat inayotujulisha kwamba kuamini ni kumtii Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) na Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kisha Anaendelea Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Kutujulisha nani hasa ni Waumini wa kweli waliosadiki:

 

إِنَّمَا الْمُؤْمِنُونَ الَّذِينَ آمَنُوا بِاللَّـهِ وَرَسُولِهِ ثُمَّ لَمْ يَرْتَابُوا وَجَاهَدُوا بِأَمْوَالِهِمْ وَأَنفُسِهِمْ فِي سَبِيلِ اللَّـهِ ۚ أُولَـٰئِكَ هُمُ الصَّادِقُونَ﴿١٥﴾

Hakika Waumini ni wale waliomwamini Allaah na Rasuli Wake, kisha wakawa si wenye shaka, na wakafanya jihaad kwa mali zao na nafsi zao katika njia ya Allaah. Hao ndio wakweli. [Al-Hujuraat: 15]

 

 

Mfano mwengine wa wale walioamini kweli katika kupigana Jihaad kwa nafsi zao katika kisa kifuatacho cha  Handhwalah Aliyeoshwa na Malaika:

 

Handhwala bin Abi 'Aamir ni Swahaba ambaye alifunga ndoa usiku ambao ulinadiwa vita vya Uhud. Aliwahi kulala na mke wake usiku huo mmoja lakini iliponadiwa sauti ya kutoka kwenda Jihaad hakuna chochote kilichomshughulisha wakati huo ila ni kutoka na kukimbilia vitani hata hakuwahi kukoga janaba.

 

Baada ya vita kumalizika Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) aliwaambia Maswahaba kwamba Malaika wamemuosha Handhwalah. Akawatuma wakaulize nyumbani kwake alitoka vipi? Mkewe akawajulisha kuwa alitoka bila ya kuwahi kukoga janaba. Walipokwenda kumtazama Handhwalah walimuona akichirizikwa na maji kama kwamba katokwa kukoshwa. Tokea siku hiyo akajulikana na kuitwa "Aliyeoshwa na Malaika."

 

Hao ndio Maswahaba walioamini kweli wakajitolea nafsi zao bila ya kuona umuhimu wa jambo lolote jengine kuliko amri ya Allaah ('Azza wa Jalla) kuhusuu Jihaad katika Njia ya Allaah.

 

 

 

Share