05-Tawbah Hukmu Na Fadhila Zake: Hatari Ya Kuchelewa Kuomba Maghfirah Na Tawbah
Tawbah Hukmu Na Fadhila Zake
05-Hatari Ya Kuchelewa Kuomba Maghfirah Na Tawbah
Muislam anapofanya maasi ni muhimu kwake atubie haraka iwezekanavyo ili apate kughufuriwa madhambi yake na ipokelewe tawbah yake kwa kufuata amri ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Anaposema:
إِنَّمَا التَّوْبَةُ عَلَى اللَّـهِ لِلَّذِينَ يَعْمَلُونَ السُّوءَ بِجَهَالَةٍ ثُمَّ يَتُوبُونَ مِن قَرِيبٍ فَأُولَـٰئِكَ يَتُوبُ اللَّـهُ عَلَيْهِمْ ۗ وَكَانَ اللَّـهُ عَلِيمًا حَكِيمًا ﴿١٧﴾
Hakika tawbah inayokubaliwa na Allaah ni ya wale wanaofanya uovu kwa ujahili kisha wakatubia haraka, basi hao Allaah Anapokea tawbah yao. Na Allaah ni Mjuzi wa yote, Mwenye hikmah wa yote. [An-Nisaa: 17]
Kuchelewa kuomba tawbah huenda kusifae tena. Huenda mtu akaendelea kufanya madhambi hadi akafika wakati wa kukata tamaa ya kuishi na mauti yakamfikia ndipo akatambua umuhimu wa kuomba tawbah kwa Rabb wake, hapo tena atakuwa kachelewa kabisa na hapo tawbah yake itakuwa haina faida tena kwani Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Anaonya:
وَلَيْسَتِ التَّوْبَةُ لِلَّذِينَ يَعْمَلُونَ السَّيِّئَاتِ حَتَّىٰ إِذَا حَضَرَ أَحَدَهُمُ الْمَوْتُ قَالَ إِنِّي تُبْتُ الْآنَ وَلَا الَّذِينَ يَمُوتُونَ وَهُمْ كُفَّارٌ ۚ أُولَـٰئِكَ أَعْتَدْنَا لَهُمْ عَذَابًا أَلِيمًا ﴿١٨﴾
Lakini tawbah si kwa wale wanaofanya maovu mpaka mauti yanapohudhuria kwa mmoja wao husema: “Hakika mimi sasa nimetubu.” Na wala wale wanaokufa na hali wao ni makafiri. Hao Tumewaandalia adhabu iumizayo. [An-Nisaa: 18]
Mfano wake kama ni mfano wa Fir'awn alivyofanya wakati anazama baharini hapo akaona hana hila ila aombe tawbah. Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):
وَجَاوَزْنَا بِبَنِي إِسْرَائِيلَ الْبَحْرَ فَأَتْبَعَهُمْ فِرْعَوْنُ وَجُنُودُهُ بَغْيًا وَعَدْوًا ۖ حَتَّىٰ إِذَا أَدْرَكَهُ الْغَرَقُ قَالَ آمَنتُ أَنَّهُ لَا إِلَـٰهَ إِلَّا الَّذِي آمَنَتْ بِهِ بَنُو إِسْرَائِيلَ وَأَنَا مِنَ الْمُسْلِمِينَ﴿٩٠﴾
Na Tukawavukisha wana wa Israaiyl bahari, basi Fir’awn akawafuata na jeshi lake kwa ukandamizaji na uadui; mpaka ilipomfikia (Fir’awn) gharka akasema: “Nimeamini kwamba hapana muabudiwa wa haki, isipokuwa Yule waliyemwamini wana wa Israaiyl, na mimi ni miongoni mwa Waislamu.” [Yuwnus: 90]
Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Akamuuliza Fir'awn wakati anatapatapa katika mauti huku akiomba na kudai kuwa kaamini:
آلْآنَ وَقَدْ عَصَيْتَ قَبْلُ وَكُنتَ مِنَ الْمُفْسِدِينَ﴿٩١﴾
“Sasa (ndio unaamini) na ihali umeasi kabla, na ulikuwa miongoni mwa mafisadi!?” [Yuwnus: 91]
Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Akaikataa Tawbah yake katika hali hii, Akasema:
فَالْيَوْمَ نُنَجِّيكَ بِبَدَنِكَ لِتَكُونَ لِمَنْ خَلْفَكَ آيَةً ۚ وَإِنَّ كَثِيرًا مِّنَ النَّاسِ عَنْ آيَاتِنَا لَغَافِلُونَ﴿٩٢﴾
Basi leo Tunakuokoa kwa (kuuweka) mwili wako ili uwe Aayah (zingatio, ishara) kwa watakaokuja nyuma yako. Na hakika watu wengi wameghafilika na Aayaat Zetu. [Yuunus: 92]
Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) vile vile hakuaacha kutufahamisha hatari ya kuchelewa kuomba tawbah katika Hadiyth zifuatazo :
1- Kuomba Maghfirah Na Tawbah kabla ya Sakaraatul-Mawt:
قال صلى الله عليه وسلم: ((إِنَّ الله عزَّ وجَلَّ يقْبَلُ توْبة العبْدِ مَالَم يُغرْغرِ)) رواه أحمد والترمذي وصححه النووي
((Hakika Allaah ‘Azza wa Jalla Huikubali tawbah ya mja Wake kabla ya roho kufika kwenye mkoromo wa mauti)) [Imesimuliwa na Ahmad na At-Tirmidhiy na kusahishwa na An-Nawawiy]
2-Kuomba Maghfirah Na Tawbah Kabla ya kuchomoza jua upande wa Magharibi:
عن أبي هريرة رضي الله عنه أن النبي صل قال : ((مَنْ تَابَ قَبْلَ أَنْ تَطْلُعَ الشَّمْسُ مِنْ مَغْرِبِهَا، تَابَ اللَّهُ عَلَيْهِ)) رواه مسلم
Kutoka kwa Abuu Hurayrah (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kwamba Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kasema: ((Atakayetubu kabla ya kuchomoza jua upande wa Magharibi, Allaah Atamkubalia tawbah yake)) [Muslim]
3-Kuomba Maghfirah Na Tawbah Kabla ya moyo kupofuka wote:
Hatari nyingine ni kuwa huenda mtu ukapofoka moyo wake akawa hajali tena kufanya maovu na hata ikawa shida tena mtu huyo kupata hidaaya kwa kuwa huwa haoni wala hasikii, bali ametumbukia katika maasi. Hadiyth ya Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ifuatayo inaelezea hali kama hiyo:
عن أبي هُرَيرة، قال: قال رسول الله صلى الله عليه وسلم: ((إنَّ العبدَ إذا أخطأَ خطيئةً نُكِتت في قلبِهِ نُكْتةٌ سوداءُ، فإذا هوَ نزعَ واستَغفرَ وتابَ سُقِلَ قلبُهُ، وإن عادَ زيدَ فيها حتَّى تعلوَ قلبَهُ، وَهوَ الرَّانُ الَّذي ذَكَرَ اللَّه عز وجل ((كَلاَّ بَلْ رَانَ عَلَى قُلُوبِهِم مَّا كَانُوا يَكْسِبُونَ)) رواه أحمد والترمذي وحسنه الألباني
Imetoka kwa Abu Hurayrah (Radhwiya Allaahu ‘anhu) ambaye amesema: Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Mja anapofanya dhambi, doa jeusi (kutu) huwekwa katika moyo wake. Akiacha dhambi hiyo, na kuomba maghfirah na kutubu, moyo wake husafishwa ukawa msafi, lakini akirudia kufanya dhambi, doa (kutu) huzidi kuenea mpaka kufunika moyo wote na hiyo ndio 'Raan' (kutu) aliyosema Allaah ‘Azza wa Jalla: ((Laa hasha! Bali imefanya kutu juu ya nyoyo zao yale waliyokuwa wakiyachuma] [Al-Mutwaffifiyn: 14] [Imesimuliwa na Ahmad, At-Tirmidhiy na Shaykh Al-Albaaniy amesema ni Hasan.
Inasikitisha kwamba baadhi ya Waislamu huchelewa kuomba Tawbah. Kuna ambao hawatilii umuhimu wake, na wengine wakijiona kuwa ni vijana bado, hivyo hutegemea kutubia wakifika uzeeni ambako hakuna uhakika wake wa kuishi mpaka huko. Huo ni uchochezi wa Ibliys anayempambia binaadamu kwa kumpa matumaini ya maisha marefu. Basi inapasa kumwepuka Ibliys na kukimbilia kutubu Tawbah ya kweli kabla ya majuto.