018 - Al-Kahf

 

الْكَهْف

 

018-Al-Kahf

 

 018-Al-Kahf: Utangulizi Wa Suwrah

 

Alhidaaya.com

 

 

بِسْمِ اللَّـهِ الرَّحْمَـٰنِ الرَّحِيمِ

 

 

الْحَمْدُ لِلَّـهِ الَّذِي أَنزَلَ عَلَىٰ عَبْدِهِ الْكِتَابَ وَلَمْ يَجْعَل لَّهُ عِوَجًا ۜ﴿١﴾

1. AlhamduliLLaah (Himdi Anastahiki Allaah) Ambaye Amemteremshia Mja Wake (Nabiy Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم) Kitabu na wala Hakukifanya kiwe upogo.[1]

 

 

 

قَيِّمًا لِّيُنذِرَ بَأْسًا شَدِيدًا مِّن لَّدُنْهُ وَيُبَشِّرَ الْمُؤْمِنِينَ الَّذِينَ يَعْمَلُونَ الصَّالِحَاتِ أَنَّ لَهُمْ أَجْرًا حَسَنًا ﴿٢﴾

2. Kimenyooka sawa ili kionye adhabu shadidi kutoka Kwake (Allaah), na kiwabashirie Waumini watendao mema kwamba watapata ujira mzuri.

 

 

 

مَّاكِثِينَ فِيهِ أَبَدًا ﴿٣﴾

3. Wakae humo abadi.

 

 

 

وَيُنذِرَ الَّذِينَ قَالُوا اتَّخَذَ اللَّـهُ وَلَدًا ﴿٤﴾

4. Na kiwaonye wanaosema: Allaah Amejifanyia mwana.

 

 

 

مَّا لَهُم بِهِ مِنْ عِلْمٍ وَلَا لِآبَائِهِمْ ۚ كَبُرَتْ كَلِمَةً تَخْرُجُ مِنْ أَفْوَاهِهِمْ ۚ إِن يَقُولُونَ إِلَّا كَذِبًا ﴿٥﴾

5. Hawana ilimu yoyote kwayo wao na hata baba zao. Neno kubwa kabisa linatoka vinywani mwao. Hawasemi isipokuwa uongo tu.

 

 

 

فَلَعَلَّكَ بَاخِعٌ نَّفْسَكَ عَلَىٰ آثَارِهِمْ إِن لَّمْ يُؤْمِنُوا بِهَـٰذَا الْحَدِيثِ أَسَفًا ﴿٦﴾

6. Basi huenda ukaiangamiza nafsi yako (kwa ghamu na huzuni ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم) kwa ajili yao kwa ghamu na huzuni kwa kuwa wao hawatoamini ujumbe huu (Qur-aan).

 

 

 

إِنَّا جَعَلْنَا مَا عَلَى الْأَرْضِ زِينَةً لَّهَا لِنَبْلُوَهُمْ أَيُّهُمْ أَحْسَنُ عَمَلًا ﴿٧﴾

7. Hakika Sisi Tumefanya vilivyoko juu ya ardhi kuwa ni pambo lake ili Tuwajaribu, nani miongoni mwao mwenye amali nzuri zaidi.

 

 

 

وَإِنَّا لَجَاعِلُونَ مَا عَلَيْهَا صَعِيدًا جُرُزًا ﴿٨﴾

8. Na hakika Sisi bila shaka Tutafanya vilivyo juu yake kuwa udongo mkavu usiomea chochote.  

 

 

 

أَمْ حَسِبْتَ أَنَّ أَصْحَابَ الْكَهْفِ وَالرَّقِيمِ كَانُوا مِنْ آيَاتِنَا عَجَبًا ﴿٩﴾

9. Je, unadhani kwamba watu wa pangoni[2] na maandiko walikuwa ni ajabu zaidi kati ya Aayaat (Ishara, Dalili) Zetu?

 

 

 

إِذْ أَوَى الْفِتْيَةُ إِلَى الْكَهْفِ فَقَالُوا رَبَّنَا آتِنَا مِن لَّدُنكَ رَحْمَةً وَهَيِّئْ لَنَا مِنْ أَمْرِنَا رَشَدًا ﴿١٠﴾

10. Pale vijana walipokimbilia katika pango wakasema: Rabb wetu! Tupe kutoka Kwako Rehma, na Tutengenezee katika jambo letu mwongozo wa sawa.

 

 

 

فَضَرَبْنَا عَلَىٰ آذَانِهِمْ فِي الْكَهْفِ سِنِينَ عَدَدًا ﴿١١﴾

11. Tukawaziba masikio yao pangoni (kuwalaza) kwa idadi ya miaka mingi.

 

 

 

ثُمَّ بَعَثْنَاهُمْ لِنَعْلَمَ أَيُّ الْحِزْبَيْنِ أَحْصَىٰ لِمَا لَبِثُوا أَمَدًا ﴿١٢﴾

12. Kisha Tukawainua ili Tupambanue nani kati ya makundi mawili lililohesabu madhubuti zaidi kuhusu muda wao waliobakia.

 

 

 

نَّحْنُ نَقُصُّ عَلَيْكَ نَبَأَهُم بِالْحَقِّ ۚ إِنَّهُمْ فِتْيَةٌ آمَنُوا بِرَبِّهِمْ وَزِدْنَاهُمْ هُدًى ﴿١٣﴾

13. Sisi Tunakusimulia (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم) khabari zao kwa haki. Hakika wao ni vijana waliomwamini Rabb wao na Tukawazidishia hidaya.

 

 

 

وَرَبَطْنَا عَلَىٰ قُلُوبِهِمْ إِذْ قَامُوا فَقَالُوا رَبُّنَا رَبُّ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ لَن نَّدْعُوَ مِن دُونِهِ إِلَـٰهًا ۖ لَّقَدْ قُلْنَا إِذًا شَطَطًا ﴿١٤﴾

14. Na Tukazitia nguvu nyoyo zao waliposimama wakasema: Rabb wetu, ni Rabb wa mbingu na ardhi. Hatutomuomba asiyekuwa Yeye kuwa mwabudiwa, (laa sivyo) kwa yakini hapo tutakuwa tumesema kauli ya kufuru na kuvuka mpaka.

 

 

 

هَـٰؤُلَاءِ قَوْمُنَا اتَّخَذُوا مِن دُونِهِ آلِهَةً ۖ لَّوْلَا يَأْتُونَ عَلَيْهِم بِسُلْطَانٍ بَيِّنٍ ۖ فَمَنْ أَظْلَمُ مِمَّنِ افْتَرَىٰ عَلَى اللَّـهِ كَذِبًا ﴿١٥﴾

15. Hawa watu wetu wamejichukulia waabudiwa wengine badala Yake. Kwa nini basi hawawatolei ushahidi wa bayana? Basi nani dhalimu zaidi kuliko anayemtungia Allaah uongo?

 

 

 

وَإِذِ اعْتَزَلْتُمُوهُمْ وَمَا يَعْبُدُونَ إِلَّا اللَّـهَ فَأْوُوا إِلَى الْكَهْفِ يَنشُرْ لَكُمْ رَبُّكُم مِّن رَّحْمَتِهِ وَيُهَيِّئْ لَكُم مِّنْ أَمْرِكُم مِّرْفَقًا ﴿١٦﴾

16. Na mkijitenga nao na vile wanavyoviabudu badala ya Allaah, basi kimbilieni pangoni. Rabb wenu Atakukunjulieni Rehma Zake, na Atakutengenezeeni kwa wepesi ya kukufaeni katika mambo yenu.

 

 

 

وَتَرَى الشَّمْسَ إِذَا طَلَعَت تَّزَاوَرُ عَن كَهْفِهِمْ ذَاتَ الْيَمِينِ وَإِذَا غَرَبَت تَّقْرِضُهُمْ ذَاتَ الشِّمَالِ وَهُمْ فِي فَجْوَةٍ مِّنْهُ ۚ ذَٰلِكَ مِنْ آيَاتِ اللَّـهِ ۗ مَن يَهْدِ اللَّـهُ فَهُوَ الْمُهْتَدِ ۖ وَمَن يُضْلِلْ فَلَن تَجِدَ لَهُ وَلِيًّا مُّرْشِدًا ﴿١٧﴾

17. Na (ungelikuweko, basi ungelikuwa) unaliona jua linapochomoza linaelemea pango lao kwa upande wa kulia, na linapokuchwa linawakwepa upande wa kushoto, nao wamo katika uwazi wa humo. Hiyo ni miongoni mwa Aayaat (Ishara, Dalili) za Allaah. Ambaye Allaah Amemwongoza, basi huyo ndiye aliyehidika. Na Anayemwacha kupotoka basi hutompatia rafiki mlinzi wa kumuongoza.

 

 

 

وَتَحْسَبُهُمْ أَيْقَاظًا وَهُمْ رُقُودٌ ۚ وَنُقَلِّبُهُمْ ذَاتَ الْيَمِينِ وَذَاتَ الشِّمَالِ ۖ وَكَلْبُهُم بَاسِطٌ ذِرَاعَيْهِ بِالْوَصِيدِ ۚ لَوِ اطَّلَعْتَ عَلَيْهِمْ لَوَلَّيْتَ مِنْهُمْ فِرَارًا وَلَمُلِئْتَ مِنْهُمْ رُعْبًا ﴿١٨﴾

18. Na (ungeliwaona, basi) utawadhania wako wamacho na hali wao wamelala. Na Tunawageuza upande wa kulia na upande wa kushoto. Na mbwa wao amenyoosha miguu yake ya mbele kizingitini. Kama ungeliwatokea, bila shaka ungegeuka kuwakimbia, na bila shaka ungejazwa tisho kubwa kuwaogopa.

 

 

 

وَكَذَٰلِكَ بَعَثْنَاهُمْ لِيَتَسَاءَلُوا بَيْنَهُمْ ۚ قَالَ قَائِلٌ مِّنْهُمْ كَمْ لَبِثْتُمْ ۖ قَالُوا لَبِثْنَا يَوْمًا أَوْ بَعْضَ يَوْمٍ ۚ قَالُوا رَبُّكُمْ أَعْلَمُ بِمَا لَبِثْتُمْ فَابْعَثُوا أَحَدَكُم بِوَرِقِكُمْ هَـٰذِهِ إِلَى الْمَدِينَةِ فَلْيَنظُرْ أَيُّهَا أَزْكَىٰ طَعَامًا فَلْيَأْتِكُم بِرِزْقٍ مِّنْهُ وَلْيَتَلَطَّفْ وَلَا يُشْعِرَنَّ بِكُمْ أَحَدًا ﴿١٩﴾

19. Na hivyo ndivyo Tulivyowaamsha (katika usingizi mrefu) ili waulizane baina yao. Msemaji miongoni mwao akasema: Muda gani mmekaa? Wakasema: Tumekaa siku moja au sehemu ya siku.  Wakasema: Rabb wenu Anajua zaidi muda mliokaa. Basi tumeni mmoja wenu mjini kwa noti zenu hizi atazame chakula chake kipi kifaacho zaidi kisha akuleteeni chakula hicho. Na awe makini na busara, na wala asikutambulisheni kwa yeyote.

 

 

إِنَّهُمْ إِن يَظْهَرُوا عَلَيْكُمْ يَرْجُمُوكُمْ أَوْ يُعِيدُوكُمْ فِي مِلَّتِهِمْ وَلَن تُفْلِحُوا إِذًا أَبَدًا ﴿٢٠﴾

20. Hakika wao wakikugundueni, watakupigeni mawe au watakurudisheni katika dini yao, na hapo hamtofaulu abadani.

 

 

 

وَكَذَٰلِكَ أَعْثَرْنَا عَلَيْهِمْ لِيَعْلَمُوا أَنَّ وَعْدَ اللَّـهِ حَقٌّ وَأَنَّ السَّاعَةَ لَا رَيْبَ فِيهَا إِذْ يَتَنَازَعُونَ بَيْنَهُمْ أَمْرَهُمْ ۖ فَقَالُوا ابْنُوا عَلَيْهِم بُنْيَانًا ۖ رَّبُّهُمْ أَعْلَمُ بِهِمْ ۚ قَالَ الَّذِينَ غَلَبُوا عَلَىٰ أَمْرِهِمْ لَنَتَّخِذَنَّ عَلَيْهِم مَّسْجِدًا ﴿٢١﴾

21. Na hivyo ndivyo Tulivyowatambulisha kwa watu ili wajue kwamba Ahadi ya Allaah ni haki. Na kwamba Saa (Qiyaamah) haina shaka yoyote. Pale walipozozana baina yao kuhusu jambo lao. Wakasema: Jengeni jengo juu yao, Rabb wao Anawajua vyema. Wakasema wale walioshinda katika shauri lao: Bila shaka tutajenga mahali pa ibaada juu yao.

 

 

 

سَيَقُولُونَ ثَلَاثَةٌ رَّابِعُهُمْ كَلْبُهُمْ وَيَقُولُونَ خَمْسَةٌ سَادِسُهُمْ كَلْبُهُمْ رَجْمًا بِالْغَيْبِ ۖ وَيَقُولُونَ سَبْعَةٌ وَثَامِنُهُمْ كَلْبُهُمْ ۚ قُل رَّبِّي أَعْلَمُ بِعِدَّتِهِم مَّا يَعْلَمُهُمْ إِلَّا قَلِيلٌ ۗ فَلَا تُمَارِ فِيهِمْ إِلَّا مِرَاءً ظَاهِرًا وَلَا تَسْتَفْتِ فِيهِم مِّنْهُمْ أَحَدًا ﴿٢٢﴾

22. Watasema: Watatu na wanne wao ni mbwa wao. Na (wengine) wanasema: Watano, na wa sita wao ni mbwa wao - kwa kuvurumisha bila ya kujua. Na (wengine) wanasema: Saba, na wa nane wao ni mbwa wao. Sema (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم): Rabb wangu Anajua zaidi idadi yao. Hakuna anayewajua isipokuwa wachache tu. Basi usibishane nao isipokuwa mabishano ya hoja kuntu (Tuliyokufunulia Wahy), na wala usimuulize yeyote kuhusu khabari zao.

 

 

 

وَلَا تَقُولَنَّ لِشَيْءٍ إِنِّي فَاعِلٌ ذَٰلِكَ غَدًا ﴿٢٣﴾

23. Na wala usiseme kamwe kwa jambo lolote lile:  Nitalifanya hilo kesho.[3]

 

 

 

إِلَّا أَن يَشَاءَ اللَّـهُ ۚ وَاذْكُر رَّبَّكَ إِذَا نَسِيتَ وَقُلْ عَسَىٰ أَن يَهْدِيَنِ رَبِّي لِأَقْرَبَ مِنْ هَـٰذَا رَشَدًا ﴿٢٤﴾

24. Isipokuwa (useme): In Shaa Allaah. Na mdhukuru Rabb wako unaposahau.[4]  Na sema: Asaa Rabb wangu Akaniongoa njia iliyo karibu zaidi ya uongofu kuliko hii.

 

 

 

وَلَبِثُوا فِي كَهْفِهِمْ ثَلَاثَ مِائَةٍ سِنِينَ وَازْدَادُوا تِسْعًا ﴿٢٥﴾

25. Na walikaa pangoni mwao miaka mia tatu na wakazidisha tisa.

 

 

 

قُلِ اللَّـهُ أَعْلَمُ بِمَا لَبِثُوا ۖ لَهُ غَيْبُ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ ۖ أَبْصِرْ بِهِ وَأَسْمِعْ ۚ مَا لَهُم مِّن دُونِهِ مِن وَلِيٍّ وَلَا يُشْرِكُ فِي حُكْمِهِ أَحَدًا ﴿٢٦﴾

26. Sema: Allaah Anajua zaidi muda waliokaa. Ni Yake Pekee ghaibu za mbingu na ardhi. Kuona kulioje Kwake na Kusikia! Hawana pasi Naye mlinzi yeyote na wala Hamshirikishi katika Hukumu Zake yeyote.

 

 

 

وَاتْلُ مَا أُوحِيَ إِلَيْكَ مِن كِتَابِ رَبِّكَ ۖ لَا مُبَدِّلَ لِكَلِمَاتِهِ وَلَن تَجِدَ مِن دُونِهِ مُلْتَحَدًا ﴿٢٧﴾

27. Na soma (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم) uliyofunuliwa Wahy katika Kitabu cha Rabb wako. Hakuna yeyote atakayeweza kubadilisha Maneno Yake, na wala hutopata kamwe makimbilio isipokuwa Kwake.    

 

 

 

وَاصْبِرْ نَفْسَكَ مَعَ الَّذِينَ يَدْعُونَ رَبَّهُم بِالْغَدَاةِ وَالْعَشِيِّ يُرِيدُونَ وَجْهَهُ ۖ وَلَا تَعْدُ عَيْنَاكَ عَنْهُمْ تُرِيدُ زِينَةَ الْحَيَاةِ الدُّنْيَا ۖ وَلَا تُطِعْ مَنْ أَغْفَلْنَا قَلْبَهُ عَن ذِكْرِنَا وَاتَّبَعَ هَوَاهُ وَكَانَ أَمْرُهُ فُرُطًا ﴿٢٨﴾

28. Na isubirishe nafsi yako pamoja na wale wanaomuomba Rabb wao asubuhi kabla jua kucha na jioni, wanataka Wajihi Wake. Na wala macho yako yasiwavuke kwa kutaka pambo la uhai wa dunia. Na wala usimtii Tuliyemghafilisha moyo wake na Ukumbusho Wetu akafuata hawaa zake, na jambo lake limekuwa la kuzidi kuvuka mipaka.

 

 

 

وَقُلِ الْحَقُّ مِن رَّبِّكُمْ ۖ فَمَن شَاءَ فَلْيُؤْمِن وَمَن شَاءَ فَلْيَكْفُرْ ۚ إِنَّا أَعْتَدْنَا لِلظَّالِمِينَ نَارًا أَحَاطَ بِهِمْ سُرَادِقُهَا ۚ وَإِن يَسْتَغِيثُوا يُغَاثُوا بِمَاءٍ كَالْمُهْلِ يَشْوِي الْوُجُوهَ ۚ بِئْسَ الشَّرَابُ وَسَاءَتْ مُرْتَفَقًا ﴿٢٩﴾

29. Na sema: Hii ni haki kutoka kwa Rabb wenu. Basi anayetaka aamini, na anayetaka akufuru. Hakika Sisi Tumewaandalia madhalimu moto ambao kuta zake zitawazunguka. Na wakiomba uokozi, watapewa maji kama masazo ya zebaki nyeusi iliyoyeyushwa yanayobabua nyuso. Ubaya ulioje kinywaji hicho, na uovu ulioje mahali pa kupumzikia!

 

 

إِنَّ الَّذِينَ آمَنُوا وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ إِنَّا لَا نُضِيعُ أَجْرَ مَنْ أَحْسَنَ عَمَلًا ﴿٣٠﴾

30. Hakika wale walioamini na wakatenda mema, hakika Sisi Hatupotezi ujira wa anayetenda amali nzuri kabisa.

 

 

 

أُولَـٰئِكَ لَهُمْ جَنَّاتُ عَدْنٍ تَجْرِي مِن تَحْتِهِمُ الْأَنْهَارُ يُحَلَّوْنَ فِيهَا مِنْ أَسَاوِرَ مِن ذَهَبٍ وَيَلْبَسُونَ ثِيَابًا خُضْرًا مِّن سُندُسٍ وَإِسْتَبْرَقٍ مُّتَّكِئِينَ فِيهَا عَلَى الْأَرَائِكِ ۚ نِعْمَ الثَّوَابُ وَحَسُنَتْ مُرْتَفَقًا ﴿٣١﴾

31. Hao watapata Jannaat za kudumu milele zipitazo chini yao mito, watapambwa humo vikuku vya dhahabu, na watavaa nguo za kijani za hariri laini na hariri nzito nyororo, wakiegemea humo kwenye makochi ya fakhari. Uzuri ulioje wa thawabu na mahali pazuri palioje pa kupumzikia!

 

 

 

وَاضْرِبْ لَهُم مَّثَلًا رَّجُلَيْنِ جَعَلْنَا لِأَحَدِهِمَا جَنَّتَيْنِ مِنْ أَعْنَابٍ وَحَفَفْنَاهُمَا بِنَخْلٍ وَجَعَلْنَا بَيْنَهُمَا زَرْعًا ﴿٣٢﴾

32. Na wapigie mfano wa watu wawili. Tulimjaalia mmoja wao bustani mbili za mizabibu, na Tukazizungushia kwa mitende, na Tukaweka baina yake mimea.

 

 

 

كِلْتَا الْجَنَّتَيْنِ آتَتْ أُكُلَهَا وَلَمْ تَظْلِم مِّنْهُ شَيْئًا ۚ وَفَجَّرْنَا خِلَالَهُمَا نَهَرًا ﴿٣٣﴾

33. Bustani zote mbili zilitoa mazao yake, na wala hazikupunguza humo chochote. Na Tukabubujua baina yake mto.

 

 

 

وَكَانَ لَهُ ثَمَرٌ فَقَالَ لِصَاحِبِهِ وَهُوَ يُحَاوِرُهُ أَنَا أَكْثَرُ مِنكَ مَالًا وَأَعَزُّ نَفَرًا ﴿٣٤﴾

34. Naye alikuwa ana mazao mengine (mbali ya bustani mbili). Akamwambia sahibu yake naye huku akizungumza na kujibishana naye: Mimi nina mali zaidi kuliko wewe, na nguvu zaidi za watu.

 

 

 

وَدَخَلَ جَنَّتَهُ وَهُوَ ظَالِمٌ لِّنَفْسِهِ قَالَ مَا أَظُنُّ أَن تَبِيدَ هَـٰذِهِ أَبَدًا ﴿٣٥﴾

35. Akaingia bustanini mwake hali ya kuwa anajidhulumu nafsi yake, akasema: Sidhani kama haya yatatoweka abadani.

 

 

 

وَمَا أَظُنُّ السَّاعَةَ قَائِمَةً وَلَئِن رُّدِدتُّ إِلَىٰ رَبِّي لَأَجِدَنَّ خَيْرًا مِّنْهَا مُنقَلَبًا ﴿٣٦﴾

36. Na wala sidhani kama Saa itasimama. Na hata kama nitarudishwa kwa Rabb wangu, bila shaka nitakuta marejeo bora kuliko haya.

 

 

 

قَالَ لَهُ صَاحِبُهُ وَهُوَ يُحَاوِرُهُ أَكَفَرْتَ بِالَّذِي خَلَقَكَ مِن تُرَابٍ ثُمَّ مِن نُّطْفَةٍ ثُمَّ سَوَّاكَ رَجُلًا ﴿٣٧﴾

37. Sahibu yake akamwambia na huku anajadiliana naye: Je, umemkufuru Yule Aliyekuumba kutokana na mchanga, kisha kutokana na manii, kisha Akakusawazisha kuwa mtu?

 

 

 

لَّـٰكِنَّا هُوَ اللَّـهُ رَبِّي وَلَا أُشْرِكُ بِرَبِّي أَحَدًا ﴿٣٨﴾

38. Lakini (mimi naamini) Yeye Allaah Ndiye Rabb wangu, na wala sitomshirikisha Rabb wangu na yeyote.

 

 

 

وَلَوْلَا إِذْ دَخَلْتَ جَنَّتَكَ قُلْتَ مَا شَاءَ اللَّـهُ لَا قُوَّةَ إِلَّا بِاللَّـهِ ۚ إِن تَرَنِ أَنَا أَقَلَّ مِنكَ مَالًا وَوَلَدًا ﴿٣٩﴾

39. Na lau ulipoingia bustanini mwako ungelisema: Maa Shaa Allaah! Hapana nguvu ila za Allaah. Japo kama unaniona mimi nina mali na watoto kidogo kuliko wewe.

 

 

 

فَعَسَىٰ رَبِّي أَن يُؤْتِيَنِ خَيْرًا مِّن جَنَّتِكَ وَيُرْسِلَ عَلَيْهَا حُسْبَانًا مِّنَ السَّمَاءِ فَتُصْبِحَ صَعِيدًا زَلَقًا ﴿٤٠﴾

40. Basi asaa Rabb wangu Akanipa yaliyo bora kuliko bustani yako, na Akaipelekea maafa kutoka mbinguni, ikapambazukiwa kuwa ardhi kame inayoteleza.

 

 

 

أَوْ يُصْبِحَ مَاؤُهَا غَوْرًا فَلَن تَسْتَطِيعَ لَهُ طَلَبًا ﴿٤١﴾

41. Au yakawa maji yake ya kudidimia kisha hutoweza kuyafuatilia (na kuyapata).

 

 

 

وَأُحِيطَ بِثَمَرِهِ فَأَصْبَحَ يُقَلِّبُ كَفَّيْهِ عَلَىٰ مَا أَنفَقَ فِيهَا وَهِيَ خَاوِيَةٌ عَلَىٰ عُرُوشِهَا وَيَقُولُ يَا لَيْتَنِي لَمْ أُشْرِكْ بِرَبِّي أَحَدًا ﴿٤٢﴾

42. Basi mazao yake yakazungukwa (na maafa), akabakia anapindua pindua viganja vyake (kusikitika) juu ya yale aliyoyagharamia humo, nayo imeporomoka juu ya chanja zake na huku anasema: Laiti nisingelimshirikisha Rabb wangu na yeyote.

 

 

 

وَلَمْ تَكُن لَّهُ فِئَةٌ يَنصُرُونَهُ مِن دُونِ اللَّـهِ وَمَا كَانَ مُنتَصِرًا ﴿٤٣﴾

43. Na hakuwa ana kundi lolote la kumnusuru pasina Allaah, na wala hakuweza kujisaidia.

 

 

 

هُنَالِكَ الْوَلَايَةُ لِلَّـهِ الْحَقِّ ۚ هُوَ خَيْرٌ ثَوَابًا وَخَيْرٌ عُقْبًا ﴿٤٤﴾

44. Huko (Aakhirah) utawala ni wa Allaah Pekee wa haki. Yeye ni Mbora zaidi wa Kulipa thawabu, na Mbora zaidi wa matokeo ya mwisho.

 

 

 

وَاضْرِبْ لَهُم مَّثَلَ الْحَيَاةِ الدُّنْيَا كَمَاءٍ أَنزَلْنَاهُ مِنَ السَّمَاءِ فَاخْتَلَطَ بِهِ نَبَاتُ الْأَرْضِ فَأَصْبَحَ هَشِيمًا تَذْرُوهُ الرِّيَاحُ ۗ وَكَانَ اللَّـهُ عَلَىٰ كُلِّ شَيْءٍ مُّقْتَدِرًا ﴿٤٥﴾

45. Na wapigie mfano wa uhai wa dunia. Ni kama maji Tuliyoyateremsha kutoka mbinguni, ikachanganyika nayo mimea ya ardhi (ikasitawi), kisha ikawa mikavu iliyovurugika, inapeperushwa na upepo. Na Allaah daima Ni Mwenye Uwezo wa juu kabisa kwa kila kitu.

 

 

 

الْمَالُ وَالْبَنُونَ زِينَةُ الْحَيَاةِ الدُّنْيَا ۖ وَالْبَاقِيَاتُ الصَّالِحَاتُ خَيْرٌ عِندَ رَبِّكَ ثَوَابًا وَخَيْرٌ أَمَلًا ﴿٤٦﴾

46. Mali na watoto ni pambo la uhai wa dunia. Na mema yanayobakia[5] ni bora mbele ya Rabb wako kwa thawabu na matumaini mema zaidi. 

 

 

 

وَيَوْمَ نُسَيِّرُ الْجِبَالَ وَتَرَى الْأَرْضَ بَارِزَةً وَحَشَرْنَاهُمْ فَلَمْ نُغَادِرْ مِنْهُمْ أَحَدًا ﴿٤٧﴾

47. Na Siku Tutakapoiendesha milima, na utaiona ardhi tambarare tupu, na Tutawakusanya wala Hatutomwacha hata mmoja katika wao.

 

 

 

وَعُرِضُوا عَلَىٰ رَبِّكَ صَفًّا لَّقَدْ جِئْتُمُونَا كَمَا خَلَقْنَاكُمْ أَوَّلَ مَرَّةٍ ۚ بَلْ زَعَمْتُمْ أَلَّن نَّجْعَلَ لَكُم مَّوْعِدًا ﴿٤٨﴾

48. Na watahudhurishwa mbele ya Rabb wako safu safu. (Allaah Atawaambia): Kwa yakini mmetujia kama Tulivyokuumbeni mara ya kwanza.[6] Bali mlidai kwamba Hatutakuwekeeni miadi (hii).

 

 

 

وَوُضِعَ الْكِتَابُ فَتَرَى الْمُجْرِمِينَ مُشْفِقِينَ مِمَّا فِيهِ وَيَقُولُونَ يَا وَيْلَتَنَا مَالِ هَـٰذَا الْكِتَابِ لَا يُغَادِرُ صَغِيرَةً وَلَا كَبِيرَةً إِلَّا أَحْصَاهَا ۚ وَوَجَدُوا مَا عَمِلُوا حَاضِرًا ۗ وَلَا يَظْلِمُ رَبُّكَ أَحَدًا ﴿٤٩﴾

49. Na kitawekwa Kitabu, basi utaona wahalifu ni wenye khofu kwa yale yaliyomo ndani yake, watasema: Ole wetu! Kitabu hiki kina nini? Hakiachi dogo wala kubwa isipokuwa kimerekodi hesabuni![7] Na watakuta yale waliyoyatenda yamehudhuria hapo. Na Rabb wako Hamdhulumu yeyote.

 

 

 

وَإِذْ قُلْنَا لِلْمَلَائِكَةِ اسْجُدُوا لِآدَمَ فَسَجَدُوا إِلَّا إِبْلِيسَ كَانَ مِنَ الْجِنِّ فَفَسَقَ عَنْ أَمْرِ رَبِّهِ ۗ أَفَتَتَّخِذُونَهُ وَذُرِّيَّتَهُ أَوْلِيَاءَ مِن دُونِي وَهُمْ لَكُمْ عَدُوٌّ ۚ بِئْسَ لِلظَّالِمِينَ بَدَلًا ﴿٥٠﴾

50. Na pindi Tulipowaambia Malaika: Msujudieni Aadam. Wakasujudu isipokuwa Ibliys, alikuwa miongoni mwa majini, akaasi Amri ya Rabb wake. Je, basi mnamfanya yeye na kizazi chake rafiki walinzi pasi Nami na hali wao kwenu ni maadui? Ubaya ulioje mbadala huu kwa madhalimu!  

 

 

 

مَّا أَشْهَدتُّهُمْ خَلْقَ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ وَلَا خَلْقَ أَنفُسِهِمْ وَمَا كُنتُ مُتَّخِذَ الْمُضِلِّينَ عَضُدًا ﴿٥١﴾

51. (Allaah Anasema): Sikuwashuhudisha kuumbwa mbingu na ardhi, wala kuumbwa nafsi zao, na wala Sikuwafanya wapotoshaji kuwa wasaidizi.

 

 

 

وَيَوْمَ يَقُولُ نَادُوا شُرَكَائِيَ الَّذِينَ زَعَمْتُمْ فَدَعَوْهُمْ فَلَمْ يَسْتَجِيبُوا لَهُمْ وَجَعَلْنَا بَيْنَهُم مَّوْبِقًا ﴿٥٢﴾

52. Na Siku Tutakayosema: Iteni mliodai kuwa ni washirika Wangu Watawaita, lakini hawatowaitikia, na Tutaweka baina yao mahali pa maangamizi.

 

 

 

وَرَأَى الْمُجْرِمُونَ النَّارَ فَظَنُّوا أَنَّهُم مُّوَاقِعُوهَا وَلَمْ يَجِدُوا عَنْهَا مَصْرِفًا ﴿٥٣﴾

53. Na wahalifu watauona moto, watajua hakika kwamba wao wataangukia humo, na hawatopata njia ya kuuepuka.

 

 

 

وَلَقَدْ صَرَّفْنَا فِي هَـٰذَا الْقُرْآنِ لِلنَّاسِ مِن كُلِّ مَثَلٍ ۚ وَكَانَ الْإِنسَانُ أَكْثَرَ شَيْءٍ جَدَلًا ﴿٥٤﴾

54. Na kwa yakini Tumesarifu namna kwa namna katika hii Qur-aan kwa watu, kwa kila mifano. Lakini binaadam amezidi kuliko kila kitu kwa ubishi.

 

 

 

وَمَا مَنَعَ النَّاسَ أَن يُؤْمِنُوا إِذْ جَاءَهُمُ الْهُدَىٰ وَيَسْتَغْفِرُوا رَبَّهُمْ إِلَّا أَن تَأْتِيَهُمْ سُنَّةُ الْأَوَّلِينَ أَوْ يَأْتِيَهُمُ الْعَذَابُ قُبُلًا ﴿٥٥﴾

55. Na hakuna kilichowazuia watu kuamini ulipowajia mwongozo na wakamwomba maghfirah Rabb wao isipokuwa iwafikie desturi ya watu wa awali,[8] au iwafikie adhabu ya kuwakabili.

 

 

 

وَمَا نُرْسِلُ الْمُرْسَلِينَ إِلَّا مُبَشِّرِينَ وَمُنذِرِينَ ۚ وَيُجَادِلُ الَّذِينَ كَفَرُوا بِالْبَاطِلِ لِيُدْحِضُوا بِهِ الْحَقَّ ۖ وَاتَّخَذُوا آيَاتِي وَمَا أُنذِرُوا هُزُوًا ﴿٥٦﴾

56. Na Hatukutuma Rusuli isipokuwa wabashiriaji na waonyaji. Na wale waliokufuru wanabisha kwa batili ili watengue haki kwa batili hiyo. Na wakazichukua Aayaat (na Ishara, Dalili, Hoja) Zangu na yale waliyoonywa nayo kuwa ni mzaha.

 

 

 

وَمَنْ أَظْلَمُ مِمَّن ذُكِّرَ بِآيَاتِ رَبِّهِ فَأَعْرَضَ عَنْهَا وَنَسِيَ مَا قَدَّمَتْ يَدَاهُ ۚ إِنَّا جَعَلْنَا عَلَىٰ قُلُوبِهِمْ أَكِنَّةً أَن يَفْقَهُوهُ وَفِي آذَانِهِمْ وَقْرًا ۖ وَإِن تَدْعُهُمْ إِلَى الْهُدَىٰ فَلَن يَهْتَدُوا إِذًا أَبَدًا ﴿٥٧﴾

57. Na nani dhalimu zaidi kuliko yule aliyekumbushwa Aayaat za Rabb wake, akazipuuza na akayasahu yale iliyotanguliza mikono yake? Hakika Sisi Tumeweka nyoyoni mwao vifuniko wasizifahamu (Aayaat), na katika masikio yao uziwi.[9] Na ukiwaita kwenye mwongozo hawataongoka abadani! 

 

 

 

وَرَبُّكَ الْغَفُورُ ذُو الرَّحْمَةِ ۖ لَوْ يُؤَاخِذُهُم بِمَا كَسَبُوا لَعَجَّلَ لَهُمُ الْعَذَابَ ۚ بَل لَّهُم مَّوْعِدٌ لَّن يَجِدُوا مِن دُونِهِ مَوْئِلًا ﴿٥٨﴾

58. Na Rabb wako ni Mwingi wa Kughufuria, Mwenye Rehma. Kama Angeliwachukulia kwa yale waliyoyachuma, Angeliwaharakizia adhabu. Bali wao wana miadi, hawatopata pasi Naye kimbilio la kuepukana nayo.

 

 

 

وَتِلْكَ الْقُرَىٰ أَهْلَكْنَاهُمْ لَمَّا ظَلَمُوا وَجَعَلْنَا لِمَهْلِكِهِم مَّوْعِدًا ﴿٥٩﴾

59. Na miji hiyo, Tuliwaangamiza (wakazi wake) walipodhulumu, na Tukaweka miadi kwa ajili ya maangamizo yao.

 

 

 

وَإِذْ قَالَ مُوسَىٰ لِفَتَاهُ لَا أَبْرَحُ حَتَّىٰ أَبْلُغَ مَجْمَعَ الْبَحْرَيْنِ أَوْ أَمْضِيَ حُقُبًا ﴿٦٠﴾

60. Na pindi Muwsaa alipomwambia kijana wake:[10] Sitoacha kuendelea (safari) mpaka nifikie zinapokutana bahari mbili, au nitaendelea muda mrefu.[11]

 

 

 

فَلَمَّا بَلَغَا مَجْمَعَ بَيْنِهِمَا نَسِيَا حُوتَهُمَا فَاتَّخَذَ سَبِيلَهُ فِي الْبَحْرِ سَرَبًا ﴿٦١﴾

61. Basi walipofika zinapoungana bahari mbili, walimsahau samaki wao, naye akachukua njia yake baharini akiponyoka chini kwa chini.

 

 

 

فَلَمَّا جَاوَزَا قَالَ لِفَتَاهُ آتِنَا غَدَاءَنَا لَقَدْ لَقِينَا مِن سَفَرِنَا هَـٰذَا نَصَبًا ﴿٦٢﴾

62. Walipokwishapita, alimwambia kijana wake: Tuletee chakula chetu cha mchana, kwa hakika tumepata machofu ya kutosha katika safari yetu hii.

 

 

 

قَالَ أَرَأَيْتَ إِذْ أَوَيْنَا إِلَى الصَّخْرَةِ فَإِنِّي نَسِيتُ الْحُوتَ وَمَا أَنسَانِيهُ إِلَّا الشَّيْطَانُ أَنْ أَذْكُرَهُ ۚ وَاتَّخَذَ سَبِيلَهُ فِي الْبَحْرِ عَجَبًا ﴿٦٣﴾

63. (Kijana wake) akasema: Unaona pale tulipopumzika katika mwamba. Basi mimi nilimsahau samaki, na hakunisahaulisha isipokuwa shaytwaan nisimkumbuke.  Akachukua njia yake baharini kimaajabu.

 

 

 

قَالَ ذَٰلِكَ مَا كُنَّا نَبْغِ ۚ فَارْتَدَّا عَلَىٰ آثَارِهِمَا قَصَصًا ﴿٦٤﴾

64. (Muwsaa) akasema: Hapo ndipo tulipokuwa tunapataka. Basi wakarudi nyuma kwa kufuata athari za nyayo zao.

 

 

 

فَوَجَدَا عَبْدًا مِّنْ عِبَادِنَا آتَيْنَاهُ رَحْمَةً مِّنْ عِندِنَا وَعَلَّمْنَاهُ مِن لَّدُنَّا عِلْمًا ﴿٦٥﴾

65. Wakamkuta mja miongoni mwa Waja Wetu (Khidhwr), Tuliyempa Rehma kutoka Kwetu, na Tumemfunza kutoka Kwetu ilimu.

 

 

 

قَالَ لَهُ مُوسَىٰ هَلْ أَتَّبِعُكَ عَلَىٰ أَن تُعَلِّمَنِ مِمَّا عُلِّمْتَ رُشْدًا ﴿٦٦﴾

66. Muwsaa akamwambia: Je, nikufuate ili unifunze katika yale uliyofunzwa ya busara?

 

 

 

قَالَ إِنَّكَ لَن تَسْتَطِيعَ مَعِيَ صَبْرًا ﴿٦٧﴾

67. (Khidhwr) akasema: Hakika hutoweza kustahamili pamoja nami.

 

 

 

 

وَكَيْفَ تَصْبِرُ عَلَىٰ مَا لَمْ تُحِطْ بِهِ خُبْرًا ﴿٦٨﴾

68. Na vipi utastahamili kwa ambayo huyaelewi vyema utambuzi wake?

 

 

 

قَالَ سَتَجِدُنِي إِن شَاءَ اللَّـهُ صَابِرًا وَلَا أَعْصِي لَكَ أَمْرًا ﴿٦٩﴾

69. (Muwsaa) akasema: Utanikuta In Shaa Allaah mwenye subira na wala sitokuasi amri.

 

 

 

قَالَ فَإِنِ اتَّبَعْتَنِي فَلَا تَسْأَلْنِي عَن شَيْءٍ حَتَّىٰ أُحْدِثَ لَكَ مِنْهُ ذِكْرًا ﴿٧٠﴾

70. (Khidhwr) akasema: Basi utakaponifuata, usiniulize kuhusu lolote mpaka nianze kukutajia.

 

 

 

فَانطَلَقَا حَتَّىٰ إِذَا رَكِبَا فِي السَّفِينَةِ خَرَقَهَا ۖ قَالَ أَخَرَقْتَهَا لِتُغْرِقَ أَهْلَهَا لَقَدْ جِئْتَ شَيْئًا إِمْرًا ﴿٧١﴾

71. Wakatoka kuendelea kwenda, mpaka walipopanda jahazi. (Khidhwr) akaitoboa. Akasema: Umeitoboa ili ugharikishe watu wake? Kwa yakini umeleta jambo zito la munkari!

 

 

 

قَالَ أَلَمْ أَقُلْ إِنَّكَ لَن تَسْتَطِيعَ مَعِيَ صَبْرًا ﴿٧٢﴾

72. (Khidhwr) akasema: Je, sikusema kwamba hakika wewe hutoweza kustahamili pamoja nami?

 

 

 

قَالَ لَا تُؤَاخِذْنِي بِمَا نَسِيتُ وَلَا تُرْهِقْنِي مِنْ أَمْرِي عُسْرًا ﴿٧٣﴾

73. (Muwsaa) akasema: Usinichukulie kwa niliyoyasahau, na wala usinifanyie tashdidi kubwa kwa jambo langu hili. 

 

 

 

فَانطَلَقَا حَتَّىٰ إِذَا لَقِيَا غُلَامًا فَقَتَلَهُ قَالَ أَقَتَلْتَ نَفْسًا زَكِيَّةً بِغَيْرِ نَفْسٍ لَّقَدْ جِئْتَ شَيْئًا نُّكْرًا ﴿٧٤﴾

74. Wakatoka kuendelea kwenda, mpaka wakakutana na ghulamu (kijana mwanamume) akamuua. (Muwsaa) akasema: Umeua mtu asiye na hatia na wala hakuua mtu? Kwa yakini umeleta jambo linalokirihisha mno lisilokubalika!

 

 

 

قَالَ أَلَمْ أَقُل لَّكَ إِنَّكَ لَن تَسْتَطِيعَ مَعِيَ صَبْرًا ﴿٧٥﴾

75. (Khidhwr) akasema: Je, sikukwambia kwamba hakika wewe hutoweza kustahamili pamoja nami?

 

 

 

قَالَ إِن سَأَلْتُكَ عَن شَيْءٍ بَعْدَهَا فَلَا تُصَاحِبْنِي ۖ قَدْ بَلَغْتَ مِن لَّدُنِّي عُذْرًا ﴿٧٦﴾

76. (Muwsaa) akasema: Nikikuuliza kuhusu chochote baada ya haya, basi usisuhubiane nami, maana umekwishapata udhuru kwangu.

 

 

 

فَانطَلَقَا حَتَّىٰ إِذَا أَتَيَا أَهْلَ قَرْيَةٍ اسْتَطْعَمَا أَهْلَهَا فَأَبَوْا أَن يُضَيِّفُوهُمَا فَوَجَدَا فِيهَا جِدَارًا يُرِيدُ أَن يَنقَضَّ فَأَقَامَهُ ۖ قَالَ لَوْ شِئْتَ لَاتَّخَذْتَ عَلَيْهِ أَجْرًا ﴿٧٧﴾

77. Wakatoka kuendelea kwenda, mpaka wakawafikia watu wa mji, wakawaomba watu wake chakula lakini walikataa kuwakaribisha. Wakakuta humo ukuta unataka kuanguka, na (Khidhwr) akausimamisha. (Muwsaa) akasema: Ungelitaka ungeliuchukulia ujira.

 

 

 

قَالَ هَـٰذَا فِرَاقُ بَيْنِي وَبَيْنِكَ ۚ سَأُنَبِّئُكَ بِتَأْوِيلِ مَا لَمْ تَسْتَطِع عَّلَيْهِ صَبْرًا ﴿٧٨﴾

78. (Khidhwr) akasema: Huku ndiko kufarikiana baina yangu na baina yako. Hivi punde nitakujulisha tafsiri ya hakika ya yale uliyoshindwa kuyavutia subira.  

 

 

 

أَمَّا السَّفِينَةُ فَكَانَتْ لِمَسَاكِينَ يَعْمَلُونَ فِي الْبَحْرِ فَأَرَدتُّ أَنْ أَعِيبَهَا وَكَانَ وَرَاءَهُم مَّلِكٌ يَأْخُذُ كُلَّ سَفِينَةٍ غَصْبًا ﴿٧٩﴾

79. Ama jahazi (niliyoitoboa), ilikuwa ya masikini wanaofanya kazi baharini. Nikataka kuitia dosari, kwani mbele yao alikuweko mfalme anayechukua kila jahazi kwa kupora.

 

 

 

وَأَمَّا الْغُلَامُ فَكَانَ أَبَوَاهُ مُؤْمِنَيْنِ فَخَشِينَا أَن يُرْهِقَهُمَا طُغْيَانًا وَكُفْرًا ﴿٨٠﴾

80. Na ama ghulamu (niliyemuua), wazazi wake wawili walikuwa Waumini. Basi Tukakhofu asije kuwatia mashakani kwa upindukaji mipaka ya kuasi na kufuru.

 

 

 

فَأَرَدْنَا أَن يُبْدِلَهُمَا رَبُّهُمَا خَيْرًا مِّنْهُ زَكَاةً وَأَقْرَبَ رُحْمًا ﴿٨١﴾

81. Tukakusudia Rabb wao Awabadilishie aliye bora zaidi kuliko yeye kiutakasifu na aliyekuwa karibu zaidi kihuruma.

 

 

 

وَأَمَّا الْجِدَارُ فَكَانَ لِغُلَامَيْنِ يَتِيمَيْنِ فِي الْمَدِينَةِ وَكَانَ تَحْتَهُ كَنزٌ لَّهُمَا وَكَانَ أَبُوهُمَا صَالِحًا فَأَرَادَ رَبُّكَ أَن يَبْلُغَا أَشُدَّهُمَا وَيَسْتَخْرِجَا كَنزَهُمَا رَحْمَةً مِّن رَّبِّكَ ۚ وَمَا فَعَلْتُهُ عَنْ أَمْرِي ۚ ذَٰلِكَ تَأْوِيلُ مَا لَمْ تَسْطِع عَّلَيْهِ صَبْرًا ﴿٨٢﴾

82. Na ama ukuta (niliounyanyua), ulikuwa ni wa ghulamu wawili mayatima katika mji ule, na kulikuweko chini yake hazina yao, na baba yao alikuwa mwema. Basi Rabb wako Alitaka wafikie umri wa kupevuka na watoe hazina yao ikiwa ni Rehma kutoka kwa Rabb wako. Na sikufanya hayo kwa amri yangu. Hiyo ni tafsiri ya hakika ya yale ambayo hukuweza kuyavutia subira.

 

 

 

وَيَسْأَلُونَكَ عَن ذِي الْقَرْنَيْنِ ۖ قُلْ سَأَتْلُو عَلَيْكُم مِّنْهُ ذِكْرًا ﴿٨٣﴾

83. Na wanakuuliza kuhusu Dhul-Qarnayn. Sema (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم): Nitakusomeeni kuhusu baadhi ya khabari zake.[12]

 

 

 

إِنَّا مَكَّنَّا لَهُ فِي الْأَرْضِ وَآتَيْنَاهُ مِن كُلِّ شَيْءٍ سَبَبًا ﴿٨٤﴾

84. Hakika Sisi Tulimmakinisha katika ardhi, na Tukampa njia ya kila kitu.

 

 

 

فَأَتْبَعَ سَبَبًا ﴿٨٥﴾

85. Basi akaifuata njia.

 

 

 

حَتَّىٰ إِذَا بَلَغَ مَغْرِبَ الشَّمْسِ وَجَدَهَا تَغْرُبُ فِي عَيْنٍ حَمِئَةٍ وَوَجَدَ عِندَهَا قَوْمًا ۗ قُلْنَا يَا ذَا الْقَرْنَيْنِ إِمَّا أَن تُعَذِّبَ وَإِمَّا أَن تَتَّخِذَ فِيهِمْ حُسْنًا ﴿٨٦﴾

86. Hata alipofika machweo ya jua, akalikuta (kama) linatua katika chemchemu ya matope meusi (au ya moto), na akakuta huko watu.  Tukasema: Ee Dhul-Qarnayn! Ima uwaadhibu au wafanyie ihsaan.

 

 

 

قَالَ أَمَّا مَن ظَلَمَ فَسَوْفَ نُعَذِّبُهُ ثُمَّ يُرَدُّ إِلَىٰ رَبِّهِ فَيُعَذِّبُهُ عَذَابًا نُّكْرًا ﴿٨٧﴾

87. (Dhul-Qarnayn) akasema: Ama aliyedhulumu, basi Tutamuadhibu, kisha atarudishwa kwa Rabb wake, Amuadhibu adhabu kali kabisa ya kukirihisha, isiyovumilika.

 

 

 

وَأَمَّا مَنْ آمَنَ وَعَمِلَ صَالِحًا فَلَهُ جَزَاءً الْحُسْنَىٰ ۖ وَسَنَقُولُ لَهُ مِنْ أَمْرِنَا يُسْرًا ﴿٨٨﴾

88. Na ama aliyeamini na akatenda mema, basi atapata jazaa nzuri kabisa. Na Tutamwambia yaliyo mepesi katika Amri Yetu.

 

 

 

ثُمَّ أَتْبَعَ سَبَبًا ﴿٨٩﴾

89. Kisha akaifuata njia.

 

 

 

حَتَّىٰ إِذَا بَلَغَ مَطْلِعَ الشَّمْسِ وَجَدَهَا تَطْلُعُ عَلَىٰ قَوْمٍ لَّمْ نَجْعَل لَّهُم مِّن دُونِهَا سِتْرًا ﴿٩٠﴾

90. Hata alipofikia panapochomoza jua, alilikuta linachomoza kwa watu Hatukuwafanyia kizuizi cha kuwakinga nalo.

 

 

 

كَذَٰلِكَ وَقَدْ أَحَطْنَا بِمَا لَدَيْهِ خُبْرًا ﴿٩١﴾

91. Ndio hivyo. Na Tulikwishazijua vyema khabari za vyote alivyonavyo.

 

 

 

ثُمَّ أَتْبَعَ سَبَبًا ﴿٩٢﴾

92. Kisha akaifuata njia.

 

 

 

حَتَّىٰ إِذَا بَلَغَ بَيْنَ السَّدَّيْنِ وَجَدَ مِن دُونِهِمَا قَوْمًا لَّا يَكَادُونَ يَفْقَهُونَ قَوْلًا ﴿٩٣﴾

93. Hata alipofikia baina ya milima miwili, akakuta nyuma yake watu ambao takriban hawafahamu neno lolote.

 

 

 

 

قَالُوا يَا ذَا الْقَرْنَيْنِ إِنَّ يَأْجُوجَ وَمَأْجُوجَ مُفْسِدُونَ فِي الْأَرْضِ فَهَلْ نَجْعَلُ لَكَ خَرْجًا عَلَىٰ أَن تَجْعَلَ بَيْنَنَا وَبَيْنَهُمْ سَدًّا ﴿٩٤﴾

94. Wakasema: Ee Dhul-Qarnayn! Hakika Yaajuwj na Maajuwj[13] ni mafisadi katika ardhi. Basi je, tukufanyie ujira ili uweke baina yetu na baina yao kizuizi?

 

 

 

قَالَ مَا مَكَّنِّي فِيهِ رَبِّي خَيْرٌ فَأَعِينُونِي بِقُوَّةٍ أَجْعَلْ بَيْنَكُمْ وَبَيْنَهُمْ رَدْمًا ﴿٩٥﴾

95. Akasema: Alivyonimakinisha Rabb wangu ni bora zaidi (kuliko ujira). Basi nisaidieni kwa nguvu (za watu), niweke baina yenu na baina yao kizuizi imara.

 

 

 

آتُونِي زُبَرَ الْحَدِيدِ ۖ حَتَّىٰ إِذَا سَاوَىٰ بَيْنَ الصَّدَفَيْنِ قَالَ انفُخُوا ۖ حَتَّىٰ إِذَا جَعَلَهُ نَارًا قَالَ آتُونِي أُفْرِغْ عَلَيْهِ قِطْرًا ﴿٩٦﴾

96. Nileteeni vipande vya chuma. Mpaka aliposawazisha kujaza baina ya kingo mbili za majabali akasema: Chocheeni moto. Hata alipovifanya moto, akasema: Nipeni nimwagie juu yake shaba iliyoyayushwa.

 

 

 

فَمَا اسْطَاعُوا أَن يَظْهَرُوهُ وَمَا اسْتَطَاعُوا لَهُ نَقْبًا ﴿٩٧﴾

97. Basi (Ya-juwj na Ma-juwj) hawakuweza kukikwea na wala hawakuweza kukitoboa.

 

 

 

 

قَالَ هَـٰذَا رَحْمَةٌ مِّن رَّبِّي ۖ فَإِذَا جَاءَ وَعْدُ رَبِّي جَعَلَهُ دَكَّاءَ ۖ وَكَانَ وَعْدُ رَبِّي حَقًّا ﴿٩٨﴾

98. (Dhul-Qarnayn) akasema: Hii ni Rehma kutoka kwa Rabb wangu. Basi itakapokuja Ahadi ya Rabb wangu[14], Atakijaalia kibomoke, kipondeke kiwe tambarare. Na Ahadi ya Rabb wangu daima ni ya kweli.

 

 

 

وَتَرَكْنَا بَعْضَهُمْ يَوْمَئِذٍ يَمُوجُ فِي بَعْضٍ ۖ وَنُفِخَ فِي الصُّورِ فَجَمَعْنَاهُمْ جَمْعًا ﴿٩٩﴾

99. Na siku hiyo Tutawaacha wasongamane kama mawimbi wenyewe kwa wenyewe.[15] Na litapulizwa baragumu, Tutawakusanya wote katika mkusanyo mmoja.

 

 

 

وَعَرَضْنَا جَهَنَّمَ يَوْمَئِذٍ لِّلْكَافِرِينَ عَرْضًا ﴿١٠٠﴾

100. Na siku hiyo Tutaiweka Jahannam kwa makafiri (waione) waziwazi.

 

 

 

الَّذِينَ كَانَتْ أَعْيُنُهُمْ فِي غِطَاءٍ عَن ذِكْرِي وَكَانُوا لَا يَسْتَطِيعُونَ سَمْعًا ﴿١٠١﴾

101. Ambao macho yao yalikuwa katika pazia wasiweze kunidhukuru na walikuwa hawawezi kusikia.

 

 

 

أَفَحَسِبَ الَّذِينَ كَفَرُوا أَن يَتَّخِذُوا عِبَادِي مِن دُونِي أَوْلِيَاءَ ۚ إِنَّا أَعْتَدْنَا جَهَنَّمَ لِلْكَافِرِينَ نُزُلًا ﴿١٠٢﴾

102. Je, wanadhania wale waliokufuru kwamba wanaweza kuwafanya Waja Wangu kuwa rafiki walinzi badala Yangu? Hakika Sisi Tumeandaa Jahannam kwa ajili ya makafiri kuwa mahala pa kuteremkia.

 

 

 

قُلْ هَلْ نُنَبِّئُكُم بِالْأَخْسَرِينَ أَعْمَالًا ﴿١٠٣﴾

103. Sema (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم): Je, Tukujulisheni wenye kukhasirika mno kwa amali?[16]

 

 

 

الَّذِينَ ضَلَّ سَعْيُهُمْ فِي الْحَيَاةِ الدُّنْيَا وَهُمْ يَحْسَبُونَ أَنَّهُمْ يُحْسِنُونَ صُنْعًا ﴿١٠٤﴾

104. Ni wale ambao juhudi zao zimepotea bure katika uhai wa dunia, na huku wao wakidhani kwamba wanafanya matendo mazuri (ya kuwanufaisha).

 

 

 

أُولَـٰئِكَ الَّذِينَ كَفَرُوا بِآيَاتِ رَبِّهِمْ وَلِقَائِهِ فَحَبِطَتْ أَعْمَالُهُمْ فَلَا نُقِيمُ لَهُمْ يَوْمَ الْقِيَامَةِ وَزْنًا ﴿١٠٥﴾

105. Hao ni wale waliozikanusha Aayaat (na Ishara, Hoja, Dalili) za Rabb wao na kukutana Naye, amali zao zikaporomoka. Hivyo Hatutowathamini wala Kuwajali hata kidogo Siku ya Qiyaamah.  

 

 

ذَٰلِكَ جَزَاؤُهُمْ جَهَنَّمُ بِمَا كَفَرُوا وَاتَّخَذُوا آيَاتِي وَرُسُلِي هُزُوًا ﴿١٠٦﴾

106. Kwa hayo, malipo yao ni Jahannam kwa sababu ya ukafiri wao, na wamezifanyia mzaha Aayaat (na Ishara, Hoja, Dalili) Zangu na Rusuli Wangu.

 

 

 

إِنَّ الَّذِينَ آمَنُوا وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ كَانَتْ لَهُمْ جَنَّاتُ الْفِرْدَوْسِ نُزُلًا ﴿١٠٧﴾

107. Hakika wale walioamini na wakatenda mema, watapata Jannaat za Al-Firdaws kuwa ni mahali pao pa makaribisho.

 

 

 

خَالِدِينَ فِيهَا لَا يَبْغُونَ عَنْهَا حِوَلًا ﴿١٠٨﴾

108. Wadumu humo, hawatotaka kuihama.

 

 

 

قُل لَّوْ كَانَ الْبَحْرُ مِدَادًا لِّكَلِمَاتِ رَبِّي لَنَفِدَ الْبَحْرُ قَبْلَ أَن تَنفَدَ كَلِمَاتُ رَبِّي وَلَوْ جِئْنَا بِمِثْلِهِ مَدَدًا ﴿١٠٩﴾

109. Sema: Kama bahari ingelikuwa ni wino wa (kuandika) Maneno ya Rabb wangu, basi ingelimalizika bahari kabla ya kumalizika Maneno ya Rabb wangu, japokuwa Tungelileta mfano wake kujaza tena.[17]

 

 

 

قُلْ إِنَّمَا أَنَا بَشَرٌ مِّثْلُكُمْ يُوحَىٰ إِلَيَّ أَنَّمَا إِلَـٰهُكُمْ إِلَـٰهٌ وَاحِدٌ ۖ فَمَن كَانَ يَرْجُو لِقَاءَ رَبِّهِ فَلْيَعْمَلْ عَمَلًا صَالِحًا وَلَا يُشْرِكْ بِعِبَادَةِ رَبِّهِ أَحَدًا ﴿١١٠﴾

110. Sema (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم): Hakika mimi ni mtu kama nyinyi, nafunuliwa Wahy kwamba: Hakika Mwabudiwa wa haki wenu ni Ilaah Mmoja Pekee. Hivyo anayetaraji kukutana na Rabb wake, basi na atende amali njema na wala asimshirikishe yeyote katika ibaada za Rabb wake.[18]

 

 

[1] Kumhimidi Allaah Kwa Kitabu Kisichokuwa Na Upogo:

 

AlhamduliLLaah, ni kumtukuza na kumsifu Allaah kwa Sifa Zake ambazo ni sifa zote za ukamilifu, na kwa Neema Zake zilizo dhahiri na siri, za kidini na kidunia. Na neema kubwa zaidi kuliko zote ni kuteremsha Kwake Kitabu hiki kitukufu kwa Mja Wake na Rasuli Wake Muhammad (صلى الله عليه وآله وسلم). Na kwa ajili hiyo, Anajihimidi Mwenyewe. Himdi hii imebeba ndani yake maelekezo kwa waja kwamba nao pia wamhimidi Yeye kwa kuwatumia Rasuli na kuwateremshia Kitabu. 

Kisha Akakielezea Kitabu hiki kuwa kina sifa mbili kusanyifu zinazokifanya kuwa ni Kitabu kikamilifu katika kila upande. Sifa ya kwanza ni kukanusha kuwepo upogo ndani yake, na ya pili ni kuthibitisha kuwa ni Kitabu kilichonyooka barabara. Kukanusha kuwa hakina upogo ndani yake, inamaanisha kuwa hakuna khabari za uwongo ndani yake, na wala hakuna dhulma wala chochote cha upuuzi au kisichokuwa na makusudio katika amri Zake na makatazo Yake.

 

Ama kuthibitisha kuwa ni Kitabu kilichonyooka barabara, hii inamaanisha kwamba, hakijulishi jambo wala amri isipokuwa ni njema, wala hakitaji lolote isipokuwa ni masuala matukufu zaidi ambayo ni masuala yanayojaza moyo ilimu, imaan na hikma, kama kujuzisha Majina ya Allaah na Sifa Zake na Matendo Yake, na visa vya ghaibu vitakavyotokea na vilivyokwishatokea. Na kwamba amri zake na makatazo yake yanatakasa na yanazitwaharisha nafsi kuzifanya zikue na ziwe njema kwa sababu zinategemea haki kamilifu, ikhlaasw, na utumwa wa kweli kwa Rabb Pekee wa ulimwengu Ambaye Hana mshirika. Na kutokana na sifa hizi zilizotajwa kuhusiana na Kitabu hiki, imekuwa ni jambo linalostahiki kwa Allaah Kujihimidi Yeye Mwenyewe kwa kukiteremsha, na kuwataka Waja Wake wamsifu kwa Sifa njema kutokana na yote yaliyomo ndani yake.

 

[2] Al-Kahf: Jina La Suwrah. Maana ya Al-Kahf na Ar-Raqiym:

 

Al-Kahf ni pango katika jabali ambalo vijana hao walikimbilia kujificha humo. Na kuhusu neno la Ar-Raqiym, kuna kauli mbalimbali za Salaf kama ifuatavyo: (i) Ibn 'Abbaas na wengineo: Bonde. (ii) Pango katika bonde na Ar-Raqiym ni jina la bonde. (iii) Ar-Raqiym inakusudiwa majengo yao. (iv) Ni bonde ambalo pango lao lilikuwepo. (v) Ni mji. (vi) Jabali ambalo pango hilo lilikuwepo. (vii) Ubamba wa jiwe wenye maandiko walioandikia kisa cha Asw-haabul-Kahf kisha wakaliweka katika maingilio ya mlango wa pango. [Tafsiyr Ibn Kathiyr]

 

[3] Amrisho La Kusema In Shaa Allaah Anapotaka Mtu Kufanya Jambo Na Hikma Zake:

 

Katazo hilo ni kama mengineyo (katika Qur-aan) ambayo yanamwelekea Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) kutokana na sababu fulani, lakini pia linawahusu wanaadam. Na hikma yake ni kutokuingilia mambo ya ghaibu, kwa sababu hakuna ajuaye kama jambo litafanyika nyakati za mbele, au kesho, au halifanyiki isipokuwa Allaah. Pia kusema In Shaa Allaah inalifanya jambo liwe jepesi na lenye baraka kwa sababu mja anakusudia kutaka msaada wa Allaah. [Tafsiyr As-Sa’diy] 

 

Ibn ‘Abbaas (رضي الله عنهما  amesema makafiri wa Kiquraysh walimtuma Yahudi amwendee Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) ili amuulize maswali matatu: (i) Kuhusu vijana wa wakati wa kale na kisa chao, kwani kisa chao ni cha kustaajabisha, nao ni Asw-haabul-Kahf (vijana wa pangoni) ambao wameelezewa katika Suwrah hii (ii) Nini kisa cha mtu aliyesafiri sana hadi akafika Mashariki na Magharibi ya dunia, yaani Dhul-Qarnayn katika Suwrah hii Al-Kahf (18:83) (iii) Kuhusu roho (nafsi) ni kitu gani hicho? Rejea Al-Israa (17:85). Kisha Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) aliwajibu kuwa atawajulisha kesho, bila ya kusema In Shaa Allaah. Akakaa siku kumi na tano bila ya Jibriyl (عليه السّلام)  kumjia kama ilivyo kawaida yake kumpa Wahyi kutoka kwa Allaah (سبحانه وتعالى). Watu wa Makkah wakaanza kumtilia shaka na kupita wakisema: "Muhammad katuahidi kutujibu mas-ala tuliyomuuliza siku ya pili na hadi leo siku ya kumi na tano zimepita hakutujibu lolote katika hayo."

Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) akafikwa na huzuni kubwa kwa kuchelewa kupata Wahyi na akadhikika kwa maneno ya watu wa Makkah waliyokuwa wakisema. Kisha Jibriyl (عليه السّلام)  akaja kumteremshia Suwrah ya Al-Kahf kwa kuanzia Aayah namba (6). Kwa hilo, Allaah (سبحانه وتعالى) Alimtahini Rasuli Wake (صلى الله عليه وآله وسلم) kama alivyotahiniwa Nabiy Sulaymaan (عليه السّلام)  kwa mujibu wa maelezo yaliyopo katika Hadiyth iliyosimuliwa na Abu Hurayrah (رضي الله عنه)

 

قَالَ اللَّيْثُ حَدَّثَنِي جَعْفَرُ بْنُ رَبِيعَةَ، عَنْ عَبْدِ الرَّحْمَنِ بْنِ هُرْمُزَ، قَالَ سَمِعْتُ أَبَا هُرَيْرَةَ ـ رضى الله عنه ـ عَنْ رَسُولِ اللَّهِ صلى الله عليه وسلم قَالَ ‏ "‏ قَالَ سُلَيْمَانُ بْنُ دَاوُدَ ـ عَلَيْهِمَا السَّلاَمُ ـ لأَطُوفَنَّ اللَّيْلَةَ عَلَى مِائَةِ امْرَأَةٍ ـ أَوْ تِسْعٍ وَتِسْعِينَ ـ كُلُّهُنَّ يَأْتِي بِفَارِسٍ يُجَاهِدُ فِي سَبِيلِ اللَّهِ، فَقَالَ لَهُ صَاحِبُهُ إِنْ شَاءَ اللَّهُ‏.‏ فَلَمْ يَقُلْ إِنْ شَاءَ اللَّهُ‏.‏ فَلَمْ يَحْمِلْ مِنْهُنَّ إِلاَّ امْرَأَةٌ وَاحِدَةٌ، جَاءَتْ بِشِقِّ رَجُلٍ، وَالَّذِي نَفْسُ مُحَمَّدٍ بِيَدِهِ، لَوْ قَالَ إِنْ شَاءَ اللَّهُ، لَجَاهَدُوا فِي سَبِيلِ اللَّهِ فُرْسَانًا أَجْمَعُونَ ‏"‏‏.‏

Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Wakati mmoja Sulaymaan bin Daawuwd (عليهما السّلام)  alisema: (Wa-Allaahi) Usiku wa leo nitawapitia wake zangu wote mia au tisini na tisa, (kwa kujimai nao), na kila mmoja wao atazaa shujaa mpandaji farasi atakayepigana katika Njia ya Allaah.” Sahibu yake akamwambia: “Sema: In Shaa Allaah (Allaah Akipenda).” Lakini yeye hakusema In Shaa Allaah.  Kwa hiyo, aliyebeba mimba na kuzaa alikuwa mwanamke mmoja peke yake, naye alizaa nusu mtu (kilema). Naapa kwa Yule Ambaye nafsi ya Muhammad iko Mikononi Mwake, lau angesema In Shaa Allaah, basi wangekuwa ni wenye kuipigania (Dini) katika Njia ya Allaah wote wakiwa juu ya farasi.” [Al-Bukhaariy]

 

Basi Allaah (سبحانه وتعالى) Ametaka kumfunza Rasuli Wake (صلى الله عليه وآله وسلم) kuhusu kurejea Kwake kwa kila jambo analotaka kufanya, kwani Yeye Allaah (سبحانه وتعالى) Ndiye Mwenye Qudra (Uwezo) wa kila kitu, Ndiye Mwenye Kudabiri mambo yote, na Ndiye Mjuzi wa mambo ya ghaibu. Hakuna jambo linaloweza kutendeka ila kwa Matakwa Yake.

 

[4] Anaposahau Mtu Kusema In Shaa Allaah:

 

Ibn 'Abbaas aliifasiri Aayah hii kuwa mtu anaweza kusema In Shaa Allaah hata baada ya mwaka ikiwa amesahau kusema baada ya kuweka kiapo au kusema atafanya jambo fulani. Hivi atakuwa amefanya Sunnah ya kusema In Shaa Allaah hata kama baada ya kuvunja kiapo. Hii vile vile ni rai ya Ibn Jariyr. Lakini kasema, hii haina maana kwamba inafidia kuvunja kiapo cha mtu, bali mtu anapovunja kiapo lazima afanye kafara yake (malipo ya kiapo). [Tafsiyr Ibn Kathiyr]

 

[5] Al-Baaqiyaatu Asw-Swaalihaatu: Mema Yanayobakia:

 

Hadiyth ifuatayo imebainisha maana ya al-baaqiyaatu asw-swaalihaatu:

 

Amesimulia Abu Sa’iyd Al-Khudriy  (رضي الله عنه)  kwamba Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم)  amesema: “Amali njema yenye kubakia ni:

لَا إِلَهَ إِلَّا اَللَّهُ، وَسُبْحَانَ اَللَّهِ، وَاَللَّهُ أَكْبَرُ، وَالْحَمْدُ لِلَّهِ، وَلَا حَوْلَ وَلَا قُوَّةَ إِلَّا بِاَللَّهِ

Hapana mwabudiwa wa haki isipokuwa Allaah, na Utakasifu ni wa Allaah, na Allaah ni Mkubwa, na Himdi Anastahiki Allaah, na hapana uwezo wala nguvu ila za Allaah.

[Imetolewa na An-Nasaaiy na akaisahihisha Ibn Hibbaan na Al-Haakim]

 

Kauli za ‘Ulamaa kuhusu maana ya al-baaqiyaatu asw-swaalihaatu:

 

‘Ulamaa wametaja kama hivyo na mfano wa kama hivyo. Ama Ibn ‘Abbaas, Sa’iyd bin Jubayr, na Salaf wengineo wamesema kuwa al-baaqiyaatu asw-swaalihaatu ni: Swalaah tano.

Na Amiri wa Waumini ‘Uthmaan bin ‘Affaan (رضي الله عنه)  aliulizwa kuhusu al-baaqiyaatu asw-swaalihaatu akasema hayo ni:

 

لا إِلَهَ إِلا اللَّهُ، وسُبْحَانَ اللَّهِ، وَالْحَمْدُ لِلَّهِ، واللَّهُ أَكْبَرُ، وَلاَ حَوْلَ ولاَ قُوَّةَ إِلاَّ بِاللَّهِ

[Tafsiyr Ibn Kathiyr(رحمه الله) ]

 

Na Imaam As-Sa’diy  (رحمه الله) amesema kuhusu:

الْمَالُ وَالْبَنُونَ زِينَةُ الْحَيَاةِ الدُّنْيَا ۖ

“Mali na watoto ni pambo la uhai wa dunia.”

 

Maana yake: Hakuna katika hayo kitu kitakachobakia nyuma, na kwamba kinachobakia kwa binaadam na kitakachomnufaisha na kumfurahisha ni al-baaqiyaatu asw-swaalihaatu (mema yatakayobakia). Na haya  yanajumuisha matendo yote ya utiifu ya faradhi na ya Sunnah katika haki za Allaah, na haki za Waja Wake; kama vile Swalaah, Zakaah, swadaqa, Hajj, ‘Umrah, Tasbiyh (Kumtakasa Allaah), Tahmiyd (Kumhimidi Allaah), Tahliyl (Kumpwekesha Allaah), Takbiyr (Kumtukuza Allaah), mja kusoma  (Qur-aan), kutafuta ilimu yenye manufaa, kuamrisha mema na kukataza munkari, “swilatur-rahim” (kuunga undugu wa uhusiano wa damu), kuwafanyia wema na ihsaan wazazi, kutimiza haki za mke na mume,  haki za watumwa, na haki za wanyama, na kila aina za ihsaan kwa viumbe. Yote haya ni al-baaqiyaatu asw-swaalihaatu (mema yatakayobakia). Basi haya yote ni

  خَيْرٌ عِندَ رَبِّكَ ثَوَابًا وَخَيْرٌ أَمَلًا

“Bora mbele ya Rabb wako kwa thawabu na matumaini mema zaidi.”  

 

Hivyo basi thawabu zake zinabakia na zinaongezeka milele, na malipo yake, nyongeza zake na manufaa yake yana dhamana ya kupatikana wakati wa kulipwa na Allaah. Basi haya ndiyo ambayo yanapaswa washindane nayo wenye kushindana (katika mema), na wayakimbilie watendao (mema), na wajitahidi kuyapata wenye kujitahidi. Na tazama utaamuli, wakati Allaah Alivyopiga mfano wa dunia, hali yake na kutoweka kwake Ametaja kuwa vilivyomo humo ni aina mbili; aina ya mapambo yake ambayo binaadam ananufaika nayo kidogo tu, kisha yanatoweka bila ya faida yake kumrudia mtu mwenyewe. Bali huenda hata hayo yakamletea madhara, nayo ni mali na watoto. Na aina nyengine ambayo inabakia na itamfaa mtu mwenyewe daima dawamu, nayo ni al-baaqiyaatu asw- swaalihaatu. [Tafsiyr As-Sa’diy]

 

[6]  Viumbe Watafufuliwa Wakiwa Kama Walivyozaliwa:

 

Amesimulia ‘Aaishah (رضي الله عنها): Nilimsikia Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) akisema: “Watu watafufuliwa Siku ya Qiyaamah ilhali hawana viatu, wako uchi, ni mazunga (hawakutahiriwa).” Nikamuuliza: Ee Rasuli wa Allaah! Wanaume na wanawake wote watatazamana? Akasema: “Ee ‘Aaishah! Hali itakuwa ngumu mno  hata hawatoweza kushughulika na jambo hilo!”

 

Katika riwaayah nyingine imesema: “Hali itakuwa ngumu mno kiasi kwamba hawatoweza kutazamana.” [Al-Bukhaariy na Muslim]

 

Rejea Al-An’aam (6:94), na Al-Anbiyaa (21:104)

 

[7] Matendo Yote Ya Binaadam Yanarekodiwa Hata Liwe Tendo Dogo Vipi:

 

Rejea Al-Israa (17:13-14) (17:71), Az-Zalzalah (99:6-8), Qaaf (50:17-18), Al-Haaqqah (69:19-29), na Al-Infitwaar (82:10-12).

 

[8] Desturi Ya Watu Wa Awali:

 

Rejea Aal-‘Imraan (3:137), Faatwir (35:43-44), Yuwsuf (12:109), Al-An’aam (6:11), An-Naml (37:69).

 

[9] Nyoyo Za Makafiri Zimefunikwa Na Masikio Yana Uziwi:

 

Rejea Al-An’aam (6:25), Al-Israa (17:45-46), Fusswilat (41:5).

 

[10] Yuwsha’ Bin Nuwn:

 

Yuwsha’ bin Nuwn ametajwa katika Hadiyth kadhaa zilizo ndefu kwenye Al-Bukhaariy na Muslim kuwa alikuwa ni kijana aliyekuwa akimhudumia Nabiy Muwsaa (عليه السّلام). Naye ndiye aliyeshika Unabii baada ya  kufariki kwa Nabiy Muwsa (عليه السّلام). Na yeye ndiye mmojawapo wa watu wawili walioingia Bayt Al-Maqdis. Rejea Suwrah Al-Maaidah (5:23).  

 

[11] Kisa Cha Nabiy Muwsaa (عليه السّلام) Na Al-Khidhwr:

 

Kuanzia Aayah hii hadi Aayah namba (82), kinazungumziwa kisa cha Nabiy Muwsaa  (عليه السّلام)  na Khidhwr ambaye amekusudiwa katika Aayah namba (65). Na ‘Ulamaa wamekhitilafiana kama Al-Khidhwr ni Nabii au laa. Lakini wengi wao wameona kuwa Al-Khidhwr si Nabii, bali ni mja mwema wa Allaah aliyepewa ilhamu, hikmah na ilimu ya hali ya juu.

 

[12]  Dhul-Qarnayn:

 

Watu wa Kitabu au washirikina (wa Makkah) walimuuliza Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) kuhusu kisa cha Dhul-Qarnayn (18:83-98). Basi Allaah (سبحانه وتعالى) Akamuamuru Rasuli Wake (صلى الله عليه وآله وسلم) awajibu:

  قُلْ سَأَتْلُو عَلَيْكُم مِّنْهُ ذِكْرًا ﴿٨٣﴾

Sema (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم): Nitakusomeeni kuhusu baadhi ya khabari zake.”

 

Khabari muhimu na za ajabu (mpate kukumbuka na kuzingatia) [Tafsiyr As-Sa’diy na At-Tafsiyr Al-Muyassar]

 

‘Ulamaa wamekubaliana kwamba Dhul-Qarnayn hakuwa Nabii, bali alikuwa ni mja mwema na mfalme miongoni mwa wafalme wa ardhi aliyezunguka duniani akilingania kwa uadilifu kutokana na khabari zilizoelezwa katika Suwrah hii Al-Kahf. Mujaahid amesema: “Ni mfalme aliyekuwa Muumini.” Ibn Kathiyr amesema: “Allaah (سبحانه وتعالى) Amemtaja huyu Dhul-Qarnayn na Akamsifu kwa uadilifu, na kwamba alifika Mashariki na Magharibi (ya dunia).” Ibn ‘Uthaymiyn amesema: “Ni mfalme muadilifu aliyekuwa wakati wa Nabiy Ibraahiym  (عليه السّلام)  na inasemekana kuwa aliizunguka Al-Ka’bah pamoja naye, na Allaah Ndiye Mjuzi zaidi. [Fataawaa Nuwr Alad-Darb (60/4)]

 

Kisa chake ndio hiki kama Alivyoelezea Allaah (سبحانه وتعالى) katika Suwrah hii  ya Al-Kahf na ambayo ni Suwrah pekee iliyotajwa khabari zake.

 

[13]  Yaajuwj Na Maajuwj Ni Katika Alama Kumi Kubwa Za Kutokea Qiyaamah:

 

Rejea Al-An’aam (6:158) kwenye Hadiyth na maelezo yanayotaja alama zote kubwa za Qiyaamah.

 

Hadiyth kadhaa nyenginezo zimethibiti kuhusu Yaajuwj na Maajuwj kwamba ni katika alama kubwa za Qiyaamah; mojawapo ni:

Amesimulia Zaynab bint Jahsh (رضي الله عنها): Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) aliamka kutoka usingizini uso wake ukiwa umeiva kwa wekundu, huku akisema:

لاَ إِلَهَ إِلاَّ اللَّهُ

“Laa ilaaha illa-Allaah! (Hapana mwabudiwa wa haki isipokuwa Allaah)

 

Ole wao Waarabu kwa shari iliyokaribia. Limefunguliwa leo tundu katika ukuta unaowazuilia Yaajuwj na Maajuwj mfano huu.” Sufyaan akaonyesha kwa kufanya namba tisini au mia kwa vidole vyake. Pakasemwa: Je, tutaangamizwa na miongoni mwetu kuna watu wema?  Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) akasema: “Ndio, pindi maovu yatakapokithiri.” [Al-Bukhaariy na Muslim]

 

Rejea pia Al-Anbiyaa (21:96-97).

 

[14]Ahadi Ya Allaah: Ni Kuchomoza Kwa  Yaajuwj na Maajuwj. 

 

[15] Watakaosongamana:

 

Huenda imekusudiwa Yaajuwj na Maajuwj watakapojitokeza kwa watu, kwa sababu ya idadi yao kubwa mno, na kufika kwao pande zote za ardhi. Hivo basi, watasongamana kama mawimbi wenyewe kwa wenyewe. 

 

Au huenda ni viumbe Siku ya kufufuliwa kwa vile watakusanywa kwa idadi kubwa mno hadi kwamba watasongamana kama mawimbi wenyewe kwa wenyewe kwa sababu ya hali ya kiwewe itakavyokuwa pamoja na tetemeko kubwa la adhi. [Tafsiyr As-Sa’diy]

 

[16] Amali Batili Hazina Thamani:

 

Aayah hii na inayofuatia (105), inathibitisha kuwa amali batili hazina thamani mbele ya Allaah na wala hazipokelewi. Ni amali zozote zile ambazo hazina dalili katika Sharia ya Dini hii tukufu. Ameonya haya Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) katika Hadiyth:

 

عن أُمِّ المُؤمِنينَ أُمِّ عَبْدِ الله عائِشَةَ رَضي اللهُ عنها قالَتْ: قالَ رسُولُ الله صلى الله عليه وسلم: (( مَنْ أَحْدَثَ في أَمْرِنا هذا ما لَيْسَ منهُ فَهُوَ رَد)) رَوَاهُ الْبُخَارِيُّ  وَمُسْلِمٌ 

 وَفِي رِوَايَةٍ لِمُسْلِمٍ :  ((مَن عَمِلَ عَمَلاً لَيْسَ عَلَيْهِ أَمْرُنَا فَهُوَ رَدٌّ ))

Amesimulia Mama wa Waumini Ummu Abdillaah ‘Aaishah (رضي الله عنها):  Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Atakayezusha katika jambo letu hili (la Dini) lolote ambalo halimo humo litarudishwa.”  [Al-Bukhaariy na Muslim]

 

Na katika riwaayah ya Muslim: ”Atakayetenda kitendo kisichokuwa chetu (katika Dini) basi kitarudishwa.”

 

Rejea Az-Zumar (39:65).

 

Na Imaam Ibn Kathiyr amesema inamaanisha: Wametenda amali batili ambazo haziendani na  Sharia inayoridhiwa na Allaah. Na wanadhani kuwa wako juu ya msingi fulani kwa matendo yao na kupendwa. [Tafsiyr Ibn Kathiyr]

 

[17] Bahari Ingekuwa Ni Wino Wa Kuandika Maneno Ya Allaah: Rejea Luqmaan (31:27).

 

[18] Aina Za Shirki: Rejea Az-Zumar (39:65).

 

Share