029 - Al-'Ankabuwt
الْعَنْكَبُوت
029-Al-‘Ankabuwt
029-Al-‘Ankabuwt: Utangulizi Wa Suwrah
بِسْمِ اللَّـهِ الرَّحْمَـٰنِ الرَّحِيمِ
الم ﴿١﴾
1. Alif Laam Miym.[1]
أَحَسِبَ النَّاسُ أَن يُتْرَكُوا أَن يَقُولُوا آمَنَّا وَهُمْ لَا يُفْتَنُونَ ﴿٢﴾
2. Je, wanadhani watu kwamba wataachwa kwa kuwa wanasema: Tumeamini, nao ndio wasijaribiwe?
وَلَقَدْ فَتَنَّا الَّذِينَ مِن قَبْلِهِمْ ۖ فَلَيَعْلَمَنَّ اللَّـهُ الَّذِينَ صَدَقُوا وَلَيَعْلَمَنَّ الْكَاذِبِينَ ﴿٣﴾
3. Kwa yakini Tuliwajaribu wale wa kabla yao. Na kwa yakini Allaah Atawatambulisha wale walio wakweli, na kwa hakika Atawatambulisha walio waongo.
أَمْ حَسِبَ الَّذِينَ يَعْمَلُونَ السَّيِّئَاتِ أَن يَسْبِقُونَا ۚ سَاءَ مَا يَحْكُمُونَ ﴿٤﴾
4. Je, wanadhania wale wanaotenda maovu kwamba watatushinda? Uovu ulioje yale wanayohukumu!
مَن كَانَ يَرْجُو لِقَاءَ اللَّـهِ فَإِنَّ أَجَلَ اللَّـهِ لَآتٍ ۚ وَهُوَ السَّمِيعُ الْعَلِيمُ ﴿٥﴾
5. Anayetaraji kukutana na Allaah basi hakika muda uliopangwa na Allaah utafika tu. Naye Ni Mwenye Kusikia yote, Mjuzi wa yote.
وَمَن جَاهَدَ فَإِنَّمَا يُجَاهِدُ لِنَفْسِهِ ۚ إِنَّ اللَّـهَ لَغَنِيٌّ عَنِ الْعَالَمِينَ ﴿٦﴾
6. Na anayefanya juhudi, basi hakika hapana isipokuwa anafanya juhudi kwa ajili ya nafsi yake. Hakika Allaah bila shaka Si Mhitaji wa walimwengu.
وَالَّذِينَ آمَنُوا وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ لَنُكَفِّرَنَّ عَنْهُمْ سَيِّئَاتِهِمْ وَلَنَجْزِيَنَّهُمْ أَحْسَنَ الَّذِي كَانُوا يَعْمَلُونَ ﴿٧﴾
7. Na wale walioamini na wakatenda mema bila shaka Tutawafutia maovu yao, na bila shaka Tutawalipa mazuri zaidi kuliko yale waliyokuwa wakitenda.
وَوَصَّيْنَا الْإِنسَانَ بِوَالِدَيْهِ حُسْنًا ۖ وَإِن جَاهَدَاكَ لِتُشْرِكَ بِي مَا لَيْسَ لَكَ بِهِ عِلْمٌ فَلَا تُطِعْهُمَا ۚ إِلَيَّ مَرْجِعُكُمْ فَأُنَبِّئُكُم بِمَا كُنتُمْ تَعْمَلُونَ ﴿٨﴾
8. Na Tumemuusia binaadam kuwafanyia wema wazazi wake wawili. Lakini wakikushikilia kuwa unishirikishe na ambayo huna ilimu nayo, basi usiwatii. Kwangu ni marejeo yenu, Nitakujulisheni yale mliyokuwa mkiyatenda.[2]
وَالَّذِينَ آمَنُوا وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ لَنُدْخِلَنَّهُمْ فِي الصَّالِحِينَ ﴿٩﴾
9. Na wale walioamini na wakatenda mazuri bila shaka Tutawaingiza pamoja na Swalihina.
وَمِنَ النَّاسِ مَن يَقُولُ آمَنَّا بِاللَّـهِ فَإِذَا أُوذِيَ فِي اللَّـهِ جَعَلَ فِتْنَةَ النَّاسِ كَعَذَابِ اللَّـهِ وَلَئِن جَاءَ نَصْرٌ مِّن رَّبِّكَ لَيَقُولُنَّ إِنَّا كُنَّا مَعَكُمْ ۚ أَوَلَيْسَ اللَّـهُ بِأَعْلَمَ بِمَا فِي صُدُورِ الْعَالَمِينَ ﴿١٠﴾
10. Na miongoni mwa watu wako wasemao: Tumemwamini Allaah. Lakini wanapoudhiwa kwa ajili ya Allaah, hufanya fitnah za watu kama kwamba ni Adhabu ya Allaah. Na inapowajia nusura kutoka kwa Rabb wako husema: Hakika sisi tulikuwa pamoja nanyi. Je, kwani Allaah Hayajui yale yaliyomo katika vifua vya walimwengu?[3]
وَلَيَعْلَمَنَّ اللَّـهُ الَّذِينَ آمَنُوا وَلَيَعْلَمَنَّ الْمُنَافِقِينَ ﴿١١﴾
11. Na bila shaka Allaah Atatambulisha wale walioamini, na bila shaka Atawatambulisha wanafiki.
وَقَالَ الَّذِينَ كَفَرُوا لِلَّذِينَ آمَنُوا اتَّبِعُوا سَبِيلَنَا وَلْنَحْمِلْ خَطَايَاكُمْ وَمَا هُم بِحَامِلِينَ مِنْ خَطَايَاهُم مِّن شَيْءٍ ۖ إِنَّهُمْ لَكَاذِبُونَ ﴿١٢﴾
12. Na wale waliokufuru wakasema kuwaambia wale walioamini: Fuateni njia yetu, nasi tutabeba madhambi yenu. Na wala wao hawatabeba katika madhambi yao chochote kile. Hakika wao ni waongo.
وَلَيَحْمِلُنَّ أَثْقَالَهُمْ وَأَثْقَالًا مَّعَ أَثْقَالِهِمْ ۖ وَلَيُسْأَلُنَّ يَوْمَ الْقِيَامَةِ عَمَّا كَانُوا يَفْتَرُونَ ﴿١٣﴾
13. Na bila shaka watabeba mizigo yao (ya dhambi) na mizigo mingine pamoja na mizigo yao. Na kwa hakika wataulizwa Siku ya Qiyaamah kuhusu yale waliyokuwa wakiyatunga ya uongo.
وَلَقَدْ أَرْسَلْنَا نُوحًا إِلَىٰ قَوْمِهِ فَلَبِثَ فِيهِمْ أَلْفَ سَنَةٍ إِلَّا خَمْسِينَ عَامًا فَأَخَذَهُمُ الطُّوفَانُ وَهُمْ ظَالِمُونَ ﴿١٤﴾
14. Na kwa yakini Tulimpeleka Nuwh kwa watu wake akakaa nao miaka elfu kasoro miaka hamsini, basi ikawachukua tufani nao ni madhalimu.
فَأَنجَيْنَاهُ وَأَصْحَابَ السَّفِينَةِ وَجَعَلْنَاهَا آيَةً لِّلْعَالَمِينَ ﴿١٥﴾
15. Basi Tukamuokoa na watu wa jahazi, na Tukaifanya kuwa ni Aayah (Ishara, Ukumbusho, Mazingatio) kwa walimwengu.
وَإِبْرَاهِيمَ إِذْ قَالَ لِقَوْمِهِ اعْبُدُوا اللَّـهَ وَاتَّقُوهُ ۖ ذَٰلِكُمْ خَيْرٌ لَّكُمْ إِن كُنتُمْ تَعْلَمُونَ ﴿١٦﴾
16. Na Ibraahiym pale alipowaambia kaumu yake: Mwabuduni Allaah na mcheni. Hivyo ni kheri kwenu mkiwa mnajua.
إِنَّمَا تَعْبُدُونَ مِن دُونِ اللَّـهِ أَوْثَانًا وَتَخْلُقُونَ إِفْكًا ۚ إِنَّ الَّذِينَ تَعْبُدُونَ مِن دُونِ اللَّـهِ لَا يَمْلِكُونَ لَكُمْ رِزْقًا فَابْتَغُوا عِندَ اللَّـهِ الرِّزْقَ وَاعْبُدُوهُ وَاشْكُرُوا لَهُ ۖ إِلَيْهِ تُرْجَعُونَ ﴿١٧﴾
17. Hakika mnaabudu badala ya Allaah masanamu, na mnaunda uzushi. Hakika wale mnaowaabudu badala ya Allaah hawakumilikiini riziki, basi tafuteni riziki kwa Allaah, na mwabuduni Yeye na mshukuruni, Kwake mtarejeshwa.
وَإِن تُكَذِّبُوا فَقَدْ كَذَّبَ أُمَمٌ مِّن قَبْلِكُمْ ۖ وَمَا عَلَى الرَّسُولِ إِلَّا الْبَلَاغُ الْمُبِينُ ﴿١٨﴾
18. Na mkikadhibisha, basi kwa yakini zilikwishakadhibisha nyumati (nyingi) kabla yenu. Na si juu ya Rasuli isipokuwa kubalighisha ujumbe bayana.
أَوَلَمْ يَرَوْا كَيْفَ يُبْدِئُ اللَّـهُ الْخَلْقَ ثُمَّ يُعِيدُهُ ۚ إِنَّ ذَٰلِكَ عَلَى اللَّـهِ يَسِيرٌ ﴿١٩﴾
19. Je, hawaoni jinsi Allaah Anavyoanzisha uumbaji kisha Anaurudisha? Hakika hayo kwa Allaah ni mepesi.
قُلْ سِيرُوا فِي الْأَرْضِ فَانظُرُوا كَيْفَ بَدَأَ الْخَلْقَ ۚ ثُمَّ اللَّـهُ يُنشِئُ النَّشْأَةَ الْآخِرَةَ ۚ إِنَّ اللَّـهَ عَلَىٰ كُلِّ شَيْءٍ قَدِيرٌ ﴿٢٠﴾
20. Sema: Nendeni katika ardhi, na mtazame jinsi (Allaah) Alivyoanzisha uumbaji. Kisha Allaah Ataanzisha umbo la Aakhirah (mtakapofufuliwa). Hakika Allaah juu ya kila kitu Ni Muweza.
يُعَذِّبُ مَن يَشَاءُ وَيَرْحَمُ مَن يَشَاءُ ۖ وَإِلَيْهِ تُقْلَبُونَ ﴿٢١﴾
21. Anamuadhibu Amtakaye, na Anamrehemu Amtakaye, na Kwake mtarudishwa.
وَمَا أَنتُم بِمُعْجِزِينَ فِي الْأَرْضِ وَلَا فِي السَّمَاءِ ۖ وَمَا لَكُم مِّن دُونِ اللَّـهِ مِن وَلِيٍّ وَلَا نَصِيرٍ ﴿٢٢﴾
22. Nanyi si wenye kuweza kukwepa ardhini na wala mbinguni. Na hamna mlinzi wala yeyote mwenye kunusuru badala ya Allaah.
وَالَّذِينَ كَفَرُوا بِآيَاتِ اللَّـهِ وَلِقَائِهِ أُولَـٰئِكَ يَئِسُوا مِن رَّحْمَتِي وَأُولَـٰئِكَ لَهُمْ عَذَابٌ أَلِيمٌ ﴿٢٣﴾
23. Na wale waliozikanusha Aayaat (na Ishara) za Allaah pamoja na kukutana Naye, hao wamekata tamaa na Rehma Yangu, na hao watapata adhabu iumizayo.
فَمَا كَانَ جَوَابَ قَوْمِهِ إِلَّا أَن قَالُوا اقْتُلُوهُ أَوْ حَرِّقُوهُ فَأَنجَاهُ اللَّـهُ مِنَ النَّارِ ۚ إِنَّ فِي ذَٰلِكَ لَآيَاتٍ لِّقَوْمٍ يُؤْمِنُونَ ﴿٢٤﴾
24. Basi halikuwa jawabu la watu wake isipokuwa kusema: Muuweni, au mchomeni moto. Basi Allaah Akamuokoa na moto. Hakika katika hayo mna Aayaat (Ishara, Mazingatio) kwa watu wanaoamini.
وَقَالَ إِنَّمَا اتَّخَذْتُم مِّن دُونِ اللَّـهِ أَوْثَانًا مَّوَدَّةَ بَيْنِكُمْ فِي الْحَيَاةِ الدُّنْيَا ۖ ثُمَّ يَوْمَ الْقِيَامَةِ يَكْفُرُ بَعْضُكُم بِبَعْضٍ وَيَلْعَنُ بَعْضُكُم بَعْضًا وَمَأْوَاكُمُ النَّارُ وَمَا لَكُم مِّن نَّاصِرِينَ ﴿٢٥﴾
25. Na (Ibraahiym) akasema: Hakika mmefanya badala ya Allaah masanamu kuwa ni mapenzi makubwa baina yenu katika uhai wa dunia, kisha Siku ya Qiyaamah mtakanushana nyinyi wenyewe kwa wenyewe, na mtalaaniana wenyewe kwa wenyewe, na makazi yenu ni moto, na hamtokuwa na wenye kunusuru.
فَآمَنَ لَهُ لُوطٌ ۘ وَقَالَ إِنِّي مُهَاجِرٌ إِلَىٰ رَبِّي ۖ إِنَّهُ هُوَ الْعَزِيزُ الْحَكِيمُ ﴿٢٦﴾
26. Luutw akamwamini. Na (Ibraahiym) akasema: Hakika mimi nahajiri kwa Rabb wangu, hakika Yeye Ndiye Mwenye Enzi ya Nguvu Asiyeshindika, Mwenye Hikmah wa yote.
وَوَهَبْنَا لَهُ إِسْحَاقَ وَيَعْقُوبَ وَجَعَلْنَا فِي ذُرِّيَّتِهِ النُّبُوَّةَ وَالْكِتَابَ وَآتَيْنَاهُ أَجْرَهُ فِي الدُّنْيَا ۖ وَإِنَّهُ فِي الْآخِرَةِ لَمِنَ الصَّالِحِينَ ﴿٢٧﴾
27. Tukamtunukia Is-haaq na (mjukuu) Ya’quwb, na Tukajaalia katika dhuria wake Unabii na Kitabu, na Tukampa ujira wake duniani, na hakika yeye katika Aakhirah bila shaka ni miongoni mwa Swalihina.
وَلُوطًا إِذْ قَالَ لِقَوْمِهِ إِنَّكُمْ لَتَأْتُونَ الْفَاحِشَةَ مَا سَبَقَكُم بِهَا مِنْ أَحَدٍ مِّنَ الْعَالَمِينَ ﴿٢٨﴾
28. Na Luutw alipowaambia watu wake: Hakika nyinyi mnaendea uchafu ambao hakuna yeyote aliyekutangulieni kwa hayo katika walimwengu.
أَئِنَّكُمْ لَتَأْتُونَ الرِّجَالَ وَتَقْطَعُونَ السَّبِيلَ وَتَأْتُونَ فِي نَادِيكُمُ الْمُنكَرَ ۖ فَمَا كَانَ جَوَابَ قَوْمِهِ إِلَّا أَن قَالُوا ائْتِنَا بِعَذَابِ اللَّـهِ إِن كُنتَ مِنَ الصَّادِقِينَ ﴿٢٩﴾
29. Je, nyinyi mnawaendea wanaume na mnawaibia (na kuwaua) wasafiri, na mnafanya katika mikutano yenu munkari? Basi halikuwa jawabu la watu wake isipokuwa kusema: Tuletee Adhabu ya Allaah ikiwa wewe ni miongoni mwa wakweli.
قَالَ رَبِّ انصُرْنِي عَلَى الْقَوْمِ الْمُفْسِدِينَ ﴿٣٠﴾
30. (Luutw) akasema: Rabb wangu! Ninusuru dhidi ya watu mafisadi.
وَلَمَّا جَاءَتْ رُسُلُنَا إِبْرَاهِيمَ بِالْبُشْرَىٰ قَالُوا إِنَّا مُهْلِكُو أَهْلِ هَـٰذِهِ الْقَرْيَةِ ۖ إِنَّ أَهْلَهَا كَانُوا ظَالِمِينَ ﴿٣١﴾
31. Na Wajumbe Wetu walipomjia Ibraahiym kwa bishara walisema: Hakika sisi tutawahiliki watu wa mji huu. Hakika watu wake wamekuwa madhalimu.
قَالَ إِنَّ فِيهَا لُوطًا ۚ قَالُوا نَحْنُ أَعْلَمُ بِمَن فِيهَا ۖ لَنُنَجِّيَنَّهُ وَأَهْلَهُ إِلَّا امْرَأَتَهُ كَانَتْ مِنَ الْغَابِرِينَ ﴿٣٢﴾
32. (Ibraahiym) akasema: Hakika humo yumo Luutw. (Malaika) wakasema: Sisi tunajua zaidi waliomo humo. Hapana shaka tutamuokoa pamoja na ahli zake isipokuwa mke wake, amekuwa miongoni mwa watakaobakia nyuma.
وَلَمَّا أَن جَاءَتْ رُسُلُنَا لُوطًا سِيءَ بِهِمْ وَضَاقَ بِهِمْ ذَرْعًا وَقَالُوا لَا تَخَفْ وَلَا تَحْزَنْ ۖ إِنَّا مُنَجُّوكَ وَأَهْلَكَ إِلَّا امْرَأَتَكَ كَانَتْ مِنَ الْغَابِرِينَ ﴿٣٣﴾
33. Na Wajumbe Wetu walipomjia Luutw aliwasikitikia, na akadhikika na kukosa raha kwa ajili yao. (Malaika) wakasema: Usikhofu na wala usihuzunike, hakika sisi tutakuokoa pamoja na ahli zako isipokuwa mke wako, amekuwa miongoni mwa watakaobakia nyuma.
إِنَّا مُنزِلُونَ عَلَىٰ أَهْلِ هَـٰذِهِ الْقَرْيَةِ رِجْزًا مِّنَ السَّمَاءِ بِمَا كَانُوا يَفْسُقُونَ ﴿٣٤﴾
34. Hakika Sisi Tutawateremshia watu wa mji huu adhabu ya kufadhaika kutoka mbinguni kwa sababu ya ule ufasiki waliokuwa wanafanya.
وَلَقَد تَّرَكْنَا مِنْهَا آيَةً بَيِّنَةً لِّقَوْمٍ يَعْقِلُونَ ﴿٣٥﴾
35. Na kwa yakini Tuliacha humo Aayah (Ishara, Athari) bayana kwa watu wanaotia akilini.
وَإِلَىٰ مَدْيَنَ أَخَاهُمْ شُعَيْبًا فَقَالَ يَا قَوْمِ اعْبُدُوا اللَّـهَ وَارْجُوا الْيَوْمَ الْآخِرَ وَلَا تَعْثَوْا فِي الْأَرْضِ مُفْسِدِينَ ﴿٣٦﴾
36. Na kwa Madyan Tulimtuma ndugu yao Shu’ayb, akasema: Enyi kaumu yangu! Mwabuduni Allaah, na tarajieni Siku ya Mwisho, na wala msifanye uovu katika ardhi mkifisidi.
فَكَذَّبُوهُ فَأَخَذَتْهُمُ الرَّجْفَةُ فَأَصْبَحُوا فِي دَارِهِمْ جَاثِمِينَ ﴿٣٧﴾
37. Wakamkadhibisha, basi likawachukuwa tetemeko kali la ardhi wakapambaukiwa majumbani mwao wenye kuanguka kifudifudi.
وَعَادًا وَثَمُودَ وَقَد تَّبَيَّنَ لَكُم مِّن مَّسَاكِنِهِمْ ۖ وَزَيَّنَ لَهُمُ الشَّيْطَانُ أَعْمَالَهُمْ فَصَدَّهُمْ عَنِ السَّبِيلِ وَكَانُوا مُسْتَبْصِرِينَ ﴿٣٨﴾
38. Na kina ‘Aad na Thamuwd. Na bila shaka (maangamizi yao) yamekwishakubainikieni katika masikani zao. Na shaytwaan aliwapambia amali zao, akawazuia na njia, japokuwa walikuwa ni wenye kumaizi na kutambua vizuri.
وَقَارُونَ وَفِرْعَوْنَ وَهَامَانَ ۖ وَلَقَدْ جَاءَهُم مُّوسَىٰ بِالْبَيِّنَاتِ فَاسْتَكْبَرُوا فِي الْأَرْضِ وَمَا كَانُوا سَابِقِينَ ﴿٣٩﴾
39. Na kina Qaaruwn, na Firawni, na Haamaan[4]. Na kwa yakini aliwajia Muwsaa kwa hoja bayana wakatakabari katika ardhi, lakini hawakuwa wenye kushinda.
فَكُلًّا أَخَذْنَا بِذَنبِهِ ۖ فَمِنْهُم مَّنْ أَرْسَلْنَا عَلَيْهِ حَاصِبًا وَمِنْهُم مَّنْ أَخَذَتْهُ الصَّيْحَةُ وَمِنْهُم مَّنْ خَسَفْنَا بِهِ الْأَرْضَ وَمِنْهُم مَّنْ أَغْرَقْنَا ۚ وَمَا كَانَ اللَّـهُ لِيَظْلِمَهُمْ وَلَـٰكِن كَانُوا أَنفُسَهُمْ يَظْلِمُونَ ﴿٤٠﴾
40. Basi kila mmoja Tulimchukuwa kumwadhibu kwa mujibu wa dhambi yake. Miongoni mwao wale Tuliowapelekea tufani, na miongoni mwao wale waliochukuliwa na ukelele angamizi, na miongoni mwao wale Tuliowadidimiza ardhini, na miongoni mwao wale Tuliowagharikisha. Na Allaah Hakuwadhulumu, lakini walikuwa wakijidhulumu nafsi zao wenyewe.[5]
مَثَلُ الَّذِينَ اتَّخَذُوا مِن دُونِ اللَّـهِ أَوْلِيَاءَ كَمَثَلِ الْعَنكَبُوتِ اتَّخَذَتْ بَيْتًا ۖ وَإِنَّ أَوْهَنَ الْبُيُوتِ لَبَيْتُ الْعَنكَبُوتِ ۖ لَوْ كَانُوا يَعْلَمُونَ ﴿٤١﴾
41. Mfano wa wale waliochukuwa badala ya Allaah walinzi ni kama mfano wa buibui alivyojitandia nyumba. Na bila shaka nyumba iliyo dhaifu kuliko zote ni nyumba ya buibui, lau wangelikuwa wanajua![6]
إِنَّ اللَّـهَ يَعْلَمُ مَا يَدْعُونَ مِن دُونِهِ مِن شَيْءٍ ۚ وَهُوَ الْعَزِيزُ الْحَكِيمُ ﴿٤٢﴾
42. Hakika Allaah Anavijua vyote vile wanavyoviomba badala Yake, Naye Ndiye Mwenye Enzi ya Nguvu Asiyeshindika, Mwenye Hikmah wa yote.
وَتِلْكَ الْأَمْثَالُ نَضْرِبُهَا لِلنَّاسِ ۖ وَمَا يَعْقِلُهَا إِلَّا الْعَالِمُونَ ﴿٤٣﴾
43. Na hiyo ni mifano Tunawapigia watu. Lakini hawaifahamu isipokuwa wenye ilimu.
خَلَقَ اللَّـهُ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضَ بِالْحَقِّ ۚ إِنَّ فِي ذَٰلِكَ لَآيَةً لِّلْمُؤْمِنِينَ ﴿٤٤﴾
44. Allaah Ameumba mbingu na ardhi kwa haki. Hakika katika hayo mna Aayah (Ishara, Dalili, Mazingatio) kwa Waumini.
اتْلُ مَا أُوحِيَ إِلَيْكَ مِنَ الْكِتَابِ وَأَقِمِ الصَّلَاةَ ۖ إِنَّ الصَّلَاةَ تَنْهَىٰ عَنِ الْفَحْشَاءِ وَالْمُنكَرِ ۗ وَلَذِكْرُ اللَّـهِ أَكْبَرُ ۗ وَاللَّـهُ يَعْلَمُ مَا تَصْنَعُونَ ﴿٤٥﴾
45. Soma (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم) uliyoletewa Wahy katika Kitabu na simamisha Swalaah, hakika Swalaah inazuia machafu na munkari. Na bila shaka kumdhukuru Allaah ndilo kubwa zaidi. Na Allaah Anajua yale mnayoyatenda.
وَلَا تُجَادِلُوا أَهْلَ الْكِتَابِ إِلَّا بِالَّتِي هِيَ أَحْسَنُ إِلَّا الَّذِينَ ظَلَمُوا مِنْهُمْ ۖ وَقُولُوا آمَنَّا بِالَّذِي أُنزِلَ إِلَيْنَا وَأُنزِلَ إِلَيْكُمْ وَإِلَـٰهُنَا وَإِلَـٰهُكُمْ وَاحِدٌ وَنَحْنُ لَهُ مُسْلِمُونَ ﴿٤٦﴾
46. Na wala msibishane na Watu wa Kitabu isipokuwa kwa yale ambayo ni mazuri zaidi, isipokuwa wale waliodhulumu miongoni mwao. Na semeni: Tumeyaamini ambayo yameteremshwa kwetu na yaliyoteremshwa kwenu, na Ilaah wetu na Ilaah wenu ni (Allaah) Mmoja Pekee, nasi Kwake tunajisalimisha.
وَكَذَٰلِكَ أَنزَلْنَا إِلَيْكَ الْكِتَابَ ۚ فَالَّذِينَ آتَيْنَاهُمُ الْكِتَابَ يُؤْمِنُونَ بِهِ ۖ وَمِنْ هَـٰؤُلَاءِ مَن يُؤْمِنُ بِهِ ۚ وَمَا يَجْحَدُ بِآيَاتِنَا إِلَّا الْكَافِرُونَ ﴿٤٧﴾
47. Na hivyo ndivyo Tulivyokuteremshia Kitabu (Qur-aan). Basi wale Tuliowapa Maandiko (Tawraat na Injiyl) wanakiamini. Na miongoni mwa hawa (Maquraysh wa Makkah) wako ambao wanakiamini. Na hawakanushi Aayaat (na Ishara) Zetu isipokuwa makafiri.
وَمَا كُنتَ تَتْلُو مِن قَبْلِهِ مِن كِتَابٍ وَلَا تَخُطُّهُ بِيَمِينِكَ ۖ إِذًا لَّارْتَابَ الْمُبْطِلُونَ ﴿٤٨﴾
48. Na wala hukuwa (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم) ukisoma kabla yake kitabu chochote, na wala hukukiandika kwa mkono wako wa kuume, kwani basi hapo wangetilia shaka wabatilifu.
بَلْ هُوَ آيَاتٌ بَيِّنَاتٌ فِي صُدُورِ الَّذِينَ أُوتُوا الْعِلْمَ ۚ وَمَا يَجْحَدُ بِآيَاتِنَا إِلَّا الظَّالِمُونَ ﴿٤٩﴾
49. Bali hizi ni Aayaat bayana (zimehifadhika) katika vifua vya wale waliopewa ilimu. Na hawazikanushi Aayaat Zetu isipokuwa madhalimu.
وَقَالُوا لَوْلَا أُنزِلَ عَلَيْهِ آيَاتٌ مِّن رَّبِّهِ ۖ قُلْ إِنَّمَا الْآيَاتُ عِندَ اللَّـهِ وَإِنَّمَا أَنَا نَذِيرٌ مُّبِينٌ ﴿٥٠﴾
50. Na wakasema: Kwa nini hakuteremshiwa Aayaat (Miujiza ya kihisia na Ishara, Dalili) kutoka kwa Rabb wake? Sema (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم): Hakika Aayaat ziko kwa Allaah, na hakika mimi ni mwonyaji mbainishaji tu.
أَوَلَمْ يَكْفِهِمْ أَنَّا أَنزَلْنَا عَلَيْكَ الْكِتَابَ يُتْلَىٰ عَلَيْهِمْ ۚ إِنَّ فِي ذَٰلِكَ لَرَحْمَةً وَذِكْرَىٰ لِقَوْمٍ يُؤْمِنُونَ ﴿٥١﴾
51. Je, haikuwatosheleza kwamba hakika Sisi Tumekuteremshia Kitabu (Qur-aan) wanachosomewa? Hakika katika hayo bila shaka kuna rehma na ukumbusho (na mawaidha) kwa watu wanaoamini.
قُلْ كَفَىٰ بِاللَّـهِ بَيْنِي وَبَيْنَكُمْ شَهِيدًا ۖ يَعْلَمُ مَا فِي السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ ۗ وَالَّذِينَ آمَنُوا بِالْبَاطِلِ وَكَفَرُوا بِاللَّـهِ أُولَـٰئِكَ هُمُ الْخَاسِرُونَ ﴿٥٢﴾
52. Sema: Anatosheleza Allaah kuwa ni Shahidi baina yangu na baina yenu. Anayajua yale yaliyomo katika mbingu na ardhi. Na wale walioamini ubatilifu na wakamkufuru Allaah, hao ndio waliokhasirika.
وَيَسْتَعْجِلُونَكَ بِالْعَذَابِ ۚ وَلَوْلَا أَجَلٌ مُّسَمًّى لَّجَاءَهُمُ الْعَذَابُ وَلَيَأْتِيَنَّهُم بَغْتَةً وَهُمْ لَا يَشْعُرُونَ ﴿٥٣﴾
53. Na wanakuharakiza adhabu. Na lau kama si muda maalumu uliokadiriwa, ingeliwajia adhabu, na bila shaka itawajia ghafla na hali wao hawahisi.[7]
يَسْتَعْجِلُونَكَ بِالْعَذَابِ وَإِنَّ جَهَنَّمَ لَمُحِيطَةٌ بِالْكَافِرِينَ ﴿٥٤﴾
54. Wanakuharakiza adhabu na hakika Jahannam bila shaka itawazunguka makafiri.
يَوْمَ يَغْشَاهُمُ الْعَذَابُ مِن فَوْقِهِمْ وَمِن تَحْتِ أَرْجُلِهِمْ وَيَقُولُ ذُوقُوا مَا كُنتُمْ تَعْمَلُونَ ﴿٥٥﴾
55. Siku itakayowafunika adhabu kutoka juu yao na kutoka chini ya miguu yao, na Atasema: Onjeni yale mliyokuwa mkitenda.
يَا عِبَادِيَ الَّذِينَ آمَنُوا إِنَّ أَرْضِي وَاسِعَةٌ فَإِيَّايَ فَاعْبُدُونِ ﴿٥٦﴾
56. Enyi Waja Wangu walioamini! Hakika Ardhi Yangu ni pana, basi Mimi Pekee Niabuduni.
كُلُّ نَفْسٍ ذَائِقَةُ الْمَوْتِ ۖ ثُمَّ إِلَيْنَا تُرْجَعُونَ ﴿٥٧﴾
57. Kila nafsi itaonja mauti, kisha Kwetu mtarejeshwa.
وَالَّذِينَ آمَنُوا وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ لَنُبَوِّئَنَّهُم مِّنَ الْجَنَّةِ غُرَفًا تَجْرِي مِن تَحْتِهَا الْأَنْهَارُ خَالِدِينَ فِيهَا ۚ نِعْمَ أَجْرُ الْعَامِلِينَ ﴿٥٨﴾
58. Na wale walioamini na wakatenda mema, bila shaka Tutawawekea makazi ya ghorofa katika Jannah, yapitayo chini yake mito, ni wenye kudumu humo. Uzuri ulioje ujira wa watendao!
الَّذِينَ صَبَرُوا وَعَلَىٰ رَبِّهِمْ يَتَوَكَّلُونَ ﴿٥٩﴾
59. Ambao walisubiri, na kwa Rabb wao wanatawakali.
وَكَأَيِّن مِّن دَابَّةٍ لَّا تَحْمِلُ رِزْقَهَا اللَّـهُ يَرْزُقُهَا وَإِيَّاكُمْ ۚ وَهُوَ السَّمِيعُ الْعَلِيمُ ﴿٦٠﴾
60. Na viumbe wangapi hawabebi riziki zao? Allaah Huwaruzuku wao na nyinyi. Naye Ndiye Mwenye Kusikia yote, Mjuzi wa yote.
وَلَئِن سَأَلْتَهُم مَّنْ خَلَقَ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضَ وَسَخَّرَ الشَّمْسَ وَالْقَمَرَ لَيَقُولُنَّ اللَّـهُ ۖ فَأَنَّىٰ يُؤْفَكُونَ ﴿٦١﴾
61. Na ukiwauliza: Ni nani aliyeumba mbingu na ardhi, na akatiisha jua na mwezi? Bila shaka watasema: Allaah. Basi vipi wanaghilibiwa?[8]
اللَّـهُ يَبْسُطُ الرِّزْقَ لِمَن يَشَاءُ مِنْ عِبَادِهِ وَيَقْدِرُ لَهُ ۚ إِنَّ اللَّـهَ بِكُلِّ شَيْءٍ عَلِيمٌ ﴿٦٢﴾
62. Allaah Anamkunjulia riziki Amtakaye kati ya Waja Wake na Humkadiria kwa kipimo (Amtakaye). Hakika Allaah kwa kila kitu ni Mjuzi.
وَلَئِن سَأَلْتَهُم مَّن نَّزَّلَ مِنَ السَّمَاءِ مَاءً فَأَحْيَا بِهِ الْأَرْضَ مِن بَعْدِ مَوْتِهَا لَيَقُولُنَّ اللَّـهُ ۚ قُلِ الْحَمْدُ لِلَّـهِ ۚ بَلْ أَكْثَرُهُمْ لَا يَعْقِلُونَ ﴿٦٣﴾
63. Na ukiwauliza: Ni nani Ateremshaye maji kutoka mbinguni, Akahuisha kwayo ardhi baada ya kufa kwake? Bila shaka watasema: Allaah. Sema: AlhamduliLLaah (Himidi Anastahiki Allaah). Bali wengi wao hawatii akilini.
وَمَا هَـٰذِهِ الْحَيَاةُ الدُّنْيَا إِلَّا لَهْوٌ وَلَعِبٌ ۚ وَإِنَّ الدَّارَ الْآخِرَةَ لَهِيَ الْحَيَوَانُ ۚ لَوْ كَانُوا يَعْلَمُونَ ﴿٦٤﴾
64. Na huu uhai wa dunia si chochote isipokuwa ni pumbao na mchezo. Na hakika Nyumba ya Aakhirah bila shaka ndiyo yenye uhai wa kweli hasa (wa milele), lau wangelikuwa wanajua!
فَإِذَا رَكِبُوا فِي الْفُلْكِ دَعَوُا اللَّـهَ مُخْلِصِينَ لَهُ الدِّينَ فَلَمَّا نَجَّاهُمْ إِلَى الْبَرِّ إِذَا هُمْ يُشْرِكُونَ ﴿٦٥﴾
65. Wanapopanda merikebu humwomba Allaah wakiwa wenye kumtakasia Yeye Duaa, lakini Anapowaokoa wakafika nchi kavu, tahamaki hao wanamshirikisha.[9]
لِيَكْفُرُوا بِمَا آتَيْنَاهُمْ وَلِيَتَمَتَّعُوا ۖ فَسَوْفَ يَعْلَمُونَ ﴿٦٦﴾
66. Ili wayakanushe yale Tuliyowapa, na ili wastarehe. Basi karibuni watakuja kujua.
أَوَلَمْ يَرَوْا أَنَّا جَعَلْنَا حَرَمًا آمِنًا وَيُتَخَطَّفُ النَّاسُ مِنْ حَوْلِهِمْ ۚ أَفَبِالْبَاطِلِ يُؤْمِنُونَ وَبِنِعْمَةِ اللَّـهِ يَكْفُرُونَ ﴿٦٧﴾
67. Je, hawaoni kwamba hakika Sisi Tumejaalia (Makkah) kuwa ni tukufu na yenye amani, na huku wananyakuliwa watu pembezoni mwao? Je, basi wanaamini baatwil, na Neema za Allaah wanazikufuru?
وَمَنْ أَظْلَمُ مِمَّنِ افْتَرَىٰ عَلَى اللَّـهِ كَذِبًا أَوْ كَذَّبَ بِالْحَقِّ لَمَّا جَاءَهُ ۚ أَلَيْسَ فِي جَهَنَّمَ مَثْوًى لِّلْكَافِرِينَ ﴿٦٨﴾
68. Na nani dhalimu zaidi kuliko yule aliyemtungia Allaah uongo, au aliyekadhibisha haki ilipomjia? Je, si katika Jahannam ndio yatakuwa makazi ya makafiri?
وَالَّذِينَ جَاهَدُوا فِينَا لَنَهْدِيَنَّهُمْ سُبُلَنَا ۚ وَإِنَّ اللَّـهَ لَمَعَ الْمُحْسِنِينَ ﴿٦٩﴾
69. Na wale waliofanya juhudi kwa ajili Yetu, bila shaka Tutawaongoza njia Zetu. Na hakika Allaah Yu Pamoja na watendao ihsaan.
[1] الحروف المقطعة (Al-Huruwf Al-Muqatw-twa’ah):
Hizi ni herufi zinazojulikana kama الحروف المقطعة (Al-Huruwf Al-Muqatw-twa’ah), ambazo hakuna ajuaye maana zake isipokuwa Allaah (سبحانه وتعالى). Rejea Tanbihi ya Al-Baqarah (2:1).
[2] Sababun-Nuzuwl (Sababu Ya Kuteremshwa) Aayah Au Suwrah/Katazo La Kuwatii Viumbe Katika Kumwasi Muumbaji Hata Kama Ni Wazazi:
Bonyeza kiungo kifuatacho:
029-Asbaabun-Nuzuwl: Al-‘Ankabuwt Aayah 08: وَوَصَّيْنَا الإِنْسَانَ بِوَالِدَيْهِ حُسْنًا
Juu ya kwamba Allaah (سبحانه وتعالى) Ametilia umuhimu mkubwa wa kuwatii wazazi, lakini utiifu kwa wazazi una mipaka. Mzazi anapomwamrisha mwanawe kumuasi Allaah (سبحانه وتعالى), basi mtoto hapaswi kumfuata katika hilo, na Hadiyth zifuatazo zimethibitisha jambo hili:
عَنْ عَلِيٍّ رَضِيَ اللَّهُ عَنْهُ عَنْ النَّبِيِّ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ قَالَ لَا طَاعَةَ لِبَشَرٍ فِي مَعْصِيَةِ اللَّهِ
Amesimulia ‘Aliy (رضي الله عنه): Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Hakuna utiifu kwa kiumbe katika maasi ya Allaah.” [Ahmad]
Na amesema pia Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم):
لَا طَاعَةَ لِمَخْلُوقٍ فِي مَعْصِيَةِ الْخَالِقِ
“Hakuna utiifu kwa kiumbe katika kumuasi Muumba” [At-Tirmidhiy]
Na amrisho la kuwafanyia ihsaan wazazi na kutokuwatii katika maasi, linawahusu wazazi Waislamu na wasiokuwa Waislamu. Na hata kama wazazi wataamrisha maasi, lakini Allaah (سبحانه وتعالى) Anaamrisha kuishi na kukaa nao kwa wema duniani, ni sawa wawe ni wazazi Waislamu au sio Waislamu.
Rejea pia Luqmaan (31:14-15).
[4] Haamaan:
Alikuwa ni waziri au mtu mwenye cheo. [Tafsiyr Ibn Kathiyr]
Ama kuhusu Qaaruwn, Rejea Al-Qaswasw (28:76).
[5] Makafiri Wa Nyumati Za Nyuma Na Aina Za Adhabu Zao:
Katika Suwrah hii ya Al-‘Ankabuwt namba (40), Allaah (سبحانه وتعالى) Ametaja aina za adhabu walizoangamizwa kwazo makafiri wa nyumati za nyuma. Adhabu hizo ni kupelekewa tufani, ukelele angamizi, kudidimizwa ardhini, kugharakishwa. Na yafuatayo ni uchambuzi wa kaumu za nyumati za nyuma, na aina za adhabu zao, na baadhi ya rejea mbali mbali za visa vyao.
(i) Kaumu ya Nabiy Nuwh (عليه السّلام):
Watu wa Nuwh (عليه السّلام) walikuwa wakimshirikisha Allaah kwa kuabudu masanamu. Na wao ni watu wa kwanza kabisa ardhini kuanzisha ibaada ya masanamu. Walianza ibaada ya masanamu baada ya kufariki waja wema ambao majina yao ni: Waddaa, Suwaa’aa, Yaghuwtha, Ya’uwqa, na Nasraa. Rejea Nuwh (71:23). Shaytwaan akawapambia kuwakurubisha nao, wakachora sura zao na kuchonga masanamu ya kuwanasabisha. Na hapo ndipo ikaendelea ibaada ya masanamu kwa Waarabu na kaumu nyenginezo karne kwa karne. Na ndio maana Nabiy Nuwh (عليه السّلام) akawa ni Rasuli wa kwanza kulingania watu katika Tawhiyd ya Allaah (Kumpwekesha Allaah). Rejea Asw-Swaaffaat (37:77).
Maangamizi Yao: Washirikina hao wa kaumu ya Nuwh (عليه السّلام) waliangamizwa kwa tufani lililowagharakisha baharini. Rejea Suwrah hii Al-‘Ankabuwt (29:14), Al-Furqaan (25:37).
Nuwh (عليه السّلام) akawalingania kaumu yake waache ushirikina wa kuabudu masanamu na badala yake akawaamrisha wamwabudu Allaah (سبحانه وتعالى), lakini Lakini walimkanusha. Akaendelea kuwalingania kwa muda wa miaka 950, lakini waliendelea kumkanusha na wakawa wanamfanyia istihzai alipokuwa akiunda jahazi. Rejea Huwd (11:38). Allaah Akafungua mbingu na ardhi zikamiminika maji hadi ikawa ni bahari. Rejea Al-Qamar (54:11-12). Mawimbi yakawafunika, wakagharakishwa katika maji hayo watu wake pamoja na mwanawe, na Allaah Akamuokoa Nuwh pamoja na walioamini ambao walipanda jahazini. Rejea Huwd (11:41-43).
Rejea Al-A’raaf (7:59-64), Yuwnus (10:71-73), Huwd (11:25-48), Al-Anbiyaa (21:76-77), Al-Muuminuwn (23:23-30), Al-Furqaan (25:37), Ash-Shu’araa (26:105-120), Al-‘Ankabuwt (29:14-15), Asw-Swaaffaat (37:75-78), Al-Qamar (54:10-15) na Suwrah ya Nuwh namba (71).
(ii) Kaumu ya ‘Aad watu wa Nabiy Huwd (عليه السّلام):
Watu wa ‘Aad walikuwa wakimshirikisha Allaah kwa kuabudu masanamu.
Maangamizi Yao: Waliangamizwa kwa tufani na upepo mbaya wa sauti na baridi kali, uvumao kwa nguvu kwa muda wa siku nane mfululizo, ukawaangamiza wakawa kama magogo ya mitende iliyo mitupu. Rejea Al-Haaqqah (69:6-8). Na pia radi na umeme angamizi. Rejea Fusw-Swilat (41:13),
Allaah (سبحانه وتعالى) Aliwajaalia kaumu ya ‘Aad wenye umbo zuri na nguvu na uwezo wa kujenga majumba ya kifakhari, na ardhi yao ilikuwa bustani ya kijani kibichi ambapo mifugo ililishwa na kuongezeka, na hivyo wakajaaliwa mali nyingi za kila aina na watoto. Nabiy wao Huwd (عليه السّلام) aliwalingania waache ibaada ya masanamu na wampwekeshe Allaah (سبحانه وتعالى), lakini walimkanusha wakaendelea na kuabudu masanamu na kutakabari na kujiona kuwa wao ni wenye nguvu zaidi wakasema: ”Nani mwenye nguvu zaidi kuliko sisi?” Rejea Fusw-Swilat (41:15). Allaah (سبحانه وتعالى) Akawaangamiza kwa tufani na upepo mbaya wa sauti na baridi kali, uvumao kwa nguvu.
Rejea Al-A’raaf (7:65-72), Huwd (11:50-60), Ash-Shu’araa (26:123-139), Fusw-Swilat (41:16), Al-Ahqaaf (46:21-25), Adh-Dhaariyaat (51:41-42), Al-Qamar (54:18-21), Al-Haaqqah (69:6-7), Al-Fajr (89:6-8).
(iii) Kaumu Ya Thamuwd Watu Wa Nabiy Swaalih (عليه السّلام):
Watu wa Thamuwd walikuwa wakimshirikisha Allaah kwa kuabudu masanamu.
Maangamizi Yao: Waliangamizwa kwa tetemeko la ardhi, rejea Al-A’raaf (7:78), na ukelele angamizi mkali mno uliovuka mipaka. Al-Haaqqah (69:5). Na pia radi na umeme angamizi. Rejea Rejea Fusw-Swilat (41:18).
Allaah (سبحانه وتعالى) Aliwajaalia kaumu ya Thamuwd neema za mabustani na chemchemu, na uwezo wa kuchonga nyumba nzuri milimani.
Nabiy wao Swaalih (عليه السّلام) aliwalingania waache ibaada ya masanamu na wampwekeshe Allaah, lakini walitakabari na wakakanusha Risala, na wakafanya ufisadi katika ardhi. Nabiy Swaalih (عليه السّلام) alipoendelea kuwalingania, walitaka muujiza kutoka kwa Allaah waletewe ngamia jike aliyekuwa na mimba atoke kwenye mwamba. Allaah (سبحانه وتعالى) Akawaitikia maombi yao, Akawatumia mbele ya macho yao ngamia na kwa sifa walizozitaka. Wakaamrishwa wamhifadhi ngamia wasimguse kwa uovu wowote ule na wafanye zamu katika kunywa maji ya kisimani; siku anywe ngamia na siku wanywe wao. Rejea Ash-Shu’araa (26:155-156) na Al-Qamar (54:27-28). Lakini walitakabari, wakamzuia ngamia asinywe maji na wakamuua, na wakafanya njama pia kumuua Nabiy Swaalih (عليه السّلام) . Rejea An-Naml (27:48-49). Basi Akaanza kuwaonyesha ishara ya adhabu siku tatu nyuso zao zikibadilika rangi kisha Allaah (سبحانه وتعالى) Akawaangamiza kwa ukelele mkali mno na tetemeko la ardhi, wakaanguka kifudifudi majumbani mwao wakiwa wamefariki.
Rejea Al-A’raaf (7:73-79), Huwd (11:61-68), Al-Israa (17:59), Ash-Shu’araa (26:141-158), An-Naml (27:45-53), Fusw-Swilat (41:17), Adh-Dhaariyat (51:43-45), Al-Qamar (54:23-31), Ash-Shams (91:11-15),
(iv) Kaumu Ya Nabiy Luutw (عليه السّلام):
Watu wa Nabiy Luutw (عليه السّلام) walikuwa wakifanya machafu ya kuwaingilia wanaume wenzao katika duburi zao.
Maangamizi Yao: Waliangamizwa kwa kupinduliwa mji wao juu chini na pia kwa ukelele angamizi. Rejea Al-Hijr (15:73-74). Pia kwa mvua ya mawe ya udongo mgumu uliookwa motoni, yametiwa alama. Rejea Huwd (11:82-83). Pia kwa tufani ya mawe. Rejea Al-Qamar (54:34).
Nabiy wao Luutw (عليه السّلام) akawalingania waache machafu hayo na badala yake wawaoe wanawake ambao ndio inavyotaka kisharia kujimai nao. Lakini walimkanusha wao pamoja na mkewe ambaye naye pia alibakishwa nyuma aingie katika maangamizi.
Rejea Al-A’raaf (7:80-84), Huwd (11:77-83), Al-Hijr (15:61-74), Ash-Shu’araa (26:160-173), An-Naml (27:54-58), Al-‘Ankabuwt (29:28-34), Al-Qamar (54:33-39),
(v) Watu Wa Madyan Ambao Ni Kaumu Ya Nabiy Shu’ayb (عليه السّلام):
Watu wa Nabiy Shu’ayb (عليه السّلام) walikuwa wakimshirikisha Allaah kwa kuabudu masanamu. Juu ya hivyo, walikuwa wakifanya ufisadi katika ardhi; wakifanya khiyana ya kupunja vipimo katika mizani, na kuzuia watu njia ya Allaah.
Maangamizi Yao: Waliangamizwa kwa tetemeko la ardhi. Rejea Al-‘Araaf (7:92). Na ukelele angamizi. Rejea Huwd (11:94).
Nabiy Shu’ayb akawalingania lakini walimkanusha wakataka kumfukuza mjini, basi Allaah (سبحانه وتعالى) Akawaangamiza kwa ukelele angamizi na tetemeko la ardhi wakafilia mbali.
Rejea Al-A’raaf (7:85-93), Huwd (11:84-95), Al-‘Ankabuwt (29:36-37).
(vi) Firawni, Haamaan Na Jeshi Lake:
Firawni alikuwa akiwatesa wana wa Israaiyl na akiwaua wanawake wao na watoto wao.
Maangamizi Yao: Waligharakishwa baharini Rejea Al-Qaswasw (28:40), Adh-Dhaariyaat (51:40).
Nabiy Muwsaa (عليه السّلام) akatumwa kwake kumlingania, lakini alitakabari na akapinduka mipaka hadi kujifanya yeye ni mwenye kustahiki kuabudiwa. Akakanusha Risala ya Rabb wake kupitia kwa Nabiy Muwsaa (عليه السّلام). Allaah (سبحانه وتعالى) Akawapelekea miujiza tisa lakini hakutaka kumwamini Allaah na akaendelea na kiburi chake na akaazimia kumuua Nabiy Muwsaa (عليه السّلام). Allaah (سبحانه وتعالى) Akamuamrisha Nabiy Muwsaa (عليه السّلام) apige fimbo yake katika bahari, basi hapo bahari ikatengana ikawa kila sehemu kama jabali kubwa. Akavuka Nabiy Muwsaa na wana wa Israaiyl, kisha Allaah (سبحانه وتعالى) Akamuangamiza Firawni na waziri wake Haamaan na jeshi lake katika bahari.
Na kisa cha Nabiy Muwsaa (عليه السّلام) na Firawni kimetajwa sehemu nyingi mno na kwa urefu kuliko Rusuli wengineo. Miongoni mwa Suwrah ambazo kimetajwa kwa wingi ni Suwrah Al-A’raaf namba (7) kuanzia Aayah namba (103) na kumalizikia Aayah namba (171). Pia Yuwnus (10:75-92). Rejea pia Huwd (11:96-99). Rejea pia Twaahaa (20:9-79), Al-Muuminuwn (23:45-48), Ash-Shu’araa (26:10-66), Al-Qaswasw (28:3-40), An-Naazi’aat (79:15-25).
Na rejea khasa Al-A’raaf (7:107-108), (7:130) na (7:133) kwenye uchambuzi bayana, kuhusu miujiza tisa ya Allaah kwa watu wa Firawni.
(vii) Qaaruwn: Alikuwa Katika Watu Wa Nabiy Muwsaa (عليه السّلام):
Qaaruwn alipinduka mipaka katika maasia, na akatakabari kwa majivuno na kujigamba kwa kujaaliwa hazina ya mali. Akajigamba kuwa mali hiyo kuwa imetokana na ujuzi wake, akamsahau Rabb wake Aliyemruzuku.
Rejea Al-Qaswasw: (28-76-82).
Maangamizi Yake: Alididimizwa ardhini. Rejea Al-Qaswasw (28:81).
[6] Masanamu Na Waabudiwa Wengineo Pasi Na Allaah Ni Kama Nyumba Ya Buibui:
Mfano wa wale waliowafanya masanamu ni walinzi badala ya Allaah na huku, wanatarajia nusura na usaidizi wao, ni kama mfano wa buibui aliyejitengenezea nyumba ili imuhifadhi (kutokana madhara ya kila aina), lakini isimfae kitu alipokuwa na haja nayo. Basi kadhaalika hivyo ndivyo hali ilivyo kwa hawa washirikiana, hawakuwafaa kitu wale waliowachukuwa kuwafanya kuwa ni walinzi wao badala ya Allaah. Na bila shaka nyumba iliyo dhaifu kuliko zote ni nyumba ya buibui. Lau wangelikuwa wanajua hilo, wasingewafanya wao ni walinzi wao wenye kutegemewa kwa sababu hawawanufaishi lolote wala hawawadhuru. [Tafsiyr Al-Muyassar]
Na Imaam Ibn Kathiyr ametafsiri: Mfano huu Allaah Anaupiga kwa washirikina waliowafanya waabudiwa asiyekuwa Allaah wakitaraji usaidizi wao (au nusura) na rizki zao, na wanawashikilia katika shida zao. Basi wao ni kama hiyo nyumba ya buibui ambayo ni dhaifu mno. Hivyo ni kwa sababu, kuwashikilia waabudiwa hawa ni kama mtu kushikilia nyumba ya buibui ambayo haimfai kitu. Na lau wangelikua wanajua hali hii, basi wasingeliwachukua asiyekuwa Allaah kuwafanya ni walinzi. Na hii ni kinyume na Muislamu Muumin ambaye moyo wake umejisabilia kwa dhati na kuelemea kwa Allaah, lakini bado anafanya matendo mema na anafuata Sharia za Allaah. Hivyo ni kwa sababu ameshikilia imara kishikilio madhubuti kisichovunjika, kutokana na nguvu yake na kuthibitika kwake. [Tafsiyr Ibn Kathiyr]
[7] Ada Ya Makafiri Kuhimiza Adhabu: Rejea: Al-Anfaal (8:32), Al-Hajj (22:47), Swaad (38:16)
[8] Washirikina Waliamini Tawhiyd Ar-Rubuwbiyyah Lakini Walikanusha Tawhiyd Al-Uluwhiyyah.
Washirikina wa Makkah waliamini yafuatayo katika kumpwekesha Allaah (سبحانه وتعالى):
(i) Allaah (سبحانه وتعالى) Ndiye Aliyewaumba: Az-Zukhruf (43:87).
(ii) Allaah (سبحانه وتعالى) Ndiye Aliyeumba mbingu na ardhi: Suwrah hii Al-‘Ankabuwt (29:61), Luqmaan (31:25) na Az-Zumar (39:38).
(iii) Allaah (سبحانه وتعالى) Ndiye Aliyetiisha jua na mwezi: Suwrah hii Al-‘Ankabuwt (29:61).
(iv) Allaah (سبحانه وتعالى) Ndiye Ateremshaye maji kutoka mbinguni, Akahuisha kwayo ardhi baada ya kufa kwake. Suwrah hii Al-‘Ankabuwt (29:63).
(v) Allaah (سبحانه وتعالى) Ndiye Anayewaruzuku na Ndiye Anayemiliki kusikia na kuona. Na Ndiye Anayehuisha na Kufisha na Ndiye Anayeendesha mambo yote ya ulimwenguni: Yuwnus (10:31), Az-Zukhruf (43:9).
Lakini walimshirikisha katika Tawhiyd Al-Uluwhiyyah ambayo ni kumpwekesha katika ibaada, yaani, kumwelekea Yeye Allaah (سبحانه وتعالى) Pekee katika kumwabudu na kumuomba duaa badala ya kuelekea masanamu au viumbe vinginevyo.
Wakamshirikisha Allaah (سبحانه وتعالى) kwa kumhusisha na viumbe Alivyoviumba kama vile kusema Ana mwana, au Malaika ni mabinti Wake, au Ana uhusiano na majini! Subhaana Allaah! (Ametakasika Allaah!). Rejea Asw-Swaaffaat (37:149).
Wakamshirikisha Allaah katika mimea na wanyama Aliyoumba. Ikawa wanapochinja hawaanzi kwa Jina la Allaah. Na pia wakawa wanakusudia kumwekea Allaah (سبحانه وتعالى) sehemu ya nyama waliyokuwa wakichinja na sehemu wakiwaekea masanamu yao! Rejea Al-An’aam (6:136), (6:138-139).
Wakamshirikisha katika Hajj, kwani kabla ya Uislamu, washirikina walikuwa wakihiji, lakini Hijjah yao ilikuwa ni ya kufru na uasi. Walikuwa wakitufu Al-Ka’bah mbele ya masanamu kwa miruzi na kupiga makofi. Rejea Al-Anfaal (8:35).
Wakamshirikisha pia katika Hajj kwenye talbiyah kwa kuongezea maneno ya kumshirikisha Allaah (سبحانه وتعالى). Walikuwa wakisema:
لبيك لا شريك لك، إلا شريكاً هو لك، تملكه وما ملك
Nimekuitikia, (ee Allaah) Huna mshirika yoyote. Isipokuwa mshirika, yeye ni Wako, Unammiliki, na yeye hamiliki chochote.
Kinyume na talbiyah ya Tawhiyd ambayo ni:
لَبَّيْكَ اللَّهُمَّ لَبَّيْكَ ، لَبَّيْكَ لاَ شَرِيكَ لَكَ لَبَّيْكَ ، إِنَّ الْحَمْدَ ، وَالنِّعْمَةَ ، لَكَ وَالْمُلْكَ ، لاَ شَرِيكَ لَكَ
"Nimekuitikia (ee Allaah) nimekuitikia (ee Allaah), nimekuitikia (ee Allaah) Huna mshirika nimekuitikia (ee Allaah), hakika Kuhimidiwa na Neema na Ufalme ni Vyako Huna mshirika."
Maneno yao hayo ya shirki, ni kama ilivyo katika Hadiyth ifuatayo:
عَنِ ابْنِ عَبَّاسٍ قَالَ: كَانَ الْمُشْرِكُونَ يَقُولُونَ: لَبَّيْكَ لَا شَرِيكَ لَكَ فَيَقُولُ رَسُولُ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ: «وَيْلَكُمْ قَدْ قَدْ» إِلَّا شَرِيكًا هُوَ لَكَ تَمْلِكُهُ وَمَا مَلَكَ. يَقُولُونَ هَذَا وَهُمْ يَطُوفُونَ بِالْبَيْتِ. رَوَاهُ مُسْلِمٌ
Amesimulila Ibn ‘Abbaas (رضي الله عنهما): “Wapagani walikuwa wanasema: Nimekuitikia, (ee Allaah) Huna mshirika yoyote. Na hapo hapo Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) huwaambia: Ole wenu! Acheni, msiongeze (mkasema): “Isipokuwa mshirika, yeye ni Wako, Unammiliki, na yeye hamiliki chochote”, wanasema haya huku wanaitufu Nyumba (Al-Ka’bah)”. [Muslim]
Sharh Ya Hadiyth:
Talbiyah wanayoileta Waislamu katika Hajji inakuwa kwa kumpwekesha Allaah (سبحانه وتعالى), kumtakasia Yeye tu Dini na kujiweka mbali na shirki. Ama mapagani, talbiyah yao katika Hajji ilikuwa kwa kumshirikisha Allaah.
Katika Hadiyth hiyo, ‘Abdullaah bin ‘Abbaas (رضي الله عنهما) anaeleza kwamba wapagani walipokuwa wanaitufu Al-Ka’bah, walikuwa wanaianza talbiyah kwa kumpwekesha Allaah (Tawhiyd) wakisema:
"لبَّيكَ لا شَريكَ لكَ"
“Nimekuitikia, (ee Allaah) Huna mshirika yoyote”.
Na kwa vile Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) alikuwa anajua nini wanataka kusema baada ya maneno hayo, alikuwa wanapoleta talbiyah mwanzo kwa kumpwekesha Allaah, huwaambia: Ole wenu! Yaani, mtapata adhabu na maangamizo kwa hayo mnayotaka kuyaongeza katika talbiyah. Acheni hayo, bali toshekeni tu na maneno ya kumpwekesha Allaah, na wala msiongeze baada yake neno lenu (la awali):
"إلَّا شَريكًا هوَ لكَ، تَملِكُه وَما ملَكَ"
“Isipokuwa mshirika, yeye ni Wako, Unammiliki, na yeye hamiliki chochote”
Mshirika wanayemkusudia hapa ni masanamu yao. Na kwa muktadha huo, maneno haya yanabeba maana mbili. Ya kwanza: Wewe Unammiliki pamoja na vyote vilivyomo ndani ya milki yake. Ya pili: Wewe Unammiliki, na yeye hamiliki chochote.
Kwa maana hii, wao wanakiri kwamba mshirika huyu hastahiki kuabudiwa kwa chochote, kwa kuwa yeye mwenyewe hamiliki chochote kwa nafsi yake wala kwa mwingine, bali mmiliki wa yote ni Allaah. Lakini pamoja na kukiri huku, wanamshirikisha na Allaah katika ibaada, ima kwa kuwa hawajui, au kwa inadi, au kwa jeuri, au kwa kibri. Allaah Amesema:
وَاتَّخَذُوا مِن دُونِهِ آلِهَةً لَّا يَخْلُقُونَ شَيْئًا وَهُمْ يُخْلَقُونَ وَلَا يَمْلِكُونَ لِأَنفُسِهِمْ ضَرًّا وَلَا نَفْعًا وَلَا يَمْلِكُونَ مَوْتًا وَلَا حَيَاةً وَلَا نُشُورًا ﴿٣﴾
“Na wakachukua badala Yake (Allaah) waabudiwa wasioumba chochote na hali wao wanaumbwa, wala hawamiliki kwa ajili ya nafsi zao dhara wala manufaa, wala hawamiliki mauti wala uhai wala ufufuo.” [Al-Furqaan (25:3)]
[9] Washirikina Walimpwekesha Allaah Katika Kumuomba Duaa Kwenye Shida Ama Kwenye Raha Walimshirikisha:
Imaam Muhammad Bin ‘Abdil-Wahhaab (رحمه الله) ametaja katika Al-Qawaaid Al-Arba’: Washirikina wa zama zetu ni waovu zaidi katika shirki zao kuliko washirikina wa zamani kwa sababu, wa zamani walimshirikisha Allaah katika raha, lakini walitakasa (ibaada zao) wakati wa shida. Ama washirikina wa sasa, shirki zao ni za kuendelea daima wakiwa katika raha au katika shida. Akatoa dalili Aayah hii ya Al-‘Ankabuwt (29:65).
Rejea pia Suwrah hii Al-‘Ankabuwt (29:61) na Yuwnus (10:31) kwenye faida ziyada.